Tafuta

Lengo la baba Mtakatifu Francisko ni kushiriki katika maadhimisho ya Kongamano la Bahrain la Majadiliano: Mashariki na Magharibi Kwa Ajili ya Kuishi Pamoja Kwa Binadamu. Lengo la baba Mtakatifu Francisko ni kushiriki katika maadhimisho ya Kongamano la Bahrain la Majadiliano: Mashariki na Magharibi Kwa Ajili ya Kuishi Pamoja Kwa Binadamu.  

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Bahrain: Umoja, Maridhiano na Amani Duniani Kwa Watu Wote

Lengo ni kushiriki Maadhimisho ya Kongamano la Bahrain la Majadiliano: Mashariki na Magharibi Kwa Ajili ya Kuishi Pamoja Kwa Binadamu. Adui mkubwa wa majadiliano ya kidini ni woga na wasiwasi usiokuwa na msingi, mambo yanayochangia waamini duniani, kushindwa kufahamiana na hatimaye, kuishi kwa amani na utulivu; umoja, upendo, mshikamano na udugu wa kibinadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya Kitume ya 39 ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Bahrain kuanzia Alhamisi tarehe 3 hadi Dominika tarehe 6 Novemba 2022 ni fursa ya kukutana na kuzungumza na waamini wa Kanisa Katoliki wapatao 80, 000, wengi wao wakiwa ni wale wanaotoka Ukanda wa Mashariki ya Kati, Sri Lanka, India na Ufilippin na wengine ni wale wanaotoka katika nchi za Magharibi. Lengo ni kushiriki katika maadhimisho ya Kongamano la Bahrain la Majadiliano: Mashariki na Magharibi Kwa Ajili ya Kuishi Pamoja Kwa Binadamu. Adui mkubwa wa mchakato wa majadiliano ya kidini ni woga na wasiwasi usiokuwa na msingi, mambo yanayochangia watu wa dini mbalimbali duniani, kushindwa kufahamiana na hatimaye, kuishi kwa amani na utulivu; umoja, upendo, mshikamano na udugu wa kibinadamu kwa kutambua kwamba, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na hivyo tofauti zao za kidini si sababu msingi ya malumbano na kinzani zisizo na tija wala mashiko, ustawi na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wa Kitume: "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” anapembua umuhimu wa ujenzi wa utamaduni wa udugu wa kibinadamu kama chombo cha ujenzi wa ushirikiano na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa kwa kubainisha njia itakayotumika na malengo yake katika uhalisia wa maisha ya watu.

Hija ya Kitume ya Papa Francisko nchini Bahrain inapania kukuza majadiliano
Hija ya Kitume ya Papa Francisko nchini Bahrain inapania kukuza majadiliano

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe Mosi Novemba 2022, Sherehe ya Watakatifu Wote amegusia hija yake ya kitume kwenye Ufalme wa Bahrain. Anawashukuru viongozi wa Serikali, Kanisa na watu wa Mungu katika ujumla wao, hasa wale wanaoendelea kujisadaka ili kuhakikisha kwamba, hija hii ya kitume inafanikiwa na hatimaye kuzaa matunda yanayokusudiwa yaani ujenzi wa udugu wa kibinadamu, kama sehemu ya mchakato wa kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano. Wakati wa hija hii ya kitume, atakapowasili majira ya jioni, baada ya kupokelewa na viongozi wa Serikali, Baba Mtakatifu atamtembelea Mfalme Hamad bin Isa Al Khalifa na baadaye atazungumza na viongozi wa Serikali, Wanadiplomasia pamoja na viongozi wa vyama vya kiraia. Ijumaa tarehe 4 Novemba 2022, Baba Mtakatifu atashiriki kufunga  maadhimisho ya Kongamano la Bahrain la Majadiliano: Mashariki na Magharibi Kwa Ajili ya Kuishi Pamoja Kwa Binadamu. Atakutana na kuzungumza na wajumbe wa Baraza Kuu la Wazee wa Kiislam kwenye Msikiti mkuu wa Sakhir. Atahitimisha siku kwa Sala ya Kiekumene itakatoadhimishwa kwenye Kanisa Kuu la Bikira Maria wa Uarabuni ambalo lina uwezo wa kuchukua waamini 2, 300 wakiwa wamekaa. Kuna Kikanisa kwa ajili ya Kuabudu Sakramenti Kuu na Kikanisa cha Bikira Maria wa Uarabuni, Mlinzi na Mwombezi wa watu wa Mungu Uarabuni. Haya ni matunda ya majadiliano ya kidini katika mchakato wa kukuza na kudumisha uhuru wa kuabudu.

Uhuru wa kidini ni msingi wa uhuru mwingine wote
Uhuru wa kidini ni msingi wa uhuru mwingine wote

Kunako tarehe 19 Mei 2014 Mfalme Hamad Bin Isa Al Khalifa alimtembelea Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican na kumwonesha michoro kwa ajili ya Kanisa Kuu la Bikira Maria wa Uarabuni. Baba Mtakatifu akamzawadia mawe ya msingi yaliyotolewa kwenye mlango wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Jiwe la msingi na hatimaye kazi ya ujenzi wa Kanisa hili ulianza tarehe 10 Juni 2018, kielelezo makini cha ushiriki mkamilifu wa Baba Mtakatifu Francisko katika ujenzi huu. Hii ni Ibada kwa ajili ya kuombea amani. Jumamosi tarehe 5 Novemba, Baba Mtakatifu ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Taifa na jioni atakutana na “kuchonga” na vijana wa kizazi kipya. Dominika tarehe 6 Novemba 2022, Baba Mtakatifu akiwa mjini Manama atasali Sala ya Malaika wa Bwana pamoja na Wakleri, watawa na wafanyakazi katika shughuli za kichungaji nchini humo. Baadaye jioni atarejea mjini Vatican kuendelea na shughuli zake. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumsindikiza kwa sala na sadaka , ili hija hii iweze kupata mafanikio yanayokusudiwa, yaani  ujenzi wa udugu wa kibinadamu na amani; mambo msingi ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza.

Wakati huo huo, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican anasema ujumbe wa Baba Mtakatifu katika hija hii ya kitume unafumbatwa katika: umoja, maridhiano na amani; mambo msingi yanayobubujika kutoka katika majadiliano ya kidini, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni wakati wa kunogesha majadiliano ya kidini ili kujenga na kudumisha amani na maridhiano kati ya watu wa Mungu katika ulimwengu mamboleo ambao umegubikwa kwa kiasi kikubwa na: vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Majadiliano ya kiekumene na kitamaduni pia ni muhimu katika kukuza mchakato wa maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu. Anasema, lengo la dini kimsingi ni kudumisha majadililiano ya kidini na kitamaduni; umoja, mshikamano na ushirikiano wa Kimataifa, ili kujielekeza zaidi katika ujenzi wa utamaduni wa amani, maridhiano, mshikamano wa kidugu na upatanisho wa Kitaifa na Kimataifa. Mambo makuu yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza ni: Udugu wa kibinadamu, Mshikamano na Amani.

Udugu wa kibinadamu, mshikamano na amani ni mambo msingi.
Udugu wa kibinadamu, mshikamano na amani ni mambo msingi.

Waamini wa dini mbalimbali wanapaswa kusimama kidete dhidi ya utamaduni wa kifo, mifumo mbali mbali ya kibaguzi, ili kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Dhana ya diplomasia inayosimamiwa na kuendeshwa na Vatican, anasema Kardinali Parolin, inafumbatwa katika amani, kwa kusimama kidete kupambana na baa la njaa na umaskini duniani; kwa kulinda na kutunza mazingira bora nyumba ya wote kwani kuna mamilioni ya watu wanaoathirika kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi na ukosefu wa fursa za ajira na maendeleo fungamani! Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni mashuhuda na wajenzi wa misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kidugu, ili kuweza kukabiliana na changamoto katika ulimwengu mamboleo. Mataifa yatambue kwamba, yanategemeana na kukamilishana na kwamba, binadamu ni kiumbe jamii. Kwa njia, hii, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kuwa ni alama ya matumaini kwa wale waliokata tamaa ya maisha kutokana na sababu mbali mbali.

Majadiliano ya kidini ni muhimu katika kudumisha misingi ya haki na amani.
Majadiliano ya kidini ni muhimu katika kudumisha misingi ya haki na amani.

Kwa upande wake, Mfalme Hamad bin Isa Al Khalifa anasema Kongamano la Bahrain la Majadiliano: Mashariki na Magharibi kwa ajili ya Kuishi Pamoja kwa Binadamu ni kutaka kuthibitisha nia yake ya kudumu ya kutaka kujenga madaraja ya majadiliano kati ya viongozi wa dini na madhehebu mbalimbali pamoja na kueneza utamaduni wa amani na wa watu kuishi kwa pamoja. Al Azhar Al Sharif Imamu Mkuu na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Kiislamu, Dk. Ahmed Mohammed Ahmed Al Tayeb, na Baba Mtakatifu Francisko ni kati ya baadhi ya watu mashuhuri wasomi na wawakilishi wa kidini kutoka nchi mbalimbali za dunia wanaoshiriki. Hili ni Kongamano ambalo limeandaliwa na Kituo cha Mfalme Hamad Cha Kimataifa kwa ajili ya kuishi pamoja kwa Amani, kwa ushirikiano na Baraza la Wazee wa Kiislamu na Baraza Kuu la Masuala ya Kiislamu. Ufalme wa Bahrain umekuwa na shauku kubwa ya kueneza utamaduni wa amani na wa waamini wa dini na madhehebu mbalimbali kuisihi kwa pamoja katika misingi ya amani na udugu wa kibinadamu.

Hija ya Kitume

 

02 November 2022, 15:35