Papa Francisko Kumbukizi ya Miaka 86 ya Kuzaliwa: Salam na Matashi Mema
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko alizaliwa tarehe 17 Desemba 1936 huko Flores, Buenos Aires, nchini Argentina. Mwaka 2022 anatimiza miaka 86 tangu alipozaliwa. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kitawa na Kikasisi, tarehe 13 Desemba 1969 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Kunako mwaka 1992 Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu na hatimaye, kuwekwa wakfu kuwa Askofu hapo tarehe 27 Juni 1992. Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu mkuu tarehe 22 Februari 1998 na hatimaye, kama Kardinali tarehe 21 Februari 2001. Tarehe 13 Machi 2013 akachaguliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro na kuanza utume wake rasmi tarehe 19 Machi 2013. Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, amejipambanua kuwa ni mtetezi wa haki na amani; kwa kuendelea kusimama kidete katika mchakato mzima wa uinjilishaji na utamadunisho kama sehemu ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi linalosimikwa katika majadiliano. Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na mapambano dhidi ya umaskini ili kulinda na kudumisha misingi ya: utu, heshima, haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa mambo yanayokita mizizi yake katika ukweli na uwazi, ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Ni katika muktadha huu, Baraza la Maaskofu Katoliki Austria katika hija yake ya kitume mjini Vatican inayoadhimishwa walau kila baada ya miaka mitano, limekuwa la kwanza kumtakia Baba Mtakatifu Francisko heri na baraka kwa Siku yake ya kuzaliwa, tarehe 17 Desemba 2022.
Kwa upande wake, Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI linasema, “Jinsi ilivyo mizuri juu ya milima Miguu yake aletaye habari njema, Yeye aitangazaye amani, Aletaye habari njema ya mambo mema, Yeye autangazaye wokovu, Auambiaye Sayuni, Mungu wako anamiliki! Isa 52:7. Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linasema, bado linayakumbuka machozi yaliyotiririka mashavuni kwake, mbele ya Sanamu ya Bikira Maria wakati wa Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, kwenye Uwanja wa Spagna mjini Roma tarehe 8 Desemba 2022 kutokana na madhara makubwa ya vita kati ya Urusi na Ukraine. Siku chache kabla ya kuadhimisha Sherehe ya Noeli, bado hakuna matumaini ya kuweza kusherehekea zawadi ya uhai kwani hakuna amani, furaha na utulivu wa ndani kutokana na utamaduni wa kifo kutawala! Watu wa Mungu nchini Italia, wanapenda kuungana na Baba Mtakatifu Francisko kuwalilia na kuwaombolezea wale wote wanaopoteza maisha kutoka na vita sehemu mbalimbali za dunia. Kwa hakika, Mwenyezi Mungu anakuja kuwafariji watu wake, kuwaganga na kuwafunga majeraha yao “Fadhili na kweli zimekutana, Haki na amani zimebusiana. Kweli imechipuka katika nchi, Haki imechungulia kutoka mbinguni. Naam, BWANA atatoa kilicho chema, Na nchi yetu itatoa mazao yake.” Zab 85: 10-12. Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linaomba ulinzi na tunza ya Bikira Maria kwa watu wa Mungu wanaoteseka kutokana na vita, ili waweze kuwa na matumaini, tayari kuanza kujielekeza zaidi katika njia ya upendo, umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu.
Kwa upande wake, Rais Sergio Mattarella wa Italia, kwa niaba ya watu wa Mungu nchini Italia katika ujumla wao, anamtakia Baba Mtakatifu Francisko heri, baraka na ustawi katika maisha na utume wake. Anasema, Mwaka 2022 umetikiswa sana na vita kati ya Urusi na Ukraine na madhara yake ni makubwa. Jumuiya ya Kimataifa imetafakari kwa kina mbinu za kuweza kusitisha vita hii inayoendelea kupandikiza utamaduni wa kifo bila mafanikio. Vita, kinzani na mipasuko ya kijamii inapelekea kusiginwa kwa: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kumbe, kuna haja ya kusimama kidete kupambana na ukosefu wa haki kwa kusimamia haki msingi za binadamu. Rais Sergio Mattarella anampongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuikumbusha Jumuiya ya Kimataifa madhara ya vita na umuhimu wa kusimamia misingi ya haki na amani. Bado mwangwi wa hotuba zake wakati wa hija za kitume ndani na nje ya Italia unaendelea kusikika katika akili na nyoyo za watu. Huu ni wito na mwaliko wa matumaini unaopaswa kujikita katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi; Upatanisho sanjari na Mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa ajili ya ustawi, maendeleo, mafao ya wengi, lakini hasa amani ya kudumu. Ni matumaini ya Rais Sergio Mattarella wa Italia kwamba, maadhimisho ya Sherehe ya Noeli yatasaidia kunogesha tunu msingi za kijamii zinazofumbatwa katika udugu wa kibinadamu. Mwishoni, amemtakia heri na baraka kwa kumbukizi ya Miaka 86 tangu alipozaliwa.