Papa Francisko Anatembelea Jimbo Katoliki la Asti, Italia: Jamaa!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Dominika ya 34 ya Mwaka, ni Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu. Huu ni Ufalme wa milele na wa Ulimwengu wote; Ufalme wa kweli na uzima; Ufalme wa utakatifu na wa neema; Ufalme wa haki, mapendo na amani. Katika Maadhimisho haya, Mama Kanisa anapenda kukazia zaidi kuhusu: Uhuru wa kidini, uhuru wa kuabudu na uhuru wa dhamiri nyofu, ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kadiri ya Maandiko Mtakatifu. Mama Kanisa anapenda kuendeleza dhamana na utume wake wa kutangaza, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu katika hija ya maisha yao hapa ulimwenguni. Lengo kuu la Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu ni kuendelea kusimama kidete kulinda na kudumisha: Utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na kukoleza maisha adili na matakatifu, ili mwisho wa siku, waamini waweze kuunganika kwa pamoja na Kristo Yesu katika Ufalme wake wa mbinguni; Ufalme ambao hauna mwisho. Huu ni wito kwa watu wa Mungu kuendelea kujiaminisha mbele ya Kristo Yesu, Bwana wa historia na nyakati zote ni zake. Katika shida na mahangaiko yao, watu wa Mungu wamkimbilie Kristo Yesu ambaye ameteswa na kufa Msalabani, ameshinda dhambi, ubaya wa moyo na mauti!
Hii ni siku ambayo pia vijana wanaungana na Maaskofu pamoja na viongozi mahalia kusherekea Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni katika ngazi ya kijimbo kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Basi Mariamu akaondoka siku hizo, akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda” (Lk 1:39). Ujumbe huu ni sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Vijana Kimataifa itakayoadhimishwa katika jimbo kuu la Lisbon nchini Ureno kuanzia tarehe 1-6 Agosti 2023. Baba Mtakatifu Francisko anatarajia kuadhimisha matukio yote haya mawili, Dominika tarehe 20 Novemba 2022 katika Kanisa kuu la Jimbo Katoliki la Asti, lililoko Kaskazini mwa Italia. Lengo ni kumtembelea binamu yake Mama Carla Rabezzana huko mjini Portacomaro, kuanzia Jumamosi tarehe 19 Novemba 2022 kama sehemu ya kumbukizi la miaka 90 tangu alipozaliwa. Ni nafasi pia ya kumpongeza Mama Delia Gai, pamoja na ndugu zake wa karibu. Hii ni ziara binafsi inayomwezesha Baba Mtalatifu kurejea tena kwenye asili yake, pamoja na kuwashirikisha watu wateule wa Mungu: Neno na Sakramenti za Kanisa, tayari kupyaisha ari na mwamko wa kimisionari, ili kuwaonjesha wengine furaha ya Injili pamoja na kuwaimarisha ndugu ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo.
Baba Mtakatifu baada ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, atawaongoza waamini katika tafakari na hatimaye Sala ya Malaika wa Bwana. Atapata chakula cha mchana, kitakachoandaliwa na Baba Mtakatifu kwa ajili ya ndugu na jamaa zake wa karibu. Mwishoni, atakutana na kuzungumza na watoto zaidi ya 1, 340 katika Uwanja wa Michezo wa Censin Bosia. Hii ni hija binafsi inayofumbatwa katika Injili ya upendo na ukarimu. Hii ni Siku ya Vijana Ulimwenguni katika ngazi ya Kijimbo. Umati mkubwa wa vijana unatarajiwa kushiriki kikamilifu. Baba Mtakatifu amewaombea wazee wote, ili jamii iweze kutambua umuhimu wa watu hawa hasa katika ulimwengu wa utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Vijana na wazee wanahitajiana na kukamilishana katika hija ya maisha yao hapa duniani. Kumbe, kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni unaowakutanisha vijana na wazee, ili kukoleza moyo wa majadiliano. Bila mchakato wa majadiliano kati ya wazee na vijana wa kizazi kipya, maisha na historia ya mwanadamu vitagonga mwamba na maisha hayataweza kusonga mbele hata kidogo! Majadiliano kati ya wazee na vijana wa kizazi kipya ni changamoto katika ulimwengu mamboleo. Wazee wanayo haki ya kuota ndoto, huku wakiwaangalia vijana. Na vijana kwa upande wao, wanayo haki na ujasiri wa kinabii, huku wakichota hekima na busara kutoka kwa wazee. Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee kabisa, anawaalika wazee na vijana wa kizazi kipya kujenga utamaduni wa kukutana na kuzungumza kwa pamoja, mwelekeo huu utakuwa ni wa manufaa kwa makundi yote mawili!