Ijumaa tarehe 4 Novemba 2022, Baba Mtakatifu ameshikiri katika kufunga Kongamano hili tayari kuanza utekelezaji wake kwa vitendo. Ijumaa tarehe 4 Novemba 2022, Baba Mtakatifu ameshikiri katika kufunga Kongamano hili tayari kuanza utekelezaji wake kwa vitendo. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Bahrain: Kongamano la Kidini

Muhimu: Mchakato wa ujenzi wa familia kubwa ya binadamu; changamoto pevu za Jumuiya ya Kimataifa kwa sasa ni baa la njaa, athari za mabadiliko ya tabianchi, magonjwa ya mlipuko na kashfa ya ukosefu wa usawa duniani, changamoto zinazogumishwa na vita na changamoto: “Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu” pamoja na “Tamko la Ufalme wa Bahrain

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mfalme Hamad bin Isa bin Salman Al Khalifa anasema Kongamano la Bahrain la Majadiliano: Mashariki na Magharibi kwa ajili ya Kuishi Pamoja kwa Binadamu ni kutaka kuthibitisha nia yake ya kudumu ya kutaka kujenga madaraja ya majadiliano kati ya viongozi wa dini na madhehebu mbalimbali pamoja na kueneza utamaduni wa amani na wa watu kuishi kwa pamoja. Al Azhar Al Sharif Imamu Mkuu na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Kiislamu, Dk. Ahmed Mohammed Ahmed Al Tayeb, Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli na Baba Mtakatifu Francisko ni kati ya baadhi ya watu mashuhuri wasomi na wawakilishi wa kidini kutoka nchi mbalimbali za dunia wanaoshiriki. Hili ni Kongamano ambalo limeandaliwa na Kituo cha Mfalme Hamad Cha Kimataifa kwa ajili ya kuishi pamoja kwa Amani, kwa ushirikiano na Baraza la Wazee wa Kiislamu na Baraza Kuu la Masuala ya Kiislamu. Ufalme wa Bahrain umekuwa na shauku kubwa ya kueneza utamaduni wa amani na wa waamini wa dini na madhehebu mbalimbali kuisihi kwa pamoja katika misingi ya amani na udugu wa kibinadamu. Ni katika muktadha huu kwamba, Hija ya 39 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Kimataifa nchini Bahrain kuanzia Alhamisi tarehe 3 hadi Dominika tarehe 6 Novemba 2022, ni kwa ajili ya kushiriki katika maadhimisho ya Kongamano la Bahrain la Majadiliano: Mashariki na Magharibi Kwa Ajili ya Kuishi Pamoja Kwa Binadamu.

Mchakato wa ujenzi wa familia kubwa ya binadamu
Mchakato wa ujenzi wa familia kubwa ya binadamu

Ijumaa tarehe 4 Novemba 2022, Baba Mtakatifu ameshikiri katika kufunga Kongamano hili. Katika hotuba yake amegusia kwa namna ya pekee: Mchakato wa ujenzi wa familia kubwa ya binadamu; changamoto pevu za Jumuiya ya Kimataifa kwa sasa ni baa la njaa, athari za mabadiliko ya tabianchi, magonjwa ya mlipuko na kashfa ya ukosefu wa usawa duniani, changamoto zinazogumishwa na vita na hivyo kupandikiza utamaduni wa kifo kati ya watu wa Mataifa. Baba Mtakatifu Francisko amegusia kuhusu changamoto zilizoibuliwa na “Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu” pamoja na “Tamko la Ufalme wa Bahrain” kuwa ni Sala inayogusa moyo wa mwamini; Elimu inayojikita katika akili pamoja na vipaumbele vyake kuwa ni elimu na ajira kwa wanawake; elimu ya uraia pamoja na matendo adili, ili kujenga dhamiri nyofu inayotambua umuhimu wa amani duniani. Baba Mtakatifu anasema Ufalme wa Bahrain unaundwa na Visiwa takribani 30, kielelezo cha umoja na mshikamano wa Familia kubwa ya binadamu, dhidi ya wimbi kubwa la vita linaoendelea kupandikiza mbegu ya kifo kati ya watu wa Mataifa. Changamoto kubwa kwa wakati huu ni kujikita katika mchakato wa majadiliano kama ilivyokaziwa kwenye maadhimisho ya Kongamano la Bahrain la Majadiliano: Mashariki na Magharibi Kwa Ajili ya Kuishi Pamoja Kwa Binadamu.

Jumuiya ya Kimataifa imeshuhudia madhara ya Vita Kuu ya Dunia pamoja na madhara ya Vita Baridi, lakini bado hata leo hii, Mataifa yanaendelea kuwekeza katika silaha, badala ya rasilimali fedha hii kutumika katika kukabiliana na changamoto za Kimataifa kama vile: baa la njaa na utapiamlo wa kutisha, athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na ongezeko kubwa la kashfa ya ukosefu wa haki duniani. Walimwengu wanaendelea kucheza na moto na matokeo yake ni kupandikiza utamaduni wa kifo, uharibifu wa mazingira nyumba ya wote; chuki na uhasama. Kumekuwepo na tabia ya Mataifa makubwa duniani kutaka kupandikiza: ukoloni mamboleo na ule wa kiitikadi; Utaifa usiokuwa na tija wala mvuto na tabia ya baadhi ya watu ndani ya jamii kutaka kujimwambafai hali inayopelekea Jumuiya ya Kimataifa kushindwa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini; kwa kusimamia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. “Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu” pamoja na “Tamko la Ufalme wa Bahrain” yanabainisha changamoto zinazoisonga Jumuiya ya Kimataifa ni pamoja na Sala inayogusa moyo wa mwamini. Kinzani na mipasuko mingi ya kijamii inapata chimbuko lake kutoka katika moyo wa mwanadamu. Rej. Gaudium et spes, 10.

Mshikamano wa udugu wa kibinadamu
Mshikamano wa udugu wa kibinadamu

Kwa msaada na neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu changamoto hizi zinaweza kupatiwa ufumbuzi wa kudumu, kwa kujikita katika sala inayowatakasa waamini dhidi ya uchoyo na ubinafsi; tabia ya kujitafuta, upotofu pamoja na ukosefu wa haki; lengo ni kusimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu. Sala inayosimikwa katika unyofu ina uwezo wa kupaa kwenda mbinguni. Waamini wajikite katika uhuru unaopata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu ili hata wao waweze kuuendeleza. Huu ni uhuru unaopaswa kumkomboa mwanadamu kutoka katika undani wa maisha yake, tayari kuambata wema na uzuri kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu amekazia kuhusu elimu inayojikita katika akili ya mwanadamu kwa kumwondolea ujinga ambao kimsingi ni adui mkubwa wa amani, unaopelekea misimamo mikali ya kidini na kiimani sanjari na vitendo vya kigaidi. Elimu aina kuwasaidia watu kusoma alama za nyakati, tayari kujenga familia kubwa ya binadamu inayosimikwa katika umoja, haki na maridhiano, tayari kukoleza moyo wa majadiliano na uvumilivu; kwa kuheshimiana, kuthaminiana na kusikilizana katika ukweli na unyofu, ili kuweza kufahamiana zaidi. Hii ndiyo dhamana kuu ya elimu, yaani kuwasaidia watu kufahamiana zaidi, mchango mkubwa unaoweza kutolewa na dini mbalimbali duniani.

Baba Mtakatifu anasema, dhana ya elimu inayogusa akili ya mwanadamu inapaswa kumwilishwa katika matendo, kwa kutambua vipaumbele vinavyopaswa kutekelezwa kwa dhati. Mosi ni elimu kwa wanawake ili kuwajengea uwezo wa kutafuta ajira na kujitegemea pamoja na kushiriki katika masuala ya kisiasa na kijamii, ili kumkomboa mwanamke na hivyo kumjengea moyo wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu, kwa kuheshimiana na kupendana kama ndugu wamoja licha ya tofauti msingi zinazoweza kujitokeza. Pili ni kuhakikisha kwamba, haki msingi za watoto zinalindwa na kudumishwa na tatu ni kuendeleza elimu ya uraia, ili kuwaondolea wananchi unyonge wa kujisikia kuwa ni dhaifu hata katika nchi yao wenyewe. Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, changamoto zote hizi zinahitaji utekelezaji wake kwa vitendo, ili kutambua ukuu na uweza wa Mwenyezi Mungu dhidi ya vita, ukosefu wa haki msingi za binadamu, vurugu, chuki na uhasama kwa sababu haya ni matendo yanayokwenda kinyume kabisa cha mapenzi ya Mungu. Waamini waepuke misimamo mikali ya kidini na kiimani na kwamba, vitendo vya kigaidi vinatishia usalama na amani duniani, kumbe vinapaswa kulaaniwa, ili kukuza na kudumisha udugu wa kibinadamu, majadiliano na amani duniani.

Mchakato wa ujenzi wa amani unahitaji uvumilivu na udumifu
Mchakato wa ujenzi wa amani unahitaji uvumilivu na udumifu

Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa waamini wa dini mbalimbali duniani kujielekeza zaidi katika mchakato wa kufahamiana; kuondokana na hofu na wasiwasi usiokuwa na mvuto wala mashiko. Uchu wa mali, utajiri wa haraka haraka na tabia ya kutaka kujikweza ni mambo ambayo yanaendelea kuhatarisha usalama na amani duniani. Kamwe matumizi ya nguvu, silaha na fedha hazitaweza kujenga na kudumisha amani duniani. Hii ni changamoto kwa waamini kujikita katika ujenzi wa dhamiri ya amani kwa ajili ya ulimwengu kwa kujenga na kudumisha mshikamano wa upendo wa kidugu; kwa kusimama kidete kupinga utamaduni wa kifo na kuendelea kuwa ni sauti ya wanyonge duniani. Kwa pamoja, waamini wa dini mbalimbali wanaweza kuwa ni manabii, mashuhuda, wajenzi wa amani na vyombo vya umoja na mshikamano wa kidugu.

Viongozi wa kidini wanao wajibu wa kukoleza maadili, utu wema na amani duniani
Viongozi wa kidini wanao wajibu wa kukoleza maadili, utu wema na amani duniani

Wakati huo huo, Mfalme Hamad bin Isa bin Salman Al Khalifa amesema, Kongamano la Bahrain la Majadiliano: Mashariki na Magharibi kwa ajili ya Kuishi Pamoja kwa Binadamu ni tukio kubwa lenye kuonesha matumaini, maendeleo, maisha yanayosimikwa katika heshima, amani na utulivu, kwa Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana na kushikamana ili kushughulikia changamoto, kinzani na migogoro inayojitokeza katika uso wa dunia, ili amani na utulivu viweze kushika mkondo wake. Wasomi washirikiane na kushikamana, ili kuimarisha tunu msingi za haki, amani na maridhiano kati ya watu; kwa kuendelea kujikita katika uadilifu ili kukuza udugu wa kibinadamu, kanuni maadili na utu wema, ili kuchochea amani duniani. Kuna haja ya kusitisha vita kati ya Urusi na Ukraine na kuanza kujikita katika majadiliano, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya binadamu wote. Ni wakati wa kudumisha misingi ya haki na amani; kuimarisha kanuni maadili na utu wema pamoja na maridhiano kati ya Jumuiya ya Kimataifa. Mwishoni mwa hotuba yake amewatakia washiriki wote: Amani, rehema na baraka za Mungu kwa ajii ya wao wote.

Wasomi wa dini ya Kiislam wasaidie kuragibisha tunu msingi za dini ya Kiislam
Wasomi wa dini ya Kiislam wasaidie kuragibisha tunu msingi za dini ya Kiislam

Wakati huo huo, Profesa Ahmed Al-Tayeb, Imamu Mkuu wa Msikiti wa Al-Azhar Al-Sharif, Cairo Misri na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Kiislamu katika hotuba yake amekazia kuhusu mchakato wa sera na mikakati ya maendeleo endelevu ya binadamu, haki msingi za binadamu na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za mazingira sanjari na kujikita katika utamaduni na utandawazi wa mshikamano wa kidugu ili kupambana na baa la umaskini unaosigina: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Takribani ya watu bilioni 4 wanaoishi katika umaskini wakati ambapo utajiri wa dunia hii unahodhiwa na watu 100 tu! Kuna haja ya kujenga mahusiano na mafungamano mapya yanayofumbatwa katika ushirikiano kati ya nchi za Magharibi na Mashariki, ili kukuza na kudumisha misingi ya utulivu, amani na haki kwa wote badala ya kuzigeuza baadhi ya nchi kuwa ni mahali pa kujipatia malighafi na masoko ya bidhaa zinazozalishwa katika nchi za Magharibi. Ni dhamana na wajibu wa wasomi wa dini ya Kiislam kuhakikisha kwamba, wanasaidia kuragibisha tunu msingi za maisha ya dini ya Kiislam kadiri ya Qurani Tukufu. Awawahimiza wasomi kuwekeza zaidi katika malezi na makuzi ya vijana wa kizazi kipya. Kujenga na kudumisha majadiliano yanayokazia udugu na hivyo kuondokana na chuki, uhasama na tabia ya kutaka kuwagawa waamini kwa misingi ya madhehebu. Imani thabiti na ya kweli kutoka kwa waamini wa dini ya Kiislam, itasaidia watu kuishi vyema na kwa amani. Vita kati ya Ukraine na Urusi.

Papa Kongamano

 

04 November 2022, 15:34