Tafuta

2022.07.03 La Messa del cardinale Pietro Parolin a Kinshasa (RD Congo)

Hija ya Kitume ya Papa Francisko DRC: Umoja na Mshikamano wa Udugu wa Kibinadamu

Wananchi wa DRC kwa sasa wanayo kiu kubwa ya amani ambalo ni jina jingine la ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini DRC., pamoja na mambo mengine inapania kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, kama zawadi inayopaswa kumwilishwa katika vipaumbele vya maisha ya wananchi wa DRC.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi Jumatano tarehe 18 Januari 2023 juu ya “Shauku ya Uinjilishaji: Bidii ya Kitume ya Mwamini: Wito wa Utume. Rej. Mt 9:9-13; alisema hii ni tema ya dharura na madhubuti kwa maisha ya Kikristo. “Naye Yesu alipokuwa akipita kutoka huko aliona mtu ameketi forodhani, aitwaye Mathayo, akamwambia, Nifuate. Akaondoka, akamfuata. Baba Mtakatifu anawaalika watu watakatifu wa Mungu kumwomba Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na faraja awakirimie moyo wa kichungaji unaoteseka na hata kujihatarisha ili kutoa ushuhuda. Hii ni heshima na wajibu wa kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu, kwa watoto wa Mama Kanisa, ambao wanakutana nao kila siku katika maisha na utume wao kama viongozi wa Kanisa.

Ni fursa ya Papa kukutana na kuzungumza na ndugu zake kutoka DRC
Ni fursa ya Papa kukutana na kuzungumza na ndugu zake kutoka DRC

Ni katika mukatdha huu, Baba Mtakatifu Francisko amepokea na kukubali mwaliko wa viongozi wa Serikali na Kanisa na ametia nia ya kutembelea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo, DRC., kuanzia tarehe 31 Januari 2023 kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Wote wapatanishwe katika Yesu Kristo.” Itakuwa ni fursa kwa Baba Mtakatifu Francisko, kukutana na ndugu zake kutoka DRC ambao wameteseka na kumwaga damu kwa miaka mingi kutokana na utajiri, amana na rasilimali za DRC ambazo kwa kiasi kikubwa zimekuwa ni chanzo cha vita, kinzani na migogoro nchini humo. Wananchi wa DRC kwa sasa wanayo kiu kubwa ya amani ambalo ni jina jingine la ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini DRC., pamoja na mambo mengine inapania kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, kama zawadi kubwa inayopaswa kumwilishwa katika vipaumbele vya maisha ya wananchi wa DRC.

Ni fursa ya kuwaimarisha nndugu zake katika imani, matumaini na mapendo
Ni fursa ya kuwaimarisha nndugu zake katika imani, matumaini na mapendo

Ratiba elekezi inaonesha kwamba, kutokana na hali tete ya usalama wa watu na mali zao, Baba Mtakatifu Francisko hataweza kwenda Goma kama ilivyokuwa imepangwa hapo awali. Askofu mkuu Ettore Balestrero, Balozi wa Vatican nchini DRC anasema, kwa sasa jambo muhimu ni kuendelea kuimarisha ulinzi na usalama wa watu wa Mungu zaidi ya milioni mbili wanaotarajiwa kuhudhuria Ibada ya Misa Takatifu, Jimbo kuu la Kinshasa. Baba Mtakatifu anapenda kupyaisha tena imani ya watu wa Mungu nchini DRC; kuimarisha furaha na matumaini kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo. Hija hii ya kitume ni ndoto ya watu wa Mungu kutoka DRC na sasa wanasubiri kuona ikitimia machoni pao. Huu ni wakati wa kupokea neno la faraja, kuganga na kuponya majeraha ambayo kwa bahati mbaya bado yanaendelea kuvuja damu, hususan maeneo ya Mashariki mwa DRC.

Hija ya Kitume DRC
28 January 2023, 16:44