Maadhimisho ya Siku ya Sita ya Maskini Duniani tarehe 13 Novemba 2022. Msidanganyike, Iweni na imani thabiti na subira. Maadhimisho ya Siku ya Sita ya Maskini Duniani tarehe 13 Novemba 2022. Msidanganyike, Iweni na imani thabiti na subira. 

Papa Francisko: Mambo ya Nyakati za Mwisho: Msidanganyike Iweni na Subira na Imani Thabiti

Papa Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya Sita ya Maskini Duniani ameielekeza tafakari yake kuhusu mang’amuzi ya mambo ya nyakati za mwisho ili waamini wasije wakadanganyika, wayaangalie mambo yote kwa jicho la imani na kwa subira wataziponya nafsi zap Ni siku ya ushuhuda wa matendo mema; muda wa kuganga na kuponya; kusikiliza na kujibu kilio cha maskini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Siku ya Maskini Duniani ni matunda ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu inayoadhimishwa Jumapili ya 33 ya Kila Mwaka wa Kanisa. Kwa mara ya kwanza Siku hii iliadhimishwa kunako mwaka 2017. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Siku ya Sita ya Maskini Duniani tarehe 13 Novemba 2022 yanayonogeshwa na kauli mbiu: “Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake.” 2Kor 8:9. Baba Mtakatifu anachambua jinsi Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ulivyo sababisha ongezeko la maskini duniani; vita inavyoendelea kuwatumbukiza watu katika baa la umaskini na kwamba, umaskini wa Kristo uwawajibishe waamini kushirikiana na kushikamana katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kama kielelezo cha tunu msingi zinazosimikwa katika mshikamano, kielelezo cha imani inayomwilishwa katika matendo. Umaskini ni matokeo ya ukosefu wa haki, unyonyaji, vita na ugawaji mbaya wa rasilimali za dunia. Umaskini wa Kristo Yesu, unawawezesha waamini kuwa ni matajiri wa huruma na mapendo, tayari kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa jirani kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Charles de Foucauld aliyetangazwa kuwa Mtakatifu tarehe 15 Mei 2022.

Kuna watakatifu ambao wamejisadaka kwa ajili ya huduma ya upendo
Kuna watakatifu ambao wamejisadaka kwa ajili ya huduma ya upendo

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake, Dominika ya 33 ya Mwaka C wa Kanisa, Siku ya Sita ya Maskini Duniani ameielekeza tafakari yake kuhusu mang’amuzi ya mambo ya nyakati za mwisho ili waamini wasije wakadanganyika, wayaangalie mambo yote kwa jicho la imani na kwa subira wataziponya nafsi zao. Hii ni fursa ya kutolea ushuhuda wa matendo mema katika maisha. Siku ya Sita ya Maskini Duniani ni muda muafaka wa kuganga na kuponya; kusikiliza na kujibu kilio cha maskini. Huu ni mwaliko kwa waamini kujizatiti kikamilifu ili wasije wakadanganyika. Hekalu la Yerusalemu lilikuwa ni utambulisho wa Waisraeli, mahali pa sala na sadaka kwa kutambua uwepo angavu wa Mungu na lilipambwa kwa mawe mazuri na sadaka za watu. Lakini watu walishangazwa sana Kristo Yesu alipowaambia kwamba, yote haya yatapita, jambo la msingi ni kuwa na mang’amuzi kwa maisha ya sasa, ili wabaki kuwa ni wanafunzi waaminifu wa Injili ya Kristo Yesu hata katika matatizo na changamoto mbalimbali wanazoweza kukabiliana nazo katika maisha. Kristo Yesu anawaonya wafuasi wake wasije wakadanganyika kwa sababu kutakuwepo na manabii wengi wa uwongo, lakini wasiwafuate hao. Huu ni mwaliko wa kuyaangalia matukio mbalimbali ya dunia kwa mwanga na jicho la imani, kinyume kabisa cha vitisho vinavyoweza kutolewa na manabii wa uwongo, wapiga ramli au watabiri wa nyota.

Waamini wajizatiti kikamilifu kutenda mema
Waamini wajizatiti kikamilifu kutenda mema

Kamwe waamini wasikubali kutwishwa “mgizo” wa woga na wasiwasi, bali watambue kwamba Mwenyezi Mungu ndiye mlinzi wao wa daima na wajitahidi kusoma matukio ya dunia kwa jicho la imani, kwani licha ya matukio yote haya kutukia na kuutikisa uso wa dunia, lakini huo bado si mwisho wa dunia. Wasikate wala kukatishwa tamaa hata pale wanapokumbana na hali tete katika maisha, kwa sababu Mungu wao ni Mungu wa Ufufuko na Matumaini; daima anawaangalia watoto wake kwa jicho la matumaini, tayari kuwainua pale walipoteleza, na pale waliopoanguka ili kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Matukio kama haya anasema Baba Mtakatifu ni fursa kwa waamini kujikita katika kutenda mema, hata kama tukio lenyewe lilikuwa na mwelekeo hasi. Changamoto za maisha ziwe ni fursa kwa waamini kupiga moyo konde na kusonga mbele, kwa usalama na kujiamini zaidi. Kristo Yesu anawaangalisha wafuasi wake kwamba, pale wanapoona matukio ya vita na fitina; matetemeko makubwa ya ardhi, njaa na magonjwa ya milipuko; mambo ya kutisha na ishara kuu kutoka mbinguni, ili fursa ya kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili.

Maskini ni sehemu ya utambulisho wa Mama Kanisa katika huduma
Maskini ni sehemu ya utambulisho wa Mama Kanisa katika huduma

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Kanisa linawajibika kimaadili kuwasaidia na kuwahudumia maskini, ndiyo maana baada ya kufunga rasmi maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ameanzisha Siku ya Maskini Duniani, ili Jumuiya za Kikristo sehemu mbalimbali za dunia, ziweze kuwa alama wazi ya huruma na upendo wa Kristo Yesu kwa maskini na wahitaji. Siku hii ni muhimu sana ili kuonesha upendeleo wa Yesu kwa maskini, mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwasikiliza, kuwahudumia na kuwaonesha maskini upendo na mshikamano, kwa kutambua kwamba, hata wao wameumbwa kw asura na mfano wa Mungu na wanapendwa na Baba yao wa mbinguni. Siku ya Maskini Duniani ni fursa ya kushikamana kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana na kusaidiana, kama alama ya: urafiki wa kijamii, umoja na udugu wa kibinadamu unaovunjilia mbali kuta za utengano. Siku ya Maskini Duniani ni nafasi ya kuwaonjesha huruma na upendo maskini na wahitaji; ni siku ya kuwakaribisha na kuwakirimia wageni inayowasaidia waamini kumwilisha imani yao katika matendo; watu wawe tayari kupokea msaada na kujitahidi kuishi kwa kuzingatia mambo msingi ya maisha, daima tayari kujiachilia kwa huruma ya Mungu.

Maskini waonjeshwe huruma na upendo katika maisha yao
Maskini waonjeshwe huruma na upendo katika maisha yao

Maadhimisho haya yakamilishwe kwa namna ya pekee Kanisa linapoadhimisha Siku kuu ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu. Huu ni ufalme wa kweli na wa uzima; ufalme wa utakatifu na wa neema; ufalme wa haki, mapendo na amani. Ufalme wa Kristo unafumbatwa kwa namna ya pekee, katika Fumbo la Msalaba ushuhuda wa utimilifu wa huruma na upendo wa Mungu, chemchem ya maisha mapya wakati wa Pasaka. Baba Mtakatifu Francisko anasema hata leo hii, ulimwengu mamboleo unaendelea kukumbana na vita, ukosefu wa haki, dhuluma na nyanyaso; athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ambalo limeacha madhara makubwa katika maisha ya watu wengi duniani: kimwili na kisaikolojia; kiuchumi na kijamii. Vita ni kati ya vyanzo vikuu ya umaskini duniani, kiasi cha kupandikiza sumu ya chuki na uhasama kati ya watu. Leo hii walimwengu wanashuhudia Vita Kuu ya Tatu ya Dunia inayopiganwa vipande vipande. Baa la njaa na utapiamlo wa kutisha, ujinga na umaskini vikasahauliwa na matokeo yake ni wakuu wa Mataifa kuongeza bajeti katika manunuzi ya silaha ili kuendeleza utamauduni wa kifo ulimwenguni.

Vita na ghasia ni vyanzo vikuu vya umaskini duniani.
Vita na ghasia ni vyanzo vikuu vya umaskini duniani.

Kuna wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutoka sehemu mbalimbali za dunia wanaotafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi; ni watu wanaotafuta pia fursa za ajira bila matumaini. Siku ya Maskini Duniani ni fursa ya kusikiliza na kujibu kilio cha maskini wa hali na kipato, kwa kuwaonesha mshikamano wa udugu wa upendo. Kristo Yesu, anawataka wafuasi wake kuwa makini ili wasidanganyike na manabii wa uwongo, wanaotaka kujimwambafai ndani ya jamii kwa kupandikiza vitisho; kwa kuendelea kufaika na ujinga wa waamini. Hawa ni manabii, wanaotangaza utajiri wa “chapuchapu”, mafanikio kama “maji kwa glasi” na kwamba, maskini katika ulimwengu mamboleo hawana chao! Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Siku ya Maskini Duniani ni fursa ya kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili inayosimikwa katika: Ukarimu, udugu wa kibinadamu; ujasiri wa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha: Utu, haki msingi za binadamu, ustawi na maendeleo ya wote, kwa kushirikiana na kushikamana na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni wajibu wa waamini kupambana kufa na kupona ili kuipatia historia uso na mwelekeo mpya zaidi, kwa kujiaminisha katika tunza na ulinzi wa Mwenyezi Mungu, ambaye anawapenda, anawajali na kuwalinda wakati wote. Waamini wajenge na kudumisha mahusiano na mafungamano ya urafiki wa kijamii. Watambue kwamba, wao, kimsingi ni Hekalu la Fumbo la Utatu Mtakatifu. Uso wa Kristo Yesu unaendelea kujifunua katika historia ya maskini, mateso na madonda yao yanayopaswa kugangwa na kuponya kwa mafuta ya huruma ya Mungu na divai ya upendo.

Papa Maskini Duniani 2022
13 November 2022, 15:22