Tafuta

Mfuko wa Kukuza Jitihada za Kusoma na Kuandika Duniani, OPAM unapania kuhakikisha kwamba, elimu inakuwa ni sehemu ya haki msingi za binadamu, kichocheo cha maendeleo endelevu. Mfuko wa Kukuza Jitihada za Kusoma na Kuandika Duniani, OPAM unapania kuhakikisha kwamba, elimu inakuwa ni sehemu ya haki msingi za binadamu, kichocheo cha maendeleo endelevu. 

Jubilei ya Miaka 50 ya Mfuko wa Kukuza Jitihada za Kusoma na Kuandika, OPAM

D. Carlo M: Mfuko wa Kukuza Jitihada za Kusoma na Kuandika Duniani, OPAM unapania kuhakikisha kwamba, elimu inakuwa ni sehemu ya haki msingi za binadamu, kichocheo cha maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu, ili kuwajengea watu uwezo wa kujiamini na hatimaye kuweza kupambana vyema na mazingira yao, ili dunia hii iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Jubilei ni kipindi cha kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini. Ni wakati muafaka wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema na baraka anazowakirimia waja wake hata bila mastahili yao. Ni muda wa kuomba msamaha kwa mapungufu yote yaliyojitokeza katika maisha na utume, tayari kuomba tena neema na baraka ya kusonga mbele kwa imani, matumaini na mapendo zaidi. Mfuko wa Kukuza Jitihada za Kusoma na Kuandika Duniani, OPAM “L’Opera Promozione Alfabetizzazione nel Mondo” ulianzishwa tarehe 24 Mei 1972 na Don Carlo Muratore, aliyepania kuhakikisha kwamba, elimu inakuwa ni sehemu ya haki msingi za binadamu, kichocheo cha maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu, ili kuwajengea watu uwezo wa kujiamini na hatimaye kuweza kupambana vyema na mazingira yao, ili dunia hii iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Jumatatu, tarehe 23 Januari 2023 anasema Padre Robert Kasereka Ngongi, Rais wa Mfuko wa Kukuza Jitihada za Kusoma na Kuandika Duniani, OPAM “L’Opera Promozione Alfabetizzazione nel Mondo” kwamba, kwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko, imekuwa ni baraka kubwa katika maadhimisho ya Jubilei yao ya Miaka 50 ya maisha na utume katika mchakato wa maboresho ya huduma katika sekta  ya elimu.

Pd. Robert Kasereka Ngongi, Rais wa OPAM
Pd. Robert Kasereka Ngongi, Rais wa OPAM

Padre Robert Kasereka Ngongi ni shuhuda wa watu waliofaidika na huduma hii, na leo hii amekuwa ni Rais wa mfuko wenyewe, kielelezo makini cha mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Mfuko huu una umati mkubwa wa watu wa kujitolea wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza katika maeneo ambamo bado utu, heshima na haki msingi za binadamu zinasiginwa na vita, magonjwa, ujinga na umaskini. Utume huu kwa muda wa miaka ishirini umetekelezwa na Don Aldo Martin, aliyejikita katika mchakato wa kumwilisha Mafundisho Jamii ya Kanisa kuhusu Elimu na hivyo kuuwezesha Mfuko wa OPAM kutekeleza miradi mbalimbali ya elimu katika nchi zinazoendelea. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake, ameelezea kuhusu elimu kama sehemu muhimu sana ya mchakato wa uinjilishaji kiroho na kimwili; amani ni jina jipya la maendeleo fungamani ya binadamu yanayosimikwa katika mchakato wa ujenzi wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu.

Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa PAM
Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa PAM

“Tunaweza hata kusema kwamba ukuaji wa uchumi unategemea maendeleo ya kijamii, lengo ambalo linatamani; na kwamba elimu ya msingi ndiyo lengo la kwanza kwa taifa lolote linalotaka kujiendeleza. Ukosefu wa elimu ni mbaya kama ukosefu wa chakula; asiyejua kusoma na kuandika ni roho ya njaa. Mtu anapojifunza kusoma na kuandika, anakuwa na vifaa vya kufanyia kazi na kubeba taaluma fulani, kusitawisha kujiamini na kutambua kwamba anaweza kufanya maendeleo pamoja na wengine… kusoma na kuandika ni "chombo cha kwanza na cha msingi zaidi cha kujitajirisha kibinafsi na ujenzi wa ushirikiano wa kijamii; na ni nyenzo muhimu zaidi ya jamii kwa ajili ya kuendeleza maendeleo na maendeleo ya kiuchumi." Ndivyo anavyosema Mtakatifu Paulo VI kuhusu umuhimu wa elimu katika maisha ya watu wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mtakatifu Yohane XXIII tarehe 11 Aprili 1963 alichapisha Waraka wake wa Kitume “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” kwa kukazia kwamba, amani inasimikwa katika misingi ya ukweli, haki, upendo na uhuru kamili. Kila mwanadamu ni nafsi yenye haki na wajibu. Hii ni haki ya kuishi na kuwa na maisha na haki za tunu za kimaadili na kiutamaduni. Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa hawaufahamu ujumbe huu, kiasi kwamba, mifumo ya maendeleo imedumaa na jitihada mbalimbali za mshikamano katika maboresho ya uchumi na maisha ya watu bado “hayayajafua dafu.” Mfuko wa OPAM unajipambanuua kwa kukazia kwamba, “Elimu ni chakula.”

Jubilei ya Miaka 50 ya OPAM shukrani kwa wadau wote
Jubilei ya Miaka 50 ya OPAM shukrani kwa wadau wote

Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru wadau mbalimbali katika elimu ambao wamechangia kwa kiasi kikubwa katika maboresho ya sekta ya elimu. Ndoto ya Kanisa ni kusaidia kukoleza mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu yanayosimikwa katika ujenzi wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watenda kazi katika sekta ya elimu kutumia Waraka wa Kitume wa "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazomsibu mwanadamu, kwa kukazia elimu makini na wadau kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana na wajibu wao. Walimu wawe ni wajenzi wa udugu wa kibinadamu na kamwe wasiwe ni sehemu ya migogoro ya kijamii. Wawe ni mashuhuda wa tunu msingi za maisha zilizoko ndani mwao. Na jambo hili linawezekana kwa njia ya ushirikiano na wamisionari mbalimbali wanaotekeleza dhamana na utume wao katika nchi zinazoendelea. OPAM inapembua kwa kiasi kikubwa kuhusu miradi mbalimbali ya elimu pamoja na kuwafadhili wanafunzi katika masomo yao. Jambo la kuzngatia ni ubora wa kazi na utume wanaoutekeleza daima wajitahidi kuboresha maisha yao kwa Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa.

Papa Opam 2023
23 January 2023, 14:50