Utume wa Mapadre Kwa Vijana wa Kizazi Kipya: Kuwasindikiza, Kuwasilikiza na Kuwashauri
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mapadre wa maisha ya kiroho katika shule zinazotumia Kifaransa kama lugha ya kufundishia nchini Uswis, wanayo dhamana nyeti sana katika kukoleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene, unaosimikwa katika moyo wa ukarimu na mapendo, kwa ajili ya huduma kwa vijana wa kizazi kipya. Haya ni matunda ya uzoefu na mang’amuzi ya maisha ya kiroho, yanayowawezesha kutembea bega kwa bega na vijana wa kizazi kipya ili; kuwasindikiza, kuwasikiliza na kuwazamisha katika maisha ya sala. Ni katika hali ya ukimya na faragha, machozi yanaweza kumiminika kama kielelezo cha furaha na uponywaji wa ndani, kiasi hata cha kuweza kuwashirikisha wengine historia, ndoto na machungu ya moyoni. Huu ni wito na dhamana inayohitaji kupyaishwa daima kwa nguvu na uweza kutoka kwa Kristo Yesu. Huu ni muhtasari wa hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 7 Oktoba 2022 alipokutana na kuzungumza na Mapadre wa maisha ya kiroho katika shule zinazotumia Kifaransa kama lugha ya kufundishia nchini Uswis. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko tarehe 25 Machi 2019 akiwa kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Loreto, alitia mkwaju kwenye Wosia wake wa Kitume “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi” na kuzinduliwa rasmi tarehe 2 Aprili 2019.
Wosia huu ni matunda ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa Mwaka 2018, yaliyoongozwa na kauli mbiu “Vijana, Mang’amuzi na Miito.” Huu pia ni mwendelezo wa mchakato wa Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu kwa ajili ya familia, kwani utume wa Kanisa kwa familia na vijana ni sawa na chanda na pete; unategemeana na kukamilishana! Ni wosia ulioandikwa katika mfumo wa barua kwa vijana na Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kwamba, Kristo Yesu anaishi na ni matumaini na uzuri wa ujana katika ulimwengu mamboleo. Yale yote yanayoguswa na Kristo Yesu yanapyaishwa na kupata uzima mpya! Ujumbe mahususi kwa vijana ni kwamba, “Kristo anaishi! Wosia huu umegawanyika katika sura tisa amana na utajiri unaobubujika kutoka katika mchakato mzima wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, iliyofikia kilele chake mwezi Oktoba 2018. Baba Mtakatifu anawaalika vijana kuendelea kuandika kurasa za maisha na utume wao kwa kuchota amana na utajiri unaobubujika kutoka katika Wosia wake wa Kitume “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi.”
Utume wa Mapadre kwa vijana wa kizazi kipya unaosimikwa katika safari ya pamoja hatua kwa hatua, kwa kusikiliza na kutafakari: matamanio halali, “ndoto za mchana” miongoni mwa vijana; karama na mapungufu yao ya kibinadamu; wasiwasi na mashaka yaliyomo ndani mwao, mwishoni vijana hawa wanapopata nafasi ya kuzungumza na Kristo Yesu kutoka katika undani wa maisha yao, matumaini mapya yanachanua kama “maua ya kondeni” na hivyo kupata ari na mang’amuzi mapya kama ilivyokuwa kwa wale wanafunzi wa Emau waliobahatika kuandamana na Kristo Yesu katika safari yao ya matumaini bila kumtambua kwani macho yao yalikuwa yamefumbwa! Lakini, wakamtambua Kristo Yesu wakati wa kuumega mkate na hapo hapo akatoweka tena machoni pao! Nao wakaambiana, Je, mioyo yetu haikuwaka ndani yetu pale alipokuwa akizungumza na kufafanua Maandiko Matakatifu? Uwepo angavu wa Kristo Yesu katika maisha ya ujana, si juhudi zao binafsi, bali ni kwa nguvu na uweza wa Roho Mtakatifu anayetenda kazi ndani mwao, jambo la msingi ni kwa vijana kuhakikisha kwamba, wanatembea bega kwa bega na Kristo Yesu Mfufuka.
Baba Mtakatifu Francisko anakazia umuhimu wa mwendelezo wa mchakato wa majadiliano ya kiekumene miongoni mwa Wakristo ili kujibu changamoto ya Kristo Yesu, kwa wafuasi wake, ili wote wawe wamoja, ili kweli Injili iweze kuwa na nguvu zaidi inapotangazwa na kushuhudiwa na Wakristo wote pasi na migawanyiko; kwa kuondokana na wasiwasi pamoja na mashaka ambayo wakati mwingine yanagumisha majadiliano ya kiekumene. Ni wajibu kwa wakristo wote kujikita katika majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika sala na maisha ya kiroho; katika ushuhuda wa damu na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Wakristo kwa pamoja wanatafuta amani ing’aayo uso wa Mungu; kwa kuwa wapatanishi; watangazaji na mashuhuda wa Injili ya Kristo na Kanisa lake. Wakristo wanapaswa kushikamana na kushirikiana, ili kutekeleza Amri ya Kristo kwa wafuasi wake, ili wote wawe wamoja. Baba Mtakatifu anawatia shime kukiza zaidi nguvu zao katika majadiliano ya kiekumene.