Tafuta

Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini DRC na Sudan ya Kusini ni kuanzia tarehe 31 Januari 2023 hadi 5 Februari 2023. Matendo makuu ya Mungu. Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini DRC na Sudan ya Kusini ni kuanzia tarehe 31 Januari 2023 hadi 5 Februari 2023. Matendo makuu ya Mungu. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko DRC na Sudan ya Kusini 31 Januari-5 Februari 2023

Baba Mtakatifu Francisko, Askofu mkuu Justin Welby, Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani na Mkuu wa Kanisa la Scotland kama kielelezo cha ushuhuda wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika huduma ya upendo, maisha ya kiroho, damu na sala watatembelea Sudan ya Kusini kuanzia tarehe 3 Februari hadi tarehe 5 Februari 2023. Papa DRC 31 Jan-3 Februari 2023

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 15 Septemba 2022 akiwa njiani kurejea mjini Vatican alipata nafasi ya “kuchonga” na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake nchini Kazakhstan. Alizungumzia kuhusu vita kati ya Urusi na Ukraine; haki ya kujilinda dhidi ya maadui, biashara haramu ya silaha na madhara yake duniani; Siasa na sera za Bara la Ulaya zinavyotishia tunu msingi za maisha ya kijamii na kiutu na hivyo kuibua viongozi wanaojitafutia umaarufu wa kisiasa ili kujimwambafai mbele ya Jumuiya ya Kimataifa. Kanisa linahitaji wachungaji wema na watakatifu na wala si tu mikakati ya shughuli za kichungaji. Baba Mtakatifu bado alisema kwamba, ametia nia ya kutembelea Sudan ya Kusini na DRC, Mwezi Februari 2023 panapo majaliwa. Ratiba elekezi iliyotolewa na Vatican inaonesha kwamba, Baba Mtakatifu tarehe 31 Januari 2023 majira ya asubuhi, ataondoka kuelekea nchini DRC na huko atapata fursa ya kumtembelea Rais wa DRC, kuzungumza na viongozi wa Serikali na Kisiasa, Wanadiplomasia pamoja na viongozi wa vyama vya kiraia. Ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Ndege wa “Ndolo”, atakutana na kuzungumza na waathirika wa vita ambayo imedumu kwa muda mrefu nchini DRC. Kwa kutambua mchango mkubwa unaotolewa na Makatekista katika maisha na utume wa Kanisa nchini DRC, Baba Mtakatifu atapata mwanya wa kuzungumza nao pamoja na kuzungumza na viongozi wa vyama na mashirika ya misaada.

Hija ya Kitume ya Papa Francisko nchini Sudan ya Kusini: Uekumene
Hija ya Kitume ya Papa Francisko nchini Sudan ya Kusini: Uekumene

Kabla ya kuondoka kuendelea na hija yake ya Kitume nchini Sudan ya Kusini, Baba Mtakatifu atapata fursa ya kuzungumza na Wayesuit wanaotekeleza utume wao nchini DRC, atazungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki DRC, CENCO na baadaye kuondoka kuelekea Juba, Sudan ya Kusini. Baba Mtakatifu Francisko akiwa ameambatana na Askofu mkuu Justin Welby, Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani na Mkuu wa Kanisa la Scotland kama kielelezo cha ushuhuda wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika huduma, maisha ya kiroho, damu na sala watatembelea Sudan ya Kusini kuanzia tarehe 3 Februari hadi tarehe 5 Februari 2023. Akiwa nchini Sudan ya Kusini, Baba Mtakatifu atazungumza na viongozi wa Serikali na Kisiasa, Wanadiplomasia pamoja na viongozi wa vyama vya kiraia nchini Sudan ya Kusini. Atapata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Makleri, Watawa na Majandokasisi, Wayesuit wanaotekeleza utume wao nchini Sudan ya Kusini pamoja na watu wasiokuwa na makazi maalum. Viongozi wakuu wa Makanisa watashiriki Sala ya Kiekumene. Dominika tarehe 5 Februari 2023 Baba Mtakatifu ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kuwaongoza waamini kwa tafakari ya Sala ya Malaika wa Bwana na baadaye, jioni ataondoka na kurejea tena mjini Vatican.

Vita inaendelea kusababisha maafa makubwa kwa maisha ya binadamu na mali zake.
Vita inaendelea kusababisha maafa makubwa kwa maisha ya binadamu na mali zake.

Itakumbukwa kwamba, viongozi wakuu wa Makanisa kutoka Sudan ya Kusini walimtembelea na kuwaomba viongozi wa Makanisa ili waende kushuhudia mateso na mahangaiko ya wananchi wa Sudan ya Kusini, wanaoendelea kupukutika kutokana na vita, njaa na magonjwa. Mashahidi wa Uganda ni mashuhuda wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika damu, kama alivyoshuhudia Mtakatifu Paulo VI alipokuwa nchini Uganda. Ni mashuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni waamini waliosimama kidete kiasi hata cha kusadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu, Kanisa, nidhamu, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kati yao walikuwemo pia Makatekista kutoka Kanisa Anglikani. Sehemu mbali mbali za dunia Kanisa Anglikani na Kanisa Katoliki wanashirikiana katika huduma kiasi cha kujenga urafiki na mshikamano kati yao. Wakati mwingine, wanashirikiana hata katika Ibada, kielelezo makini cha utajiri wa maisha ya kiroho. Baba Mtakatifu anasema, itapendeza ikiwa kama Makanisa Barani Ulaya yatawatuma majandokasisi kwenda katika nchi za kimisionari kujifunza uhai na kipaji cha ugunduzi, ili kusaidia mchakato wa majadiliano ya kiekumene.

Papa DRC na Sudan ya Kusini
KISWAHILI 01122022
01 December 2022, 14:58