Msimamo wa Kanisa Katoliki Kuhusu Shauku ya Jinsia ya Aina Moja: Ushoga na Usagaji!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kifo cha Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI na shutuma zilizojitokeza baadaye; changamoto ya kuondokana na ubaguzi ndani ya Kanisa kwa kuanzia na watu wanaojihusisha na ndoa za jinsia moja; bado kuna umuhimu wa kuendeleza majadiliano ya kina na China, wasiwasi wa kiitikadi katika mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu nchini Ujerumani pamoja na kashfa ya Padre Marko Ivan Rupnik, Myesuit ni kati ya mambo mazito yaliyozungumzwa na Baba Mtakatifu Francisko katika mahojiano maalum na Nicole Winfield wa Shirika la Habari la Associated Press, (AP) katika lugha ya Kihispania, tarehe 24 Januari 2023. Haya ni mahojiano yaliyodumu kwa muda wa masaa mawili ambayo yamezua taharuki kubwa kwenye vyombo na mitandao ya kijamii, hasa kuhusiana na wazo la Baba Mtakatifu Francisko kuhusu umuhimu wa kutofautisha kati dhambi na jinai kwa watu wanaojihusisha na ndoa za watu wa jinsia moja, hawa ni mashoga na wasagaji. Kimsingi hizi ni tabia zinazokwenda kinyume kabisa cha mila, desturi na tamaduni nyingi duniani, sanjari na imani kwa watu wengi. Katekisimu ya Kanisa Katoliki, muhtasari wa: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili na Sala kuhusu makosa dhidi ya usafi wa moyo inasema: “Shauku ya jinsia ya aina moja inamaanisha uhusiano kati ya wanaume au kati ya wanawake wanaoonja mvuto wa kijinsia kuelekea kwa watu wa jinsia ileile tu au wanaooonja mvuto zaidi kwa watu wa jinsia ileile. Shauku hii imechukua sura mbalimbali katika mwenendo wa karne na katika tamaduni mbalimbali. Mwanzo wake kisaikolojia unabaki kwa vikubwa hauelezeki.
Yakijitegemeza katika Maandiko Matakatifu yanayaonesha matendo ya kujamiana ya jinsia moja kama matendo yenye uovu mkubwa, mapokeo yametamka daima kwamba “matendo ya kujamiana ya jinsia moja ni maovu kwa yenyewe.” Ni matendo dhidi ya sheria ya maumbile. Yanatenga paji la uhai na tendo la kijinsia. Kwa namna yoyote ile hayawezi kuidhinishwa. Idadi ya wanaume na wanawake waliozama katika maelekeo ya shauku ya jinsia ya aina ileile sio ya kupuuzia. Hawayachagui maelekeo haya na kwa walio wengi ni swala la kujaribu. Uhusiano nao wapaswa kuwa wa heshima, huruma, na uangalifu. Kila ishara ya ubaguzi usio wa haki iepukwe. Watu hawa wanaitwa kutimiza mapenzi ya Mungu katika maisha yao, na kama Wakristo, kuunganisha magumu wanayoweza kukutana nayo kutokana na hali yao na sadaka ya Msalaba wa Bwana. Watu wa shauku ya jinsia moja wanaitwa kuwa na usafi wa moyo. Kwa fadhila za kujitawala zinazowafundisha uhuru wa ndani na mara nyingine kwa kushikizwa na urafiki usiojitafuta, kwa sala na neema ya Sakramenti, wanaweza, na wanatakiwa polepole na kwa uthabiti kukaribia ukamilifu wa Kikristo.” KKK 2357-2359.
Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anasema shauku ya jinsia ya aina moja “Homosexuality” si kosa la jinai, bali ni hali ya kibinadamu; watu na jamii yenye mwelekeo huo wana haki zao msingi. Lakini ikumbukwe kwamba, wote ni watoto wa Mungu na anawapenda jinsi walivyo na kwa nguvu kwamba, kila mmoja wao ajitahidi kupambania utu, heshima na haki zake msingi, kumbe, kuwa na shauku ya jinsia ya aina moja si kosa la jinai linalopelekea hata wahukumiwe kifungo au kupewa adhabu ya kifo. Shauku ya jinsia ya aina moja ni dhambi. Kumbe, kuna haja kwa watu kutofautisha kati ya kosa la jinai na dhambi. Ni dhambi pia kwa kumkosea jirani yako upendo, anakaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Ni katika mwelekeo huu, Baba Mtakatifu Francisko anapinga sheria zinazowatia hatiani wanaume na wanawake waliozama katika maelekeo ya shauku ya jinsia ya aina ileile. Kuna zaidi ya nchi 50 ambazo watu wenye mwelekeo huu wakikamatwa wanatiwa hatiani. Kuna nchi zaidi ya 10 watu kama hawa wakikamatwa adhabu yao ni kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa. Baba Mtakatifu anatoa mwaliko kwa Maaskofu Katoliki kuwa na mwelekeo utakaosaidia kujenga uhusiano na jumuiya za LGBTQ na watu kama hawa kwa kuwaheshimu, kuwahurumia pamoja na kuwa waangalifu mintarafu Mafundisho ya Katekisimu ya Kanisa Katoliki. Huu ni mwelekeo unaopaswa kutolewa hata kwa wauaji na watu katili katika jamii. Kila mwamini anapaswa kuwa na “dirisha” la maisha yake, mahali pa kushuhudia matumaini na hatimaye kuona utu wa Mungu.
Hayati Papa Benedikto wa XVI alifariki dunia tarehe 31 Desemba 2022. Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 5 Januari 2023, akaongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya mazishi ya Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na baadaye Sala ya Mwisho na Ibada ya Buriani “Ultima Commendatio & Valedictio” na mazishi kufanyika kwenye Makaburi yaliyoko chini kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican “Grotte Vaticane.” Baba Mtakatifu Francisko anasema, kwa hakika amempoteza “Baba ambaye kwake alikuwa ni nguzo salama.” Katika wasiwasi na mashaka, alimkimbilia ili kupata ushauri. Anasema, ikiwa kama atalazimika kung’atuka kutoka katika Kiti cha Ukulu wa Mtakatifu Petro atabakia kuwa Askofu mstaafu wa Jimbo kuu la Roma na ataenda kuishi kwenye nyumba ya Mapadre Wazee, Jimboni Roma. Hayati Papa Benedikto wa XVI hata baada ya kung’atuka kutoka madarakani, bado alikuwa amefungamanishwa na Ukulu wa Mtakatifu Petro.
Baba Mtakatifu Francisko tarehe 13 Machi 2023 anafanya kumbukizi ya Miaka 10 tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro akitoa kipaumbele cha kwanza kwa: Maskini, Amani na Utunzaji Bora wa Mazingira nyumba ya wote. Mwanzo, watu wengi ndani na nje ya Kanisa walimpokea kwa mikono miwili, lakini kwa sasa wameanza kuona pia udhaifu na mapungufu yake ya kibinadamu. Kuna baadhi ya viongozi wa Kanisa pamoja na baadhi ya watu, wameandika vitabu na nyaraka mbalimbali kumshutumu kwa mambo mengi. Kukosoana katika upendo ni jambo jema linalosaidia ukuaji na ukomavu wa mtu, lakini shutuma hizi zingepaswa kuelekezwa kwake mubashara, bila kuzunguka mbuyu! Kwa mtindo huu, pande zote mbili zingeweza kupata ukomavu. Kuna baadhi yao, waliweza kuzungumza mubashara kama wanavyozungumza watu wazima katika ukweli na uwazi, kila mmoja akionesha mawazo yake. Baba Mtakatifu Francisko anakaribisha wale wenye nia ya kumkosoa kujitokeza ili wajadiliane kwa pamoja.
Mkataba wa Kihistoria wa Muda Mfupi kati ya Vatican na China Kuhusu Uteuzi wa Maaskofu Mahalia ulitiwa saini kwa mara ya kwanza tarehe 22 Septemba 2018. Kwa kutambua umuhimu wake, ukapyaisha tena tarehe 22 Oktoba 2020 na hatimaye, Oktoba 2022 Mkataba umeongezwa tena kwa muda wa miaka miwili. Katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuonesha uvumilivu unaosimikwa katika matumaini, ili kuhakikisha kwamba, Kanisa linaipatia Jumuiya ya Waamini Wakatoliki nchini China wachungaji bora na waaminifu watakaotekeleza vyema utume wao. Lengo la Vatican ni kuendeleza maisha na utume wa Kanisa Katoliki, ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini China. Pili ni kuwapata wachungaji wema, bora na waaminifu watakaotekeleza dhamana na utume wao kadiri ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, huku wakiongozwa na ukarimu katika huduma kwa watu wa Mungu, katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Kanisa liko makini sana katika maisha, historia na maendeleo ya Kanisa nchini China. Huu ni mchakato wa majadiliano ya kina ulioasisiwa na Mtakatifu Yohane Paulo II, ukaendelezwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI na hatimaye, Papa Francisko anaendelea kushuhudia matunda ya juhudi hizi katika ukweli na uwazi na kwamba, leo hii, Wakatoliki nchini China wanajitahidi kuuishi Ukristo wao kwa kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili; kwa kupata katekesi na mafundisho msingi ya Kanisa, huku wakiendelea kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa kwa furaha, imani na matumaini, kielelezo makini cha imani inayomwilishwa katika upendo na ukarimu kwa watu wa Mungu nchini China.
Hii ni hatua kubwa ya ushirikiano na mshikamano kati ya Vatican, Serikali kuu ya China, Maaskofu mahalia na waamini wao pamoja na viongozi mahalia. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Vatican itaendeleza mchakato wa majadiliano na Serikali ya China. Baba Mtakatifu amezungumzia kuhusu kashfa ya Padre Marko Ivan Rupnik, Myesuit maarufu katika sanaa na taalimungu, aliyeshutumiwa kwa nyanyaso za kijinsia takribani miaka 30 iliyopita, kesi ambayo imeshughuliwa na Shirika la Wayesuit na kuruhusu sheria ichukue mkondo wake katika Mahakama ya kiraia, ili haki iweze kutendeka. Papa Francisko amegusia pia mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Katoliki nchini Ujerumani, unaotekelezwa na wasomi wachache; bila ya kuwahusisha watu wa Mungu katika ujumla wao na hivyo kuchukua mwelekeo wa kiitikadi zaidi, hatari sana kwa maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu amesema, Kardinali Joseph Zen Ze-Kiun, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Hong Kong, China anaendelea na utume wake miongoni mwa wafungwa na askari magereza huku akiwa kifungoni. Ni mcheshi na kiongozi jasiri na mwenye Ibada kwa Bikira Maria wa Sheshan, kiasi kwamba, alipoiona Sanamu ya Bikira Maria kwenye Hosteli ya “Santa Marta” mjini Vatican alitokwa machozi kama mtoto mdogo. Baba Mtakatifu anasema, ucheshi unamsaidia kupambana na changamoto za kiafya, kiasi kwamba, anaendelea kupata huduma bora za kitabu na ameanza kutembea peke yake, chini ya uangalizi wa madaktari wake na kwamba, wakati wowote Mwenyezi Mungu akitaka anaweza kumwita kwake, lakini kwa sasa anaendelea vizuri ukizingatia umri wake. Baba Mtakatifu Francisko anamwomba Mwenyezi Mungu amkirimie neema ya kuendelea kuwa mcheshi.