Tafuta

Baba Mtakatifu akiwa njiani kurejea mjini Vatican, Dominika tarehe 6 Novemba 2022 alipata nafasi ya “kuchonga” na waandishi 66 wa habari waliokuwa kwenye msafara wake kutoka Bahrain. Baba Mtakatifu akiwa njiani kurejea mjini Vatican, Dominika tarehe 6 Novemba 2022 alipata nafasi ya “kuchonga” na waandishi 66 wa habari waliokuwa kwenye msafara wake kutoka Bahrain. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Bahrain: Mahojiano Maalum: Mambo Mazito!

Kongamano la Bahrain la Majadiliano; Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu; Mchango wa wanawake katika: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; Vita kati ya Ukraine na Urusi. Nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo pamoja na umuhimu wa kujenga na kudumisha ushirika wa Kanisa, hakuna sababu kwa Ujerumani kumeguka tena! Ushirika na Udugu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya 39 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Kimataifa nchini Bahrain kuanzia Alhamisi tarehe 3 hadi Dominika tarehe 6 Novemba 2022, ilikuwa ni kumwezesha kushiriki katika maadhimisho ya Kongamano la Bahrain la Majadiliano: Mashariki na Magharibi Kwa Ajili ya Kuishi Pamoja Kwa Binadamu. Baba Mtakatifu akiwa njiani kurejea mjini Vatican, Dominika tarehe 6 Novemba 2022 alipata nafasi ya “kuchonga” na waandishi 66 wa habari waliokuwa kwenye msafara wake kutoka Bahrain. Baba Mtakatifu ametoa majibu na ufafanuzi wa kina kwa maswali saba aliyoulizwa. Kongamano la Bahrain la Majadiliano: Mashariki na Magharibi Kwa Ajili ya Kuishi Pamoja Kwa Binadamu; Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu; Utu, heshima, haki msingi za binadamu na mchango wa wanawake katika: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; Vita kati ya Ukraine na Urusi na madhara yake katika Jumuiya ya Kimataifa; Nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo na umuhimu wa kujenga na kudumisha ushirika wa Kanisa, hakuna sababu kwa Ujerumani kumeguka tena, Kanisa la Kiinjili la Kiluteri ni kubwa la kutosha! Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu ilitiwa saini kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari 2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu.

Baraza Kuu la Wazee wa Kiislam: Utunzaji Bora wa Mazingira Nyumba ya Wote.
Baraza Kuu la Wazee wa Kiislam: Utunzaji Bora wa Mazingira Nyumba ya Wote.

Huu ni mwaliko na changamoto kwa waamini wa dini mbalimbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu wa kibinadamu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hati hii ni nguzo msingi ya haki, amani na upatanisho. Hati inakazia pamoja na mambo mengine kwamba: binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu; wanatakiwa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha: uhai wa binadamu, mazingira nyumba ya wote, sanjari na kushikamana na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Lengo ni kunogesha majadiliano ya kidini ili kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu, kwa kujenga umoja unaosimikwa katika tofauti msingi kati ya waamini. Ni dhamana na wajibu wa wanataalimungu kujadili na kupembua kwa kina masuala msingi ya kitaalimungu, lakini waamini wanapaswa kutembea kwa pamoja kama ndugu, rafiki na jirani wema. Amewapongeza wajumbe wa Baraza Kuu la Wazee wa Kiislam “Muslim Council of Elders” kwenye Msikiti Mkuu wa Sakhir. Lengo ni kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano miongoni mwa Jumuiya za waamini wa dini ya Kiislam, kwa kusimama kidete kulinda na kutetea tunu msingi za dini ya Kiislam, Kiutu na Kijamii, kwa kukazia maridhiano dhidi chuki na ghasia zinazotaka kuwagawa waamini katika madhehebu. Jambo la msingi ni waamini wa dini zote kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote.

Majadiliano ya kidini ni kwa ajili ya kujenga misingi ya haki, amani na maridhiano
Majadiliano ya kidini ni kwa ajili ya kujenga misingi ya haki, amani na maridhiano

Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli anasema, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya imani kwa Wakristo inayofumbatwa katika maadhimisho ya Liturujia Takatifu. Maisha na utume wa Kanisa unamwilishwa katika matukio mbalimbali yanayogusa na kumwambata mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Taalimungu ya kiikolojia inagusa pamoja na mambo mengine: Umuhimu wa kujizatiti katika kukabiliana na changamoto zinazoibuliwa kutokana na uchafuzi wa mazingira ambao unaendelea kusababisha athari kubwa katika mabadiliko ya tabianchi. Utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na utunzaji bora wa kazi ya uumbaji mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa ni mambo msingi katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Mazingira ni sehemu ya kazi ya uumbaji ambayo imepewa nafasi ya pekee katika Liturujia Takatifu, hususan katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, kielelezo makini cha muhtasari wa utimilifu wa nyakati. Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwamba, Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli ni kiongozi ambaye amejipambanua sana katika majadiliano ya kiekumene na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Ufalme wa Bahrain imejengeka katika mchakato wa watu wa Mungu kukutana na kushuhudia utamaduni ambao uko wazi kwa watu wote kuweza kufanya kazi sanjari na kudumisha uhuru wa kuabudu kwa watu wanaoishi katika Ufalme wa Bahrein.

Nyaraka zinazopata chimbuko lake katika urafiki na udugu wa kibinadamu.
Nyaraka zinazopata chimbuko lake katika urafiki na udugu wa kibinadamu.

Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari 2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu walitia saini kwenye “Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu.” Hii ni changamoto kwa waamini wa dini mbalimbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu wa kibinadamu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hati hii ni nguzo msingi ya haki, amani na upatanisho. Hati inakazia pamoja na mambo mengine kwamba: binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu; wanatakiwa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha: uhai wa binadamu, mazingira nyumba ya wote, sanjari na kushikamana na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Baba Mtakatifu Francisko anasema majadiliano ya kidini si alama ya udhaifu, bali ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Majadiliano ya kidini hayana mbadala, kwani waamini wa dini zote wanapaswa kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hii ni hati ambayo inapata chimbuko lake katika udugu, ukarimu, upendo na sadaka na huo ni mwanzo wa urafiki wa dhati kati yake na Dr. Ahmad Al-Tayyib.

Majadiliano ya kidini yanasimikwa katika maisha ya kila siku
Majadiliano ya kidini yanasimikwa katika maisha ya kila siku

Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”, unapata chimbuko lake katika Udugu na urafiki wa kijamii na ni dira na mwongozo wa mchakato wa ujenzi wa ulimwengu ulio bora zaidi na unaosimikwa katika misingi ya haki, amani na utulivu, dhamana na wajibu wa: watu wote pamoja na taasisi mbalimbali. Malengo ya Waraka wa Kitume:"Fratelli tutti" ni kuhamasisha ujenzi wa mshikamano wa kidugu unaoratibiwa na kanuni auni, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Hii ni dhana inayokumbatia maisha ya kifamilia, kijamii, kitaifa na kimataifa. Ili kufikia lengo hili, kuna haja ya kujenga na kudumisha tasaufi ya udugu wa kibinadamu kama chombo cha kufanyia kazi katika medani za kimataifa, ili kusaidia kupata suluhu ya matatizo yanayoikumba Jumuiya ya Kimataifa. Huu ni msaada mkubwa katika kupambana na changamoto mamboleo kama vile: Vita na kinzani mbali mbali; baa la njaa na umaskini duniani pamoja na athari za uharibifu wa mazingira nyumba ya wote. Kipaumbele cha kwanza ni ustawi, maendeleo na mafao ya wengi Mshikamano wa kidugu usaidie ujenzi wa mahusiano na mafungamano ya Jumuitya ya Kimataifa kama ilivyo pia miongoni mwa wananchi wenyewe. Ujasiri na ukarimu ni mambo yanayohitajika ili kufikia malengo ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kusema, “Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu” inaendelea kusambazwa sehemu mbalimbali za dunia, ili iweze kufahamika hata kule Lebanon, ili kujenga na kudumisha haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mungu. Lebanon ni kielelezo cha ukarimu, mshikamano na mafungamano ya kibinadamu, huu ni utume ambao Lebanon inapaswa kuutekeleza.

Lebanon inapitia kipindi kigumu katika historia ya maisha yake.
Lebanon inapitia kipindi kigumu katika historia ya maisha yake.

Baba Mtakatifu anasikitika kuona vitendo vya ukatili, unyanyasaji na dhuluma dhidi ya wanawake na wasichana, kwani haya ni mambo yanayokwenda kinyume kabisa cha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Wanawake na wasichana wanapokabiliana na changamoto za ukatili wa majumbani, wasiogope kumwangalia Bikira Maria aliyekumbana na changamoto nyingi katika hija ya maisha yake hapa duniani kama Mama wa Mungu, kiasi cha kufuata ile Njia ya Msalaba, na hatimaye, kushuhudia ukatili dhidi ya Kristo Yesu aliyetundikwa Msalabani. Bikira Maria ni kielelezo cha imani na ujasiri katika maisha. Jamii ijitahidi kuwajengea wanawake uwezo wa kijamii, kisiasa na kiuchumi, ili kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha wanazokumbana nazo katika ulimwengu mamboleo. Mila na desturi za ukeketaji zimepitwa na wakati ni kinyume cha haki msingi za binadamu. Kuna haja ya kukuza na kudumisha uaminifu kati ya mwanamke na mwanaume katika maisha ya ndoa na familia; wanapaswa kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Na hiki ni kielelezo cha mabadiliko makubwa yanayoendelea kutekelezwa katika Sekretarieti kuu ya Vatican kwa kuwaingiza wanawake wenye sifa katika maisha na utume wa Kanisa; lengo ni kuliwezesha Kanisa kutangaza na kushuhudia ile sura ya Umama wa Kanisa na usawa wa kijinsia ili kutajirishana na kukamilishana, ili kuleta mabadiliko makubwa katika jamii.

Vita kati ya Ukraine na Urusi ina madhara makubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa
Vita kati ya Ukraine na Urusi ina madhara makubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa

Baba Mtakatifu Francisko anasema vita kati ya Urusi na Ukraine ni hatari sana kwa: usalama, amani, mshikamano na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa. Hii inatokana na ukweli kwamba, Mataifa yanaendelea kutengeneza na kulimbikiza silaha za nyuklia. Kuna haja ya ulimwengu kuondokana na hofu ya silaha za nyuklia na kwamba, wamiliki wa silaha hizi za maangamizi, wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuchangia utekelezaji wake, kwa Mataifa kuendelea kuaminiana na kuheshimiana, tayari kusimama kidete kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu anaendelea kujitahidi kutumia njia mbalimbali ili kuhakikisha kwamba, nchi hizi mbili zinarejea katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi, tayari kusitisha vita na kuanza kuandika historia mpya ya maisha ya watu wa Mungu inayosimikwa katika Injili ya amani duniani. Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia ya Mwaka 1914-1918 na Vita Pili ya Dunia ya Mwaka 1929 hadi 1945 vilisababisha madhara makubwa kwa watu na mali zao, lakini bado watu wanaendekeza dhana ya vita kama ilivyo kwa wakati huu, Vita ya Tatu ya Dunia inayopiganwa vipande vipande. Hii ni kazi kubwa inayofanywa na biashara haramu ya silaha duniani. Kuna wafanyabiashara wanaoendelea kuuza silaha nchini Yemen, Ukraine na Urusi; Rohingya na Siria na watu wanaendelea kupoteza maisha sehemu mbalimbali za dunia kutokana na vita. Baba Mtakatifu anawasihi waandishi wa habari kuwa ni vyombo na mashuhuda wa kuragibisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa.

Nyanyaso za kijinsia ni kashfa kwa maisha na utume wa Kanisa
Nyanyaso za kijinsia ni kashfa kwa maisha na utume wa Kanisa

Baba Mtakatifu Francisko anasema, nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ndani ya Kanisa ni kashfa ambayo imechafua maisha na utume wa Kanisa kiasi kwamba, haiwezi kamwe kufichwa, kuikataa wala kuibeza kwani ni ukweli usioweza kufumbiwa macho wala kuvumiliwa. Ukweli huu unapaswa kupokelewa na hatimaye, kumwilishwa katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani, wema na utakatifu wa maisha; kwa kuganga na kutibu madonda ya kashfa ya nyanyaso za kijinsia, tayari kuambata upendo na huruma ya Mungu, ili kuanza upya kwa kuchuchumilia: kanuni maadili, utu wema na utakatifu wa maisha. Lengo kuu ni kuzuia kashfa ya nyanyaso za kijinsia isijitokeze tena ndani ya Kanisa. Hii ni kashfa ambayo imegharimu maisha ya viongozi wa Kanisa sehemu mbalimbali za dunia. Hili ni jukumu linalopaswa pia kusimamiwa kidete na: Umoja wa Mataifa, UN na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF. Baba Mtakatifu Francisko anamshukuru na kumpongeza Kardinali Sean Patrick O’Malley, Mwenyekiti wa Tume ya Kipapa ya Kulinda Watoto Wadogo, PCPM. Kwa kusimama kidete kulinda na utu, heshima na haki msingi za watoto dhidi ya nyanyaso za kijinsia. Huu ni mchakato unaohitaji moyo mkuu na ujasiri kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa katika ujumla wake. Kanisa linaundwa na watakatifu pamoja na wadhambi wanaopaswa kutubu na kumwongokea Mungu. Jambo la kwanza ni kusikia aibu kwa vitendo kama hivi ndani ya Kanisa, tayari kutubu, kuongoka na kuomba msamaha, tayari kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu.

Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji linahitaji mshikamano wa udugu
Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji linahitaji mshikamano wa udugu

Baba Mtakatifu Francisko anasema, sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi na usalama wa maisha. Cyprus, Ugiriki, Italia na Hispania ni kati ya nchi ambazo zimepokea na kutoa hifadhi kwa wakimbizi wengi katika Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, EU. Poland na Bielorussi nazo zimekuwa mstari wa mbele kwa ajili ya kutoa huduma kwa wakimbizi na wahamiaji. Wengi wao wanatumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu pamoja na viungo vyake pamoja na mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo. Sera na mikakati kwa ajili ya huduma kwa wakimbizi na wahamiaji Barani Ulaya inapaswa kusimikwa katika makubaliano ya pamoja chini ya udhamini wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, EU pamoja na kuendeleza mshikamano wa upendo. Kwanza ni kuokoa maisha ya wahamiaji na wakimbizi ni kipaumbele cha kwanza. Pili ni kuzisaidia na kuzijengea uwezo nchi za Kiafrika ili kuwahudumia wahamiaji na wakimbizi. Baba Mtakatifu anamtakia heri na baraka Giorgia Meloni, Waziri mkuu mpya wa Italia pamoja na Serikali yake, ili iweze kutekeleza wajibu wake kadiri ya Katiba ya nchi na hivyo kuachana na tabia ya kuangusha Serikali kwa sababu tu ya kutofautiana kisiasa!

Serikali ya Italia inahitajji kujenga utamaduni wa udumifu.
Serikali ya Italia inahitajji kujenga utamaduni wa udumifu.

Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo anakazia kuhusu: Ukuhani wa waamini wote; umuhimu wa waamini walei kushiriki kikamilifu Sakramenti za Kanisa; Umuhimu wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni; Umuhimu wa kupyaisha ari na mwamko wa kimisionari pamoja na waamini walei kuendelea kuwa ni chachu ya uinjilishaji mpya na utakatifu kwa njia ya ushuhuda wa maisha, kama kielelezo makini cha imani tendaji! Umoja, upendo na mshikamano wa dhati ni mambo msingi katika utangazaji na ushuhuda wa Injili ya upendo kwa watu wa Mataifa. Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa inazingatia mambo makuu yafuatayo: Ufahamu wa kina wa Neno la Mungu; umuhimu wa toba na wongofu wa ndani pamoja na ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Haya ni mambo msingi katika mchakato mzima wa uinjilishaji mpya katika ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu Francis anasema, hakuna sababu za msingi kwa Kanisa nchini Ujerumani kugawanyika na kumeguka tena, badala yake, wajenge na kudumisha umoja na udugu wa Kikanisa na Kiinjili badala ya kuibua mijadala inayowagawa na kuwatenganisha watu wateule na watakatifu wa Mungu. Ni wakati wa kuzama zaidi katika mambo msingi ya imani, matumaini na mapendo; maadili na utu wema. Waamini wajenge utamaduni wa kukutana na Kristo Yesu katika Neno, Sakramenti, Sala, Jirani na historia ya kila mwamini. Ni wakati wa kwenda pembezoni mwa vitaumbele vya maisha ya kijamii na hata kimaadili na utu wema. Kristo Yesu anataka kuzima kiu ya wale wote wanaomtafuta kwa unyenyekevu na moyo mkuu!

Papa Mahojiano

 

07 November 2022, 14:32