Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 5 Desemba 2022 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwombea na kumuaga rasmi Kardinali Richard Kuuia Baawobr, MAfr.. Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 5 Desemba 2022 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwombea na kumuaga rasmi Kardinali Richard Kuuia Baawobr, MAfr.. 

Hayati Kardinali Richard Kuuia Baawobr Ni Nyota Iliyozimika Mapema. Kifo!

Kardinali Richard Kuuia Baawobr, MAfr., alikuwa ameweka msingi wa maendeleo makubwa katika huduma kwa watu wa Mungu nchini Ghana, kwa Kanisa la Kiulimwengu na kwa familia; Fumbo la kifo kadiri ya imani na matumaini ya Kanisa, wasifu wa maisha na utume wake, uliofanya kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili uinjilishaji wa kina, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kifo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa anawaalika waamini kujiandaa kikamilifu ili kukabiliana na Fumbo la Kifo katika hija ya maisha yao, huku wakijitahidi kukesha kwani hakuna mtu anayejua siku ya kufa kwake. Fumbo la Kifo linabaki kuwa ni tete katika maisha ya mwanadamu anayesafiri, huku bondeni kwenye machozi. Mababa wa Kanisa wanasema, maana ya Kikristo ya kifo imefunuliwa katika mwanga wa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo ambaye ndani yake mna tumaini la Wakristo. Mkristo anayekufa katika Kristo huuacha mwili ili kwenda kukaa pamoja na Mwenyezi Mungu, milele yote! Kwa Mkristo, siku ya kifo huanzisha, mwishoni mwa maisha yake ya Kisakramenti, utimilifu wa kuzaliwa kwake upya kulikoanzishwa na Sakramenti ya Ubatizo, kufanana kamili na sura ya Mwana, kulikotolewa kwa Mpako wa Roho Mtakatifu na ushirika katika karamu ya Ufalme, uliotangulizwa katika Ekaristi, hata kama ana lazima bado kutakaswa zaidi ili kuvikwa vazi la arusi! Baba Mtakatifu Francisko anawahamasisha waamini kulitafakari Fumbo la kifo, kama sehemu ya matumaini ya Kikristo kwani, Kristo Yesu mwenyewe anasema, ndiye ufufuo na uzima na kwamba, yeyote anayemwamini ajapokufa atakuwa anaishi na kwamba, heri yao wale wote wanaokufa katika Kristo Yesu. Matumaini ya Kikristo yawasaidie waamini kukabiliana na Fumbo la kifo kwa imani na matumaini na kwamba hata ustaarabu wa watu wa kale umepitia katika fumbo hili na kwa hakika, ibada ya kifo ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu.

Ni katika muktadha huu, Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 5 Desemba 2022 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa ajili ya kumwombea na kumuaga rasmi Hayati Kardinali Richard Kuuia Baawobr, MAfr., Askofu wa Jimbo la Wa, nchini Ghana kilichotokea tarehe 27 Novemba 2022 katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli, mjini Roma ambako alikuwa anapatiwa matibabu akiwa na umri wa mika 63 tangu alipozaliwa. Katika mahubiri yake, Kardinali Giovanni Battista Re, amebainisha kwamba, Hayati Kardinali Richard Kuuia Baawobr, MAfr., alikuwa ameweka msingi wa maendeleo makubwa katika huduma kwa watu wa Mungu nchini Ghana, kwa Kanisa la Kiulimwengu na kwa familia ya Mungu katika ujumla wake; Fumbo la kifo kadiri ya imani na matumaini ya Kanisa, wasifu wa maisha na utume wake, uliomfanya kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili uinjilishaji wa kina, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kwa hakika njia za Mungu ni tofauti kabisa na mawazo ya binadamu. Huu ni mwaliko kwa waamini kufanya tafakari ya kina kuhusu kujiweka tayari kwa kuongozwa na maneno ya Mwinjili Luka anayesema “Viuno vyenu na viwe vimefungwa, na taa zenu ziwe zinawaka.” Lk. 12: 25. “Nanyi jiwekeni tayari, kwa kuwa saa msiyodhani ndipo ajapo Mwana wa Adamu.” Lk 12: 40.

Matumaini katika Fumbo la Kifo: NI katika mateso, kifo na ufufuko wa Yesu
Matumaini katika Fumbo la Kifo: NI katika mateso, kifo na ufufuko wa Yesu

Huu ni mwaliko unaotolewa na Mama Kanisa kwa watoto wake ili kutafakari hali ya maisha yao na umuhimu wa kuishi upendo wa Mungu na jirani katika utimilifu wake. Kwa sasa roho ya Hayati Kardinali Richard Kuuia Baawobr, MAfr., iko mikononi mwa Mungu, hatima ya maisha ya wenye haki.Katika muktadha wa imani, Hayati Kardinali Richard Kuuia Baawobr, MAfr., awe ni chemchemi ya matumaini, kama mtangulizi wa watu wa Mungu wanaosafiri huku bondeni kwenye machozi, ili siku moja waweze kuunganika pamoja naye, bila woga wala wasiwasi, waweze kumpenda tena. Kadiri ya mpango wa Mungu, waamini wajikite zaidi katika upendo kwa Mungu na jirani kama wasifu wa maisha ya Hayati Kardinali Richard Kuuia Baawobr, MAfr., yanavyodhihirisha. Itakumbukwa kwamba, Hayati Kardinali Richard Kuuia Baawobr, MAfr., alizaliwa tarehe 21 Juni 1959, Jimboni Wa, nchini Ghana kutoka katika familia ya wachamungu, lakini kazi kubwa ya malezi na makuzi yake ilitekelezwa na Mama yake mzazi aliyekuwa mchamungu kweli kweli na hivyo kuwa ni katekista wa kwanza katika maisha na wito wake. Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa na kikasisi, tarehe 5 Desemba 1986 akaweka nadhiri zake za daima. Tarehe 18 Julai 1987 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tangu wakati huo, amekuwa ni Paroko msaidizi kwenye Parokia la Livulu, Jimbo kuu la Kinshasa, DRC. Kuanzia mwaka 1991 hadi mwaka 1996 alikuwa masomoni kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian akichukua masomo ya Sayansi ya Biblia na baadaye akatunukiwa Shahada ya Uzamivu katika somo la Taalimungu Biblia.

Sayansi ya Maandiko Matakatifu
Sayansi ya Maandiko Matakatifu

Kunako mwaka 1996 hadi mwaka 1999 akatumwa nchini Tanzania kama mlezi kwenye nyumba ya Shirika la Wamissionari wa Afrika, huko Kahangala, Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania, hapa watu wa Mungu Jimbo kuu la Mwanza wanamkumbuka kwa utume wa familia kama Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Hapa ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Kuanzia mwaka 1999 hadi mwaka 2004 akateuliwa kuwa Mkurugenzi wa nyumba ya malezi huko Tolosa, nchini Ufaransa. Kunako mwaka 2004 hadi mwaka 2010 akachaguliwa kuwa ni kati ya washauri wakuu wa Shirika la Wamisionari wa Afrika, maarufu kama “White Fathers.” Kunako mwaka 2010 akachaguliwa kuwa Mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Afrika, akiwa ni Mwafrika wa kwanza kuchaguliwa kuliongoza Shirika hili tangu kuanzishwa kwake! Amekuwa pia ni Makamu mkuu wa Taasisi ya Masomo ya Kiarabu na Kiislam mjini Roma, PISAI. Kunako mwaka 2015 alishiriki katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya familia baada ya kuchaguliwa kuwakilisha Shirikisho la Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume Duniani kuanzia tarehe 4-25 Oktoba 2015. Daima aliwataka Wamisionari wa Afrika kutambua kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili, watu ambao wanapaswa kuwa tayari kujisadaka kwa ajili ya uinjilishaji unaopania kuleta upyaisho katika maisha ya watu na kama njia ya kutamadunisha Injili ili kuinjilisha tamaduni mintarafu tunu msingi za Kiinjili. Wawe wepesi kujifunza lugha na tamaduni njema za watu wanaowahudumia kielelezo cha upendo kwa watu wa Mungu, huku wakiguswa na furaha, changamoto, matatizo na fursa katika maisha yao.

Ameiongoza SECAM kwa muda mfupi sana
Ameiongoza SECAM kwa muda mfupi sana

Kama wamisionari wawe tayari kusoma alama za nyakati, tayari kujikita katika uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko katika kuzima kiu ya Neno la Mungu, mchakato wa upyaishaji wa imani na ushuhuda wa tunu msingi za Kikristo. Tarehe 17 Februari 2016 Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Wa nchini Ghana na kuwekwa wakfu tarehe 7 Mei 2016. Akaonesha utii na uaminifu kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro; Ukaribu, upendo kwa mihimili ya uinjilishaji pamoja na watu wa Mungu nchini Ghana katika ujumla wake. Alitambua dhamana na wajibu wake kama Askofu jimbo na daima alipokutana na watu wa Mungu alikuwa na ujumbe mahususi. Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, kuanzia tarehe 25 Julai hadi tarehe 1 Agosti 2022, liliadhimisha mkutano wake mkuu wa 19 huko Accra, nchini Ghana kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Umiliki wa SECAM: Usalama na Uhamiaji Barani Afrika na Visiwani na kumchagua Askofu Richard Kuuia Baawobr, WF., kuwa Rais wa SECAM. Tarehe 27 Agosti 2022, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa ni Kardinali. Tarehe 27 Novemba 2022 akafariki dunia katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli, iliyoko mjini Roma.

Hakubahatika kuhudhuria Ibada ya Kuwatangaza na Kuwasimika Makardinali
Hakubahatika kuhudhuria Ibada ya Kuwatangaza na Kuwasimika Makardinali

Kwa ufupi kabisa, Hayati Kardinali Richard Kuuia Baawobr, MAfr., amelitumikia Kanisa kama Padre kwa muda wa miaka 35, kama Askofu akifundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa muda wa miaka 6 na kama Kardinali, Mshauri wa Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa muda wa miezi miwili tu. Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali anakiri kwamba, Hayati Kardinali Richard Kuuia Baawobr, MAfr., alijikita zaidi katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina, kwa ajili ya wokovu wa roho za watu. Mama Kanisa awashukuru Wamisionari wa Afrika, MAfr. Kwa kumwandaa na hatimaye, kutekeleza dhamana na nyajibu mbalimbali alizokabidhiwa kuzitenda. Huu ni wakati wa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani, lakini zaidi ni kumwomba Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma, upendo na msamaha, ili aweze kumpokea Hayati Kardinali Richard Kuuia Baawobr, MAfr., katika huruma na upendo wake wa daima, kama anavyosema Mwinjili Mathayo kwa watoto wa Kanisa waliothubutu kutumia vyema karama na mapaji ya Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa kwa kusema “Vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako.” Mt. 25:21.

Hayati Kardinali Baawobr
05 December 2022, 16:19