Wanadiplomasia na Ujenzi wa Haki, Amani na Maridhiano
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Balozi Georgios F. Poulides, Dekano wa Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican yapatayo 183 kutoka Cyprus katika hotuba kwa Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya salam na matashi mema kwa Mwaka mpya wa 2023 amewasilisha salam rambirambi kwa Baba Mtakatifu Francisko kufuatia kifo cha Baba Mtakatifu Benedikto XVI kilichotokea tarehe 31 Desemba 2022 na kuzikwa tarehe 5 Januari 2023. Madhara makubwa ya UVIKO-19, Sala ya Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili tarehe 8 Desemba 2022; umuhimu wa kutafuta na kudumisha amani duniani pamoja na changamoto zake; Hija za Kitume zilizofanywa na Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwaka 2022 huko Malta na Canada pamoja na umuhimu wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni pamoja na matashi mema kwa Baba Mtakatifu katika hija yake ya kitume nchini DRC na Sudan ya Kusini. Balozi Georgios F. Poulides, Dekano wa Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican, tarehe 9 Januari 2023 amewasilisha salam za rambirambi kutoka kwa Mabalozi na wawakilishi wa Shirika ya Kimataifa kwa Baba Mtakatifu Francisko kufuatia kifo cha Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, kiongozi aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo Yesu. Katika maisha na utume wake, alibahatika kufanya hija za kitume 24 sehemu mbalimbali za dunia, ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo.
Jumuiya ya Kimataifa inakumbuka madhara yaliyosababishwa na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 na Vita kati ya Urusi na Ukraine inayoendelea kusababisha maafa makubwa kwa wat una mali zao. Kumbe, kuna haja ya kusali kwa ajili ya kuombea amani na viongozi wenyewe kuendelea kujikita katika mchakato wa hija ya amani. Balozi Georgios F. Poulides anakumbuka Sala ya Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili tarehe 8 Desemba 2022 kwenye Uwanja wa Spagna, alipotoa machozi kwa uchungu, ili Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili ili awaombee, amani iweze kutawala katika nyoyo za watu dhidi ya chuki na uhasama; ukweli na msamaha viweze kung’ara dhidi ya uwongo na uchochezi; msamaha dhidi ya mashambulizi; amani ya kweli dhidi ya vita. Haya ni maneno ambayo yameitia yanaendelea kuihamasisha Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika ujenzi wa utamaduni wa kusikilizana na kujadiliana; kuwakubali na kuwapokea wengine jinsi walivyo; kujikita katika ujenzi wa utamaduni amani dhidi ya vita. Ujumbe wa Siku ya 56 ya Kuombea Amani Duniani ulinogeshwa na kauli mbiu “Hakuna mtu anayeweza kujiokoa mwenyewe. Kupambana na UVIKO-19 na kwa pamoja kujielekeza kwenye njia za amani.”
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe huu anagusia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kuwa makini kwa kujikita katika haki na ukweli; madhara yaliyosababishwa na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19; changamoto na mambo mazuri yaliyoibuliwa na UVIKO-19 na kwamba, walimwengu waendelee kujifunza kutokana na historia ya maisha ya mwanadamu. Mtakatifu Paulo katika Waraka wake wa kwanza kwa Wathesalonike anasema “Lakini, ndugu, kwa habari ya nyakati na majira, hamna haja niwaandikie. Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku.” 1The 5:1-2. Baba Mtakatifu Francisko anasema, huu ni mwaliko kwa waamini kuwa na matumaini pamoja na kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu anayewaongoza kwa huruma na mapendo; wakianguka, anawainua na kuwaelekeza katika njia salama, licha ya matukio ya ukosefu wa haki, mateso na mahangaiko mbalimbali. Huu ni wakati wa kuamka kutoka usingizini, ili kuondokana na woga, majonzi na hali ya kujikatia tamaa na badala yake, wainue macho yao kwa mng’ao wa mwanga hata katika giza nene! Baba Mtakatifu amekazia hasa umuhimu wa kujenga diplomasia inayosimikwa katika mshikamano wa upendo, uwajibikaji wa pamoja; toba na wongofu wa ndani; mshikamano wa udugu na upendo wa kibinafamu; kwa kukazia umoja unaofumbatwa hata katika tofauti msingi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.
Balozi Georgios F. Poulides anampongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yanayonogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Lengo kuu la Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu ni kuliwezesha Kanisa kuendelea kujizatiti katika ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza na kuwashirikisha waamini walei katika maisha na utume wake. Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu yanapania pia kujenga na kudumisha urika wa Maaskofu, tayari kumsikiliza Roho Mtakatifu, Mhimili mkuu wa mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha. Huu ni utamaduni wa watu wa Mungu kusikilizana kwa makini! Ni kusikiliza Neno la Mungu, ili kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha katika uhalisia na vipaumbele vya maisha ya waamini. Kusikiliza ni kujenga utamaduni wa kusali pamoja na Neno la Mungu, “Lectio Divina.” Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yamegawanywa sasa katika awamu kuu mbili. Awamu ya kwanza ni kuanzia tarehe 1-29 Oktoba 2023 na Awamu ya Pili itaadhimishwa Mwezi Oktoba 2024. Lengo ni kuendelea kufanya mang’amuzi ya kina kuhusu dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, chombo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa katika mchakato wa watu wa Mungu katika ujumla wao kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili. Mwishoni, anatakia heri na baraka katika Hija ya Kitume nchini DRC kuanzia tarehe 31 Januari 3 Februari na Sudan ya Kusini ni kuanzia tarehe 3 Februari hadi tarehe 5. Baba Mtakatifu anatembelea huko kama hujaji wa amani na upatanisho.