Papa Francisko Asikitishwa na Mauaji ya Kinyama Nchini DRC
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 26 Oktoba 2022 ameonesha masikitiko yake makubwa kutokana na matukio ya kutisha yanayoendelea kusababisha umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia huko Maboja, Kivu, Kaskazini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo. Amesikitishwa na kufadhaishwa sana na shambulio lililotokea hivi karibuni huko Maboja ambako Vituo viwili vya afya vya Jimbo Katoliki la Butembo-Beni vimechomwa moto na watu saba kuuwawa kikatili akiwemo Sr. Marie-Sylvie Kavuke Vakatsuraki, wa Shirika la Masista Dada Wadogo wa Mama Yetu Bikira Maria Kutolewa Hekaluni: “Petites Sœurs de la Présentation de Notre-Dame” lililoanzishwa kunako mwaka 1952, huko Butembo-Beni.
Sr. Marie-Sylvie Kavuke Vakatsuraki, alikuwa anahudumia Vituoni hapo kama Daktari. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wenye mapenzi kuwakumbuka na kuwaombea waathirika pamoja na familia zao, Jumuiya hii ya Kikristo pamoja na wakazi wa eneo hili ambao kimsingi wamechoswa na vurugu kwa muda mrefu sana.