Tafuta

Waamini wanahimizwa kulisoma, kulitafakari, kulisali na kuendelea kulijifunza Neno la Mungu katika maisha yao. Waamini wanahimizwa kulisoma, kulitafakari, kulisali na kuendelea kulijifunza Neno la Mungu katika maisha yao.  (Vatican Media)

Dominika ya IV ya Neno la Mungu: Jengeni Utamaduni wa Kusoma na Kutafakari Neno la Mungu

Waamini kama wafuasi na Mitume wa Kristo Yesu wanao upendeleo, dhamana na wajibu wa kulisoma, kulitafakari na kulimwilisha Neno la Mungu. Ile hamu ya waamini kutaka kupata furaha ya kweli katika maisha yao kama mtu binafsi, familia na jamii katika ujumla wake, wataipata kwa kujichimbia katika hekima na busara ya Kimungu, chemchemi ya: upendo, amani na udugu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Waamini wanahimizwa kugundua uzuri wa Maandiko Matakatifu, ambayo kimsingi ni Neno la Mungu yaani ni Mungu mwenyewe anayezungumza na waja wake, kwa njia ya Biblia, Neno la Mungu. Huu ni mwaliko wa kulisoma, kulitafakari, kulisali na kuendelea kulijifunza katika maisha. Waamini wanahimizwa kujenga na kudumisha utamaduni wa kujisomea Neno la Mungu walau kila siku. Na kwa njia ya hii, Kristo Yesu anazungumza pamoja na waja wake, anawaangazia nuru yake na kuwaongoza katika njia zake. Waamini wajenge pia utamaduni wa kutembea na Biblia katika maisha yao. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake Jumatano tarehe 25 Januari 2023 kuhusu “Shauku ya Uinjilishaji: Bidii ya Kitume ya Mwamini: Wito wa Utume. Rej. Mt 9:9-13” anasema, Waamini kama wafuasi na Mitume wa Kristo Yesu wanao upendeleo, dhamana na wajibu wa kulisoma, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu kama lilivyoandikwa kwenye Biblia Takatifu. Ile hamu ya waamini kutaka kupata furaha ya kweli katika maisha yao kama mtu binafsi, familia na jamii katika ujumla wake, wataipata kwa kujichimbia katika hekima na busara ya Kimungu, chemchemi ya: upendo, amani na udugu wa kibinadamu.

Neno la Mungu liwe ni dira na mwongozo wa maisha ya ndoa na familia
Neno la Mungu liwe ni dira na mwongozo wa maisha ya ndoa na familia

Baba Mtakatifu amewakumbusha waamini, mahujaji na wageni waliohudhuria Katekesi yake kuhusu umuhimu wa Neno la Mungu katika maisha yao. Maadhimisho ya Dominika ya Neno la Mungu tarehe 22 Januari 2023 yamenogeshwa na kauli mbiu “Hilo tuliloliona na kulisikia, twawahubiri na ninyi; ili nanyi pia mpate kushirikiana nasi: na ushirika wetu ni pamoja na Baba, na pamoja na Mwana wake Yesu Kristo.” 1Yn 1:3. Baba Mtakatifu Francisko anasema Dominika ya Neno la Mungu ni kwa ajili ya kuliadhimisha, kulitafakari, kulieneza na kulishuhudia Neno la Mungu, dira na mwongozo wa maisha. Maadhimisho ya Dominika ya Neno la Mungu ni matunda ya Mwaka wa Jubilei ya Huruma ya Mungu na pia yana mwelekeo wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika: Uekumene wa damu, maisha ya kiroho, sala na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kielelezo cha ushuhuda wa Injili ya upendo wa Kristo Yesu inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu!

Neno la Mungu liwe ni chachu ya ushuhuda wa ukarimu kuanzia kwenye familia
Neno la Mungu liwe ni chachu ya ushuhuda wa ukarimu kuanzia kwenye familia

Dominika hii imeadhimishwa wakati wa Juma la 56 la kuombea Umoja wa Wakristo na maadhimisho haya kwa mwaka 2023 yanaongozwa na kauli mbiu “Jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki” Isa 1:17. Baba Mtakatifu Francisko katika Tafakari yake, Dominika ya Neno la Mungu, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amejikita zaidi katika mambo makuu matatu: Wakaacha yote na kumfuasa Kristo Yesu, ili wawe wavuvi wa watu, kukaa na Kristo Yesu kunahitaji ujasiri wa kuachana na mazoea pamoja na dhambi, vikwazo vya kuonana na Kristo Yesu na umuhimu wa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Mababa wa Sinodi ya Neno la Mungu wanasema, malezi ya kweli kutoka kwa wazazi na walezi ni kuhakikisha kwamba, wanawarithisha watoto wao imani na ushuhuda wa maana ya maisha ya Kikristo: kwa njia ya uaminifu wao na umoja wa maisha ya kifamilia. Wazazi, walezi na wanandoa watambue kwamba, wao kimsingi ni watangazaji na mashuhuda wa Neno la Mungu kwa watoto wao. Ni kutokana na muktadha huu, Mababa wa Sinodi wanawahimiza wanafamilia kuhakikisha kwamba, kila kaya inakuwa na Biblia yake, iwekwe mahali panapofaa na itumike kwa tafakari, sala na maombi. Rej. Verbum domini, 85.

Neno la Mungu linapaswa: kusomwa, kutafakarikiwa na kumwilishwa
Neno la Mungu linapaswa: kusomwa, kutafakarikiwa na kumwilishwa

Mababa wa Sinodi ya Neno la Mungu wanakaza kusema, kadiri ambavyo waamini wanajitahidi kuwa wazi mbele ya Neno la Mungu, ndivyo wanavyoweza kutambua kwamba, hata leo hii pia Fumbo la Pentekoste linaendelea kufanyika katika maisha na utume wa Kanisa la Mungu. Roho Mtakatifu anaendelea kumimina karama na mapaji yake juu ya Kanisa, ili kuwaongoza waamini na watu wote wenye mapenzi mema katika kweli yote, ili kuwaonesha maana ya Maandiko Matakatifu na hatimaye, kuwawezesha kuwa ni watangazaji na mashuhuda wa Neno la Wokovu kwa watu wa Mataifa. Rej. Verbum domini, 123.

Neno la Mungu
25 January 2023, 14:50