Salini na kumwombea Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kwa sasa ni mgonjwa sana na yuko kitandani hawezi, ili katika mateso, sala na ukimya wake, aendelee kulitegemeza Kanisa. Salini na kumwombea Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kwa sasa ni mgonjwa sana na yuko kitandani hawezi, ili katika mateso, sala na ukimya wake, aendelee kulitegemeza Kanisa. 

Papa Francisko: Hali ya Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI Ni Tete Sana!

Papa Francisko: Salini kwa ajili ya Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI ambaye kwa sasa ni mgonjwa sana na yuko kitandani hawezi, ili katika mateso, sala na ukimya wake, aendelee kulitegemeza Kanisa. Waamini wamwombee ili Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, apate kumfariji na kumtegemeza katika ushuhuda wa upendo na uaminifu wake kwa Kanisa

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake Jumatano tarehe 28 Desemba 2022 kuhusu Sherehe ya Noeli, Mwaliko kwa waamini kutafakari pamoja na Wasalesian wa Don Bosco, Mama Kanisa anapoanza kuadhimisha Jubilei ya Miaka 400 tangu Mtakatifu Francisko wa Sales, Askofu, Mwalimu wa Kanisa na Msimamizi wa Waandishi wa Habari alipofariki dunia tarehe 28 Desemba 1622, amewaalika kwa namna ya pekee kabisa, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali na kumwombea Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI ambaye kwa sasa ni mgonjwa sana na yuko kitandani hawezi, ili katika mateso, sala na ukimya wake, aendelee kulitegemeza Kanisa. Waamini wamwombee ili Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, apate kumfariji na kumtegemeza katika ushuhuda wa upendo na uaminifu wake kwa Kanisa hadi mwisho. Tarehe 16 Aprili 2022, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI aliadhimisha Kumbukizi ya Miaka 95 tangu alipozaliwa. Tangu mwaka 2013 amekuwa akiishi kwenye Hosteli Mater Ecclesiae iliyoko ndani ya Bustani za Vatican. Haya ni maisha yanayosimikwa katika sala, tafakari ya Neno la Mungu, Muziki pamoja na kujisomea binafsi.

Hali ya Afya ya Papa Mstaafu Benedikto XVI ni tete kwa sasa
Hali ya Afya ya Papa Mstaafu Benedikto XVI ni tete kwa sasa

Itakumbukwa kwamba, Tarehe 1 Desemba 2022, Baba Mtakatifu Francisko alitoa tuzo kwa washindi wa mwaka 2022 kati yao ni: Padre Michel Fédou pamoja na Professa Joseph Halevi Horowitz Weiler. Utangulizi wa maadhimisho haya umetolewa na Padre Federico Lombardi, SJ., Rais wa Mfuko wa Joseph Ratzinger – Benedetto XVI, pamoja na Kardinali Gianfranco Ravasi, Rais wa Baraza la Kipapa la Utamaduni. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake ameelezea mchango wa Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika maisha na utume wa Kanisa hususan katika maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, Taalimungu; Mchango wa Padre Michel Fédou pamoja na Professa Joseph Halevi Horowitz Weiler.  Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kuanzia tarehe 11 Oktoba 1962 hadi mwaka 1965, yalipaniwa sana na Mtakatifu Yohane XXIII, ili kuhakikisha kwamba, unaadhimishwa, kama tukio la kihistoria kwa maisha na utume wa Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake. Huu ni Mtaguso endelevu ambao bado haujafahamika na wengi; kiasi cha kumwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa, changamoto kwa Mama Kanisa ni kusimama kidete, ili kuhakikisha kwamba, maamuzi ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican yanatekelezwa kikamilifu.

Papa Mstaafu Benedikto XVI tarehe 16 Aprili 2022 ameadhimisha Miaka 95 ya kuzaliwa
Papa Mstaafu Benedikto XVI tarehe 16 Aprili 2022 ameadhimisha Miaka 95 ya kuzaliwa

Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ni mchakato ambao umeliwezesha Kanisa kupyaisha maisha na utume wake, changamoto na mwaliko kwa watu wa Mungu nyakati hizi, kujizatiti kikamilifu katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Hili ni Kanisa linalosimikwa katika: Umoja, Ushiriki na Utume wa Kanisa kwa kukazia utamaduni wa kusikiliza, ushiriki mkamilifu wa watu wateule wa Mungu, lakini zaidi kwa kumsikiliza kikamilifu Roho Mtakatifu, ili kusoma alama za nyakati. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican pamoja na mambo mengine umekazia kuhusu: Taifa jipya la Mungu, Watu wa Mungu; Ukuhani wa watu wote; Hisia ya imani na karama katika taifa la Mungu “Sensus fidei.” Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alishiriki kikamilifu katika maadhimisho haya wakati wa ujana wake na akawa pia ni chimbuko la nyaraka mbalimbali za Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Mtakatifu Yohane Paulo II akautambua mchango wake na kumwalika kuja Vatican kufanya kazi begakwa bega na hatimaye, akachaguliwa kuwa Kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI amelisaidia sana Kanisa kusoma, kuzitafakari na hatimaye, kuzipyaisha Nyaraka za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Amekazia asili na utume wa Kanisa katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mungu katika ulimwengu mamboleo.

Papa Francisko amekuwa akimtembelea mara kwa mara
Papa Francisko amekuwa akimtembelea mara kwa mara

Machapisho ya kazi za Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI “Opera Omnia” yanayoendelea kutafsiriwa katika lugha mbalimbali ni msingi wa safari ya Kanisa katika mchakato wa kumwilisha ushirika, hii ndiyo dhana ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi linaoongozwa na la Roho Mtakatifu, wazi kwa ajili ya utume wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu na huduma ya upendo kwa walimwengu. Mfuko wa Joseph Ratzinger, Benedikto XVI, ulioanzishwa rasmi tarehe 1 Machi 2010 na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI umesaidia sana kuendelea kupyaisha mawazo na mchango wa Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika mchakato wa kujenga na kudumisha majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni hususan katika: Ikolojia fungamani, haki msingi za binadamu. Umefika wakati kwa Mifuko ya Yohane Paulo wa Kwanza na ule wa Mtakatifu Yohane Paulo II kushirikiana kwa pamoja, ili kujenga umoja kwa ajili ya Kanisa la Kristo Yesu. Padre Michel Fédou katika maisha na utume wake, amejipambanua sana kama Gwiji wa Taalimungu ya Kikristo, kwa kujikita katika masomo na tafiti za Mababa wa Kanisa kutoka Mashariki na Magharibi na ukuaji wa sayansi ya maisha ya Kristo Yesu katika historia. Amejielekeza zaidi katika ufahamu wa imani kwa kujielekeza zaidi katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, kidini na kitamaduni. Kwa hakika Padre Michel Fédou amechangia sana kukuza taalimungu ya Kanisa la Kifaransa, kwa kufuata mifano kama ile ya Padre Henri De Lubac ambaye ametoa mchango mkubwa katika taalimungu na matunda yake yameonekana katika maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Papa Mstaafu Benedikto XVI amechangia sana ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa
Papa Mstaafu Benedikto XVI amechangia sana ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, matunda haya yataendelea kuchanua zaidi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo Yesu, kwa kipindi kirefu zaidi. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Professa Joseph Halevi Horowitz Weiler. Ni mwamini wa dini ya Kiyahudi, ambaye amebahatika kutunukiwa tuzo hii, kutokana na juhudi zake zilizomwezesha kujikita katika maisha na utume wa Madhehebu mbalimbali ya Kikristo. Hii ni dhamana ambayo ameitekeleza katika hali na mazingira magumu, daima watu walimtilia shaka kuhusu ushiriki wake katika maisha na utume wa Madhehebu ya Kikristo. Kazi hii ni mchango mkubwa katika mchakato wa upatanisho kati ya Wakristo na waamini wa dini mbalimbali duniani, kuanzia kwenye Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Majadiliano na Wayahudi ni tema ambayo Baba Mtakatifu Francisko anasema, ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wake tangu hata akiwa Argentina, lengo ni kujenga na kudumisha majadiliano na urafiki wa kijamii. Professa Joseph Halevi Horowitz Weiler anakazia pamoja na mambo mengine majadiliano kati ya imani na uwezo wa mwanadamu kufikiri na kutenda; uhuru wa kidini na kuabudu katika ulimwengu ambao unataka kuuweka uhuru huu katika dhana ya mtu binafsi. Ameonesha umuhimu wa kufanya mang’amuzi ya kina ili kubainisha tunu msingi za maisha, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Waamini wa dini mbalimbali wanaweza kuungana kwa pamoja katika fadhila ya matumaini. Tuzo ya Mfuko wa Joseph Ratzinger, Benedikto XVI ni kutambua kazi kubwa iliyotendwa na wahusika katika masomo, maisha na utume wao; changamoto ni kuhakikisha kwamba, mchango huu unafahamika kwa wengi.

Papa Mstaafu B16

 

28 December 2022, 15:25