Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 17 Oktoba 2022 amekutana na Wanachama wa Shirikisho la Kihispania la Vyama vya Wafanyabiashara Vijana na Shirikisho la Wajasiriamali wa Galicia. Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 17 Oktoba 2022 amekutana na Wanachama wa Shirikisho la Kihispania la Vyama vya Wafanyabiashara Vijana na Shirikisho la Wajasiriamali wa Galicia. 

Wito kwa Wafanyabiashara na Wachumi Vijana: Tengenezeni Ajira

Vijana wachumi wanapaswa kuwa ni manabii wanaotangaza, kushuhudia, kujenga na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote; kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kuendeleza Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Vijana wajenge na kuimarisha mahusiano na mafungamano yao na Mwenyezi Mungu kwa njia ya toba na wongofu wa ndani, ili kuleta wongofu wa kiuchumi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wanachama wa Shirikisho la Kihispania la Vyama vya Wafanyabiashara Vijana na Shirikisho la Wajasiriamali wa Galicia ni alama ya Injili ya matumaini miongoni mwa vijana katika mchakato wa kutengeza fursa za ajira. Maisha ya kiuchumi na kijamii hadhi na wito halisi wa binadamu hauna budi kuzingatiwa, kuheshimiwa na kustawishwa kwa kuzingatia: mafao ya wengi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, binadamu ni mtendaji, kiini na ukomo wa maisha kiuchumi na kijamii. Vijana wachumi wanapaswa kuwa ni manabii wanaotangaza, kushuhudia, kujenga na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote; kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kuendeleza Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Vijana wajenge na kuimarisha mahusiano na mafungamano yao na Mwenyezi Mungu kwa njia ya toba na wongofu wa ndani, ili kuleta wongofu wa kiuchumi. Vijana wawe ni wafanyakazi bora wanaotekeleza dhamana na wajibu wao kwa bidii, juhudi na maarifa kama sehemu ya mchakato wa kupambana na baa la umaskini unaosigina: utu, heshima na haki msingi za binadamu, kwa wao kujikita katika mchakato wa ujenzi wa mahusiano baina ya siasa na uchumi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Vijana wafanyakazi na wachumi wajiaminishe chini ya ulinzi na tunza ya Mtakatifu Yosefu. Mtakatifu Yosefu ni mfano bora wa kuigwa na akina baba wa familia, kwa kuonesha upendo wa dhati, kwa kujali na kuwajibika vyema katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya maisha na utume wa familia. Mtakatifu Yosefu ni shuhuda na mfano wa Injili ya familia katika ulimwengu mamboleo. Ni Baba aliyejinyima mambo mengi, akajisadaka kwa ajili ya ulinzi, tunza, usalama, ustawi na maendeleo ya Bikira Maria na Mtoto Yesu.

Wachumi na wafanyabiashara vijana wajitahidi kutengeneza ajira
Wachumi na wafanyabiashara vijana wajitahidi kutengeneza ajira

Kwa muhtasari huu ndio wosia makini uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 17 Oktoba 2022 alipokutana na kuzungumza na Wanachama wa Shirikisho la Kihispania la Vyama vya Wafanyabiashara Vijana na Shirikisho la Wajasiriamali wa Galicia kutoka Hispania ambao kwa hakika, wanaonekana kama mashuhuda na vyombo vya Injili ya matumaini miongoni mwa vijana wa kizazi kipya. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, katika masuala ya kiuchumi na kijamii binadamu anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza kwa sababu yeye ni kiini na ukomo wa maisha ya shughuli zote za kiuchumi na kijamii. Uchumi unapaswa kujikita katika kukidhi mahitaji msingi ya binadamu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, sera, mipango na mikakati ya maendeleo ya kiuchumi haina budi kuzingatia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, badala ya kutawaliwa na uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka unaokwenda kinyume cha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Utu wa binadamu na mahitaji yake msingi vipewe kipaumbele cha kwanza na kwamba, kuna haja ya kuwa na ulinganifu wa kiuchumi na ule wa kijamii, ili kuondokana na kinzani na migogoro inayoweza kujitokeza. Lengo ni kudumisha, haki, usawa na wajibu. Rej. Gaudium et spes, n.63. Wachumi na wafanyakazi waendelee kujikita katika mchakato unaopania kuikwamua Jumuiya ya Kimataifa kutokana na kinzani na changamoto zilizopo.

Wazingatie kanuni maadili na utu wema
Wazingatie kanuni maadili na utu wema

Baba Mtakatifu anawataka vijana kuwa ni Manabii wanaotangaza na kushuhudia haki, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu hasa katika ulimwengu mamboleo ambamo kuna vita, uchafuzi mkubwa wa mazingira nyumba ya wote na aina mbalimbali za kinzani. Vijana wanaitwa na kuhamaishwa kuwa ni watunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; mashuhuda wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; vyombo na mashuhuda wa misingi ya haki na amani duniani. Vijana katika masuala ya kiuchumi na kijamii, wajitahidi pia kuboresha maisha yao ya kiroho, kiutu na kijamii kwa kujenga mahusiano na mafungamano ya dhati na Mwenyezi Mungu; kwa Neno, Sala, Sakramenti za Kanisa na Matendo ya huruma; Kiroho na Kimwili. Huu ni mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, chachu ya wongofu wa kiuchumi unaojikita katika mshikamano wa upendo; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, ili kuondokana na ukame wa mapendo. Vijana wajitahidi kufanya kazi kwa juhudi, weledi na maarifa ili kupambana na baa la umaskini unaosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Vijana wa kizazi kipya wapambane kufa na kupona dhidi ya umaskini wa hali na kipato. Watambue kwamba, wamekirimiwa na Mwenyezi rasilimali fedha wanayoweza kuitumia kwa ajili ya kutengeneza ajira, ili kuwanyanyua maskini na wale wasiokuwa na fursa za ajira.

Vijana wajiaminishe katika ulinzi na tunza ya Mungu
Vijana wajiaminishe katika ulinzi na tunza ya Mungu

Sura na mwelekeo mpya wa uchumi hauna budi kujikita katika kipaji cha ubunifu, kanuni maadili na utu wema, kwa kutambua kwamba, uchumi unapaswa kuwa ni kwa ajili ya huduma kwa binadamu. Vijana wanawajibika kulinda na kutunza mazingira. Watambue kwamba, kazi nyingi za binadamu zimekuwa ni chanzo cha uharibu wa mazingira nyumba ya wote. Mtakatifu Yosefu ni mfano bora wa kuigwa na akina baba wa familia, kwa kuonesha upendo wa dhati, kwa kujali na kuwajibika vyema katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya maisha na utume wa familia. Mtakatifu Yosefu ni shuhuda na mfano wa Injili ya familia katika ulimwengu mamboleo. Ni Baba aliyejinyima mambo mengi, akajisadaka kwa ajili ya ulinzi, tunza, usalama, ustawi na maendeleo ya Bikira Maria na Mtoto Yesu.

Vijana Wachumi
18 October 2022, 16:05