UNIAPAC imekuwa mstari wa mbele katika kuwafahamisha wanachama wake masuala muhimu mintarafu biashara na mwenendo wa kiuchumi. UNIAPAC imekuwa mstari wa mbele katika kuwafahamisha wanachama wake masuala muhimu mintarafu biashara na mwenendo wa kiuchumi.  

Ujumbe Kwa Shirikisho la Vyama Vya Wajasiriamali Wakatoliki: Ajira

Mfumo mpya wa uchumi: Umuhimu wake ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ili kung’oa umaskini kwa kutengeneza fursa za ajira; mchakato unaosimikwa katika upendo wa udugu wa kibinadamu na urafiki wa kijamii. Mfumo unajikita katika mshikamano kwa kusimikwa katika utu, heshima na haki msingi za wafanyakazi, pamoja na kuwasaidia kupata fursa za ajira.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Wajasiriamali Wakatoliki, UNIAPAC linaundwa na vyama vya wajasiriamali kutoka nchini: Uholanzi, Ubelgiji, Ufaransa na watazamaji kutoka Italia, Ujerumani na Czechoslovakia). UNIAPAC ni matunda ya maadhimisho ya miaka arobaini tangu kuchapishwa kwa Waraka wa “Rerum novarum” yaani “Mambo Mapya”, kwa lengo la kuwakusanya pamoja wajasiriamali na watendaji ambao, kwa ajili ya kutekeleza wajibu na kazi zao za kitaaluma, wanatiwa moyo na Mafundisho Jamii ya Kanisa. Itakumbukwa kwamba, Kanisa Katoliki lina amana na utajiri mkubwa wa Mafundisho Jamii yanayopata chimbuko lake katika Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Leo XIII; Mambo Mapya; Rerum Novarum. Lengo la UNIAPAC ni:Kuwaunganisha, kuwaongoza na kuwatia moyo viongozi wa biashara ili, kwa kuzingatia Mafundisho Jamii ya Kikristo, wajitolee kwa: Majiundo yao binafsi; wasaidie mchakato wa kufanya mabadiliako kwenye Makampuni na mazingira yao; sanjari na kuendelea kujikita katika ujenzi wa jamii inayosimikwa katika haki, utu na heshima ya binadamu. Baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, UNIAPAC ilianza kujipanua katika nchi nyingine za Ulaya na Amerika ya Kusini. Katika miaka ya 1960, Muungano huo ukachukua mwelekeo wa Kiekumene, ukichukua jina lake la sasa, na kuendelea kujivumuisha vyama kutoka Asia na Afrika miongoni mwa wanachama wake.

UNIAPAC imekuwa mstari wa mbele katika kuwafahamisha wanachama wake masuala muhimu mintarafu biashara na mwenendo wa kiuchumi. Shirikisho hili lina uhusiano na Vatican, Baraza la Makanisa ya Kiekumene na linao pia wanachama watazamaji kama: Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO, Shirika la Uhasibu la Italia, OIC; Shirika la Kazi Duniani, ILO, pamoja na Tume ya Kiuchumi ya Amerika ya Kusini. UNIAPAC kuanzia tarehe 20-22 Oktoba 2022 inaadhimisha Kongamano la 27 la UNIAPAC, linalonogeshwa na kauli mbiu “Ujasiri wa kubadilika”: “The XXVII UNIAPAC World Congress “Courage to Change.” Ijumaa tarehe 21 Oktoba 2022 wameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Kardinali Michael Czerny SJ, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu na Fungamani ya Binadamu na baadaye wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko amekazia umuhimu wa sera na mbinu mkakati wa kiuchumi unaojielekeza katika: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ili kung’oa umaskini kwa kutengeneza fursa za ajira; mchakato unaosimikwa katika upendo wa udugu wa kibinadamu na urafiki wa kijamii. Mfumo wa Uchumi mpya ni kwa ajili ya mafao ya wengi kwa kujikita katika mshikamano na mafungamano ya kijamii, kwa kusimikwa kikamilifu katika utu, heshima na haki msingi za wafanyakazi, pamoja na kuwasaidia kupata fursa za ajira ili waweze kujitegemea badala ya kuwa ni ombaomba wa rasilimali fedha.

Mfumo mpya wa uchumi kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi
Mfumo mpya wa uchumi kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi

Uchumi mpya unapaswa kujielekeza katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Dhana ya “Uchumi wa Francesco” huko Assisi “Economy of Francesco”  inapania kuragibisha “Agano la pamoja” kama sehemu ya mchakato wa mabadiliko ya uchumi ulimwenguni kwa kuwakumbatia na kuwaambata watu wote bila ya kujali tofauti za imani wala utaifa wao, bali watu ambao wanaongozwa na dhana ya udugu wa kibinadamu kwa kuwajali maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Vijana wa kizazi kipya wamependekeza uchumi wa Injili. Baba Mtakatifu Francisko anasema, sera na mbinu mkakati wa uchumi unapaswa kwanza kabisa kutambulika kuwa ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kuelekezwa katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, ili kupambana na baa la umaskini linalosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu, ili kuwajengea watu wa Mungu matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Changamoto hii inaweza kutekelezwa kwa makini, ikiwa kama itasimikwa na kujengeka katika upendo wa udugu wa kibinadamu na urafiki wa kijamii. Mfumo wa uchumi mpya unapaswa kujielekeza zaidi katika mafao ya wengi, ili kukazia: mshikamano wa udugu wa kibinadamu, haki jamii, ustawi na maendeleo ya familia yote ya Mungu.

Mfumo mpya wa uchumi unapaswa kuwa ni mchakato unaojenga umoja na mafungamano kati ya watu wa Mataifa, kwa binadamu na mahitaji yake msingi akipewa kipaumbele cha kwanza, kwa kuzingatia madhara makubwa yaliyojitokeza wakati wa maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Wafanyakazi wa kawaida wamechagia sana katika kushikilia uchumi wakati wa UVIKO-19. Ni katika muktadha huu, utu, heshima na haki msingi za wafanyakazi zinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, ili hatimaye kuondokana na kazi hatarishi, chafu na fursa zisizoheshimu wala kuthamini utu na heshima ya binadamu. Sura na mwelekeo wa mfumo mpya wa uchumi hauna budi kujikita katika kipaji cha ubunifu, kanuni maadili na utu wema, kwa kutambua kwamba, uchumi unapaswa kuwa ni kwa ajili ya huduma kwa binadamu. Kazi ni utimilifu wa utu na heshima ya binadamu ambaye ameumbwa ili kufanya kazi. Kazi ni sehemu muhimu sana ya maisha, ni njia ya makuzi, ustawi, maendeleo na furaha ya mwanadamu. Kutoa msaada wa fedha kwa maskini, linapaswa liwe suluhisho la muda katika mahitaji msingi. Lengo madhubuti la kuwasaidia maskini ni fursa ya kujijengea heshima kwa njia ya kufanya kazi. Rej. Laudato si, n. 128. Utu na heshima ya mwanadamu inasimikwa na kupata ukamilifu wake katika kufanya kazi sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

UVIKO-19 umekuwa na madhara makubwa katika medani mbalimbali za maisha.
UVIKO-19 umekuwa na madhara makubwa katika medani mbalimbali za maisha.

Ni katika muktadha huu wa umuhimu wa kazi kama sehemu ya utu, heshima na haki msingi za binadamu, Baba Mtakatifu Francisko amependa kuwashirikisha mapendekezo yaliyotolewa hivi karibuni na  vijana wa kizazi kuhusu Injili ya Uchumi: Kwamba, huu ni mfumo wa uchumi mpya kwa mafao ya wote. Uchumi wa Injili", ambao, pamoja na mambo mengine, unajumuisha: Uchumi wa amani na si wa vita;Uchumi unaotunza kazi ya uumbaji na kutoupoka; Uchumi unaojikita katika huduma ya mtu, familia na Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo ; uchumi unaoheshimu watu na zaidi ya yote walio dhaifu na walio hatarini. Huu ni uchumi ambapo utunzaji unachukua nafasi ya upotevu na kutojali. Ni mfumo wa uchumi usiomwacha mtu nyuma, ili kujenga jamii ambamo mawe yaliyotupwa na fikra tawala huwa msingi. Ni mfumo wa uchumi unaotambua na kulinda kazi nzuri na salama kwa wote. Ni uchumi ambao fedha ni rafiki na mshirika wa uchumi halisi na wa kazi na wala si kinyume chake. Baba Mtakatifu Francisko mwishoni mwa hotuba yake analitaka Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Wajasiriamali Wakatoliki, UNIAPAC kushikamana na wachumi na wafanyabiashara vijana, ili kusaidia kuleta mchakato wa mwelekeo wa mfumo mpya wa uchumi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Vijana wa kizazi kipya wamependekeza Injili ya Uchumi 2022
Vijana wa kizazi kipya wamependekeza Injili ya Uchumi 2022

Kwa upande wake, Kardinali Michael Czerny SJ, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu na Fungamani ya Binadamu katika mahubiri yake amekazia umuhimu wa watu wa Mungu kujikita katika misingi ya haki, amani, ustawi, maendeleo na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kila mtu ajitahidi kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa ari na moyo mkuu; katika msingi ya ukweli, uwazi, haki na uaminifu. Wajumbe wa UNIAPAC wawe ni manabii wanaotangaza, kushuhudia, kujenga na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote; kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kuendeleza Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Wajenge na kuimarisha mahusiano na mafungamano yao na Mwenyezi Mungu kwa njia ya toba na wongofu wa ndani, ili kuleta wongofu wa kiuchumi. Wawe ni wafanyakazi bora wanaotekeleza dhamana na wajibu wao kwa bidii, juhudi na maarifa kama sehemu ya mchakato wa kupambana na baa la umaskini unaosigina: utu, heshima na haki msingi za binadamu, kwa wao kujikita katika mchakato wa ujenzi wa mahusiano baina ya siasa na uchumi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Papa Uchumi
21 October 2022, 15:36