Tafuta

Baraza la Kipapa la Huduma ya Upendo “Elemosineria Apostolica”, kwa mara ya kwanza limeanzisha na kutoa Tuzo ya Mama Theresa wa Calcutta kwa mashuhuda wa Injili ya upendo kwa maskini. Baraza la Kipapa la Huduma ya Upendo “Elemosineria Apostolica”, kwa mara ya kwanza limeanzisha na kutoa Tuzo ya Mama Theresa wa Calcutta kwa mashuhuda wa Injili ya upendo kwa maskini. 

Tuzo ya Mama Theresa wa Calcutta: Miaka 25 ya Kifo: Maskini, Sala na Huduma ya Upendo

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 17 Desemba 2022, kwa mara ya kwanza amatoa Tuzo ya Mama Theresa wa Calcutta kwa: Padre Hanna Jallouf, Bwana Gian Piero na kwa Bw. Silvano Pedrollo. Kielelezo cha ushuhuda wa Mama Theresa wa Calcutta aliyefungua dirisha Mwenyezi Mungu akachungulia kwa furaha, akawafariji na kuwarejea waja wake utu, heshima na haki zao msingi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Theresa wa Calcutta, mwanzoni alijulikana kama “Anjezë Gonxhe Bojaxhiu” au “Agnes Gonxha Bojaxhiu” alizaliwa tarehe 26 Agosti 1910 huko Skopje, Macedonia na wazazi wake walikuwa wanatoka Albania. Akiwa na umri wa miaka 18 akajiunga na Shirika la Watawa wa Bikira Maria wa Loreto. Kunako mwaka 1928 akatumwa kwenda Ireland na baada ya mwaka mmoja akatumwa nchini India. Kunako mwaka 1931 akaweka nadhiri zake za kwanza na kupewa jina la Sr. Maria Theresa wa Mtoto Yesu. Kwa muda wa miaka 20 akafundisha historia na jiografia huko Calcutta na huko akakutana na watu ambao utu, heshima na haki zao msingi zilikuwa zimesiginwa na umaskini wa hali na kipato. Tarehe 10 Septemba 1946 akiwa njiani kuelekea mjini Darjeeling akasikia sauti ikimwambia ndani mwake “nina kiu” na hivyo akayakumbuka maneno ya Yesu pale Msalabani! Haya ni maneno ambayo yataendelea kuandikwa kwenye nyumba zote zilizoanzishwa na Mama Theresa wa Calcutta, kama muasisi wa Shirika la Wamisionari wa Upendo na kwamba, huduma ya upendo ni utambulisho na karama yao! Tarehe 16 Agosti 1948 akaondoka kutoka katika Shirika la Bikira Maria wa Loreto, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maskini na watu waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii.

Mashuhuda wa huruma na mapendo kwa Mungu na jirani
Mashuhuda wa huruma na mapendo kwa Mungu na jirani

Kunako mwaka 1949 akaungana na baadhi ya wanafunzi wake kuanzisha Shirika Jipya la kitawa kwa ajili ya kuwahudumia maskini kati ya maskini pamoja na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii, huku akijitahidi kufuata na kuiga mfano wa Mtakatifu Francisko wa Assisi. Tarehe 7 Oktoba 1950 Shirika lake likatambuliwa rasmi na Kanisa mahalia, wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Rozari Takatifu, muhtasari wa historia ya ukombozi. Mama Theresa wa Calcutta akaliweka Shirika lake chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Rozari Takatifu sanjari na Moyo Safi wa Bikira Maria. Licha ya nadhiri ya usafi wa moyo, ufukara na utii, watawa wa Mama Theresa wa Calcutta wanaweka pia nadhiri ya huduma kwa maskini zaidi. Kunako mwaka 1952 Mama Theresa wa Calcutta akafungua nyumba kwa ajili ya watu waliokuwa kufani na hatimaye, huduma hii ikapanuka kwa ajili ya wagonjwa na watoto yatima. Kunako mwaka 1965 Mtakatifu Paulo VI akalipatia Shirika la Wamisionari wa Upendo hadhi na haki za Kipapa. Mwaka 1981 tawi la tafakari likaanzishwa kwa ajili ya Mapadre wa Jimbo, huku wakiwa na Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu. Sifa, unyenyekevu na huduma makini ya Mama Theresa wa Calcutta ikaenea kwa kasi sehemu mbalimbali za dunia.

Mama Theresa wa Calcutta ni mfano wa Msamaria mwema.
Mama Theresa wa Calcutta ni mfano wa Msamaria mwema.

Kunako mwaka 1979 akatunukiwa Tuzo ya Amani Duniani kwa kutambua mchango wake katika mapambano dhidi ya umaskini na hali ngumu ya maisha. Kutokana na utume wake kwa maskini, akajenga urafiki wa karibu sana na Mtakatifu Yohane Paulo II, kiasi cha kumwezesha kufungua nyumba tatu mjini Roma. Tarehe 5 Septemba 1997 Mama Theresa wa Calcutta akiwa na umri wa miaka 87 akafariki dunia na kuzikwa tarehe 13 Septemba 1997 kwenye Nyumba mama ya Shirika. Mwezi Julai 1999 mchakato wa kumtangaza kuwa Mwenyeheri ukaanza rasmi kwa ridhaa ya Mtakatifu Yohane Paulo II. Tarehe 19 Oktoba 2003 atakatangazwa kuwa Mwenyeheri na mfano wa Msamaria mwema, aliyethubutu kumwilisha tunu msingi za Injili katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani. Akajitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya wagonjwa, maskini na watoto yatima; huduma iliyorutubishwa kwa sala na tafakari ya Neno la Mungu sanjari na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu. Tarehe 17 Desemba 2015 Baba Mtakatifu Francisko akatambua muujiza uliotendwa kwa maombezi ya Mama Theresa wa Calcutta na huo ukawa ni mwanzo wa mchakato wa kumtangaza kuwa Mtakatifu. Mama Theresa wa Calcutta ni shuhuda na chombo cha huruma na upendo wa Mungu kwa maskini, tarehe 4 Septemba 2016 akatangazwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Mtakatifu.

Mama Theresa ameacha amana na utajiri mwingi
Mama Theresa ameacha amana na utajiri mwingi

Miaka 25 imegota tangu Mama Theresa wa Calcutta alipofariki dunia. Ni katika muktadha wa kumbukumbu ya Miaka 86 tangu Baba Mtakatifu Francisko alipozaliwa, Baba wa maskini, mtetezi wa amani na mpenda mazingira bora, Baraza la Kipapa la Huduma ya Upendo “Elemosineria Apostolica”, kwa mara ya kwanza limeanzisha na kutoa Tuzo ya Mama Theresa wa Calcutta. Hii ni tuzo ambayo imetolewa kwa watu ambao wamejipambanua katika huduma kwa maskini kati ya maskini zaidi. Hawa ni Padre Hanna Jallouf, Mfranciskani ambaye ameendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa maskini na waathirika wa vita nchini Siria. Bwana Gian Piero, maarufu kama Wuè, maskini kati ya maskini wa Roma, anayetumia msaada anaoupata kila siku kutoka kwa Wasamaria wema kwa ajili ya kuwahudumia maskini zaidi. Na hatimaye ni Mfanyabiashara Silvano Pedrollo kutoka mjini Verona ambaye anatumia sehemu kubwa ya mapato yake kwa ajili ya huduma kwa maskini, ili kuhakikisha kwamba, walau baadhi ya watu kutoka Afrika, India na Amerika ya Kusini wanapata mahitaji yao msingi; kwa kuwekeza katika ujenzi wa shule ili watoto waweze kupata elimu bora zaidi; uchimbaji wa visima kwa ajili ya maji safi na salama pamoja na ujenzi wa hospitali na zahanati kama sehemu ya mchakato wa maboresho ya huduma ya afya. Kwa hakika Mama Theresa wa Calcutta ni shuhuda na chombo cha huruma na upendo wa Mungu kwa maskini na katika maisha na utume wake, ameacha amana na urithi mkubwa kwa kuwathamini maskini kati ya maskini zaidi.

Maisha ya sala, tafakari, Neno la Mungu na Ekaristi
Maisha ya sala, tafakari, Neno la Mungu na Ekaristi

Shirika la Wamisionari wa Upendo lina zaidi ya watawa 6, 000 wanaowahudumia maskini zaidi katika nyumba 762 katika Mataifa 139! Kwa hakika huu ni muujiza wa aina yake, wakati ambapo baadhi ya Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, yanateseka kwa ukame wa miito sehemu mbalimbali za dunia. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 17 Desemba 2022 katika maadhimisho ya kumbukizi ya miaka 86 tangu alipozaliwa, kwa mara ya kwanza amatoa Tuzo ya Mama Theresa wa Calcutta kwa: Padre Hanna Jallouf, Bwana Gian Piero na kwa Mfanyabiashara Silvano Pedrollo. Kielelezo cha ushuhuda wa Mama Theresa wa Calcutta aliyefungua dirisha kama alivyowahi kusema Mtakatifu Yohane Paulo II, Mwenyezi Mungu akachungulia kwa furaha, akawafariji na kuwarejeshea waja wake utu, heshima na haki zao msingi. Huu ni mwaliko kwa kila mwamini kuwa ni dirisha la Mungu ambalo daima liko wazi kwa ajili kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma na mapendo kwa maskini na wote wanaosukumiziwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru wale wote waliotunukiwa Tuzo ya Mama Theresa wa Calcutta pamoja na wale wote waliohudhuria tukio hili adhimu linalosheheni ujumbe wa: Umaskini, ujirani mwema, udugu wa kibinadamu pamoja na sala, amana, utajiri na urithi mkubwa kutoka kwa Mama Theresa wa Calcutta. Baba Mtakatifu anawahimiza waamini kujenga utamaduni wa sala kwani ni kwa njia ya sala, Mama Theresa wa Calcutta aliweza kuvuka vizingiti na dhoruba za maisha ya kiroho. Baba Mtakatifu anamwomba Mama Theresa wa Calcutta huko mbinguni aliko, awaombee na kuwasaidia waamini kuweza kuuishi ufukara katika hali ya kawaida pasi na makuu, daima ukisindikizwa na maisha ya sala, tayari kuwasaidia jirani wenye mahitaji zaidi. Wito wa Mkristo unasimikwa katika ujirani mwema, matendo ya huruma na maisha ya sala.

Tuzo Mama Theresa
17 December 2022, 15:50