Siku ya 56 ya Kuombea Amani Duniani 2023: Kauli mbiu “Hakuna mtu anayeweza kujiokoa mwenyewe. Kupambana na UVIKO-19 na kwa pamoja kujielekeza kwenye njia za amani.” Siku ya 56 ya Kuombea Amani Duniani 2023: Kauli mbiu “Hakuna mtu anayeweza kujiokoa mwenyewe. Kupambana na UVIKO-19 na kwa pamoja kujielekeza kwenye njia za amani.”  

Siku ya 56 ya Kuombea Amani Duniani 1 Januari 2023: UVIKO-19

Siku ya 56 ya Kuombea Amani Duniani tarehe 1 Januri 2023 unanogeshwa na kauli mbiu “Hakuna mtu anayeweza kujiokoa mwenyewe. Kupambana na UVIKO-19 na kwa pamoja kujielekeza kwenye njia za amani.” Papa anagusia umuhimu wa kuwa makini kwa kujikita katika, haki na ukweli; madhara ya UVIKO-19; changamoto na mambo mazuri yaliyoibuliwa na UVIKO-19. Umoja!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ujumbe Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya Siku ya Kuombea Amani Duniani hutumwa kwa wakuu wa nchi na Jumuiya ya Kimataifa na pia ujumbe huu huonesha dira na mwelekeo wa utendaji wa shughuli za kidiplomasia zitakazotekelezwa na Vatican katika kipindi cha mwaka mzima. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya Siku ya 56 ya Kuombea Amani Duniani tarehe 1 Januri 2023 unanogeshwa na kauli mbiu “Hakuna mtu anayeweza kujiokoa mwenyewe. Kupambana na UVIKO-19 na kwa pamoja kujielekeza kwenye njia za amani.” Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe huu anagusia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kuwa makini kwa kujikita katika haki na ukweli; madhara yaliyosababishwa na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19; changamoto na mambo mazuri yaliyoibuliwa na UVIKO-19 na kwamba, walimwengu waendelee kujifunza kutokana na historia ya maisha ya mwanadamu. Ujumbe huu umewasilishwa kwenye vyombo vya mawasiliano ya jamii Ijumaa tarehe 16 Desemba 2022 na Kardinali Michael Czerny SJ, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu na Fungamani ya Binadamu, Sr. Alessandra Smerilli, F.M.A, Katibu mkuu pamoja na Dk. Maximo Torero, Mchumi mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO).

Kuna mamilioni ya watu wamefariki kwa UVIKO-19
Kuna mamilioni ya watu wamefariki kwa UVIKO-19

Kardinali Michael Czerny SJ, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu na Fungamani ya Binadamu, amekumbushia madhara makubwa yaliyosababishwa na maambukizi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, kiasi cha kuzua taharuki kati ya watu wa Mataifa, kwa kukosa habari sahihi na za kweli kuhusu UVIKO-19, Dawa za kupambana na kukinga gonjwa hili hatari na wala hapakuwepo na mbinu mkakati wa kuzuia maambukizi makubwa ya gonjwa hili. Tume ya UVIKO-19 ya Vatican, “Vatican COVID-19 Commission” ilianzishwa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 20 Machi 2020 na kuwekwa chini ya Baraza la Kipapa la Maendeleo Endelevu na Fungamani ya Binadamu kwa kushirikiana na Sekretarieti kuu ya Vatican. Lengo ni kuliwezesha Kanisa kujiandaa kikamilifu kukabiliana na changamoto zinazojitokeza kutokana na wimbi kubwa la maambukizi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Kipaumbele cha kwanza ni: Kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu na hasa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Tume ya UVIKO-19 ya Vatican: Haki Msingi za Binadamu
Tume ya UVIKO-19 ya Vatican: Haki Msingi za Binadamu

Tume imefanya upembuzi yakinifu na wakisayansi ili kuweza kutoa ushauri muafaka kwa Kanisa, kwa kuzingatia: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Msukumo wa pekee ni ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Utawala bora usaidie kukuza amani na usalama mambo msingi katika kukuza na kudumisha mshikamano wa udugu wa kibinadamu kitaifa na Kimataifa. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya 56 ya Kuombea Amani Duniani anawauliza waamini na watu wenye mapenzi mema kile ambacho Jumuya ya Kimataifa imejifunza kutokana na UVIKO-19, Yepi ambayo watu wanaweza kuendelea kujifunza kutokana na kipeo hiki cha afya duniani; Yepi ambayo yamekuwa ni alama za matumaini licha ya athari kubwa zilizojitokeza? Ni nini mwono wa binadamu na jamii kwa siku za usoni? Wakati wa amani na utulivu, Je, ni yepi ambayo watu wa Mungu wanaweza kujifunza kutokana na UVIKO-19. Baba Mtakatifu Francisko anawahamasisha watu wa Mungu kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu katika kupambana na changamoto mbalimbali zinazoendelea kujitokeza katika uso wa dunia.

Mshikamano wa Kimataifa dhidi ya UVIKO-19
Mshikamano wa Kimataifa dhidi ya UVIKO-19

Kwa upande wake, Sr. Alessandra Smerilli, F.M.A, Katibu mkuu wa Baraza amesema Tume ya UVIKO-19 ya Vatican, “Vatican COVID-19 Commission” iliyoanzishwa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 20 Machi 2020 inahitimisha utume wake mwishoni mwa mwaka 2022 na kuendelea kujikita katika majadiliano katika ukweli na uwazi; uhalisia wa maisha ya Makanisa mahalia pamoja na kushirikiana kwa karibu zaidi na Sekretarieti kuu ya Vatican. Baada ya Urusi kuivamia Ukraine kumeundwa “Kikosi Kazi cha Wakatoliki Kwa Ajili ya Ukraine, “Catholic Response For Ucraine, CR4U”. Lengo ni kuwasaidia na kuwahudumia waathirika wa vita kati ya Urusi na Ukraine.

Vita Kati ya Urusi na Ukraine vimechangia kuibuka kwa majanga duniani.
Vita Kati ya Urusi na Ukraine vimechangia kuibuka kwa majanga duniani.

Naye Dk. Maximo Torero, Mchumi mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) katika hotuba yake kwa njia ya video amegusia kuhusu vipeo mbalimbali vinavyoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo ikiwa ni pamoja na: kumong’onyoka kwa kanuni maadili na utu wema; mipasuko ya kisiasa na kijamii; athari za myumbo wa uchumi Kitaifa na Kimataifa; Athari za mabadiliko ya tabianchi; Vita, baa la njaa, umaskini na magonjwa, kiasi kwamba, idadi ya watu wanaosiginwa na baa la njaa imeongezeka kutoka milioni 828 katika kipindi cha mwaka 2021 hadi kufikia ongezeko la watu milioni 150 tangu mwaka 2019. Na zaidi ya watu milioni 670 wataendelea kukabiliwa na baa la njaa hadi kufikia mwaka 2030. Haya ni madhara ya ongezeko kubwa la kiwango cha umaskini duniani; Ukosefu wa usawa, vita na kinzani zinazoendelea kuibuka kila kukicha sehemu mbalimbali za dunia. Athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na vita kati ya Urusi na Ukraine, yamechangia sana kupanda kwa bei ya mazao ya chakula duniani. Zaidi ya dola za Kimarekani bilioni 25 zimeongezeka kwa ajili ya manunuzi ya chakula kutoka nje, kwa nchi 62 duniani, ikiwa ni sawa na asilimia 39% ikilinganishwa na mwaka 2020.

Baa la njaa linasigina utu na heshima ya watu wengi duniani
Baa la njaa linasigina utu na heshima ya watu wengi duniani

Maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 yamepelekea maafa makubwa katika nguvu kazi kwenye sekta ya kilimo, kiasi cha kutishia mafanikio ya Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu kufikia mwaka 2030. Kupanda kwa gharama ya pembejeo za kilimo kumepelekea mfumuko wa bei ya chakula duniani, changamoto kwa sasa ni kukuza na kudumisha umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo zinazoendelea kuibuliwa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia. Ushirikiano na mshikamano ni mambo yanayopewa kipaumbele cha kwanza na Baba Mtakatifu Francisko, sanjari na kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu, daima utawala wa sheria ukizingatiwa ili haki iweze kutendeka. Changamoto hii inakwenda sanjari na uhakika wa usalama wa chakula na lishe bora; pamoja na wananchi kuhakikisha kwamba wanapata mahitaji yao msingi kwa gharama nafuu. Amani ni jina jipya la maendeleo fungamani ya binadamu; uhakika na usalama wa chakula na lishe bora pamoja na huduma bora za afya ni mambo msingi katika kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo ulimwenguni. Changamoto mamboleo, ziwafunde wanadamu kuishi vyema, huku wakijitahidi kushirikiana na kushikamana kwa leo na kesho iliyo bora zaidi.

Amani Duniani 2023
16 December 2022, 14:44