Kumbukumbu ya Miaka 500 tangu Mtakatifu Inyasi wa Loyola alipotubu na kumwongokea Mungu. Kumbukumbu ya Miaka 500 tangu Mtakatifu Inyasi wa Loyola alipotubu na kumwongokea Mungu. 

Jubilei ya Miaka 500 ya Wongofu wa Mtakatifu Inyasi wa Loyola

Kumbukumbu ya Miaka 500 tangu Mtakatifu Inyasi wa Loyola alipotubu na kumwongokea Mungu, wakati akiwa njiani kuelekea Nchi Takatifu, huo ukawa ni mwanzo wa sadaka na majitoleo ya imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Alipata majeraha makubwa mwilini na rohoni, kiasi cha kuuvua utu wa kale, kusudi aweze kumfuasa Kristo Yesu katika ufukara na katika unyenyekevu mkuu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kuanzia tarehe 20 Mei 2021 hadi tarehe 31 Julai 2022, Kumbukumbu ya Mtakatifu Inyasi wa Loyola, Wayesuit wameadhimisha Mwaka wa Mtakatifu Inyasi wa Loyola. Tarehe 20 Mei ni kumbukumbu ya siku ile ambayo Mtakatifu Inyasi alijeruhiwa vitani huko Pamplona Hispania, kunako mwaka 1521. Huo ukawa ni mwanzo wa mchakato wa toba na wongofu wake wa ndani na mageuzi makubwa katika maisha, historia na utume wa Kanisa Katoliki na sasa imegota miaka 500. Maadhimisho haya yamenogeshwa na kauli mbiu “Angalieni mambo yote mapya katika Kristo”. Mwaka wa Mtakatifu Inyasi wa Loyola umeratibiwa kwa Mpango Mkakati wa Maisha na Utume wao katika kipindi cha miaka kumi yaani kuanzia mwaka: 2019-2029. Askofu mkuu Francisco Pérez González wa Jimbo kuu la Pamplona na Tudela nchini Hispania, ndiye aliongoza Ibada ya Misa Takatifu ya Kufunga Mwaka wa Mtakatifu Inyasi wa Loyola pamoja na wanashirika kujiweka wakfu kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu. Ni katika muktadha huu wa maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Inyasi wa Loyola, Baba Mtakatifu Francisko amemwandikia barua Kardinali Juan José Omella Omella, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Barcelona na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania, kama sehemu ya maadhimisho ya Kumbukumbu ya Miaka 500 tangu Mtakatifu Inyasi wa Loyola alipotubu na kumwongokea Mungu, wakati akiwa njiani kuelekea Nchi Takatifu, huo ukawa ni mwanzo wa sadaka na majitoleo ya imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Jubilei ya Miaka 500 ya toba na wongofu wa Mtakatifu Inyasi wa Loyola
Jubilei ya Miaka 500 ya toba na wongofu wa Mtakatifu Inyasi wa Loyola

Mtakatifu Inyasi wa Loyola alipata majeraha makubwa mwilini na rohoni, kiasi cha kuuvua utu wa kale, kusudi aweze kumfuasa Kristo Yesu katika ufukara na katika unyenyekevu mkuu. Watu wateule na watakatifu wa Mungu nchini Hispania, tarehe 14 Novemba 2022 wameadhimisha Jubilei ya Miaka 500 tangu kuongoka kwa Mtakatifu Inyasi wa Loyola. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwatakia heri na baraka katika maadhimisho haya. Watu wengi wanamkumbuka Mtakatifu Inyasi wa Loyola kwa utakatifu na uadilifu wake; thabiti katika imani na matumaini na wanashirika wake wanamheshimu na kumuenzi kama Muasisi wa Shirika la Wayesuit. Mwenyezi Mungu katika huruma na upendo wake wa daima, alitumia Vita ya Pamplona na ugonjwa wa tauni, kama fursa ya toba na wongofu wa ndani, na huo ukawa ni mwanzo mpya wa historia na maisha ya Mtakatifu Inyasi wa Loyola. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, Mwenyezi Mungu kwa njia ya kinzani na migogoro mbalimbali katika maisha, anayeweza kubadili miito na mipango ya wanadamu kadiri ya mapenzi yake ya daima, kwani huruma na upendo wa Mungu ndio vinavyoratibu mwenendo wa ulimwengu. Mtakatifu Inyasi wa Loyola akaona wito huu kuwa ni neema na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ili kuwasaidia wengine, kukutana na Mwenyezi Mungu katika historia ya maisha yao na hivyo kujiruhusu kutumiwa na Mwenyezi Mungu kama chombo na daraja la kuwakutanisha watu.

Wayesuit wamekuwa mstari wa mbele katika huduma ya maisha ya kiroho.
Wayesuit wamekuwa mstari wa mbele katika huduma ya maisha ya kiroho.

Ni katika hali ya neema na unyenyekevu kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Benedikto, alivyotumiwa na Mtakatifu Theresa. Au ngazi ya Yakobo iliyokuwa inashuka na kupanda mbinguni, ndivyo ambavyo Mwenyezi Mungu alivyomtumia hata Mtakatifu Inyasi wa Loyola ili kukutana na watu mbalimbali kutoka katika undani wa maisha yao. Itakumbukwa kwamba, Padre Arturo Marcelino Sosa Abascal, Mkuu wa Shirika ya Wayesuit katika mahubiri ya kufunga Mwaka wa Mtakatifu Inyasi wa Loyola kwa kuwataka Wayesuit popote pale walipo, kuendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani. Watambue na kukiri upendo na ukuu wa Mungu katika maisha yao kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Inyasi wa Loyola. Toba na wongofu wa ndani, uwawezeshe kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wawe ni vyombo na mashuhuda wa ujenzi wa dunia inayosimikwa katika msingi wa haki na udugu wa kibinadamu. Maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Inyasi wa Loyola imekuwa ni fursa ya kushirikiana na wadau mbalimbali katika maisha na utume wa Wayesuit, ili kuweza kuyapatanisha yote na Kristo Yesu, anayepaswa kupewa kipaumbele cha kwanza! Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 23 Mei 2021 katika ujumbe wake kwa njia ya video, aliungana na mahujaji wa Kiyesuiti kwa ajili ya kusali katika maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Inyasi wa Loyola. Anasema, jeraha la Mtakatifu Inyasi wa Loyola limekuwa ni chanzo cha mageuzi makubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Ndoto ya awali ya Mtakatifu Inyasi “ikatoweka kama umande wa asubuhi.”

Karama ya Mtakatifu Inyasi wa Loyola imeenea sehemu nyingi za dunia.
Karama ya Mtakatifu Inyasi wa Loyola imeenea sehemu nyingi za dunia.

Mwenyezi Mungu akamkirimia ndoto kubwa zaidi kwa ajili ya wokovu wa roho za watu. Toba na wongofu wa ndani ni mchakato wa maisha ya kila siku, kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Inyasi wa Loyola. Toba, wongofu wa ndani na mang’amuzi ya maisha ni mambo ambayo yamekuwa ni dira na mwongozo wa maisha na utume wa Mtakatifu Inyasi wa Loyola, chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu anayewawezesha waamini kukutana na Kristo Yesu katika maisha yao. Kama mahujaji “huku bondeni kwenye machozi”, Wayesuit wanakutana pia na watu wa Mungu kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Inyasi wa Loyola. Huu ni mwaliko wa kuendelea kutubu na kumwongekea Mungu, ili kuweza kuisikiliza sauti ya Mungu anayezungumza nao kwa njia yao. Wayesuit wajifunze kusoma alama za nyakati na kuendeleza mchakato wa majadiliano na jirani pamoja na ulimwengu katika ujumla wake.   Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, wale wote wanaokumbatia tasaufi ya Mtakatifu Inyasi wa Loyola, wataweza kusafiri pamoja kama wanafamilia moja ya Mtakatifu Inyasi wa Loyola. Mwaka huu imekuwa ni fursa ya kuuendea ulimwengu, kusaidia roho za watu na kuyaangalia mambo yote mapya katika jicho la Kristo Yesu. Wayesuit wanahimizwa kujinyenyekesha na kuwaachia wengine nafasi ili waweze kuwasaidia. Hii inatokana na ukweli kwamba, hakuna mtu anayeweza kujiokoa mwenyewe. Wote wanaweza kuokolewa kama jumuiya au kuangamia na wala hakuna njia ya mkato. Ni Yesu peke yake ambaye amewaonesha njia, hivyo ni wajibu wao kusaidiana kutafuta na hatimaye, kuambata njia inayokwenda kwa Kristo Yesu.

Kumbukumbu ya Miaka 500 ya toba na wongofu wa Mt. Inyasi wa Loyola
Kumbukumbu ya Miaka 500 ya toba na wongofu wa Mt. Inyasi wa Loyola

Tarehe 12 Machi 2022 Wayesuit wameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu mjini Roma kama sehemu ya kumbukumbu ya Miaka 400 tangu Mtakatifu Inyasi wa Loyola, Mtakatifu Francisko Xavier, Mtakatifu Theresa wa Yesu, Mtakatifu Isidore Labrador pamoja na Mtakatifu Philip Neri walipotangazwa na Mama Kanisa kuwa ni Watakatifu. Karama ni chemchemi ya maisha na utume wa Shirika, mwaliko na changamoto ya kujenga ukaribu zaidi katika utume ambao Shirika ambalo limekabidhiwa na Roho Mtakatifu, ili mwaliko huu uweze kuingia na kugusa undani wa maisha ya watu zaidi. Wayesuit wanataka kujifunza kutoka kwa vijana, ili waweze kuwasindikiza, ili kugundua maana ya maisha kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Inyasi wa Loyola. Lengo ni kuwajengea vijana uwezo wa kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi; mahali ambapo utu, heshima na haki msingi za binadamu zinaheshimiwa na kuthaminiwa, sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Wayesuit wanataka kushirikiana na vijana wa kizazi kipya: Muda, ndoto na matumaini waliyo nayo!

Kwa Wayesuit waliotawanyika sehemu mbali mbali za dunia, huu ni muda wa kufuata nyayo za Mtakatifu Inyasi wa Loyola, hujaji maarufu, kwa njia ya mapambano ya maisha ya kiroho, toba na wongofu wa ndani, ili kujenga mahusiano ya karibu na Mwenyezi Mungu kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Inyasi wa Loyola. Ukaribu na upendo kwa Mwenyezi Mungu, uwasaidie Wayesuit kujenga na kudumisha umoja katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Maisha na Utume wao katika kipindi cha Miaka 10. Wao ni warithi wa karama ambayo imesheheni tunu msingi za maisha ya kimisionari. Ufukara pamoja na kutekeleza mapenzi ya Mungu ni kati ya mambo ambayo Mtakatifu Inyasi wa Loyola aliyapokea kama zawadi kutoka juu. Mfano wa maisha ya Mtakatifu Inyasi wa Loyola na wale wenzake, uwawezeshe Wayesuit kujenga mahusiano ya pekee na Kristo Yesu, ili aweze kuwakirimia amani na utulivu wa ndani. Wawe mstari wa mbele katika kuwahudumia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hii ni sehemu ya urithi na amana inayobubujika kutoka katika Karama ya Wayesuit. Huu ni wakati wa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na wale wote ambao utu, heshima na haki zao msingi zinasiginwa kila kukicha! Lengo ni kushikamana na maskini, ili kuleta mageuzi katika miundo mbinu inayokandamiza utu na heshima ya binadamu. Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 imesababisha madhara makubwa katika medani mbali mbali za maisha ya binadamu.

Mtakatifu Inyasi: Utakatifu, Uadilifu, imani na matumaini.
Mtakatifu Inyasi: Utakatifu, Uadilifu, imani na matumaini.

Mpasuko mkubwa kati ya maskini na matajiri umeonekana wazi wazi. Kumekuwepo na kinzani katika Jumuiya ya Kimataifa pamoja na uwiano tenge katika masuala ya kiikolojia. Wayesuit waungane na Kristo Yesu pamoja na maskini, kwa kuishi na kuukumbatia ufukara wao, kama ushuhuda wa upendo wao kwa Kristo Yesu. Wayesuit watambue na kukiri dhambi na mapungufu yao ya kibinadamu, daima wakijitahidi kujitambulisha na Kristo Yesu, ili aweze kuwasaidia kutubu na kumwongokea. Wawe tayari kuleta mabadiliko katika maisha ya maskini, kwa kusoma alama za nyakati, kwa toba na wongofu wa ndani ili kupyaisha karama ya Shirika. Wayesuit wajenge umoja na mshikamano na Kristo Yesu, ndugu na rafiki yao mpendwa, ili aweze kuwakirimia imani, matumaini na mapendo kwa kuendelea kukaaa pamoja nao, chini maongozi ya Roho Mtakatifu. Shirika la Wayesuit lililoanzishwa na Mtakatifu Inyasi wa Loyola katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa, linapaswa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mambo makuu yafuatayo: Kuendeleza mchakato wa mang’amuzi na mafungo ya maisha ya kiroho; Kushikamana na maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; Kuwasindikiza vijana katika safari ya maisha yao; Mwishoni, ni utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Huduma kwa wakimbizi ni utambulisho wa Wayesuit.
Huduma kwa wakimbizi ni utambulisho wa Wayesuit.

Haya ni mambo ambayo yanabainishwa na Baba Mtakatifu Francisko katika barua aliyomwandikia hivi karibuni Padre Arturo Sosa Abascal, Mkuu wa Shirika ya Wayesuit kama sehemu ya Mpango Mkakati wa Maisha na Utume wao katika kipindi cha miaka kumi yaani kuanzia mwaka 2019-2029. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hivi pia ndivyo vipaumbele vya Kanisa la Kiulimwengu kwa wakati huu! Mambo ambayo yanapaswa kumwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya Sinodi za Maaskofu na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia. Vipaumbele hivi vinachota utajiri wake kutoka katika Wosia wa Kitume, “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili.” Vipaumbele vya Wayesuit katika kipindi cha miaka kumi ni msingi wa mahusiano na mafungamano kati ya Wayesuit na Kristo Yesu; mambo yanayomwilishwa katika maisha binafsi na katika Jumuiya inayosali na kufanya mang’amuzi ya pamoja. Vipaumbele hivi ni sehemu ya mchakato wa maisha na utume wa Wayesuit ambao umefanyiwa kazi katika kipindi cha miaka miwili, ili kuhakikisha kwamba, Wayesuit wanatumia kikamilifu rasilimali watu, vitu na fedha, ili kufikia lengo hili muhimu, daima wakiendelea kusoma alama za nyakati. Hapa kinachohitajika ni kukuza na kudumisha kipaji cha ubunifu, kwa kuwashirikisha watu kutoka katika makundi na medani mbali mbali za maisha, ili kugundua amana na utajiri unaofumbatwa katika mafungo ya kiroho yanayotolewa na Wayesuit.

Wayesuit wawe mstari wa mbele kusoma alama za nyakati
Wayesuit wawe mstari wa mbele kusoma alama za nyakati

Lengo ni kuhakikisha kwamba, haki jamii inapewa msukumo wa pekee, ili kweli mabadiliko makubwa yanayojitokeza katika masuala ya: kiuchumi, kijamii na kisiasa, yanazingatia haki msingi, utu na heshima ya binadamu. Kuwasindikiza vijana katika safari ya maisha yao ni pamoja na kuyaangalia yale mema, mazuri na matakatifu yanayowazunguka vijana katika “vijiwe vyao”, kwa kusikiliza na kujibu kiu na matamanio yao halali kadiri ya mabadiliko ya jamii; kwa kuendelea kusoma alama za nyakati. Hii ni changamoto ya kuwapatia vijana fursa ya kuonesha vipaji na ubunifu wao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Umefika wakati kwa viongozi wa Kanisa kujifunza kutoka kwa vijana wa kizazi kipya! Mwishoni, ni utunzaji wa mazingira nyumba ya wote. Huu ni mwaliko wa kushiriki katika sera, mbinu na mikakati ya utunzaji bora wa mazingira, pamoja na kuangalia sera mbadala, ili kuweza kudhibiti uharibifu wa mazingira unaoendelea kusababisha majanga makubwa katika maisha ya watu wengi duniani. Hii ni changamoto ya kushirikiana na wadau mbali mbali kama sehemu ya mbinu mkakati wa utekelezaji wa malengo haya katika maisha na utume wa Wayesuit.

Mt. Inyasi 500 Yrs
15 November 2022, 15:35