Siku ya Kimataifa ya Watu Wenye Ulemavu Duniani inaadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 3 Desemba Siku ya Kimataifa ya Watu Wenye Ulemavu Duniani inaadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 3 Desemba  

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko Kwa Walemavu 2022

Siku ya Walemavu Duniani: Ni hamasa ya kushuhudia upendo na huruma ya Mungu; kuendelea kuwa na imani kwa Mungu, kiini halisi cha Mamlaka fundishi ya Kanisa kuhusu udhaifu wa mwanadamu, karama ambayo walemevu wanaishirikisha kwa Kanisa kwa uwepo wao, mwaliko ni kutembea pamoja kama sehemu ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi linalosimikwa katika umoja!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Siku ya Kimataifa ya Watu Wenye Ulemavu Duniani inaadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 3 Desemba na kwa mwaka huu 2022 kauli mbiu ambayo imenogesha maadhimisho haya ni: "Suluhisho la Mabadiliko kwa Maendeleo Jumuishi: Nafasi ya Ubunifu katika Kuchagiza Dunia fikivu yenye Usawa.” Siku hii ilianzishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kunako mwaka 1992 na azimio la 47/3. Lengo kuu ni kukuza uelewa wa masuala ya ulemavu na kuhamasisha uungwaji mkono kwa ajili ya utu, heshima, haki, ustawi, mafao na maendeleo wa watu wenye ulemavu. Pia inalenga kuongeza ufahamu wa mafanikio yatakayopatikana kutokana na ushirikiano wa watu wenye ulemavu katika medani mbalimbali za maisha hususan katika masuala ya: kisiasa, kijamii, kiuchumi na kiutamaduni. Ujumbe wa Baba Mtakatifu kwa Walemevu mintarafu Mamlaka fundishi ya Kanisa yaani “Magisterium” kuhusu ulemavu anasema: Ni hamasa ya kutangaza na kushuhudia upendo na huruma ya Mungu; kuendelea kuwa na imani kwa Mwenyezi Mungu, kiini halisi cha Mamlaka fundishi ya Kanisa kuhusu udhaifu wa mwanadamu, karama ambayo walemevu wanaishirikisha kwa Kanisa kwa uwepo wao, mwaliko na changamoto ya kutembea pamoja kama sehemu ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi linalosimikwa katika umoja, ushiriki na utume wa Kanisa.

Ni wakati wa kujenga na kudumisha upendo na mshikamano
Ni wakati wa kujenga na kudumisha upendo na mshikamano

Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, maisha ya mwanadamu ni ya thamani kubwa, lakini hazina hii inahifadhiwa katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu na wala si kutoka kwa mwanadamu. Rej. 2Kor 4:7. Siku ya Kimataifa ya Watu Wenye Ulemavu Duniani ni wakati muafaka wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa kutoa fursa kwa watu wengine pia kuweza kuwainjilisha, kwa kutumia mbinu mbalimbali ili kuhakikisha kwamba, Kristo Yesu anafika na kugusa medani mbalimbali za maisha yao kama waamini. Huu ni ushuhuda wa wazi wa upendo unaookoa, licha ya kasoro za kibinadamu, bado anaonesha ukaribu na ujirani kwa Neno na nguvu yake anayapata maisha ya waja wake maana bora zaidi. Katika moyo wako unatambua kwamba kuna kitu ambacho kilikusaidia nkuishi na kukupa matumaini, ndicho unachohitaji pia kusilisha kwa wengine. Udhaifu na mapungufu ya kibinadamu iwe ni nyenzo msingi katika kutangaza na kushuhudia imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, huu ni utume na dhamana kwa kila mwamini aliyeguswa na kuonja urafiki na Kristo Yesu.

Maisha ya mwanadamu yamehifadhiwa kwenye chombo cha udongo
Maisha ya mwanadamu yamehifadhiwa kwenye chombo cha udongo

Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kujenga imani, uzoefu na mang’amuzi ya huruma na upendo wa Mungu katika maisha ya mwanadamu. Huruma na upendo wa Mungu ni changamoto kwa waamini kushirikishana na kushikamana na watu wote wa Mungu bila ubaguzi. Kwa huruma yake kuu, Mwenyezi Mungu aliamua kushirikiana na kushikamana na binadamu hata katika udhaifu wake, mang’amuzi ambayo yanamwondoa mwaamini kutoka katika ulimwengu wa kufikirika, ombwe na hali ya manung’uniko, tayari kujiaminisha na kuzama katika nguvu ya Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Kristo Yesu alionja udhaifu na ukatili wa hali ya juu kabisa wa mwanadamu. Hiki ni kiini halisi cha Mamlaka fundishi ya Kanisa kuhusu udhaifu wa mwanadamu. Na ikiwa kama watu wenye ulemavu wangesikilizwa kwa makini, wangesaidia sana mchakato wa ujenzi wa jamii zinazokita mizizi yake katika ut una udugu wa kibinadamu, kwa kushirikishana mema ya nchi na jirani. Hali hii ingesaidia kuvunjilia mbali kuta za utengano, kwa kukuza na kuimarisha mahusiano na mafungamano ya kijamii, hali ambayo kimsingi ingesaidia pia ujenzi wa amani duniani.

Walemavu wanaoishi katika maeneo ya vita wamo hatarini zaidi
Walemavu wanaoishi katika maeneo ya vita wamo hatarini zaidi

Baba Mtakatifu anawakumbuka na kuwaombea walemavu ambao wako kwenye maeneo ya vita na kwamba hawana uwezo wa kukimbia ili kusalimisha maisha yao na matokeo yake, hatima na usalama wa maisha yao yako mikononi mwa misaa ya kimataifa. Mamlaka fundishi ya Kanisa yaani “Magisterium” kuhusu ulemavu na udhaifu wa waamini yanakazia umuhimu kwa walemavu kuchangia katika amana na utajiri wa Kanisa, kwa uwapo wao na kwa kusikilizwa kwa umakini mkubwa, kama sehemu ya ushiriki wao katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Walemavu ni watu wanaopaswa kushirikisha kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa; kwa kusikilizwa; kwa kutambua na kuheshimu utu na haki zao msingi; kwa kushiriki vyema kupokea Sakramenti za Kanisa. Hawa ni watu wanaopaswa kuokolewa kutoka katika vitendo vya dhulumuana nyanyaso na kwamba, maisha yao yanathamani kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.

Watu wenye ulemavu wanapaswa kushiriki katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi
Watu wenye ulemavu wanapaswa kushiriki katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi

Huu ni wakati wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi kwa kutembea bega kwa bega; kwa kusikilizana; kwa kushirikiana kama wamoja, bila utengeno; kwani utu na heshima ni sehemu ya Fumbo la Umwilisho, kiasi kwamba, kila mwamini kwa njia ya Ubatizo, anaitwa na kutumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa! Kwa hakika watu wenye ulemavu wanapaswa kushiriki kikamilifu maisha na utume wao kama wabatizwa; kwa kuwapokea na kuwashirikisha kikamilifu. Baba Mtakatifu anawataka watu wenye ulemavu kuwa makini, kwani kila siku ya maisha yao, wanauendea uzee, mwaliko kwa watu wa Mungu kuwa makini katika mchakato wa safari ya maisha ya hapa duniani kwani “kwa hakika ukichezea ujana, fainali, utaikuta uzeeni.” Ni wakati wa kuyaangalia mambo yeota haya kwa “jicho jipya”, lakini utu na heshima yao kama watoto wa Mungu inabaki pale pale. Mwenyezi Mungu anawajali na kuwapenda wote katika huruma yake ya kibaba.

Ujumbe Kwa Walemavu 2022

 

 

20 December 2022, 16:48