Tafuta

Fumbo la Msalaba wa Kristo Yesu yaani: Mateso, kifo na ufufuko wake ni kilele cha ufunuo wa: huruma, upendo, ukuu, utukufu na utakatifu wake Fumbo la Msalaba wa Kristo Yesu yaani: Mateso, kifo na ufufuko wake ni kilele cha ufunuo wa: huruma, upendo, ukuu, utukufu na utakatifu wake 

Mtakatifu Yohane wa Msalaba, Padre na Mwalimu wa Kanisa: Fumbo la Msalaba

Mtakatifu Yohane wa Msalaba, Padre na Mwalimu wa Kanisa, ni Baba wa maisha ya kiroho, shuhuda wa utekelezaji mapenzi ya Mungu katika uhalisia wa maisha ya watu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na wenye mapenzi kuwakumbuka na kuwaombea watu wanaoteseka sehemu mbalimbali za dunia kutokana na vita, lakini kwa namna ya pekee nchini Ukraine.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Msalaba katika mapokeo ya kale, ilikuwa ni alama ya uovu wa kutisha na hali ya kukatisha tamaa, lakini, kwa njia ya Kristo Yesu Mkombozi wa dunia, Msalaba umepata maana mpya katika maisha ya mwanadamu. Msalaba sasa ni kielelezo cha ushujaa wa Kristo Yesu na mashuhuda wa imani, wanaoendelea kuteseka pamoja na kuyamimina maisha yao kwa ajili ya imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake sehemu mbalimbali za dunia. Msalaba ni chombo cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu! Ni ishara ya mapendo, neema, sala, msamaha, upatanisho na matumaini. Ni kutokana na maana hii mpya, Mama Kanisa anaona fahari kuu kuutangaza utukufu na kuimba sifa kuu za Msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Msalaba unaendelea kumfunza mwamini kwamba, hakuna mapendo kamili yasiyokuwa na mateso na matumaini ya uzima wa milele. Changamoto kwa waamini katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo ni kuuangalia, kuutafakari, kuushangaaa, kuusikiliza, kuuheshimu, kuutukuza na kuuabudu kwa imani, matumaini na mapendo, kwani ni kielelezo ambacho wokovu wa dunia umetundikwa juu yake! Fumbo la Msalaba wa Kristo Yesu yaani: Mateso, kifo na ufufuko wake ni kilele cha ufunuo wa: huruma, upendo, ukuu, utukufu na utakatifu wake, changamoto kwa waamini ni kushikamana pamoja na Kristo Yesu katika mapambano, ili siku moja waweze kushinda pamoja naye!

Msalaba ni kielelezo cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu.
Msalaba ni kielelezo cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu.

Huu ndio ujumbe wa matumaini unaofumbatwa kwa namna ya pekee katika Fumbo la Msalaba, mwaliko kwa waamini kumtafakari Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kuwa ni kiini cha imani ya Kikristo. Waamini watambue ukuu wa Msalaba na wala si tu kama kito cha thamani wanachovaa shingoni au kupamba majumbani mwao, bali ni dira, mwongozo na mwaliko wa kuutafakari upendo wa Kristo Yesu aliyejisadaka kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Fumbo la Msalaba ni alama ya upendo wa Mungu kwa binadamu; kielelezo cha sadaka ya hali ya juu kabisa ya Kristo dhidi ya ukosefu wa haki msingi za binadamu; ubinafsi, dhuluma na nyanyaso. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 14 Desemba 2022, Kumbukumbu ya Mtakatifu Yohane wa Msalaba, Padre na Mwalimu wa Kanisa, amewaalika kwa namna ya pekee kabisa: vijana, wagonjwa, wazee na wanandoa wapya, kujiaminisha chini ya ulinzi na tunza ya huyu. Mtakatifu Yohane wa Msalaba, Padre na Mwalimu wa Kanisa, ni Baba wa maisha ya kiroho, shuhuda wa utekelezaji mapenzi ya Mungu katika uhalisia wa maisha ya watu.

Msalaba ni Mti wa Ujumbe wa Matumaini
Msalaba ni Mti wa Ujumbe wa Matumaini

Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wenye mapenzi kuwakumbuka na kuwaombea watu wanaoteseka sehemu mbalimbali za dunia kutokana na vita, lakini kwa namna ya pekee kabisa nchini Ukraine. Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yohane wa Msalaba, Padre, Mwalimu wa Kanisa na Shuhuda wa imani ya Fumbo la Msalaba alizaliwa tarehe 24 Juni1542 huko Fontiveros nchini Hispania. Alijiunga na Wakarmeli na hatimaye kuweka nadhiri zake za daima mwaka 1564 na hatimaye, kupewa Daraja Takatifu ya Upadre mwaka 1567. Kwa hakika, alibahatika kupata majiundo makini ya kitaalimungu na ndiyo maana Mtakatifu Theresa wa Avila akamshirikisha katika mchakato wa kupyaisha Shirika la Wakarmeli na matunda ya kazi hii ngumu ni kuzaliwa kwa Shirika la Wakarmeli Peku, waliorejea kwenye sheria, kanuni na taratibu asilia kwa kujikita katika nidhamu, tafakuri na nadhiri ya ufukara, daima wakijitahidi kufanya rejea kwenye Fumbo la Msalaba, mchango mkubwa uliotolewa na Mtakatifu Yohane wa Msalaba. Aliwahi kutekwa nyara na watawa wenzake, akashutumiwa kwa uongo na hatimaye kufungwa gerezani kwa muda wa miezi tisa. Mtakatifu Yohane wa Msalaba daima alipata faraja kwa kuthamini uwepo wa Mwenyezi Mungu katika mahaingaiko yake, akazama zaidi katika Maandiko Matakatifu, Sala na Fadhila za Kimungu, kiasi hata cha kuwa Padre bora mwongozi wa maisha ya kiroho. Hatimaye akafariki dunia tarehe 14 Desemba 1591. Siku ya mwisho watu watahukumiwa kwa kipimo cha upendo. Papa Clement X akamtangaza kuwa Mwenyeheri tarehe 25 Oktoba 1675. Papa Benedikto XIII akamtangaza kuwa ni Mtakatifu na hatimaye, Papa Pio XI akamtangaza kuwa ni Mwalimu wa Kanisa.

Msalaba ni Mti wa Ujumbe wa Matumaini
Msalaba ni Mti wa Ujumbe wa Matumaini

Msalaba ni alama ya ushindi dhidi ya dhambi na kifo. Msalaba ni kielelezo cha mateso, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo wanaouwawa kikatili kwa kuchomwa moto wangali hai; na wakati mwingine nyanyaso na dhuluma hizi zinatendwa katika hali ya ukimya mkubwa. Kwa njia ya Fumbo la Msalaba, Yesu anaungana na mamillioni ya watu wanaoteseka kutokana na baa la njaa duniani wakati ambapo kuna sehemu nyingine za dunia wanakula na kusaza! Anajiunga na wale wanaoteswa na kudhulumiwa kutokana na imani, mawazo na rangi ya ngozi yao. Kristo Yesu anaendelea kujiunga na umati mkubwa wa vijana uliopoteza dira, mwelekeo na matumaini ya maisha kutokana na wanasiasa wanaowaongoza kuelemewa mno na uchoyo, ubinafsi, rushwa na ufisadi. Yesu anaendelea kuungana kwa njia ya Fumbo la Msalaba na waamini ambao wamepoteza imani yao kwa Mungu na Kanisa kutokana na kashfa na utepetevu wa imani unaoneshwa na mihimili ya Uinjilishaji. Yesu anayapokea yote haya kwa mikono miwili na kujitwika mabegani mwake pamoja na Misalaba ya wafuasi wake, tayari kuwaambia, jipeni moyo kwani yuko pamoja nao na kwamba, ameshinda dhambi na mauti na yuko kati yao ili kuweza kuwakirimia matumaini na maisha tele! Fumbo la Msalaba ni mwaliko kwa kila mwamini kuwa kama Simoni wa Kirene, aliyemsaidia Kristo Yesu kubeba Msalaba, Mtakatifu Veronica aliyeupangusa Uso wa Yesu, kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria na kwa wanawake wengine watakatifu, waliopiga moyo konde, wakaifuata ile Njia ya Msalaba; “Via Crucis”; Njia ya uchungu “Via Dolorosa” wakiwa wamesheheni upendo na huruma hadi chini ya Msalaba, wakiwa wamesheheni matumaini kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu.

Yohane wa Msalaba
14 December 2022, 14:34