Tafuta

Kauli mbiu “Shule ya Kikatoliki kama chombo cha matumaini ya kubadilisha ulimwengu. Tujenge Pamoja Kijiji cha Elimu." Kauli mbiu “Shule ya Kikatoliki kama chombo cha matumaini ya kubadilisha ulimwengu. Tujenge Pamoja Kijiji cha Elimu." 

Papa Francisko: Vigezo Vya Elimu Katoliki: Malezi na Makuzi: Kiroho na Kimwili

Kongamano la Elimu Katoliki Duniani lilifunguliwa huko Marsiglia nchini Ufaransa Kauli mbiu “Shule ya Kikatoliki kama chombo cha matumaini ya kubadilisha ulimwengu. Tujenge Pamoja Kijiji cha Elimu.” Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake amekazia kuhusu: Elimu ambayo kwa sasa ni changamoto pevu, mchango wa elimu Katoliki sanjari na tabia za mfumo wa elimu Katoliki.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa “Global Compact on Education” ulitiwa mkwaju hapo tarehe 15 Oktoba 2020. Baba Mtakatifu Francisko anakazia kuhusu: Janga la elimu duniani, maana ya elimu, umuhimu wa kupyaisha mfumo wa elimu na hatimaye, mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa katika maboresho ya mfumo wa elimu Kimataifa. Hii ni pamoja na kuragibisha utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; haki na amani; mafao ya wengi, ukarimu kwa wageni, wakimbizi na wahamiaji pamoja na ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Hii ni changamoto ambayo imeanza kuvaliwa njuga na viongozi wa kidini, shule, taasisi za elimu ya juu pamoja na vyuo vikuu. Kongamano la Elimu Katoliki Duniani lilifunguliwa huko Marsiglia nchini Ufaransa tarehe 1 Desemba na linahitimishwa tarehe 3 Desemba 2022 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Shule ya Kikatoliki kama chombo cha matumaini ya kubadilisha ulimwengu. Tujenge Pamoja Kijiji cha Elimu.” Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliomwandikia Philippe Richard, Katibu mkuu wa Ofisi ya Kimataifa ya Elimu Katoliki, (OIEC) amekazia kuhusu: Elimu ambayo kwa sasa ni changamoto pevu, mchango wa elimu Katoliki sanjari na tabia za mfumo wa elimu Katoliki. Elimu makini ni kati ya vipaumbele vinavyotolewa na Mama Kanisa kwa ajili ya malezi, makuzi na majiundo ya watoto na vijana wa kizazi kipya.

Utambulisho wa elimu katoliki ni malezi na majiundo ya mtu mzima
Utambulisho wa elimu katoliki ni malezi na majiundo ya mtu mzima

Elimu ni kati ya changamoto pevu katika ulimwengu mamboleo na kwa upande wa Kanisa huu ni ushiriki mkamilifu wa utume wa Mama Kanisa alioachiwa na Kristo Yesu na kwamba, huu ni wito wake wa asili kabisa. Shule za Kikatoliki hazi budi kuwafunda wanafunzi barabara katika utimilifu wao, kwa kuwasaidia kujifahamu jinsi walivyo, kwamba, ni watu wenye uwezo wa kupenda na kupendwa. Baba Mtakatifu anakaza kusema, si kazi wala wajibu wa shule za Kikatoliki, kuwaongoa watu kwa shuruti, bali iwe ni fursa ya ushiriki mkamilifu kutoka kwenye familia na jamii inayozizunguka shule hizi, ili kuragibisha na kuendeleza majadiliano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Haya ni majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni. Wadau wakuu wa shule za Kikatoliki, watambue kwamba, wanaitwa na kutumwa na Mama Kanisa kufundisha kama kielelezo cha utii na upendo, ili kila mtu kadiri ya uwezo na nafasi yake, aweze kushirikisha ujumbe wa matumaini unaopania kujenga na kudumisha ushirika kati ya wanajumuiya na Mwenyezi Mungu pamoja na Kanisa mahalia na Kanisa la Kiulimwengu.

Elimu ni kati ya changamoto pevu kwa sasa duniani.
Elimu ni kati ya changamoto pevu kwa sasa duniani.

Hii inatokana na ukweli kwamba, kama familia kubwa ya watu wa Mungu, wanatembea na kufanya kazi kwa pamoja kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Pili, Mama Kanisa daima yuko safarini na Kristo Yesu anawaita na kuwatuma wafuasi wake kwenda kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Kumbe shule za Kikatoliki hazina budi kuwa ni mahali pa watu kukutana bila ubaguzi, ili kuwapatia wanafunzi wote elimu bora itakayowasaidia kuboresha hali yao na kupambana na changamoto wanazokutana nazo katika safari ya maisha yao. Daima wakumbuke kwamba, wao ni vyombo vinavyotumiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kuwafunda watoto na vijana wa kizazi kipya. Wadau wa Elimu Katoliki wawe na ujasiri wa kumwomba Roho Mtakatifu ili aweze kuwakirimia karama na mapaji yake, ili hatimaye, waweze kutekeleza vyema wajibu wao. Roho Mtakatifu awaangazie katika shughuli na utume wao; awakirimie: elimu, sayansi na ujuzi, ili hatimaye, waweze kumfahamu, kumpenda, kumtumikia na mwisho waweze kufika juu mbinguni.

Papa Elimu Katoliki
02 December 2022, 15:31