Hija ya Kitume ya Papa Francisko Bahrain:Mkutano na mapadre,watawa&wahudumu kichungaji
Na Angella Rwezaula ,– Vatican.
Ni jumuiya ya Kikristo yenye kuwa na ladha ya kikatoliki yaani, ya ulimwenguni pote, kwa sababu imeundwa na watu wanaotoka sehemu mbalimbali za dunia na kwa pamoja wanakiri imani moja katika Kristo ambayo imekuwa na Mkutano wa sala na maaskofu, mapadre, waseminari , watawa na wahudumu wa kichungaji katika Kanisa la Moyo Mtakatifu huko Manama, Bahrain. Hawa wamekuwa ni taswira ya kale ya nyuso za wakristo. Wote wako katika usimamizi wa Kitume ya Kaskazini mwa Arabia, ambao ni mapadre wapatao 60 na makatekista zaidi ya 1300 wanaofanya kazi kati ya Wakatoliki wapatao milioni 2 tu waliopo Bahrain, Kuwait, Qatar na Saudi Arabia. Kutokana na kukumbatia jumuiya hiyo ya watu wengi, maneno ya amani bado yamesikika kwa mara nyingine tena ya Baba Mtakatifu Francisko, Domika tarehe 6 Novemba 2022 . Kuhusiana na hilo amesema kwamba katika miezi ya hivi karibuni tumekuwa tukiomba sana amani, katika muktadha huo makubalianoambayo yametiwa saini na ambayo yanahusu hali ya Ethiopia kwa maana hiyo yanajumuisha matumaini.
Baba Mtakatifu Francisko hivyo amewahimiza watu wote kuunga mkono dhamira hiyo ya amani ya kudumu ili kwa msaada wa Mungu wote waweze kundelee kutembea katika njia za mazungumzo na mapema iwezekanavo wananchi wapate maisha ya amani na yenye heshima. Hata hivyo akiendelea amesema hataka kusahau kuwaomba wasali kwa ajili ya nchi ya Ukraine inayoteswa ili vita viishe. Mkutano na Sala ya Malaika wa Bwana kwa watu waliokwekwa wakfu kwa Bwana yalitanguliwa na maneno ya makaribisho kutoka kwa Askofu Mkuu Paul Hinder, msimamizi wa kitume wa Kaskazini mwa Arabia ambapo amesema wale ambao walikuwa katika Kanisa hilo huko Manama, Kanisa la kwanza kujengwa kwenye mwambao wa Ghuba ni wawakilishi wa Kanisa la wahamiaji katika kanda hiyo. Ni watu wanaojishughulisha na uchungaji katika eneo hilo. Kwa maana hiyo maneno ya Papa yamefungamanishwa na macho ya watu wanaopenda Injili ambao mara nyingi huvuka maisha yao na mateso ya wale wanaoishi katika mazingira magumu, kama vile wale waliofungwa gerezani au wale ambao, kwa sababu za kazi, wako mbali na familia zao.
Mara baada ya kusikiliza shuhuda za Chris Noronha, Mhudumu wa Kichungaji aliyezaliwa Bahreain na kubatizwa katika Kanisa hilo, la Moyo Mtakatifu, Sr. Rose Celine mmsionari wa Shirika la Wakarmeli wa Mitume ambao mara baada ya kuanzisha shirika walikaribishwa huko Bahrain, ardhi ya tabasamu, Papa amekumbuka kwanza kabisa zizi dogo ambalo limeundwa na wahamiaji kutoka mbali na nchi zao za asili. Na zaidi baada ya kuona hata waamini kutoka Lebanon, aliwahakikishia sala na ukaribu wake katika nchi hiyo pendwa ambayo imechoka sana na kujaribiwa na hata watu wote wanaoteseka katika nchi za Mashariki ya Kati. Inapendeza kuwa mshiriki wa Kanisa linaloundwa na historia na nyuso tofauti, ambazo zinapata maelewano katika uso mmoja wa Yesu. Na aina hiyo amebainisha alivyoina kwa siku hizo kuwa ndiyo kioo cha nchi hiyo, ya watu wanaoishi lakini pia ya mandhari inayoitambulisha na ambayo, ingawa inatawaliwa na jangwa, inajivunia uwepo wa mimea na viumbe hai wa aina mbalimbali.
Akijikita kutazama Injili iliyosomwa, Baba Mtakatifu amekazia kusema, kwamba hata jangwani na kati ya udhaifu wa ubinadamu, maji yenye uwezo wa kufanya upya maisha yanatiririka. Maneno ya Yesu ambayo yamesikika yalizungumza juu ya maji ya uzima yanayotiririka kutoka kkwake Kristo na kutoka kwa waamini ( Yn 7:37-39). Kwa maana hiyo yamfanya afikirie ardhi hiyo kwamba ni kweli kuna jangwa kubwa, lakini pia kuna vyanzo vya maji safi ambayo yanatiririka kimya kimya chini ya ardhi, na kumwagilia. Ni taswira nzuri ya ya kuonesha kuwa wao ni nani na zaidi ya yote imani ambayo inafanya kazi katika maisha ya ubinadamu ambao wakati mwingine unajitokeza kijuu juu, ukiwa umechoshwa na udhaifu mwingi, hofu, changamoto inazopaswa kukabiliwa, maovu ya kibinafsi na ya kijamii ya aina mbalimbali. Lakini nyuma ya nafsi, katika vilindi vya moyo, maji matamu ya Roho hutiririka kwa utulivu na kimya, ambayo humwagilia jangwa zetu, hurejesha nguvu kwa kile kinachoelekea kukauka, huosha kile kinachotufanya kuwa wabaya, hukata kiu yetu kwa furaha. Baba Mtakatifu ameongeza kusema na daima hufanya kupyaishwa kwa maisha. Ni maji haya ya uzima ambayo Yesu alizungumza, hiki ndicho chanzo cha maisha mapya anachoahidi yaani zawadi ya Roho Mtakatifu, uwepo wa Mungu mwororo, wa upendo na wa kuzaliwa kwa upya ndani mwetu.
Maji ya uzima mpya yanatiririka katika saa ile Yesu alipokufa msalabani na kutoka ubavu ulio wazi wa Kristo. Maji, yanayokusudiwa kuzaliwa upya ubinadamu wote kwa kuwaweka huru kutoka katika dhambi na kifo. Kanisa lilizaliwa hapo, lilizaliwa kutoka ubavu ulio wazi wa Kristo, kutoka katika kuoga na kuzaliwa upya katika Roho Mtakatifu (taz. Tt 3:5). Sisi si Wakristo kwa sababu ya sifa zetu au kwa sababu tunashikamana na kanuni ya imani tu, bali kwa sababu katika Ubatizo tumepewa maji ya uzima wa Roho, ambayo hutufanya tuwe watoto wa Mungu na ndugu kati yetu, na kutufanya viumbe vipya. Kila kitu hutiririka kutoka katika neema, kila kitu hutoka kwa Roho Mtakatifu, amesisitizia Papa Francisko. Kwa kuendelea na tafakari yake ametazama juu ya"karama kuu tatu ambazo Roho Mtakatifu anatukabidhi na ameomba zikaribishwe na kuziishi ambazo ni furaha, umoja, unabii. Kwanza kabisa, Roho ndiye chanzo cha furaha. Maji safi ambayo Bwana anataka kutiririsha katika majangwa ya ubinadamu wote, yakichanganyika na ardhi na udhaifu, ni uhakika wa kutowahi kuwa peke yake katika safari ya maisha. Roho kiukweli ndiye asiyetuacha peke yake, yeye ndiye Msaidizi; anatufariji kwa uwepo wake wa busara na wa manufaa, anasindikiza kwa upendo, anasaidia katika mapambano na shida, uhimiza ndoto za kila mmoja nzuri zaidi na shauku kuu ya kila mmoja na kuweza kufungulia kwa kila mtu maajaubu na uzuri wa maisha.
Kwa wale ambao wamechagua kuweka maisha yao wakfu kwa Bwana, Papa Francisko amewageukia kwa namna ya pekee na kuwapa mawaidha kwamba wao, ambao mmegundua furaha hiyo na kuiishi katika jumuiya, waitunze na zaidi wazidishe mara mbili. Na njia gani ya ubora ya kufanya hivyo ni kuitoa. Ndiyo hivyo kwani furaha ya Kikristo inaambukiza, kwa sababu Injili inamfanya mtu atoke nje ya nafsi yake ili kuwasilisha uzuri wa upendo wa Mungu. Kwa hiyo ni muhimu kwamba katika jumuiya za Kikristo furaha isipunguzwe na kushirikishwa na kwamba wasijiwekee kikomo kwa kurudia ishara za mazoea, bila shauku na bila ubunifu. Kinyume chake, watakapopoteza imani na kuwa jumuiya ya kuchosha, hiyo ndiyo mbaya! Ni muhimu kwamba, kwa pamoja na Liturujia, hasa adhimisho la Misa, ambacho ni chanzo na kilele cha maisha ya Kikristo (taz.Sacrosanctum Concilium, 10), pia waifanye furaha ya Injili isambae katika matendo ya kichungaji yaliyo changamfu, hasa kwa ajili ya vijana, kwa ajili ya familia na kwa ajili ya miito kwa maisha ya kipadre na kitawa.
Furaha ya Kikristo haiwezi kujiweka peke yake inapaswa iwe ya mzunguko na kuongezeka. Kwa maana hiyo Papa amesisitiza kwamba “Roho Mtakatifu ndiye chanzo cha umoja. Wale wanaomkaribisha hupokea upendo wa Baba na kuwa watoto wake. Hakuwezi kuwa na nafasi kwa ajili ya matendo ya mwili, yaani, ubinafsi ya migawanyiko, ugomvi, kashfa, na masengenyo. Papa Francisko amewaomba kama kawaida yake kujihadhari na soga, kwa maana amesisitiza kuwa gumzo na masengenyo huharibu jumuiya. Migawanyiko ya ulimwengu na pia tofauti za kikabila na kiutamaduni, haziwezi kudhuru au kuhatarisha umoja wa Roho. Kinyume chake, moto wake unachoma matamanio ya kidunia na kuyaangazia maisha yote kwa upendo ule wa kukaribisha na wa huruma ambao Yesu anapenda wote ili wote wapendane kwa njia hiyo.
Kwa sababu hiyo, Roho wa Mfufuka anaposhuka juu ya wanafunzi, anakuwa chanzo cha umoja, na chanzo cha udugu dhidi ya ubinafsi wote; huzindua lugha pekee ya upendo, ili lugha tofauti za kibinadamu zisibaki mbali na zisizoeleweka; huvunja vizuizi vya kutoaminiana na chuki, ili kuunda nafasi za kukaribisha na mazungumzo; inaweka huru dhidi ya woga na inatia moyo wa kutoka nje kukutana na wengine kwa nguvu ya kuwapokonya silaha. Umoja pia ni nguzo ya udugu. Papa Francisko amethibitisha kwamba kuaminika katika mazungumzo na wengine ni suala muhimu katika kuishi udugu kati ya wote. Kwa maana hiyo ameomba wafanye hivyo katika jumuiya, wakithamini karama za wote bila kumuudhi mtu; waifanye katika nyumba za watawa, kama ishara hai za maelewano na amani; waifanye katika familia, ili kifungo cha upendo wa sakramenti kitafsiriwe katika mitazamo ya kila siku ya huduma na msamaha;waache waifanye pia katika jamii nyingine za dini nyingi na tamaduni nyingi mahali pa kuishi kila wakati kwa kupendelea mazungumzo, wasukaji wa umoja na ndugu wa madhehebu mengine.
Hatimaye, Baba Mtakatifu Fransisko amesisitiza kwamba “Roho ndiye chanzo cha unabii”. Historia ya wokovu, kama inavyojulikana, imejaa manabii wengi ambao Mungu aliwaita,aliwaweka wakfu na kuwatuma kati ya watu ili kunena kwa niaba yake. Kwa maana hiyo hata watu wa Mungu wana wito huo wa kinabii. Kwani wote waliobatizwa wamepokea Roho na wote ni manabii. Na kwa hivyo haiwezekani kujifanya kutoona matendo ya uovu, kubaki katika maisha tulivu ili kutojichafua mikono. Mkristo mapema au baadaye anapaswa kuchafua mikono yake ili kuishi maisha yake ya Kikristo na kutoa ushahidi. Kwa sababu kwa kupokea Roho wa unabii ni katika kupelekea Injili na mwanga na ushuhuda wa maisha ya kila mtu. Unabii huwezesha kufanya mazoezi ya heri ya kiinjili katika hali za kila siku, yaani, kujenga kwa upole thabiti ule Ufalme wa Mungu ambao upendo, haki na amani vinapinga kila aina ya ubinafsi, ya vurugu na uharibifu. Kwa maana hiyo Baba Mtakatifu Francisko ametoa salamu za mwisho kwa umma katika ardhi ya Bahrain ambayo ilikuwa ni shukrani kwamba kwa moyo uliojaa shukrani aliwabariki wote na wale ambao wasafiri kwa ajili ya hija hiyo. Na hatimaye amemshukuru sana Mfalme na mamlaka ya nchi hiyo ikiwa ni pamoja na Waziri wa Sheria, aliyekuwapo hapo kwa ukarimu wao wa ajabu.