Tafuta

Kuanzia tarehe 23-24 Januari 2023, kunafanyika Kongamano la Kimataifa Kuhusu Ugonjwa wa Ukoma. Siku ya Ukoma Duniani inaadhimishwa 30 Januari 2023. Kuanzia tarehe 23-24 Januari 2023, kunafanyika Kongamano la Kimataifa Kuhusu Ugonjwa wa Ukoma. Siku ya Ukoma Duniani inaadhimishwa 30 Januari 2023. 

Kongamano la Kimataifa Kuhusu Ugonjwa wa Ukoma: Utu, Haki na Heshima ya Binadamu

Kongamano la Kimataifa Kuhusu Ugonjwa wa Ukoma linanogeshwa na kauli mbiu: "Asiachwe Mtu yeyote Nyuma" Wito kwa Dunia: Kuondoa unyanyapaa na ubaguzi dhidi ya watu walioathirika kwa ugonjwa wa Ukoma. Baba Mtakatifu Francisko anawapongeza kwa jitihada zao katika kulinda, na kudumisha: Utu, heshima na haki msingi za wagonjwa na waathirika wa Ukoma. Utu muhimu

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Ukoma Duniani ni changamoto inayogusa kimsingi: tiba, mapambano dhidi ya: umaskini, ubaguzi na unyanyapaa, ili hatimaye, wagonjwa na waathirika wa Ukoma waweze kuheshimiwa na kuthaminiwa utu wao kama binadamu. Kristo Yesu katika maisha na utume wake, alikutana na wagonjwa wa Ukoma, akawagusa, akawafariji na kuwaponya, kiasi kwamba, Msamaria mmoja tu kati ya wale wagonjwa kumi ndiye aliyethubutu kurejea kwa Kristo Yesu, ili kumpatia Mungu utukufu. Yesu alihitimisha mkutano huo kwa kumwambia yule Msamaria, “Inuka, enenda zako, imani yako imekuokoa.” Lk. 17:19. Kristo Yesu katika maisha na utume wake, alitangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, akawaganga na kuwaponya magonjwa na udhaifu wao wa kimwili, ili kuwarejeshea tena ule utu, heshima na haki zao msingi. Wadau mbali mbali kwa kushirikiana na Mfuko wa Afya wa Sasakawa kutoka Japan, Jeshi la Malta, Mfuko wa Raoul Follereau pamoja na Mfuko wa Msamaria mwema, wanaendelea kuhimiza umuhimu wa viongozi wa kidini kusaidia kuelimisha umma dhidi ya tatizo la kuwabagua na kuwanyanyapalia wagonjwa wa ukoma sehemu mbalimbali za dunia. Siku ya Ukoma Duniani iliasisiwa na Raoul Follereau kutoka Ufaransa kunako mwaka 1953, kama kumbukumbu ya kifo cha Mahatma Ghandi, kilichotokea tarehe 30 Januari 1948.

Kongamano la Kimataifa Ugonjwa wa Ukoma: Utu na heshima
Kongamano la Kimataifa Ugonjwa wa Ukoma: Utu na heshima

Kunako mwaka 2016 kulifanyika Kongamano la Kwanza la Kimataifa kuhusu Ugonjwa wa Ukoma, mjini Vatican kwa kujikita zaidi katika huduma kamili ya wagonjwa wa Ukoma, kwa kujali na kuheshimu: haki zao msingi, utu na heshima yao. Madhara makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona- UVIKO-19, yalipelekea kushuka kwa kiasi kubwa huduma kwa wagonjwa wa Ukoma. Kwa mwaka huu wa 2023 wadau mbalimbali kwa kushirikiana kwa karibu sana na Mfuko wa Afya wa Sasakawa kutoka Japan, Mfuko wa Raoul pamoja na Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu, kuanzia tarehe 23-24 Januari 2023, wanafanya Kongamano la Kimataifa Kuhusu Ugonjwa wa Ukoma, kwa kunogeshwa na kauli mbiu: "Asiachwe Mtu yeyote Nyuma" Wito kwa Dunia: Kuondoa unyanyapaa na ubaguzi dhidi ya watu walioathirika kwa ugonjwa wa Ukoma. Watu wengi wameathirika kutokana na UVIKO-19. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko amependa kuwatumia wajumbe wa kongamano hili ujumbe wa matashi mema, akiwapongeza kwa jitihada zao katika kulinda, na kudumisha: Utu, heshima na haki msingi za wagonjwa na waathirika wa Ukoma. Baba Mtakatifu anasema, watu wanaoteseka walikuwa na nafasi ya pekee katika maisha na utume wa Kristo Yesu, kiasi hata cha kujifananisha na Msamaria mwema aliyejitaabisha kuwahudumia watu kwa mafuta ya faraja na kuwaganga kwa divai ya matumaini. Kwa hakika Kristo Yesu ni mganga wa kweli: kiroho na kimwili.

Kuna watu wameathirika sana na Ugonjwa wa Ukoma
Kuna watu wameathirika sana na Ugonjwa wa Ukoma

Hii ni changamoto kwa wadau mbalimbali kusimama kidete kulinda, na kudumisha haki msingi za wagonjwa wa Ukoma, kwani bado Ukoma unaendelea kusababisha madhara makubwa sehemu mbalimbali za dunia, hasa katika nchi maskini zaidi. Kwa kuzingatia wito wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu, kuna haja ya kugusa na kufunga madonda ya wagonjwa wa Ukoma, kwa kuondokana na changamoto ya woga usiokuwa na mvuto wala mashiko. Maadhimisho ya Siku ya 70 ya Ukoma Duniani tarehe 29 Januari 2023 yasaidie kupembua na kuangalia mifumo ya maendeleo ili hatimaye, kurekebisha na kuondokana na mifumo ya kibaguzi na unyanyapaa kwa wagonjwa wenye Ukoma, ili kupyaisha na kujenga jamii shirikishi, bila kumwacha mtu awaye yote nyuma. Jamii inapaswa kusimikwa katika fadhila ya upendo na haki. Baba Mtakatifu Francisko anasema Makanisa mahalia yanaweza kusaidia mchakato wa maendeleo endelevu na fungamani. Wadau mbalimbali wanapaswa kushirikiana na kushikamana na waathirika wa Ugonjwa wa Ukoma, ili kudumisha haki zao msingi na kuwawezesha kuishi kikamilifu katika jamii zao; daima: utu, heshima na haki msingi za binadamu zikipewa uzito wa pekee.

Wadau wasimamie haki msingi za binadamu.
Wadau wasimamie haki msingi za binadamu.

Baba Mtakatifu anawaalika wajumbe, kuonesha mshikamano na ukaribu wao: kiroho na kimwili kwa kuhakikisha kwamba, wanapata huduma bora za kiafya na kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi ya binadamu. Bikira Maria na watakatifu wote waliosimama kidete kuwahudumia, kuwatetea na kuwategemeza waathirika wa ugonjwa wa Ukoma, kwa kumtambua Kristo Yesu miongoni mwa wagonjwa hawa, wawasaidie hata wao kutekeleza wajibu huu wa upendo, ili wote wawe na uzima, kisha wawe nao tele! Rej. Yn 10:10.

Kongamano la Ukoma KImataifa

 

23 January 2023, 15:23