Mtakatifu Francisko Mfano wa Kuigwa Katika Huduma na Tafakari
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Bunge la Italia kunako mwaka 2005 lilitangaza kwamba, tarehe 4 Oktoba, Sikukuu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi itakuwa ni sikukuu na mapumziko ya kitaifa, ni siku maalum ya kutafakari kuhusu amani, mshikamano wa udugu wa kibinadamu; kanuni na maadili mema pamoja na mshikamano na maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, Mtakatifu Francisko wa Assisi anatambulikana na wengi kwa kujisadaka kwa ajili ya utu, heshima na haki msingi za binadamu na hasa zaidi za maskini; ni mtu aliyejitaabisha kutafuta amani na uhuru wa kuabudu kwa njia ya majadiliano ya kidini na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 5 Oktoba 2022 amewakumbushia waamini kwamba, Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 4 Oktoba anaadhimisha Sikukuu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi, Mlinzi na Mwombezi wa Italia. Mtakatifu huyu ni mfano bora wa kuigwa katika mchakato wa kujiweka wakfu kwa Mwenyezi Mungu na huduma kwa jirani sanjari na ujenzi wa mahusiano ya kidugu na viumbe vyote. Mtakatifu Francisko wa Assisi awe ni dira na mfano bora wa kuigwa na waamini. Wagonjwa, wazee, wanandoa wapya, wafuate mfano wa Mtakatifu Francisko wa Assisi, katika kupenda na kutafakari: huruma na upendo wa Mungu uliotundikwa juu ya Msalaba.
Mtakatifu Francisko wa Assisi aliishi kati ya Mwaka 1181 hadi tarehe 3 Oktoba 1226. Alibatizwa na kupewa jina la Yohane, akachezea ujana wake kwa kupenda sana anasa na matanuzi ya “kufa mtu.” Lakini baadaye alitubu na kumwongokea Mungu, kiasi cha kusadaka maisha yake kwa ajili ya huduma kwa maskini na wakoma waliokuwa wametengwa. Akajitahidi kumfuasa Kristo Yesu, Mwenye moyo mpole na mnyenyekevu, ili kukumbatia na kuambata huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani. Katika maisha yake, Mtakatifu Francisko wa Assisi alishangazwa sana na huruma, upendo na unyenyekevu wa Mungu, uliopelekea hata akatungwa mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu akazaliwa na Bikira Maria Pangoni, mahali pa kulishia wanyama. Safari hii ya unyenyekevu, ya Kristo Yesu, Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, ikapata maana ya pekee kama “Njia ya Msalaba” hata akatundikwa na kufa Msalabani, kifo cha aibu. Hii ni sadaka inayoendelezwa na Mama Kanisa katika Ibada ya Misa Takatifu inayotolewa sehemu mbalimbali za dunia.
Mtakatifu Francisko wa Assisi alijisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu kwenye nchi za Kiislam huku akitumia silaha ya IMANI na huo ukawa ni mwanzo wa mchakato wa majadiliano ya kidini na kwamba, alikuwa tayari kuyamimina na maisha yake kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Vijana wengi wakavutwa na mtindo wa maisha ya Mtakatifu Francisko kiasi hata cha kulazimika kauanzisha Shirika la Ndugu Wadogo wa Mtakatifu Wafrancisko wa Assisi na kanuni ya Shirika hili ikaridhiwa na Papa Onorio wa III kunako mwaka 1223. Katika maisha na utume wake, akabahatika kupata makovu ya madonda Matakatifu mwilini mwake. Aliwapenda sana wanyama na kuyaona mazingira kuwa ni nyumba ya wote, kiasi cha kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu hadi kifo, kiasi cha kulikumbatia Fumbo la kifo kama dada.