Katekisimu ya Kanisa Katoliki Ni Urithi Kutoka Kwa Papa Mstaafu Benedikto XVI
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Katekisimu ya Kanisa Katoliki ni amana, urithi na utajiri wa imani; matunda ya Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na ni chombo cha kusaidia mchakato wa uinjilishaji mpya na ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni chachu ya utakatifu wa maisha yenye mvuto na mashiko katika azma nzima ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Katekisimu ambayo ni muhtasari wa Imani ya Kanisa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, Kanisa na Mambo ya nyakati. Ni muhtasari wa adhimisho la Fumbo la Pasaka katika Sakramenti za Kanisa, Sakramenti za Kristo, Sakramenti za wokovu, imani na uzima wa milele. Lengo ni kumtukuza Mwenyezi Mungu na mwanadamu kutakatifuzwa. Katekisimu ni muhtasari wa dira na mwongozo wa maisha ya kikristo unaofumbatwa katika Amri kumi za Mungu zinazopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha: kwa kuonesha upendo kwa Mungu na jirani, kama muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu. Katekisimu ni muhtasari wa Maisha ya Sala kama ilivyokuwa kwenye Agano la Kale na Sala kuu ya Baba Yetu kama ilivyofundishwa na Kristo Yesu kwa kubeba muhtasari wa mafundisho mazito katika maisha na utume wake.
Hii ni kazi iliyovaliwa njuga na Mtakatifu Yohane Paulo II kama chombo muhimu sana cha maisha na utume wa Kanisa katika kukabiliana na changamoto mamboleo. Itakumbukwa kwamba, Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican hawakuona umuhimu wa kuagizwa kuchapishwa kwa Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki, kwani Nyaraka za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican zilisheheni amana na utajiri mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa, tofauti na Maagizo ya Mtaguso wa Trento. Lakini, Mababa wa Sinodi ya Maaskofu ya Mwaka 1985 katika mapendekezo yao, wakalishauri Kanisa kuandika Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki na dhamana hii, akakabidhiwa Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI. Tayari alikuwa amekwisha kuzungumzia kuhusu umuhimu wa Kupyaisha Katekisimu ya Kanisa Katoliki akifanya rejea ya Katekisimu ya Kirumi ya Mwaka 1566, ili kukabiliana na changamoto za kitaalimungu zilizokuwa zinaibuka kwa kasi sana katika kipindi hiki. Huu ni ushuhuda wa Kardinali Christoph Schönborn, Askofu mkuu wa Vienna, Austria, wakati huu, Mama Kanisa anapoomboleza kifo cha Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, Mwamba wa Taalimungu katika nyakati zetu!
Katekisimu ya Kanisa Katoliki ni kazi ya Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa, inayowawezesha waamini kusoma alama za nyakati, ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo. Katekisimu hii imekwisha kutafsiriwa katika lugha mbali mbali duniani, ikiwemo pia na lugha ya Kiswahili, iliyochapishwa kunako mwaka 2000, chombo thabiti na halali kwa ajili ya kufundishia Imani Katoliki anasema katika dibaji Askofu Mstaafu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki la Morogoro, aliyekuwa Mwenyekiti wa Idara ya Katekesi, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC. Hii ni amana na utajiri wa imani unaopaswa kurithishwa kwa jamii ya nyakati hizi. Hiki ni chombo cha majadiliano ya kiekumene, ili umoja katika imani ambayo ni chemchemi na msingi wake ni Fumbo la Utatu Mtakatifu, uenezwe hadi miisho ya dunia. Katekisimu ya Kanisa Katoliki inafumbata utajiri mkubwa wa: Maandiko Matakatifu, Mababa wa Kanisa, Mafundisho ya Mitaguso Mikuu, Mchango na mafundisho ya waalimu wa Kanisa, Watakatifu na viongozi wa Kanisa. Katekisimu iliidhinishwa rasmi kwa Waraka wa Mtakatifu Yohane wa Pili: “Fidei depositum” yaani “Amana ya Imani” uliosindikiza kuchapishwa kwa Katekisimu ya Kanisa Katoliki, hapo tarehe 11 Oktoba 1992 na kuanza kutumika rasmi kama kitabu cha kufundishia: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maadili na Maisha ya Sala ya Kanisa Katoliki tarehe 15 Agosti 1997.
Katekisimu ya Kanisa Katoliki ilihakikiwa na mabingwa pamoja na wataalam wa Sayansi ya Maandiko Matakatifu, kiasi kwamba ni Hati ambayo imetengezwa vyema kama kitabu cha kufundishia imani na maadili. Mwongozo kuhusu ufafanuzi wa Maandiko Matakatifu unafuata ule ulioelekezwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, “Dei Verbum” yaani “Ufunuo”: Mwenyezi Mungu katika Maandiko Matakatifu ameongea kwa njia ya wanadamu na kwa mtindo wa kibinadamu, lakini yanapaswa kusomwa na kufafanuliwa kwa msaada wa Roho Mtakatifu. Katekisimu ya Kanisa Katoliki inarutubishwa kwa Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa. Hizi ni nyenzo zinazomsaidia mwamini kufungua hazina ya moyo wake ili kumfahamu na kumtumikia Mwenyezi Mungu aliyefunuliwa kwa njia ya Kristo Yesu. Katekisimu ni mchango wa Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, kama sehemu ya mchakato wa kupyaisha maisha na utume wa Kanisa. Katekisimu ni chombo makini cha uinjilishaji na ufundishaji wa kweli za kiinjili na kiimadili; kwa kuendelea kuwa aminifu na chombo cha neema ya Mungu. Mama Kanisa amekabidhiwa dhamana na wajibu wa kuwarithisha watu amana na utajiri wa imani na maadili na kwamba, Roho Mtakatifu ni kiini cha Uinjilishaji.
Padre Federico Lombardi, SJ, Rais wa Mfuko wa Joseph Ratzinger – Benedetto XVI, anasema, Katekisimu ya Kanisa Katoliki ilianza kufanyiwa kazi kunako mwaka 1985, kama sehemu ya kumbukizi ya Miaka 20 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kwa ombi maalum kutoka kwa Maaskofu Katoliki duniani. Hii ilikuwa ni changamoto iliyotishia umoja na utofauti wa Kanisa na mchakato wa utamadunisho. Kipaumbele cha kwanza kikawa ni: Kanuni ya Imani, Amri za Mungu, Heri za Mlimani na Sala ya Baba Yetu kama nguzo msingi za Katekesi kwa Kanisa Katoliki. Muswada wa kwanza ulichapishwa kwa lugha ya Kifaransa na kupata masahihisho 24, 000 kutoka sehemu mbalimbali za dunia, hasa sehemu ya tatu kuhusu maisha adili. Ilikuwa ni tarehe 11 Oktoba 1992, Kumbukumbu ya Miaka 30 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, Katekesimu ya Kanisa Katoliki ilipozinduliwa rasmi na Mtakatifu Yohane Paulo II, kielelezo cha sadaka na majitoleo makubwa kutoka kwa Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI. Kunako mwaka 1997 “Editio Typica” ya Katekisimu ya Kanisa Katoliki ikachapishwa kwa Lugha ya Kilatini na hivyo Matoleo mengine yote yalipaswa kuzingatia tafsiri hii mpya. Baba Mtakatifu Francisko ameendelea kuitumia Katekisimu ya Kanisa Katoliki hasa kuhusu: Ekaristi Takatifu, Sakramenti za Kanisa na Maisha ya Sala pamoja na Mafundisho Jamii ya Kanisa.
Baada ya Mtakatifu Yohane Paulo II Kuchapisha Wosia wa Kitume: Injili ya Uhai, “Evangelium vitae” iliyochapishwa tarehe 25 Machi 1995 alifuta adhabu ya kifo kama sehemu ya Mafundisho ya Kanisa Katoliki kwani adhabu hii ilikuwa inakwenda kinyume cha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Lengo ni kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Hii ni amana ya imani ya Kanisa Katoliki mintarafu mwanga wa Injili. Adhabu hii ni kielelezo cha ukatili wa hali ya juu kabisa na wala haiwezi kukubalika tena, kwani inakwenda kinyume cha mwanga wa Injili. Hii ni changamoto kwa Serikali na wadau mbalimbali kujizatiti katika kulinda, kutunza na kudumisha uhai wa binadamu ambao kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kwa nchi zile ambazo bado zinaendekeza adhabu ya kifo, sasa ni wakati wa kutafuta adhabu mbadala, ili kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, changamoto ambayo Baba Mtakatifu Francisko anataka kuwarithisha vijana wa kizazi kipya. Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na maendeleo makubwa juu ya tafsiri na uelewa wa Mafundisho ya Kanisa kuhusu utu na heshima ya binadamu kadiri ya mwanga wa Injili, hali ambayo imepelekea hata Baba Mtakatifu Francisko kuamua kufanya mabadiliko kwenye kifungu cha Katekisimu ya Kanisa Katoliki kinachofuta adhabu ya kifo kama sehemu ya Mapokeo na Mafundisho ya Kanisa.
Ikumbukwe kwamba, Baba Mtakatifu Francisko katika mawazo yake kuhusu adhabu ya kifo anakazia umuhimu wa kulinda uhai wa binadamu na kuuendeleza, changamoto na mwaliko wa kuleta mwono na mwelekeo mpya kuhusu: maisha, utu, heshima ya binadamu na haki zake msingi. Hii ni hatua kubwa na muhimu katika kutafsiri Mapokeo na Mafundisho hai ya Kanisa kadiri ya Mwanga wa Injili na kwa kusoma alama za nyakati. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika Wosia wa Kitume, “Africae munus” yaani Dhamana ya Afrika, akakazia kufutwa kwa adhabu ya kifo. Baba Mtakatifu Francisko “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” akatangaza kwamba, uchafuzi wa mazingira ni dhambi ya kiikolojia dhidi ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Katekisimu ya Kanisa Katoliki ni zawadi na chombo makini cha Uinjilishaji Mpya unaokita mizizi yake katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu katika ujumla wao kujitahidi kusoma alama za nyakati kwa kujikita zaidi na zaidi katika maisha ya: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maadili na Sala. Huu ni urithi mkubwa ambao Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto wa XVI ameliachia Kanisa la Kristo Yesu.