Papa Francisko: Chakula na maji ni kati ya haki msingi za binadamu na haki nyingine zote zinapata umuhimu wake katika: Chakula bora na Maji safi na salama. Papa Francisko: Chakula na maji ni kati ya haki msingi za binadamu na haki nyingine zote zinapata umuhimu wake katika: Chakula bora na Maji safi na salama. 

Ujumbe wa Papa Francisko: Kongamano la Chakula Duniani 2022: Chakula Ni Haki Msingi

Papa Francisko katika Maadhimisho ya Kongamano la Chakula Duniani kwa mwaka 2022, anaipongeza FAO kwa mikakati inayopania kung’oa kabisa baa la njaa duniani. Chakula ni sehemu ya haki msingi za binadamu, kumbe, kinapaswa kuwa ni kitovu cha sera na mikakati ya shughuli za chakula na kilimo, kwa kujikita katika mshikamano na udugu wa kibinadamu ili kujenga umoja.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuwalisha wenye njaa na kuwanywesha wenye kiu ni dhamana ya kimaadili kwa Kanisa la Kiulimwengu. Chakula na maji ni kati ya haki msingi za binadamu na haki nyingine zote zinapata umuhimu wake katika: Chakula na Maji. Hii ni changamoto kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujenga moyo wa upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu ili kuhakikisha kwamba, watu wengi zaidi wanapata chakula bora na maji safi na salama kwa ajili ya matumizi yao kama sehemu ya haki msingi za binadamu pasi na ubaguzi. Chakula bora ni sehemu ya haki msingi za binadamu, utu na heshima yake. Balaa la njaa ni kashfa kubwa inayopaswa kuvaliwa njuga na wadau mbalimbali kwa kujenga uchumi fungamani na endelevu; kwa kuondokana na mifumo inayozalisha ukosefu wa haki msingi za binadamu, sanjari na kujikita katika kanuni maadili na utu wema. Jumuiya ya Kimataifa ijenge na kudumisha utamaduni wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Watu washirikishwe katika mchakato huu na asiwepo hata mtu mmoja anayebaki nyuma ya mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Jumuiya ya Kimataifa ijenge mazingira ya usawa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Watu wawe na uhakika wa kupata chakula bora na kwa bei wanayoweza kuimudu kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao. Mambo yote haya yanafumbatwa katika msingi wa haki jamii, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote sanjari na ujenzi wa uchumi unaokita malengo na sera zake kwa mahitaji msingi ya binadamu na utu wake ukipewa kipaumbele cha kwanza.

Chakula ni sehemu ya haki msingi za binadamu kiheshimiwe na kutunzwa
Chakula ni sehemu ya haki msingi za binadamu kiheshimiwe na kutunzwa

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa kuanzia tarehe 17 hadi tarehe 21 Oktoba 2022 linaendesha Kongamano la Chakula Duniani, linalonogeshwa na kauli mbiu "Lishe zenye Afya. Sayari yenye Afya” na linafanyika kwenye Makao makuu ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) mjini Roma nchini Italia. Jumuiya ya Kimataifa imeendelea kujizatiti katika mapambano dhidi ya baa la njaa na umaskini duniani, unaosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu, lakini matukio ya hivi karibuni yanaonesha kukwamisha harakati hizi. Vita kati ya Urussi na Ukraine, Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi zinaendelea kudumaza mchakato wa mapambano dhidi ya baa la njaa na umaskini duniani. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Dr. QU Dongyu, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO, kama sehemu ya Maadhimisho ya Kongamano la Chakula Duniani kwa mwaka 2022, anaipongeza FAO kwa sera na mikakati inayopania kung’oa kabisa baa la njaa duniani. Chakula ni sehemu ya haki msingi za binadamu, kumbe, kinapaswa kuwa ni kitovu cha sera na mikakati ya shughuli za chakula na kilimo, kwa kujikita katika mshikamano na udugu wa kibinadamu ili kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano kati ya watu wa Mataifa. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Mkurugenzi mkuu wa FAO, anaishukuru na kuipongeza FAO katika jitihada zake za kutaka kung’oa kabisa kutoka katika uso wa dunia kashfa ya baa la njaa. Hii ni inatokana na ukweli kwamba, chakula ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu na utakatifu wake.

Vita, UVIKO-19 Athari za mabadiliko ya tabia njema zimeathiri uzalishaji wa chakula
Vita, UVIKO-19 Athari za mabadiliko ya tabia njema zimeathiri uzalishaji wa chakula

Kumbe, chakula kinapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na kamwe kisigeuzwe kuwa kama bidhaa nyingine sokoni. Chakula kiheshimiwe na kuthaminiwa kama Ekaristi Takatifu kwa Wakristo kwani Kristo Yesu anasema “Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.” Yn 6: 51. Ili kutambua na kuthamini umuhimu wa chakula na utakatifu wake katika maisha ya mwanadamu, kuna haja kwa wadau mbalimbali kutambua kwamba, chakula ni zawadi kutoka kwa Mungu na kwamba, mwanadamu amepewa dhamana ya kukisimamia na kukiratibu. Kipaumbele cha kwanza ni utu na heshima ya binadamu; haki na mahitaji yake msingi hasa miongoni mwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Huu ni mwaliko wa kujenga na kudumisha mshikamano wa udugu wa kibinadamu, si tu kwa kuwalisha na kuwanywesha watu, bali watu wenyewe wajitoe sadaka kwa ajili ya huduma kwa jirani zao; binadamu akipewa upendeleo wa pekee. Jambo hili linawezekana anasema Baba Mtakatifu Francisko ikiwa kama mshikamano na udugu wa kibinadamu vitapewa kipaumbele cha kwanza, ili kujenga mshikamano na mafungamano ya kijamii kati ya watu wa Mataifa, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Vita imeathiri sana uzalishaji na usambazaji wa chakula ulimwenguni
Vita imeathiri sana uzalishaji na usambazaji wa chakula ulimwenguni

Ni katika muktadha huu, vijana wanapaswa kuwezeshwa zaidi, katika shughuli za kilimo ili Jumuiya ya Kimataifa iweze kuwa na uhakika wa usalama wa chakula, tayari kujizatiti katika mapambano dhidi ya baa la njaa duniani. Kongamano la Chakula Duniani kwa mwaka 2022 linashirikisha Jukwaa la Vijana, WFF, Jukwaa la Sayansi na Ubunifu la FAO na Jukwaa la Uwekezaji na Mshikamano na FAO. Lengo la ushiriki wa Mabaraza haya matatu ni kuunganisha nguvu ili kuchochea mifumo ya sekta ya kilimo kwa kuzingatia majanga ya sasa na changamoto zake; kwa kuonesha umuhimu wa ushirikiano na mshikamano wa kidugu katika masuala ya sayansi, teknolojia na uvumbuzi, ili kuchangia katika mchakato wa uwekezaji katika maeneo muhimu ya chakula na kilimo. Kongamano linawahusisha pia wakulima na wazalishaji wadogo wadogo, wazawa, watunga sera na mikakati ya shughuli za kilimo bila kuwasahau wawekezaji katika sekta ya kilimo, lengo ni kufikia mustakabali wa usalama na uhakika wa chakula kwa wote, bila kumwacha mtu awaye yote nyuma.

Kongamano FAO
18 October 2022, 15:22