Jumuiya ya Kimataifa bado haijajifunza vya kutosha kuhusiana na madhara ya vita duniani. Idadi kubwa ya silaha ulimwenguni ni tishio la ustawi, haki, amani na maridhiano kati ya watu. Jumuiya ya Kimataifa bado haijajifunza vya kutosha kuhusiana na madhara ya vita duniani. Idadi kubwa ya silaha ulimwenguni ni tishio la ustawi, haki, amani na maridhiano kati ya watu.  

Mahojiano Maalum Papa Francisko Na "La Stampa": Amani Duniani

Papa ameelezea: Madhara ya biashara haramu ya silaha, Diplomasia ya Vatican na Urusi katika mchakato wa amani na upatanisho;Viongozi kamwe wasiwasahau watu wanaosiginwa na umaskini; dhamana na nafasi ya wazee katika kuwarithisha vijana wa kizazi kipya imani na tunu msingi za maisha; Utandawazi; Wito, Utume na Maisha yake ndani ya Kanisa; Fumbo la Maisha na Msalaba.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi tarehe 19 Novemba 2022 anatembelea Jimbo Katoliki la Asti, Kaskazini mwa Italia, lengo kuu ni kumtembelea binamu yake Mama Carla Rabezzana huko mjini Portacomaro, kama sehemu ya kumbukizi ya miaka 90 tangu alipozaliwa. Ni nafasi pia ya kumpongeza Mama Delia Gai, pamoja na ndugu zake wa karibu kwa maadhimisho mbalimbali yaliyojitokeza katika siku za hivi karibuni. Baba Mtakatifu katika mahojiano maalum na Bwana Domenico Agasso wa Gazeti la “La Stampa” linalochapishwa kila siku nchini Italia anaelezea madhara ya biashara haramu ya silaha ulimwenguni; Diplomasia ya Vatican na Urusi katika mchakato wa amani na upatanisho kati ya Ukraine na Urusi; Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kamwe wasiwasahau watu wanaosiginwa na umaskini; dhamana na nafasi ya wazee katika kuwarithisha vijana wa kizazi kipya imani na tunu msingi za maisha; Utandawazi; Wito, Utume na Maisha yake ndani ya Kanisa; Fumbo la Maisha na Msalaba. Umefika wakati wa kufanya mageuzi makubwa katika maisha ya binadamu, kwa kugeuza silaha za vita kuwa ni vyombo vya kazi na fursa za kukoleza mchakato wa maendeleo endelevu.

Bado walimwengu hawajajifunza vya kutosha kutokana na vita duniani
Bado walimwengu hawajajifunza vya kutosha kutokana na vita duniani

Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, Vita Kuu ya Pili ya Dunia na Sasa Vita Kuu ya Tatu inayopiganwa vipande vipande ni hatari sana kwa mchakato wa usalama, ustawi na maendeleo ya wengi Jumuiya ya Kimataifa bado haijajifunza vya kutosha kuhusiana na madhara ya vita duniani. Idadi kubwa ya silaha ulimwenguni ni tishio la ustawi, haki, amani na maridhiano kati ya watu. Ujenzi wa haki, amani na maridhiano hauna budi kujikita katika toba na wongofu wa ndani. Toba hii, iwasaidie viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa na wanasiasa katika ujumla wao, kuongoka na kuwa ni mashuhuda na vyombo vya amani inayobubujika kutoka katika undani wa nyoyo zao. Amani ya kweli na ya kudumu ndiyo suluhu pekee, ambayo watu wa Mungu wanatamani kuiona nchini Ukraine na kwenye maeneo ambayo kuna vita, kinzani na migogoro mbalimbali. Ujenzi wa haki na amani ni mchakato endelevu na fungamani unaotekelezwa kila siku, lakini hatua kwa hatua.

Diplomasia ya Vatican inaendelea kutafuta suluhu ya migogoro ya kivita
Diplomasia ya Vatican inaendelea kutafuta suluhu ya migogoro ya kivita

Diplomasia ya Vatican inaendelea kufanya kazi, ili kuhakikisha kwamba, vita kati ya Urusi na Ukraine inakoma na amani inapatikana; kwa kujenga mtandao wa mahusiano pamoja na kuendelea kuwasaidia wakimbizi, wahamiaji na mateka wa vita. Baba Mtakatifu ana matumaini makubwa kwamba, iko siku vita kati ya Urusi na Ukraine vitakoma, lakini ikumbukwe kwamba, amani ya kweli inajengeka juu ya majadiliano katika ukweli na uwazi; sanjari na kuondokana na uchoyo na ubinafsi. Viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa katika sera na mikakati yao, kamwe wasiwasahau maskini na wale wote ambao utu, heshima na haki zao msingi zinaendelea kusiginwa na umaskini, ujinga na maradhi. Wasimame kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu. Huu ni ujumbe mahususi kwa Italia na viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wao. Tabia ya kutaka kujimwambafai na umaarufu usiokuwa na tija wala mashiko ni hatari sana. Dominika tarehe 20 Novemba 2022 ni Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu sanjari na Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni. Baba Mtakatifu anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Jimbo la Asti kwa ushiriki mkubwa wa vijana wa kizazi kipya.

Siku ya Vijana Duniani Ngazi ya Kijimbo: Ushuhuda wa Furaha ya Injili
Siku ya Vijana Duniani Ngazi ya Kijimbo: Ushuhuda wa Furaha ya Injili

Baba Mtakatifu anasema, ana mahusiano na mafungamano ya karibu na ndugu zake na kabla ya kuchaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, alikuwa amejijengea utamaduni wa kuwatembelea na kuwasalimia ndugu zake na kurejea tena kwenye asili yake na kwa hakika anajisikia kuwa ni sehemu ya wenyeji wa Piemonte. Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia kuna haja ya kuhakikisha kwamba kuna majadiliano ya kweli kati ya wazee na vijana wa kizazi kipya kwa kukazia asili yao kama sehemu ya mchakato wa ukuaji: kiroho, kimwili, kiutu, kitamaduni na kijamii. Kuna umati mkubwa wa watoto wanaoteseka kwa baa la njaa na utapiamlo wa kutisha. Huu ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kujifunga kibwebwe kupana kufa na kupona na baa la njaa linalosigina: utu, heshima na haki msingi za watu. Baa la njaa duniani ni kashfa kubwa na aibu kwa Jumuiya ya Kimataifa. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 19 Machi 2013 alianza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, sanjari na Maadhimisho ya Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, Mume wa Bikira Maria na Baba mlishi wa Mtoto Yesu. Kumbukizi ya Miaka 10 ni wakati wa kufanya tathmini kwa kuchunguza dhamiri ili kufanya upembeuzi kuhusu: mafanikio, mapungufu na hatimaye, maboresho ya maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Papa Francisko: Amani na utulivu; ushuhuda wa huduma ya upendo
Papa Francisko: Amani na utulivu; ushuhuda wa huduma ya upendo

Mkazo zaidi ni: Toba na wongofu wa ndani; Upatanisho; Udugu na urafiki wa kijamii badala ya kuendekeza tabia ya kutaka kulipiza kisasi, migogoro na wakati mwingine mtu kutaka kujimwambafai. Baba Mtakatifu anamshukuru Mungu kwa nafasi mbalimbali ambazo amemkirimia katika maisha na utume wake bila hata mastahili yake, kwanza kabisa kama Padre Myesuit, Askofu na sasa kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Katika maisha ya uzee wake, anapenda kupata amani na utulivu wa ndani; furaha ya kweli inayojikita katika uchaji wa Mungu. Haya ni mambo msingi yanayopata chimbuko lake katika: Sala, Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa pamoja na mchakato wa ujenzi wa madaraja ya kukutana na watu mbalimbali katika maisha na utume wake. Mbele ya Fumbo la Msalaba, waamini wajifunze kukaa kimya na kumsikiliza Kristo Yesu anataka kuwaambia nini. Wajifunze kuona ukweli wa mambo hata kama una unang’ata, tayari kujisadaka katika huduma kwa ajili ya watu wa Mungu.

Papa Mahojiano
18 November 2022, 14:00