Papa Francisko Asikitishwa na Shambulio la Kigaidi Nchini Uturuki
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na ongezeko kubwa la uvunjwaji wa haki ya uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini; hali inayojikita katika: vita, chuki na uhasama; misimamo mikali ya kidini na kiimani; pamoja na vitendo vya kigaidi vinavyotishia misingi ya haki, amani, umoja na mafungamano ya kijamii. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusimama kidete kupambana na vitendo vya kigaidi vinavyohatarisha usalama, maisha, mafungamano ya kijamii pamoja na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali na miundo mbinu ya umma. Vitendo vya kigaidi ni kinyume kabisa na uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini. Hivi ni vitendo ambavyo vinapaswa kulaaniwa na kushutumiwa na Jumuiya ya Kimataifa bila “kupepesa pepesa macho.” Ni katika hali na mazingira kama haya, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano, tarehe 16 Novemba 2022 amewakumbuka na kuwaombea waathirika wa mlipuko wa bomu uliotokea kwenye barabara ya Istiklal, iliyoko kati kati ya mji wa Istanbul, nchini Uturuki, Dominika tarehe 13 Novemba 2022 na kusababisha watu 6 kufariki dunia na wengine 80 kujeruhiwa vibaya. Taarifa rasmi zinaonesha kwamba, tayari majeruhi 50 wamekwisha kuruhusiwa kutoka hospitalini, ili kuendelea na shughuli zao mbalimbali.
Wakati huo huo, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko amemtumia salam za rambirambi Askofu mkuu Marek Solczyński, Balozi wa Vatican nchini Uturuki kufuatia shambulio hili na kigaidi. Baba Mtakatifu anamwomba, afikishe salam za rambirambi za Baba Mtakatifu Francisko kwa wale wote walioguswa na kutikiswa na msiba huu mzito. Marehemu wapate rehema kwa Mungu wapumzike kwa amani na majeruhi waweze kupona haraka na kurejea katika shughuli zao za kila siku. Baba Mtakatifu anaendelea kusali, ili kwamba, familia ya watu wa Mungu nchini Uturuki isikatishwe tamaa na vitendo hivi vya kigaidi, bali waendelee kujikita katika mchakato wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika tunu msingi za: Udugu wa kibinadamu, haki na amani. Ikumbukwe kwamba, Serikali zinalo jukumu la kulinda usalama wa raia na mali zao, sanjari na kujenga utamaduni wa haki, amani, maridhiano pamoja na mafungamano ya kijamii. Ili kukabiliana na vitendo vya kigaidi sehemu mbali mbali za dunia, kuna haja kwanza kabisa: kujenga na kudumisha utamaduni wa maridhiano na mafungamano ya kijamii; kwa kuheshimu uhai kama zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu; kwa kuthamini haki msingi za binadamu, utu na heshima yake.
Pili ni kuhakikisha kwamba, watu wote wanakuwa na haki sawa mbele ya sheria za nchi bila upendeleo wa mahali anakotoka mtu, dini, kabila au nafasi yake katika jamii. Pale haki msingi za baadhi ya raia zinapovunjwa, sheria ichukue mkondo wake. Tatu, ni kutenganisha utendaji wa Serikali na dini; kwa kukazia ushirikiano na mshikamano kwa ajili ya kukuza na kudumisha utu, heshima, ustawi na maendeleo ya wengi. Kuna hatari kwa viongozi wa kiserikali kutumia dini kwa ajili ya mafao binafsi pamoja na kujijenga kisiasa, kiuchumi na kijamii, hatari kubwa inayoweza kusababisha machafuko katika nchi. Nne, ni kuhakikisha kwamba, viongozi wa kiserikali, kijamii na kidini, kwa pamoja wanaungana kukemea na kulaani watu wanaotumia dini kuchochea chuki, uhasama na mipasuko ya kijamii inayopelekea hata kushamiri kwa vitendo vya kigaidi. Kamwe jina la Mwenyezi Mungu haliwezi kutumiwa kwa ajili ya kusababisha vita! Askofu mkuu Auza anasema, tano ni kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inawashughulikia na kuwahudumia waathirika wote wa vitendo vya kigaidi na wasiwepo wale wanaobaki nyuma! Jumuiya ya Kimataifa haina budi kupambana na hofu dhidi ya waamini wa dini wa Kiislam, Wayahudi na Wakristo. Hapa inasikitisha kuona kwamba, mara nyingi Wakristo wanaposhambuliwa na vikundi vya kigaidi, viongozi na hata wakati mwingine, vyombo vya mawasiliano ya kijamii vinashindwa kutaja moja kwa moja matukio haya kwa kutafuta lugha laini.
Jambo la sita ni kuhakikisha kwamba, waamini wa dini na madhehebu mbalimbali wanaendeleza majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni kama njia ya kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano. Huu ni mchakato wa ujenzi wa mshikamano na udugu wa kibinadamu, ili kufahamiana, kuheshimiana na kuthaminiana hata katika tofauti hizi msingi ambazo ni amana na utajiri kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Serikali mbali mbali zinapaswa kuunga mkono jitihada za majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wao! Jambo la saba ni elimu makini inayokita mizizi yake kwenye majadiliano, kanuni maadili na utu wema; haki, amani na upatanisho pamoja na kuheshimu utawala wa sheria. Kamwe mitandao ya kijamii isitumike kuwavuruga vijana kwa kuwapandikizia misimamo mikali ya kidini na kiimani. Ikumbukwe kwamba, mapambano dhidi ya vitendo vya kigaidi ni mchakato unaoweza kuchukua muda mrefu. Kumbe, kuna haja ya kujikita katika fadhila ya uvumilivu na udumifu; hekima, busara na ujasiri pamoja na uongozi bora!