Tafuta

Maadhimisho ya Misa Takatifu Ufunguzi wa Mwaka wa Mahakama kuu ya Rufaa ya Kipapa, Rota Romana kwa mwaka 2023 Maadhimisho ya Misa Takatifu Ufunguzi wa Mwaka wa Mahakama kuu ya Rufaa ya Kipapa, Rota Romana kwa mwaka 2023  (Vatican Media)

Ndoa Inaundwa na Mwanaume na Mwanamke: Msingi wa Familia na Kanisa Dogo la Nyumbani

Mahakama Kuu ya Rufaa ya Kipapa imezindua rasmi Mwaka wa Mahakama 2023 kwa kukutana na Baba Mtakatifu Francisko ambaye amekazia kuhusu: dhamana, wajibu na huduma ya Kanisa katika familia, ndoa kadiri ya ufunuo wa Kikristo, Sakramenti ya Ndoa inayojikita katika upendo wa Kimungu, ushuhuda wa uwepo wa Mungu unaosimikwa katika kifungo cha upendo na utakatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Agano la ndoa, ambalo kwalo mume na mke huunda kati yao jumuiya ya ndani ya uzima na mapendo, limeanzishwa na kupewa sheria zake na Muumba. Kwa maumbile yake limepangiwa kwa ajili ya mema ya watu wa ndoa, pia kwa ajili ya kuzaa na kulea watoto. Kati ya wabatizwa limeinuliwa na Kristo katika hadhi ya Sakramenti. Kumbe, Sakramenti ya Ndoa ni ishara ya umoja wa Kristo na Kanisa. Inawapatia watu wa ndoa neema ya kupendana kwa mapendo ambayo kwayo Kristo Yesu amelipenda Kanisa lake. Neema ya Sakramenti ya Ndoa hukamilisha mapendo ya kibinadamu ya mume na mke, huthbitisha umoja wao usiovunjika na huwatakasa katika safari ya uzima wa milele. Ndoa hutegemezwa juu ya ukubaliano wa wanaofunga ndoa, yaani juu ya nia ya kujitoa mmoja kwa mwingine na kamili, kwa lengo la kuishi agano la mapendo amani na ya uzazi.

Ufunguzi wa Mwaka wa Mahakama 2023
Ufunguzi wa Mwaka wa Mahakama 2023

Umoja, kutovunjika na uwazi kwa uzazi ni hali za lazima za ndoa. Mitara haiendani na umoja wa ndoa; talaka hutenganisha kile alichounganisha Mungu; kukataa uzazi kwayanyima maisha ya ndoa “zawadi yake ya thamani kubwa sana,” mtoto. Nyumba ya kikristo ni mahali ambapo watoto wanapokea tangazo la kwanza la imani. Kwa sababu hii nyumba ya familia imeitwa kwa haki “Kanisa dogo la nyumbani,” jumuiya ya neema na sala; shule ya fadhila za kibinadamu na mapendo ya Kikristo. Rej. KKK 1602-1666. Ni katika muktadha huu, Mahakama Kuu ya Rufaa ya Kipapa “Rota Romana”, imezindua rasmi Mwaka wa Mahakama 2023 kwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Katika hotuba yake amegusia kuhusu: dhamana, wajibu na huduma ya Kanisa katika familia, ndoa kadiri ya ufunuo wa Kikristo, Sakramenti ya Ndoa inayojikita katika upendo wa Kimungu, ushuhuda wa uwepo wa Mungu unaosimikwa katika kifungo cha upendo. Ndoa ni chachu ya utakatifu wa maisha, lakini ina changamoto zake.

Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru na kuwapongeza wajumbe Mahakama Kuu ya Rufaa ya Kipapa “Rota Romana”, kwa huduma yao kwa Kanisa na waamini katika ujumla wao mintarafu maisha ya ndoa na familia. Kuna haja ya kugundua tena maana na umuhimu wa ndoa inayosimikwa katika upendo kati ya mwanaume na mwanamke, msingi wa familia. Kati ya vipeo vinavyoendelea kuiandama taasisi ya ndoa na familia ni: ujinga kuhusu ndoa unaojionesha katika ngazi ya mtu binafsi na jamii katika ujumla wake. Maisha ya ndoa na familia ni kielelezo cha: Ukuu, uzuri, utakatifu na ushuhuda wa Injili ya familia unaobubujika kutoka katika sura na mfano wa Mungu. Ndani ya familia kuna matatizo na changamoto zake, lakini waamini wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kwa kuendelea kufuata mfano wa Kristo Yesu aliyekuja kuhudumia.

Kanisa lipo kwa ajili ya huduma kwa familia, Kanisa dogo la nyumbani.
Kanisa lipo kwa ajili ya huduma kwa familia, Kanisa dogo la nyumbani.

Mama Kanisa anatambua kwamba, huduma ni wajibu wake wa kwanza kwa familia na kwamba, familia ni njia ya Kanisa. Ndoa ni sehemu ya mpango wa Mungu kwa mwanadamu na inasimikwa katika kifungo cha upendo, unaowafanya mwanaume na mwanamke kuwa ni kitu kimoja. “Akajibu, akawaambia, Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke, akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja? Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe.” Mt 19: 4-6. Hii ni siri kubwa ambayo Mtakatifu Paulo anasema ni kuhusu Ndoa, akifanya rejea kwa Kristo Yesu na Kanisa lake anayeipyaisha wakati wa maadhimisho ya Sakramenti ya Ndoa, inayowawezesha wanandoa kushirikishana utimilifu wa upendo na hatimaye, kufunga Agano Jipya na la milele kwa njia ya miili yao. Familia ni kiini na msingi wa jamii. Lakini sasa kuna mwelekeo wa kuiona ndoa kama njia fulani ya kutimiza haja ya kimhemuko inayoweza kuundwa kwa namna yoyote au kubadilishwa kulingana na matashi ya mtu wenyewe. Rej. Evangelii gaudium, 66.

Kristo Yesu katika mafundisho yake alikazia kwa namna ya pekee kabisa udumivu katika ndoa, kwa sababu Mwenyezi Mungu ndiye chimbuko la ndoa yenyewe inayowawezesha kuwa kitu kimoja. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wanapozungumzia kuhusu utakatifu wa ndoa na familia wanasema Mungu mwenyewe ndiye muundaji wa ndoa na Kristo Yesu anawaendea wanafamilia kwa njia ya Sakramenti ya Ndoa. Ndoa ni zawadi ya Mungu kwa wanandoa inayosimikwa katika uaminifu kwa Mungu, kwa kutambua pia udhaifu na mapungufu ya kibinadamu. Upendo thabiti ni kiungo makini cha ndoa na familia. Hii ni Amri ya upendo kama Kristo anavyo lipenda Kanisa lake katika huruma na uamainifu; uhuru kamilifu na mapungufu yao, wakitambua kwamba, wanapaswa kupendana, huku wakisaidiana kujitakasa; kukua na kukomaa; kwa kufahamiana na kusameheana.

Huduma kwa Sakramenti ya Ndoa: wema, malezi na makuzi ya watoto
Huduma kwa Sakramenti ya Ndoa: wema, malezi na makuzi ya watoto

Ndoa ina uzuri, utakatifu na changamoto zake. Uwepo wa Mungu ndani ya familia unajikita katika elimu ya maisha ya kiroho kuhusu ushirika wa Kimungu katika hali halisi katika furaha na matumaini, yote haya yanafumbatwa katika kifungo cha upendo. Kwa hakika kwa ajili ya mema ya watu wa ndoa wenyewe, ni chachu ya utakatifu wa maisha, lakini pia ina changamoto zake. Kuna familia ambazo zinaogelea katika shida na magumu ya maisha. Mama Kanisa anahamasishwa kuwasindikiza wanandoa hawa katika upendo na matumaini; kwa kuendelea kuwarithisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sayansi ya binadamu, ili kuanzisha mchakato wa kujipatanisha kwa nguvu za Roho Mtakatifu.

Wahudumu wa mchakato wa maisha ya ndoa na fanukua
Wahudumu wa mchakato wa maisha ya ndoa na fanukua

Kwa upande wake, Monsinyo Alejandro Arellano Cedillo, Dekano wa Mahakama Kuu ya Rufaa ya Kipapa “Rota Romana”, katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko amekazia kuhusu tunu msingi za Kiinjili zinazopaswa kumwilishwa katika maisha ya ndoa na familia, ili katika ulimwengu ambao umegeuka na kuwa kama kijiji, uweze kusimikwa katika upendo unaofunuliwa na Kristo Yesu kwa waja wake; amani na mshikamano wa dhati; ukweli na haki ili kuweza kutuliza dhamiri za watu wengi wanaoteseka. Wanamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa Mamlaka Fundishi ya Kanisa: Magisterium kuhusu maisha ya ndoa na familia na kwamba, wataendelea kutenda haki kwa watu wa Mungu, kwa kutambua kwamba, hata wao wanahamasishwa kuwa wakamilifu kama Baba yao wa mbinguni alivyo mkamilifu. Wao wataendelea kuwa ni watumishi wa haki, “ministerium iustitiae.”

Rota Romana Ndoa
27 January 2023, 15:23