Tarehe 2 Novemba 2022, Baba Mtakatifu ameweka rekodi kwa kutembelea Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu mara 100 tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki mwaka 2013. Tarehe 2 Novemba 2022, Baba Mtakatifu ameweka rekodi kwa kutembelea Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu mara 100 tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki mwaka 2013. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Bahrain: Ametembelea Kanisa Kuu la B. Maria Mkuu mara 100

Tarehe 2 Novemba 2022, Papa Francisko ameweka rekodi kwa kutembelea Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu mara 100 tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki mwaka 2013. Lengo la hija hii ya kitume ya Baba Mtakatifu nchini Bahrein ni kushiriki katika maadhimisho ya Kongamano la Bahrain la Majadiliano: Mashariki na Magharibi Kwa Ajili ya Kuishi Pamoja Kwa Binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kukimbilia na kuambata huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao kwa kufanya tafakari ya kina kuhusu: Fumbo la Msalaba linaloonesha sadaka na majitoleo ya Kristo Yesu hadi kifo cha aibu! Waamini wawe na ujasiri wa kuangalia undani wa Fumbo la Msalaba. Ibada kwa Madonda Matakatifu ya Yesu, iwawezeshe waamini kuzama katika Moyo wake Mtakatifu, ili kujifunza na hatimaye, kutambua Fumbo la maisha na utume wa Kristo Yesu, hii ndiyo maana ya: Ukuu na Hekima ya Msalaba. Kumbe, Fumbo la Msalaba ni chemchemi ya maisha mapya. Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, Kristo Yesu ameweza kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na kifo na hivyo, kumkirimia maisha mapya yanayopatanishwa katika upendo. Kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, Kristo Yesu amelipa fidia ya wengi, hiki ndicho kiini cha Fumbo la maisha ya Yesu Baba Mtakatifu anasema Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ni sadaka ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo. Ni karamu ya Bwana, kusanyiko la Kiekaristi; Ukumbusho wa mateso kifo na ufufuko wa Bwana, Sadaka Takatifu ya Misa; ni ishara ya umoja na kifungo cha mapendo, karamu ya Pasaka. Ekaristi ni kitovu na kilele cha maisha ya Kanisa, kwa kuwa kwayo Kristo Yesu anachagamana na Kanisa na waamini wake wote! 

Papa Francisko amekwisha kutembelea Kanisa la B.Maria Mkuu mara 100
Papa Francisko amekwisha kutembelea Kanisa la B.Maria Mkuu mara 100

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kukuza na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Bikira Maria ni Mama wa Mungu na Kanisa, kwani ndani ya Moyo wake safi usiokuwa na doa, watu wote wanapata utambulisho wao, kwa kupenda na kupendwa, hali inayoonesha uwepo wa Mungu kati ya watu wake. Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Mama wa Mlango wa Mbinguni ni “Bikira Maria Mama wa huruma na matumaini.” Ni Mama ambaye daima ameonesha ulinzi na tunza kwa watu wanaomkimbilia katika shida na mahangaiko yao; upendo ambao umeendelezwa hadi nyakati hizi. Bikira Maria ni dira na kielelezo cha njia ya kwenda mbinguni; Njia ambayo kamwe haiwezi kumpotezesha mtu mwelekeo wa maisha! Njia hii, ni Kristo ambaye pia ni ukweli na uzima. Yesu ni mlango wa mbingu, unaowaalika wote kushiriki furaha ya uzima wa milele. Anawasubiri kwa moyo wa huruma na mapendo, wale wote wanaomwendea kwa toba na wongofu wa ndani. Bikira Maria, nyota ya asubuhi anawaongoza waamini kwa Kristo Yesu, ambaye ni Lango la huruma ya Mungu. Ni katika muktadha wa Hija ya 39 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Bahrain kuanzia Alhamisi tarehe 3 hadi Dominika tarehe 6 Novemba 2022, amekwenda kutembelea na kusali kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu Jimbo kuu la Roma, tarehe 2 Novemba 2022.

Hija ya Kitume ya Papa Francisko nchini Bahrain inapania kukuza majadiliano
Hija ya Kitume ya Papa Francisko nchini Bahrain inapania kukuza majadiliano

Tarehe 2 Novemba 2022, Baba Mtakatifu ameweka rekodi kwa kutembelea Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu mara 100 tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki mwaka 2013. Lengo la hija hii ya kitume ya Baba Mtakatifu nchini Bahrain ni kushiriki katika maadhimisho ya Kongamano la Bahrain la Majadiliano: Mashariki na Magharibi Kwa Ajili ya Kuishi Pamoja Kwa Binadamu. Baba Mtakatifu amejikabidhi katika ulinzi na tunza ya Bikira Maria afya ya Warumi “Salus Populi Romani.” Alhamisi tarehe 3 Novemba 2022, Baba Mtakatifu amekutana na kuzungumza na kikundi cha wakimbizi na wahamiaji kutoka Ukraine, kinachohifadhiwa na baadhi ya wananchi wa Italia. Akiwa njiani kwenda kwenye Ufalme wa Bahrain, Baba Mtakatifu amewatumia wakuu wa nchi ya: Italia, Ugiriki, Cyprus, Misri, Yordan pamoja na Saudi Arabia ujumbe wa amani na matashi mema. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa Rais Sergio Mattarella kwa niaba ya familia ya Mungu nchini Italia amemwelezea kwamba anakwenda kwenye Ufalme wa Bahrain kama hujaji wa amani na udugu wa kibinadamu, ili kushuhudia umuhimu wa tamaduni mbalimbali kukutana. Anawatakia watu wa Mungu nchini Italia: Ustawi na maendeleo ya maisha ya kiroho, kiraia na kijamii na hatimaye amewapatia baraka zake za kitume. Kwa Marais na wakuu wa nchi mbalimbali amewatakia: Baraka, heri, furaha ya kweli, amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Papa Francisko amepata mapokezi makubwa katika hija hii.
Papa Francisko amepata mapokezi makubwa katika hija hii.

Wakati huo huo, Rais Sergio Mattarella kwa niaba ya watu wa Mungu nchini Italia amemshukuru Baba Mtaatifu Francisko kwa ujumbe wake, akiwa njiani kuelekea Bahrein. Hija hii ya Kitume kama sehemu ya maadhimisho ya Kongamano la Bahrain la Majadiliano: Mashariki na Magharibi Kwa Ajili ya Kuishi Pamoja Kwa Binadamu ni fursa makini ya kuendeleza mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu unaosimikwa katika amani na haki msingi za binadamu. Rais Sergio Mattarella amemtakia heri na baraka katika hija hii ya kitume kwenye Ufalme wa Bahrain.

Papa Ibada B. Maria
03 November 2022, 15:13