Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu, tarehe 9 Januari 2023 amekutana na kuzungumza na wanadiplomasia pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican. Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu, tarehe 9 Januari 2023 amekutana na kuzungumza na wanadiplomasia pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Hotuba ya Papa Francisko Kwa Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa.

Papa amegusia kuhusu: Msiba mkubwa wa Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, wajibu wa kidiplomasia, Mkataba kati ya Vatican na China Kuhusu Uteuzi wa Maaskofu Mahalia, Kumbukizi ya Miaka 60 ya Waraka wa Kitume wa “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani." Hija ya Kitume nchini DRC kuanzia tarehe 31 Januari 3 Februari na Sudan ya Kusini: tarehe 3 Februari hadi tarehe 5 Feb.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu, tarehe 9 Januari 2023 amekutana na kuzungumza na wanadiplomasia pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican kama sehemu ya mapokeo na utaratibu wa kutakiana heri na baraka kwa mwaka mpya wa 2023. Katika mkutano huu, Baba Mtakatifu amegusia kuhusu: Msiba mkubwa wa Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, wajibu wa kidiplomasia, Mkataba wa Kihistoria wa Muda Mfupi kati ya Vatican na China Kuhusu Uteuzi wa Maaskofu Mahalia, Kumbukizi ya Miaka 60 ya Waraka wa Kitume wa “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” uliochapishwa tarehe 11 Aprili 1963, Hija ya Kitume nchini DRC kuanzia tarehe 31 Januari 3 Februari 2023 na Sudan ya Kusini ni kuanzia tarehe 3 Februari hadi tarehe 5 Februari 2023. Amani duniani inapaswa kusimikwa katika: ukweli, haki, mshikamano na uhuru wa kweli. Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii kuwatakia Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa, heri na baraka za Mwaka Mpya 2023. Amewashukuru viongozi wote waliomtumia salam za rambirambi pamoja na kuonesha uwepo wao wakati wa maombolezo na hatimaye mazishi ya Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI. Kwa Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana, Dominika tarehe 8 Januari 2023 Wakristo wamehitimisha Kipindi cha Noeli, ambamo wameadhimisha Fumbo la Umwilisho yaani kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, na Mfalme wa amani. Rej. Isa 9: 6.

Ubatizo wa Bwana unafunga Kipindi cha Noeli ya Bwana.
Ubatizo wa Bwana unafunga Kipindi cha Noeli ya Bwana.

Dhamana ya diplomasia ya Kimataifa ni kujitahidi kujenga mazingira ya ushirikiano, mshikamano na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa, maskini na wahitaji zaidi wakipewa kipaumbele cha kwanza, kama ushuhuda wa unyenyekevu unaoshinda kiburi na tabia ya kutaka kujimwambafai. Baba Mtakatifu anazipongeza nchi za: Uswis, DRC, Msumbiji na Azerbaijan kwa kuteuwa Mabalozi wakazi mjini Roma. Vatican imetiliana mkwaju wa ushirikiano na Jamhuri ya Watu wa Sao Tome na Principe pamoja na Kazakhstan. Mkataba wa Kihistoria wa Muda Mfupi kati ya Vatican na China Kuhusu Uteuzi wa Maaskofu Mahalia ulitiwa saini kwa mara ya kwanza tarehe 22 Septemba 2018. Kwa kutambua umuhimu wake, ukapyaishwa tena tarehe 22 Oktoba 2020 na hatimaye, Oktoba 2022 Mkataba umeongezwa tena kwa muda wa miaka miwili. Katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuonesha uvumilivu unaosimikwa katika matumaini, ili kuhakikisha kwamba, Kanisa linaipatia Jumuiya ya Waamini Wakatoliki nchini China wachungaji bora na waaminifu watakaotekeleza vyema utume wao. Lengo la Vatican ni kuendeleza maisha na utume wa Kanisa Katoliki, ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini China. Pili ni kuwapata wachungaji wema, bora na waaminifu watakaotekeleza dhamana na utume wao kadiri ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, huku wakiongozwa na ukarimu katika huduma kwa watu wa Mungu, katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Kanisa liko makini sana katika maisha, historia na maendeleo ya Kanisa nchini China.

Vatican inaendelea kufanya majadiliano na China
Vatican inaendelea kufanya majadiliano na China

Huu ni mchakato wa majadiliano ya kina ulioasisiwa na Mtakatifu Yohane Paulo II, ukaendelezwa na Hayati Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI na hatimaye, Papa Francisko anaendelea kushuhudia matunda ya juhudi hizi katika ukweli na uwazi na kwamba, leo hii, Wakatoliki nchini China wanajitahidi kuuishi Ukristo wao kwa kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili; kwa kupata katekesi na mafundisho msingi ya Kanisa, huku wakiendelea kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa kwa furaha, imani na matumaini, kielelezo makini cha imani inayomwilishwa katika upendo na ukarimu kwa watu wa Mungu nchini China. Hii ni hatua kubwa ya ushirikiano na mshikamano kati ya Vatican, Serikali kuu ya China, Maaskofu mahalia na waamini wao pamoja na viongozi mahalia. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, huu ni mchakato wa majadiliano ya kina kati ya Vatican na Serikali ya China na ana tumaini kwamba majadiliano haya, hatimaye yatasaidia kuleta maboresho ya maisha na utume wa Kanisa Katoliki sanjari na ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini China. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Vatican itaendelea kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano kutoka katika Sekretarieti kuu ya Vatican, kwa kuzingatia Katiba mpya ya Kitume. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko tarehe 19 Machi 2022, Sherehe ya Mtakatifu Yosefu Mume wake Bikira Maria, aliridhia Katiba mpya ya Kitume inayojulikana kama “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu.” Katiba imeanza kutumika rasmi tarehe 5 Juni 2022, Sherehe ya Pentekoste na hivyo kuchukua nafasi ya Katiba ya Kitume “Pastor bonus” ya tarehe 28 Juni 1988 iliyoanza kutumika rasmi 1 Machi 1989.

Katiba ya Kitume Predicate evangelium ni utekelezaji wa ushauri wa Makardinali.
Katiba ya Kitume Predicate evangelium ni utekelezaji wa ushauri wa Makardinali.

Mtakatifu Yohane XXIII tarehe 11 Aprili 1963 alichapisha Waraka wake wa Kitume “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” kumbe Mama Kanisa linajiandaa kuadhimisha kumbukizi ya Miaka 60 tangu kuchapishwa kwake. Mtakatifu Yohane XXIII anasema, amani inasimikwa katika misingi ya ukweli, haki, upendo na uhuru kamili. Kila mwanadamu ni nafsi yenye haki na wajibu. Hii ni haki ya kuishi na kuwa na maisha na haki za tunu za kimaadili na kiutamaduni. Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, mashindano ya utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha, zikiwemo silaha za nyuklia yanaendelea kukomba rasilimali za dunia ambazo zingeweza kutumika vyema zaidi kwa ajili ya kunogesha mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Kunahitajika mkakati wa Kimataifa ili kusitisha hatari inayoweza kusababishwa na mashindano ya silaha kwani madhara yake ni makubwa kama inavyojionesha huko nchini Ukraine. Kuna Vita Kuu ya Tatu ya Dunia inayopiganwa sehemu mbalimbali za dunia na madhara yake ni makubwa kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha na kuchechemea kwa hali ya maisha; kukosekana kwa uhakika na usalama wa chakula duniani hasa Barani Afrika na Mashariki ya Kati. Vita imeendelea kuwatumbukiza watu wengi katika umaskini wa hali na kipato kama inavyojionesha nchini Siria. Kumbe, kuna haja ya kukazia majadiliano ya kidini na kiekumene; ili kukuza na kudumisha amani, utulivu na maridhiano kati ya watu; hali inayopaswa kusimikwa katika majadiliano. Israeli na Palestina ni nchi mbili zinazopaswa kufuata sheria za Kimataifa na maamuzi yaliyokwisha kufikiwa na Umoja wa Mataifa.

Watu wa Mungu wanahitaji haki, amani, upendo na mshikamano
Watu wa Mungu wanahitaji haki, amani, upendo na mshikamano

Baba Mtakatifu Francisko akiwa ameambatana na Askofu mkuu Justin Welby, Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani na Mheshimiwa Dr Iain Greenshields Mkuu wa Kanisa la “Presbyterian la Scotland kama kielelezo cha ushuhuda wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika huduma, maisha ya kiroho, damu na sala watatembelea Sudan ya Kusini kuanzia tarehe 3 Februari hadi tarehe 5 Februari 2023. Lengo ni kupaaza sauti zao kulilia amani katika nchi hizi mbili sanjari na kusaidia mchakato wa upatanisho wa Kitaifa kwa nchi hizi mbili. Bado kuna maeneo ambamo watu wanateseka kutokana na vita kama vile: Caucaso, na kwamba kwa kutoa msamaha kwa wafungwa wa kisiasa na kijeshi, itakuwa ni hatua kubwa katika ujenzi wa upatanisho wa Kitaifa. Hali ni tete Afrika Magharibi kutokana na vitendo vya kigaidi hasa nchini Burkina Faso, Mali na Nigeria. Nchi nyingine ni Sudan Kongwe, Mali Chad, Guinea na Burkina Faso na Myanmar. Nchi zote hizi zinahitaji upatanisho wa Kitaifa unaosimikwa katika ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba Korea itaanza kujikita katika mchakato wa upatanisho wa Kitaifa na ujenzi wa haki na amani. Mtakatifu Yohane XXIII anasema, amani inasimikwa katika misingi ya ukweli, haki, upendo na uhuru kamili. Hizi ni nguzo kuu zinazosimika mchakato wa amani ya kweli, mahusiano na mafungamano ya watu wa Mungu katika ujumla wao wanaounda jumuiya ya Kisiasa. Amani katika ukweli inafumbatwa katika mchakato wa kuheshimu utu na haki msingi za binadamu; kutafuta na kuuambata ukweli; uhuru wa kujieleza pamoja na uwepo wa mazingira bora ya kila mtu kuweza kutekeleza dhamana na wajibu wake.

Utamaduni wa kifo ni hatari kwa ustawi, mafao na maendeleo ya wengi
Utamaduni wa kifo ni hatari kwa ustawi, mafao na maendeleo ya wengi

Huu ni wajibu wa kusimama kidete dhidi ya utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera za utoaji mimba na kifo laini, bila kusahau mauaji ya vikongwe, wagonjwa na walemavu. Haki ya maisha, ipewe kipaumbele cha kwanza dhidi ya hukumu ya kifo ambayo kwa sasa imepitwa na wakati. Injili ya uhai ipewe kipaumbele cha pekee kwa kuzingatia Mapokeo ya kidini na kitamaduni. Vatican itaendelea kuhimiza umuhimu wa vijana wa kizazi kujikita katika elimu shirikishi itakayomwezesha mwanafunzi kuweza kukua kiroho, kimwili, kiakili na kitaaluma bila kuwabagua na kuwatenga baadhi ya watu ndani ya jamii kama inavyojionesha nchini Afghanstan, kwa wanawake kubaguliwa na kutengwa. Kumbe, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kufanya maamuzi magumu na yenye ujasiri, ili kuwa na elimu bora ifikapo mwaka 2030, kwa kuongeza bajeti ya elimu na kupunguza kiwango cha fedha ya umma inayowekezwa katika manunuzi ya silaha za vita. Amani ya kweli inasimikwa katika uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini, dhidi ya dhuluma na nyanyaso za kidini. Inasikitisha kuona kwamba, dhuluma na ukatili dhidi ya Wakristo umeongezeka sehemu mbalimbali za dunia. Uhuru wa kuabudu ni sehemu ya mafao ya wengi na mahali pa kufikiri na kutenda kadiri ya dhamiri nyofu katika maisha ya hadhara, mwamini anapotekeleza uhuru wa dhamiri nyofu.

Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa ajili ya amani duniani 4 Febr. 2019
Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa ajili ya amani duniani 4 Febr. 2019

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari 2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu walitia mkwaju kwenye “Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu.” Hii ni changamoto kwa waamini wa dini mbalimbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu wa kibinadamu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hati hii ni nguzo msingi ya haki, amani na upatanisho kati ya watu wa Mataifa. Hati inakazia pamoja na mambo mengine kwamba: binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu; wanatakiwa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha: uhai wa binadamu, mazingira nyumba ya wote, sanjari na kushikamana na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Hii ni hati inayonogesha utamaduni wa watu kukutana na kujadiliana kama inavyoshuhudiwa na Bunge la Timor ya Mashariki.

Majadiliano ya kidini ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi
Majadiliano ya kidini ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi

Kongamano la Saba la Viongozi Wakuu wa Dini Duniani na Dini za Jadi limeadhimishwa mjini Kaza, Nur Sultan huko nchini Kazakhstan kuanzia tarehe 13-15 Septemba 2022, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Mchango wa Viongozi wa Dini Duniani na Dini za Jadi katika mchakato wa maendeleo ya kijamii na kiroho baada ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.” Hii ilikuwa ni hija ya 38 ya Baba Mtakatifu Francisko Kimataifa, lengo ni kuendelea kuragibisha mchakato wa majadiliano ya kidini kwa ajili ya kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Tamko la Kongamano la Saba la Viongozi Wakuu wa Dini Duniani na Dini za Jadi lililotolewa tarehe 15 Septemba 2022 ni muhtasari wa mafundisho makuu ya dini mbalimbali duniani. Tamko linakemea kwa nguvu zote misimamo mikali ya kidini na kiimani; vitendo vya kigaidi; chuki na uhasama, ghasia na kwamba, vita havina uhusiano wowote ule na misingi ya imani ya kweli na mambo haya yanapaswa kupingwa kwa nguvu zote. Mwenyezi Mungu aliwaumba watu wote kwa mfano na sura yake, katika usawa. Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Bahrein ni hatua muhimu katika mchakato wa majadiliano ya kidini kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kwa Wakristo amani ya kweli inasimikwa katika toba, wongofu wa ndani na umwilishaji wa fadhila mbalimbali katika uhalisia wa maisha. Rej. Mk 7: 21.

Vita inakwamisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi
Vita inakwamisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, amani inasimikwa katika nguzo ya haki, usawa, kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja, kwa kutengeneza fursa za watu kujadiliana katika ukweli na uwazi, ili kuepukana na ukoloni wa kiitikadi kama masharti ya kupokea misaada, hali ya kutovumiliana na matokeo yake ni uvunjwaji wa uhuru wa mawazo na dhamiri nyofu. Ukoloni umepelekea madhara makubwa katika maisha ya watu wengi. Kumbe, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujielekeza zaidi katika mchakato wa majadiliano, utamaduni wa kusikiliza, kwa kujitahidi kufanya kazi kwa ushirikiano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; mambo yanayojikita katika mshikamano wa utu wa kibinadamu. Amani katika mshikamano inasimikwa katika nguzo ushirika unaoiwezesha Jumuiya ya binadamu kupokeana jinsi walivyo kama sehemu ya mchakato wa kukamilishana. Changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani haina budi kuzingatia Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji wa mwaka 2018, yaani “Global Compact 2018.” Ni Mkataba unaolenga kuratibu na kuboresha mchakato wa wahamiaji na wakimbizi duniani, ili kulinda na kudumisha haki msingi, utu na heshima ya wahamiaji! Unakazia umuhimu wa jamii kusikiliza na kujibu kilio cha wakimbizi na wahamiaji duniani; kwa kukusanya maoni; kwa kupunguza gharama za kuwahudumia wahamiaji sanjari na kudumisha usalama na hivyo, kuendeleza mchakato wa maboresho ya maisha yao. Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa wahamiaji unapania pamoja na mambo mengine kuboresha: ulinzi na usalama; haki msingi za binadamu pamoja na kupatiwa huduma ya msaada wa kisheria pale haki zao zinapovunjwa. Mkataba huu unawatupia jicho wakimbizi na wahamiaji hatari kwa maisha na usalama wa raia wengine. Watu hatari wanaweza kurejeshwa makwao; uwezekano wa kudhibiti uhuru wa wakimbizi.

Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote wajibu wa wote
Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote wajibu wa wote

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, amani katika mshikamano inapaswa kudhihirishwa katika masuala ya kiuchumi na fursa za kazi, vijana wakiwa wamepewa kipaumbele cha pekee sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Athari za mabadiliko ya tabianchi zinaendelea kusababisha madhara makubwa kwa watu na mali zao sehemu mbalimbali za dunia. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP27) uliofanyika huko Sharm El-Sheikh, Misri kuanzia tarehe 6-18 Novemba 2022, pamoja na Mkutano wa 15 wa Umoja wa Mataifa wa Bioanuwai (COP-15) uliofanyika kuanzia tarehe 7-19 Desemba 2022 huko Montreal, Canada, itasaidia kuunganisha familia ya binadamu katika mchakato wa kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi yanayoendelea kuwatumbukiza watu wengi katika dimbwi la umaskini na magonjwa ya mlipuko. Ikolojia ya maisha ya kiroho iwahamasishe waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa na shauku ya kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, kwa kufungamanisha maisha ya kiroho na utunzaji bora wa mazingira, kwa kutambua uwepo angavu wa Mungu katika kazi ya uumbaji, kwa kuonesha moyo wa ukarimu na kujali, kwa kutambua kwamba, ulimwengu ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, huu ni mwaliko wa kujitoa sadaka kwa ajili ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo cha upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu.

Vatican ina uhusiano wa kidiplomasia na nchi 183
Vatican ina uhusiano wa kidiplomasia na nchi 183

Baba Mtakatifu Francisko anasema amani inasimikwa katika uhuru wa kupendana na kuheshimiana kama ndugu; ukarimu na upendo dhidi ya tabia ya uchoyo unaochochea ubaguzi na hatimaye vita na waathirika wakuu ni wanawake, wazee na watoto wadogo. Kuchechemea kwa demokrasia ya kweli, kumepelekea machafuko, mipasuko ya kijamii na vita kama inavyojioneshanchini Perù, Haiti, Brazil na Lebanon ambayo hadi wakati huu haina Rais na inaendelea kuathirika zaidi kiuchumi na kijamii na kisiasa. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Jumuiya ya Kimataifa itaweza kujenga utamaduni wa kukutana na hivyo kujadiliana katika ukweli na uwazi; kwa kutambua kwamba, licha tofauti zao msingi lakini wote wanaunganishwa pamoja na kifungo cha upendo na wala si woga; wanapaswa kujielekeza zaidi katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa kushirikiana na kushikamana.

Papa Diplomasia 2023
09 January 2023, 15:13