Papa Francisko ametuma baraka ya kitume Jimbo kuu Belém do Pará,Brazil
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika kuadhimisha miaka Mia mbili na thelathini ya Cirio ya Nazareti, Baba Mtakatifu Francisko ametuma Baraka ya Kitume kwa Askofu mkuu Alberto Taveira Corrêa wa Jimbo Kuu Katoliki la Belém do Pará nchini Brazil. Katika ujumbe huo uliotiwa saini na Kardinali Pietro Parolin, Katibu wa Vatican kwa niaba ya Baba Mtakatifu, unasomeka kwamba, Papa anataka kuunga mkono, kujitoa kwa waamini ambao wanakimbilia ulinzi wa Mama Yetu wa Nazareti, akiweka chini ya vazi lake la upendo na ulinzi wa kimama nia zote walizobeba mioyoni mwao.
Tamasha kubwa sana nchini Brazil
Hili ni Tamasha la Círio de Nazaré huko Belém ambalo kwa kawaida humheshimu Mama Yetu wa Nazareti na kwa maana hiyo katika Dominika ya pili ya Oktoba, kwa namna hiyo tarehe 9 Oktoba 2022, picha ya mbao ya Mama Yetu hutolewa nje ya Kanisa Kuu hadi kwenye uwanja wa Madhabahu hiyo katika kile ambacho ni mojawapo ya maandamano makubwa zaidi ya kidini duniani. Idadi kubwa ya mahujaji husafiri kutoka nchini kote Brazil ili kuhudhuria tamasha hilo na kutoa heshima yao.
Kwa maana hiyo huku macho yake yakiwa yameelekezwa kwa Mlezi wa Jimbo Kuu la Belém do Pará na Malkia wa Amazonia, Baba Mtakatifu Francisko amekumbusha kila mtu kwamba: “Maria aliweka vitu vyote kuwa hazina, huku akiyatafakari moyoni mwake”, hivyo kama Mama na Mwalimu amesema "anaweza kutusaidia kutunza na kutafakari kila kitu, bila kuogopa majaribu, kwa uhakika wa furaha kwamba Bwana ni mwaminifu na anajua jinsi ya kubadilisha misalaba kuwa ufufuko."
Mwisho wa ujumbe huo Baba Mtakatifu Francisko anabainisha kwamba: “Utakatifu wake Mama Bikira wa Upendo amwombe Mwanae ili neema tele iweze kumiminwa kwa watu wa Pará na Brazili, ili kusaidia kila mtu kuishi Injili”. Kwa kuwa na uhakika wa maombi hayo Baba Mtakatifu, kwa moyo wake wote amewapatia Baraka ya Kitume, huku akiwaomba kila mmoja hasisahau kusali kwa ajili yake.