Baba Mtakatifu Francisko anatambua na kuthamini kazi, muda na ujuzi unaotolewa na watu wa kujitolea sehemu mbalimbali za dunia. Nia za Jumla Mwezi Desemba 2022. Baba Mtakatifu Francisko anatambua na kuthamini kazi, muda na ujuzi unaotolewa na watu wa kujitolea sehemu mbalimbali za dunia. Nia za Jumla Mwezi Desemba 2022. 

Nia za Papa Francisko Kwa Mwezi Desemba 2022: Watu wa Kujitolea: Mashuhuda wa Huruma!

Baba Mtakatifu Francisko katika Nia zake za Jumla kwa Mwezi Desemba 2022, katika ujumbe wake kwa njia ya video, inayosambazwa na Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa, anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali na kuyaombea Mashirika ya Kujitolea Yasiyo na Faida, yanayoendelea kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka tarehe 5 Desemba, inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kujitolea, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa watu wote duniani kutambua mchango wa watu wanaojitolea na pia kujifunza kutoka kwao ili kila mtu atoe mchango wa kutengeneza mstakabali mwema kwa watu wote. Hii ni siku iliyoanzishwa na Umoja wa Mataifa katika Azimio lake la tarehe 1 Desemba 1985. Hii ni Siku ambayo Jumuiya ya Kimataifa inaheshimu watu wa kujitolea wanaoendelea kusadaka: muda, vipaji, uzoefu na mang’amuzi mbalimbali kama sehemu ya mchakato wa ujenzi jamii inayosimikwa kwenye usawa. Watu wa kujitolea kwa njia ya huduma yao inayosimikwa katika mshikamano wa upendo wa kidugu kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa ulimwengu unaokita mizizi yake katika haki, amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ni muhimu sana katika ulimwengu mamboleo. Huu ni utajiri na amana kwa binadamu wote na chachu ya watu kutajirishana na kushirikishana muda, vipaji, uzoefu na mang’amuzi. Hii ni nguvu ya ujenzi wa jamii, kielelezo makini cha upendo na ukarimu.

Watu wanaojitolea ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu
Watu wanaojitolea ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, kazi nyingi za kujitolea si rasmi kwani takribani asilimia 70% ya watu wanaojitolea wanafanya kazi katika jumuiya zao, ili kuwasaidia na kuwahudumia watu wanaowazunguka. Baba Mtakatifu Francisko anatambua na kuthamini kazi, muda na ujuzi unaotolewa na watu wa kujitolea sehemu mbalimbali za dunia. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika Nia zake za Jumla kwa Mwezi Desemba 2022, katika ujumbe wake kwa njia ya video, inayosambazwa na Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa, anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali na kuyaombea Mashirika ya Kujitolea Yasiyo na Faida, yanayoendelea kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, yatafute watu wa kujitolea na kujisadaka kwa ajili ya mafao ya wengi pamoja na kutafuta njia mpya za ushirikiano na mafungamano ya Kimataifa. Ulimwengu unawahitaji watu wanaoweza kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Watu wa kujitolea ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu
Watu wa kujitolea ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu

Hii ni huduma inayowafanya watu kujisikia kuwa huru na kuwajibika zaidi kwa watu pamoja watu wanaowahudumia. Huduma hii mara nyingi inaleta mafao makubwa, ikiwa kama watu wa kujitolea wanashirikiana barabara na wenyeji pamoja na Serikali husika, ili kupanga, kuratibu na kutekeleza utume wao kadiri ya vipaumbele. Mara nyingi anasema Baba Mtakatifu Francisko watu wa kujitolea hawana mtaji mkubwa wala vifaa vya kuweza kutosheleza utekelezaji wa majukumu yao, lakini, rasilimali kidogo iliyopo, watu hawa mara nyingi wanatenda miujiza kwa kuwatangaza na kushuhudia nguvu ya matumaini. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kushirikiana pamoja naye kwa ajili ya kuwaombea watu wa kujitolea pamoja na kuyaombea Mashirika ya Kujitolea Yasiyo na Faida, ili daima yaweze kupata watu ambao wako tayari kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi sanjari na kuendelea kutafuta njia mpya za ushirikiano na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa.

Nia Desemba 2022

 

19 December 2022, 14:43