Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu.  

Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu: Mwanga wa Huruma na Wokovu

Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinatangazwa tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kushikamana. Maisha ya ndoa na familia ni wito kwa waamini wengi ndani ya Kanisa. Yataka moyo kwa mwamini kuamua kufunga ndoa na kuwa tayari kupata watoto.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii kama sehemu ya maadhimisho ya Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, tarehe 30 Desemba 2022 anasema kwamba, “Iesus infans cum Matre sua Maria et sancto Ioseph humanam familiam et singulas familias misericordiae salutisque luce collustrant. Quae nos suscitat, ut humanum calorem praebeamus familiis in difficultatibus versantibus.” Yaani “Mtoto Yesu pamoja na Mama yake Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu wanaiangazia familia ya binadamu na kila familia kwa mwanga wa huruma na wokovu. Na hivyo kuzichochea ili kutoa joto la kibinadamu kwa familia zinazokabiliana na shida.” Mama Kanisa anaendelea kuwekeza katika maisha na utume wa familia, ili kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima; ukuu na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia, tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya familia inayojikita katika: Uhai, huruma na mapendo. Familia za Kikristo hazina budi kusimama kidete kulinda na kutetea tunu msingi za maisha ya ndoa na familia dhidi ya vikwazo na kinzani zinazojitokeza katika maisha na utume wa familia katika ulimwengu mamboleo.

Yataka moyo wa uvumilivu na upendo kuadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya Ndoa
Yataka moyo wa uvumilivu na upendo kuadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya Ndoa

Ikumbukwe kwamba, familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinatangazwa, zinashuhudiwa na zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kushikamana kama ndugu wamoja. Maisha ya ndoa na familia ni wito kwa waamini wengi ndani ya Kanisa. Yataka moyo kwa mwamini kuamua kufunga ndoa na kuwa tayari kupata watoto. Huu ni wito na jibu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kumbe, kuna haja ya kuendelea kuwapatia wanandoa katekesi endelevu. Huu ndio mwelekeo wa pekee uliotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, changamoto inayofanyiwa kazi kwa namna ya pekee na Baba Mtakatifu Francisko, ili kweli familia ziweze kuwa ni mashuhuda wa Injili ya familia, kielelezo cha ukomavu wa imani. Kanisa linatambua kwamba, ndoa inaundwa na mahusiano thabiti kati ya bwana na bibi na wala hakuna mkanganyiko na mifumo mingine ya maisha inayopendekezwa na baadhi ya serikali kwa kutaka kuhalalisha hata ndoa za watu wa jinsia moja, kielelezo chakumong’onyoka, kukengeuka na watu kutaka kumezwa na utamaduni wa kifo!

Waamini simameni kidete kutangaza na kushuhudia utakatifu wa familia
Waamini simameni kidete kutangaza na kushuhudia utakatifu wa familia

Waraka wa Kitume wa Mtakatifu Yohane Paulo II, “Injili ya uhai” “Evangelium vitae” unaendelea kuwa ni hazina muhimu sana katika kukuza na kudumisha Injili ya uhai inayofumbatwa na kushuhudiwa katika Injili ya familia dhidi ya utamaduni wa kifo. Baraza la Kipapa la familia, tangu kuanzishwa kwake, limekuwa mstari wa mbele kulinda, kutetea na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ili kweli familia ziweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba, kifo laini na ndoa za watu wa jinsia moja, ni kati ya changamoto ambazo zimefanyiwa kazi na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha, ili kutangaza na kushuhudia ukuu, uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu wote. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa kuendelea kuwasha moto wa Injili ya familia katika maisha na utume wa Kanisa kwa kutambua kwamba, leo hii familia ni kati ya taasisi zinazokabiliwa na matatizo pamoja na changamoto nyingi sehemu mbalimbali za dunia.

Jamii inawajibu wa kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya kifo
Jamii inawajibu wa kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya kifo

Wanafamilia wasimame kidete kulinda, kutetea na kushuhudia Injili ya familia na kamwe wasikubali kuyumbishwa na mitandao ya kijamii na baadhi ya wanasiasa wanaotaka kufaidika kutokana na myumbo wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ili kujijenga kisiasa na kiuchumi. Mama Kanisa anaendelea kuwahimiza wanafamilia kumwilisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku katika ukweli na uwazi; unyofu na upole wa moyo. Lengo ni kuwawezesha wanafamilia kuendeleza hija ya maisha ya ndoa na familia huku wakiwa wameshikamana na kufungamana kwa dhati licha ya kutambua matatizo na changamoto zinazowakabili baadhi ya wanafamilia. Kuna maendeleo makubwa ya dhana ya familia kama ilivyoibuliwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kwa kukazia kanuni maadili inayofumbata sheria. Leo hii kuna hatua moja mbele, yaani kanuni maadili inayofumbata sheria na maadili ya binadamu.

Familia ni msingi na chimbuko la miito yote ndani ya Kanisa
Familia ni msingi na chimbuko la miito yote ndani ya Kanisa

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika viongozi wa Kanisa kuhakikisha kwamba, wanawasaidia wanandoa wanaogelea katika shida na mahangaiko mbalimbali ya maisha, ili kuonja upendo na huruma ya Mungu inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kanisa lioneshe ukaribu na watu hawa wanaoteseka: kwa kuwafahamu; kuwapokea na kuwasindikiza kwa huruma na upendo wa Mungu. Lengo ni kuwawezesha wanandoa kumwilisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, tayari kushuhudia Injili ya familia; ili kwa kushirikiana na watu wote wa Mungu, waweze kujikita zaidi na zaidi katika mchakato wa Uinjilishaji mpya unaofumbatwa kwa namna ya pekee katika ushuhuda wa maisha, kielelezo cha imani tendaji.

Familia Takatifu
30 December 2022, 17:19