Hija ya Kitume ya Papa Francisko Bahrain: Uekumene wa Sala na Ushuhuda wa Huduma!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, mchakato wa majadiliano ya kiekumene unafumbatwa katika: Uekumene wa damu, maisha ya kiroho, sala na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kielelezo cha ushuhuda wa Injili ya Kristo inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Kanisa Kuu la Bikira Maria wa Uarabuni huko nchini Bahrain. Haya ni matunda ya majadiliano ya kidini katika mchakato wa kukuza na kudumisha uhuru wa kuabudu. Kunako tarehe 19 Mei 2014 Mfalme Hamad Bin Isa Al Khalifa alimtembelea Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican na kumwonesha michoro kwa ajili ya Kanisa Kuu la Bikira Maria wa Uarabuni. Baba Mtakatifu akamzawadia mawe ya msingi yaliyotolewa kwenye mlango wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Jiwe la msingi na hatimaye kazi ya ujenzi wa Kanisa hili ulianza tarehe 10 Juni 2018, kielelezo makini cha ushiriki mkamilifu na Kanisa la Roma. Ujenzi ulianza kusimamiwa na Askofu mkuu Francisco Montecillo Padilla aliyekuwa Balozi wa Vatican nchini Qatar, Kuwait, Yemen, Bahrein na kwenye Nchi za Falme za Kiarabu na hatimaye, kukamilishwa na Askofu Paul Hinder, O.F.M. Cap. aliyeteuliwa hivi karibuni kuwa Msimamizi wa Kitume wa Kanisa Kaskazini mwa Falme za Kiarabu na Kuwait.Kanisa Kuu la Bikira Maria wa Uarabuni lina uwezo wa kuchukua waamini 2, 300 wakiwa wamekaa. Kuna Kikanisa kwa ajili ya Kuabudu Sakramenti Kuu na Kikanisa cha Bikira Maria wa Uarabuni, Mlinzi na Mwombezi wa watu wa Mungu Uarabuni.
Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 4 Novemba 2022 ameongoza Ibada ya Kiekumene kwenye Kanisa Kuu la Bikira Maria wa Uarabuni huko kwenye Ufalme wa Bahrain. Katika mahubiri yake, amekazia kuhusu dhamana ya Roho Mtakatifu katika mchakato wa ujenzi wa umoja wa Kanisa unaofumbatwa katika umoja na utofauti pamoja na ushuhuda wa maisha katika kumsifu na kumtukuza Mwenyezi Mungu alama ya ushirika wa Kanisa unaomwilishwa katika upendo kwa Mungu na jirani. Baba Mtakatifu amegusia mambo makuu yaliyojitokeza Siku ile ya Pentekoste ya kwanza, Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume na kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe. Mdo 2: 9-11. Roho Mtakatifu ni kiini cha ushirika na mshikamano wa waamini ndani ya Kanisa, changamoto na mwaliko kwa waamini kuzungumza lugha ya Kanisa, kwa kutambua kwamba, wote wanashiriki Ubatizo mmoja kwa maondoleo ya dhambi. Lakini umoja wa Kanisa umejeruhiwa na sasa kuna hamu kubwa ya kurejesha umoja wa Wakristo. Baba Mtakatifu anasema, huu ni ushirika unaosimikwa katika umoja na utofauti, ili kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu. Wakristo wa Makanisa na Madhehebu mbalimbali nchini Bahrain wanajisikia wamoja katika imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.
Huu ni umoja unaofumbatwa katika ushirika katika uekumene wa sala, ili kumtukuza Mwenyezi Mungu na hivyo kuwaleta karibu, ili kupata faraja ya Roho Mtakatifu na hatimaye, kuchota nguvu ya Roho Mtakatifu ili hatimaye warejee katika ujenzi wa umoja wa Kanisa. Wakristo wahakikishe kwamba, Makanisa yao yanajikita katika sala, hata pale wanapotindikiwa na wachungaji, kwani Roho Mtakatifu anapenda kufanya makao yake katika sakafu ya nyoyo za waamini wake. Kimsingi, Wakristo wote wanaitwa na kuhamasishwa kujenga ushirika mkamilifu na Mwenyezi Mungu. Kanisa linasafiri katika mchakato wa ujenzi wa umoja na utofauti, kwa kutambua kwamba, Roho Mtakatifu anawawezesha kuzungumza kwa lugha mbalimbali, inayowawezesha kujifunza kujenga madaraja ya kukutana na watu wengine katika imani na kwamba, hii ndiyo njia ya kiekumene. Waamini wajibidiishe kuifahamu historia ya Makanisa yao na kuendelea kujihusisha zaidi na Makanisa yao.
Baba Mtakatifu anawahimiza Wakristo kutoa ushuhuda kwa Makanisa yao kwa njia ya matendo adili na matakatifu na kama Wakristo wanahimizwa pia kuwapenda jirani zao, maana ni kiiini cha utambulisho wao. Wawe ni waelewaji, wanyenyekevu, na wafurahivu katika maisha, wapole na watu wanaopenda kujikita katika majadiliano, ili hatimaye, kujenga na kudumisha amani duniani. Heri za Mlimani ziwe ni utambalisho wa wamini unaofumbatwa katika ushuhuda. Umoja wa Kanisa ulenge kudumisha amani. Ushirika na Ushuhuda ni sawa na chanda na pete, kama kielelezo cha uwepo angavu wa Mungu katika maisha ya waja wake. Roho Mtakatifu awasaidie waamini kujenga na kudumisha ushirika, tayari kutumwa kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Yote haya yafumbatwe katika maisha ya sala, hija ya pamoja, ili kupokea neema na baraka za Roho Mtakatifu ili kujenga umoja unaosimikwa katika amani. Ratiba elekezi inaonesha kwamba, Baba Mtakatifu Jumamosi tarehe 5 Novemba 2022 majira ya asubuhi anaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Taifa wa Ufalme wa Bahrain, baadaye atatembelea Shule ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, inayoendeshwa na kusimamiwa na Kanisa Katoliki mjini Manama, iliyojengwa kunako mwaka 1953. Jioni atahitimisha siku kwa kukutana na kuzungumza na vijana wa kizazi kipya.