Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko kwenye Ufalme wa Bahrain unapania kukuza na kudumisha diplomasia kwa ajili ya majadiliano ya kidini, haki na amani duniani. Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko kwenye Ufalme wa Bahrain unapania kukuza na kudumisha diplomasia kwa ajili ya majadiliano ya kidini, haki na amani duniani. 

Papa Francisko: Diplomasia na Majadiliano ya Kidini: Haki, Amani Na Maridhiano

Baba Mtakatifu ametia nia ya kufanya hija ya kitume kwenye Ufalme wa Bahrein kuanzia tarehe 3 hadi 6 Novemba 2022. Lengo ni kushiriki katika maadhimisho ya Kongamano la Bahrain la Majadiliano: Mashariki na Magharibi Kwa Ajili ya Kuishi Pamoja Kwa Binadamu. Adui mkubwa wa mchakato wa majadiliano ya kidini ni woga, kushindwa kufahamiana na kuishi kwa amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 27 Oktoba 2022 amepokea hati za utambulisho kutoka kwa Muhammad Abdul Ghaffar, Balozi wa Ufalme wa Bahrein mjini Vatican. Hili ni tukio la kihistoria hasa wakati huu ambapo Baba Mtakatifu Francisko ametia nia ya kufanya hija ya kitume kwenye Ufalme wa Bahrein kuanzia tarehe 3 hadi 6 Novemba 2022. Lengo ni kushiriki katika maadhimisho ya Kongamano la Bahrain la Majadiliano: Mashariki na Magharibi Kwa Ajili ya Kuishi Pamoja Kwa Binadamu. Adui mkubwa wa mchakato wa majadiliano ya kidini ni woga na wasiwasi usiokuwa na msingi, mambo yanayochangia watu wa dini mbalimbali duniani, kushindwa kufahamiana na hatimaye, kuishi kwa amani na utulivu; umoja, upendo, mshikamano na udugu wa kibinadamu kwa kutambua kwamba, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na hivyo tofauti zao za kidini si sababu msingi ya malumbano na kinzani zisizo na tija wala mashiko, ustawi na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wa Kitume: "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” anapembua utamaduni wa udugu wa kibinadamu kama chombo cha ujenzi wa ushirikiano na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa kwa kubainisha njia itakayotumika na malengo yake katika uhalisia wa maisha ya watu.

Diplomasia ya Vatican inalenga kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano
Diplomasia ya Vatican inalenga kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano

Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa ujenzi wa ushirikiano na mafungamano yanayokita mizizi yake katika maendeleo na ushirikiano katika masuala ya kiuchumi kwa kuzingatia majadiliano ili kufikia malengo yaliyokusudiwa yaani amani. Kwa sababu vita inasababisha maafa kwa watu na mali zao; vita ina sababisha vifo, inaharibu mazingira pamoja na kufisha matumaini ya watu. Majadiliano katika ukweli na uwazi yanavunjilia mbali kuta za utengano: kiroho na kiakili; yanafungua nafasi ya msamaha na kukoleza upatanisho. Majadiliano ni chombo cha haki kinachochochea na kuimarisha mahusiano na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa kwa kukazia amani. Majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni yanapaswa kufumbata uvumilivu, yanajielekeza katika mchakato wa ushuhuda kama chombo cha ujenzi wa udugu wa kibinadamu, upendo na mafao ya wengi. Malengo ya Waraka wa Kitume:"Fratelli tutti" ni kuhamasisha ujenzi wa mshikamano wa kidugu unaoratibiwa na kanuni auni, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Kongamano la Bahrain la Majadiliano 3-4 Novemba 2022
Kongamano la Bahrain la Majadiliano 3-4 Novemba 2022

Itakumbukwa kwamba, Balozi Muhammad Abdul Ghaffar wa Ufalme wa Bahrein mjini Vatican, alizaliwa Manama tarehe 15 Januari 1949, ameoa na kubahatika kupata watoto watano! Baada ya masomo yake na hatimaye, kujipatia Shahada ya uzamivu katika Sayansi ya Siasa jamii kunako mwaka 1974 kutoka Chuo Kikuu cha Poona nchini India, mwaka 1975 akaanza rasmi shughuli za kidiplomasia na kubahatika kutekeleza dhamana hi inchini Yordan, Umoja wa Mataifa na kuanzia mwaka 1993 hadi mwaka 2001 akateuliwa kuwa ni Balozi wa Ufalme wa Bahrein nchini Marekani, Argentina kuanzia 1995 hadi mwaka 2001 kama Balozi asiye mkazi. Kati ya Mwaka 2001 hadi mwaka 2005 aliteuliwa kuwa ni Waziri wa mambo ya nchi za nje. Mwaka 2005 hadi mwaka 2007 akateuliwa kuwa ni Waziri wa Habari na Mwaka 2008 hadi mwaka 2009 akateuliwa kuwa ni Balozi wa Ufalme wa Bahrein nchini Ubelgiji. Kati ya mwaka 2009 hadi mwaka 2014 aliteuliwa kuwa ni Mshauri wa Mfalme katika masuala ya Kidiplomasia. Kati ya Mwaka 2015 hadi mwaka 2021 alikuwa ni Balozi wa Ufalme wa Bahrein nchini Ufaransa na Vatican. Mwaka 2022 alikuwa ni Balozi wa Ufalme wa Bahrein nchini Ufaransa. Na tarehe 27 Oktoba 2022 akawasilisha hati zake za utambulisho kwa Baba Mtakatifu Francisko kama Balozi mpya wa Ufalme wa Bahrein mjini Vatican.

Majadiliano ya Kidini

 

30 October 2022, 15:12