Papa,Miaka 60 ya Mtaguso II wa Vatican:uchaguzi wa njia ya amani katika tishio la nyuklia!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Mara baada ya misa takatifu ya kuwatangaza Watakatifu na kabla ya sala ya Malaika wa Bwana, katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, Dominika tarehe 9 Oktoba 2022, Baba Mtakatifu Francisko amesema kwamba: “Kabla ya kuhitimisha maadhimisho haya ya Ekaristi, ninawasalimia na kuwashukuru wote mliofika kuwaheshimu watakatifu wapya! Ninawasalimia makardinali, maaskofu, mapadre, watawa, kwa namna ya pekee wamisionari wote kike na kiume wa Mtakatifu Karoli Borromea na Ndugu wa Kisalesiani. Ninawasalimia na kuwa na utambuzi wa Uwakilishi wa maafisa".
Mwenyeheri mpya Maria Costanza Panas
Baba Mtakatifu Francisko akiendelea alikumbusha jinsi ambavyo Dominika jioni wangemtangaza kuwa mwenyeheri Maria Costanza Panas, mmonaki wa ndani, ambaye ni Mkapuchini aliyeishi kwenye Monasteri ya Fabriano nchini Italia mnamo 1917 -1963, ambapo aliitwa na mwenyezi Mungu. Papa amesema kwamba alikuwa akikiwakaribisha wale wote waliokuwa wakibisha hodi katika mlango wa Monasteri yake huku akieneza kwa wote utulivu na imani. Katika miaka ya mwisho akiwa mgojwa sana, alitoa mateso yake kwa ajili ya Mtaguso II wa Vatican na ambapo tukio la kufunguliwa kwake litatakumbukwa miaka 60, mnamo Jumanne tarehe 11 Oktoba. Mwenyeheri Maria Costanza, Papa ameongeza kusema atusaidie kuwa wenye imani daima kwa Mungu na kuwakaribishwa jirani.
Miaka 60 ya kutangazwa kwa Mtaguso wa II wa Vatican
Papa Francisko akikumbuka ufunguzi wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Kanisa Katoliki iliofanyka miaka 60 iliyopita, ambapo ulianza mnamo tarehe 11 Oktoba 1962 hadi tarehe 8 Desemba 1965, amesema hatuwezi kusahau hatari za vita vya kunyuklia ambapo hasa wakati huo vilikuwa tishio ulimwenguni. Je kwa nini tusijifunze kutoka katika historia? Hata katika wakati ule kulikuwa na migogoro na mivutano mikubwa, lakini walichagua njia ya amani. Imeandikwa katika Biblia kwamba: “Bwana asema hivi: simaneno katika njia kuu, mkaone, mkauliza habari za mapito ya zamani, i wapi njia iliyo njema ? mkaende katika njia hiyo nanyi mtajipatia rha katika nafasi zenu (Yer 6,16).
Waathirika wa Thailand
Papa vile vile, amekumbuka matukio ya vurugu ya hivi karibuni kwamba: “Ninawahakikisha sala zangu waathirika wa matendo ya kipuuzi ya vurugu zilizojitokeza siku tatu zilizopita nchini Thailand, na kwa uchungu huo anawakabidhi kwa Baba wa maisha, kwa namna ya pekee watoto wadogo na familia zao. Kwa maana hiyo Papa amemgeukia Bikira Maria ili aweze kusaidia kuwa mashuhuda wa Injili, wanaoongozwa na mifano ya Watakatifu.
Kuhusiana na mauaji nchini Thailand inasemekana watu 38, wakiwemo watoto 24, ni idadi kubwa ya mauaji katika shule moja huko Uthai Sawan, kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo, kwa njia ya mikono ya polisi wa zamani ambaye lakini alijiua. Mwanamume huyo pia alimuua mkewe, mwanawe na wanafamilia wengine. Muuaji, huyo inasemekana ni mwenye umri wa miaka 34, alikuwa polisi wa zamani ambaye alikuwa amefukuzwa kazi hivi karibuni kwa sababu ya matatizo ya dawa za kulevya. Miongoni mwa waathirika pia ni mwalimu mwenye ujauzito wa miezi 8.