Papa Francisko Kesha la Noeli 2022: Ukaribu, Ufukara na Uhalisia
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi tarehe 24 Desemba 2022 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu Mkesha wa Noeli katika Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, amewaalika waamini kuongozwa na Maandiko Matakatifu ili waweze kutambua mahali alipo Mwenyezi Mungu, tayari kutekeleza mapenzi yake. Baba Mtakatifu anasema, Pango la Noeli ni mahali ambapo panaonesha alipozaliwa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu, alama hai ya Injili, mwaliko wa kutafakari Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu alipofanyika mwanadamu, ili kukutana na watu wote, ili kuwaonjesha upendo wake na hatimaye, waweze kuunganika pamoja naye. Pango la Noeli ni Ishara: Ukaribu wa Mungu, Ufukara na Uhalisia wa maisha na utume wa Kristo Yesu unaosimikwa katika huruma na mapendo ya dhati. Baba Mtakatifu anawaalika Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema kuzingatia maana halisi ya Sherehe za Noeli kwa kufuata Maandiko Matakatifu na kamwe wasipoteze dira na mwelekeo sahihi kwa kuigeuza Noeli kuwa na mwelekeo wa kibiashara zaidi. Hakuna mabadiliko makubwa ya muktadha wa kuzaliwa kwa Kristo Yesu zama zile na wakati wa sasa. Wahusika wakuu katika Sherehe ya Noeli ni Bikira Maria, Wachungaji waliokuwa wakikaa kondeni na Hori ya kulishia Wanyama, ishara wazi ya Ukaribu wa Mungu, Ufukara na Uhalisia wa maisha na utume wa Kristo Yesu. Hapa ni mahali ambapo Mwenyezi Mungu anazaliwa katika historia ya mwanadamu ili kupyaisha historia hii ni kuirejesha katika uhalisia wake.
Ukaribu huu wa Mungu ni mwaliko wa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Lengo ni kuhakikisha kwamba, sera na mbinu mkakati wa kisiasa zilenge kuwalinda watoto dhidi ya uchu wa mali na madaraka unaopelekea: vita, kinzani na ukosefu wa haki, usawa na amani duniani. Neno wa Mungu amezaliwa ulimwenguni ili kuwaonesha walimwengu mahali penye shida. Kristo Yesu anazaliwa kwenye Hori ya kulishia Wanyama, ili aweze kuwa ni chakula cha wasafiri; apate kuwalisha na kuwashibisha kwa chakula kilichoshuka kutoka mbinguni sanjari na kuwaonjesha huruma na upendo wake usiokuwa na kifani na kwamba, nguvu pekee inayoongoza historia ya mwanadamu, katika umaskini na unyenyekevu wa moyo na wala si sehemu ya utambulisho wake kwa kujinasibu kibabe na kutaka kujimwambafai. Kristo Yesu anazaliwa kwenye Hori ya kulishia Wanyama, kwani anataka kujisadaka na kujimega kama Mkate unaozima njaa na kiu ya haki; chakula kinachowahamasisha watu wa Mungu kusimama kidete dhidi ya umaskini wa hali na kipato.
Pango la Noeli ni mahali ambapo panaonesha alipozaliwa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu, huku akiwa amezungukwa na Bikira Maria, Mtakatifu Yosefu pamoja na wachungaji wa waliokuwa wanaishi kondeni, watu walionesha upendo wa dhati kwa Mtoto Yesu pasi na makuu, ni watu wa kawaida na maskini. Amana na utajiri mkubwa unaoibuliwa hapa ni mahusiano na mafungamano ya watu katika kifungo cha upendo na wala si uchu wa: fedha, mali na madaraka, chanzo kikuu cha kinzani na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Hii ni changamoto kwa waamini kujenga Kanisa maskini kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni mwaliko kwa Kanisa kuwa ni chachu ya mchakato wa mageuzi: kijamii, kiuchumi na kisiasa, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa ajili ya maskini, kwa kutokubali kumezwa na malimwengu. Hakuna Sherehe ya kweli ya Noeli ya Kristo Yesu pasi na maskini. Ufukara wa Mungu uwe ni chemchemi ya upendo usiokuwa na kifani miongoni mwa familia ya binadamu Baba Mtakatifu anakaza kusema Pango la Noeli panaonesha mahali alipozaliwa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu, kielelezo halisi cha uwepo wa Neno wa Mungu aliyefanyika mwili.
Kristo Yesu alizaliwa katika hali ya umaskini na hatimaye, akateswa na kufa katika hali ya umaskini nje ya mji wa Yerusalemu. Kristo Yesu ameishi ufukara hata kama hauzungumzia sana hali hii ya maisha katika utume wake, lakini aliwapenda watu wake, akawapenda upeo hadi kufa Msalabani. Huu ni mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanarutubisha imani yao katika ibada na matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo makini cha imani tendaji. Kristo Yesu ni ukweli wa huruma na upendo wa Mungu uliotundikwa Msalabani. Sherehe za Noeli iwe ni fursa kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha huruma na upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kuwamegea matumaini wale waliokata tamaa, wakavunjika na kupondeka moyo! Amana na utajiri wa kweli unamwilishwa katika huduma kwa watu wa Mungu na hasa maskini zaidi. Nia ya Ibada ya Misa Takatifu Kesha la Noeli kwa Mwaka 2022 imekuwa ni kwa ajili pia ya kuwakumbuka na kuwaombea watu wa mungu sehemu mbalimbali ambao wanaendelea kuathirika kutokana na vita. Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 umepata chanjo, lakini vita, migogoro na mipasuko ya kijamii, bado inaendelea kupekenya utu, heshima na haki msingi za binadamu. Watoto kutoka: Italia, India, Ufilippini, Mexico, San Salvador, Corea, DRC na Sudan ya Kusini walibeba mashada ya maua kwenda kupamba Pango la Mtoto Yesu. DRC na Sudan ya Kusini ni nchi ambazo, zinatarajiwa kutembelewa na Baba Mtakatifu Francisko mwanzo mwa Mwaka 2023.