Kongamano limechota amana na utajiri mkubwa kutoka katika Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: “Gaudete et exsultate” Kongamano limechota amana na utajiri mkubwa kutoka katika Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: “Gaudete et exsultate”  

Watakatifu Ni Amana, Utajiri na Katekesimu ya Kanisa Katoliki

Watakatifu ni amana na utajiri wa Kanisa unaofafanua tunu msingi za Kiinjili. Ni Katekisimu inayofafanua: Imani, Sakramenti, Maisha adili na Sala. Ni watu wenye mvuto na mashiko kwa maisha na utume wa Kanisa katika imani, matumaini na mapendo thabiti. Hii ni changamoto kwa Kanisa na Jamii kwa kutambua alama na ishara za utakatifu wa maisha, hata katika njia zisizofahamika bado.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Waamini Kuwa Wenyeheri na Watakatifu, kuanzia tarehe 3-6 Oktoba 2022 limekuwa likiendesha kongamano la Kimataifa, ambalo limenogeshwa na kauli mbiu “Utakatifu kwa Nyakati Hizi.” Kongamano limechota amana na utajiri mkubwa kutoka katika Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo.” Na hatimaye, washiriki wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi tarehe 6 Oktoba 2022. Upendo wa dhati ni njia inayoweza kuwapeleka waamini katika utakatifu wa maisha! Wanapaswa pia kusikiliza, kutafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao; wajitahidi kushiriki mara kwa mara Sakramenti za Kanisa; kwa kujitia uthabiti katika kusali, kujinyima pamoja na kutekeleza matendo ya huruma: kiroho na kimwili kwa wahitaji zaidi. Hii ndiyo changamoto inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo.” Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu Fumbo la Kanisa wanasema, Wakristo wote wanaitwa na kuhamasishwa kushiriki utakatifu mmoja, kwa kumtii na kumwabudu Mwenyezi Mungu katika roho na kweli; kwa kumfuasa Kristo Yesu aliyekuwa ni: mtii, fukara na mnyenyekevu wa moyo, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kwa njia hii, wastahilishwe kushiriki utukufu wa Kristo Yesu!

Utakatifu umwilishwe katika uhalisia wa maisha ya kila siku
Utakatifu umwilishwe katika uhalisia wa maisha ya kila siku

Watu wote wa familia ya Mungu wanaitwa kuwa ni watakatifu, kwani haya ni mapenzi ya Mungu. Kristo Yesu ndiye chemchemi na utimilifu wa utakatifu wote! Baba Mtakatifu anasema, utakatifu ni mwaliko kwa waamini wote na wala si kwa watu wachache tu ndani ya Kanisa! Huu ni mwaliko wa kuongeza jitihada za kukutana na Kristo Yesu katika maisha kwa njia ya toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata: huruma na upendo wa Mungu katika maisha. Watakatifu ni watu wa kawaida kabisa, ni wadhambi waliotubu na kumwongokea Mungu, leo hii wamekuwa ni marafiki zake wa karibu! Watakatifu ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao! Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, Wakristo wote wamejichukulia dhamana ya kuanza mchakato wa safari ya utakatifu wa maisha! Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanazungumzia kuhusu wito wa watu wote katika Kanisa kuwa watakatifu; namna nyingine za kutekeleza utakatifu ulio mmoja na mwishoni ni njia za utakatifu. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake, amegusia kuhusu utakatifu wa maisha, mifano bora ya watakatifu, mashuhuda na waalimu wa imani. Utakatifu unapaswa kupata chimbuko na asili yake katika jumuiya ya waamini; sifa za utakatifu na mchango wa vyombo vya mawasiliano ya jamii katika kuwaibua watakatifu watarajiwa. Baba Mtakatifu anasema, lengo la wosia huu ni mwaliko wa kuwa watakatifu kila mtu kadiri ya hali na wito wake; kwa kutambua vizingiti, changamoto na fursa ambazo zinaweza kutumiwa na waamini kufikia utakatifu wa maisha. Kristo Yesu anawaalika waja wake ili wawe watakatifu, watu wasiokuwa na hatia mbele zake katika upendo. (Rej. Ef. 1:4).

Utakatifu ni safari ya maisha ya mwamini kuambata tunu za Kiinjili
Utakatifu ni safari ya maisha ya mwamini kuambata tunu za Kiinjili

Huu ni utakatifu unaoshuhudiwa na watu wa ndoa katika malezi na makuzi ya watoto wao; wafanyakazi katika sekta ya afya, wanaowatunza na kuwahudumia wazee na wagonjwa bila kusahau ushuhuda wa maisha ya waamini unaokita mizizi yake katika maadili na utu wema; wito wa utakatifu wa maisha ni mwaliko kwa mtu mmoja mmoja pia. Mama Kanisa anayo mifano ya watakatifu, mashuhuda na Mababa wa imani, walioneshwa na huruma na upendo wa Mungu katika maisha na utume wao, wakawa kweli ni chemchemi ya furaha, imani na matumaini kwa wale waliokuwa wanawazunguka. Kati yao ni Mwenyeheri Yohane Paulo wa Kwanza, Carlo Acutis ni mfano wa utakatifu miongoni mwa vijana wa kizazi kipya pamoja na Mtakatifu Francisko wa Assisi, mfano bora wa kuigwa katika huduma kwa maskini, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote sanjari na kuchuchumilia amani na udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, utakatifu unafumbatwa katika uhalisia wa maisha ya watu ndani ya familia, maeneo ya kazi, maisha ya kijamii, kiuchumi na kisiasa, daima waamini wakijitahidi kusoma alama za nyakati, ili kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Huu ni utakatifu unaosimikwa katika ushuhuda wa tunu msingi za Kiinjili zinazomwilishwa katika uhalisia wa maisha, kiasi cha kutangaza na kushuhudia kwa ushupavu fadhila za Kikristo, chemchemi ya utakatifu kwa kuwa na umaarufu wa utakatifu “fama sanctitatis” hawa ndio mashuhuda wa Kristo wanaokita maisha yao katika Heri za Mlimani, muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu. Huu ni utakatifu unaodumu na wala si kama “moto wa mabua.”

Watakatifu ni Katekisimu ya Imani, Sakramenti, Maisha adili na Sala.
Watakatifu ni Katekisimu ya Imani, Sakramenti, Maisha adili na Sala.

Baba Mtakatifu anasema, njia za mawasiliano ya jamii katika ulimwengu mamboleo zinaweza kulisaidia Kanisa kutambua watakatifu watarajiwa, lakini kuna haja ya kuwa waangalifu ili mitandao hii isije ikapotosha ukweli wa mambo. Wale wote wanaojihusisha na mchakato wa utakatifu wa maisha ya waamini wanapaswa kuzingatia: Umaarufu wa Utakatifu, Umaarufu wa Ushuhuda wa Imani kwa kifodini na Umaarufu wa ukuu wa Mungu kwa njia ya ishara na maajabu yaani “fama sanctitatis, fama martirii, fama signorum.” Watakatifu ni watu ambao kwa njia ya sala na sadaka zao, wanawasaidia jirani zao kupata huruma na baraka za Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, watakatifu ni amana na utajiri wa Kanisa unaofafanua tunu msingi za Kiinjili. Ni Katekisimu ya Kanisa Katoliki inayofafanua: Imani, Sakramenti, Maisha adili na Sala. Ni watu wenye mvuto na mashiko kwa maisha na utume wa Kanisa katika imani, matumaini na mapendo thabiti, kiasi cha kuwavuta wengi kuambata tunu msingi za Kiinjili, kwa imani na matumaini thabiti. Hii ni changamoto kwa Kanisa na Jamii katika ujumla wake, kutambua na kuthamini alama na ishara za utakatifu wa maisha, hata katika njia zile ambazo si rahisi sana kufikirika.

Papa Utakatifu
06 October 2022, 15:03