Papa atuma salamu za rambi rambi huko Nepal kufuatia ajali ya ndege
Na Angella Rwezaula; – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko , Jumatatu tarehe 16 Januari 2023 ametuma telegramu ya salamu zake za rambirambi kufuatia na ajali ya ndege iliyotokea Dominika asubuhi tarehe 15 Januari 2022 huko Nepal. Ndege ya Shirika la Yeti ilianguka karibu na Pokhara ambapo inasadikika waathrika 68, wakiwemo watoto watatu na mtoto mchanga. Katika telegramu yake kwa rais wa Nepal, Bwana Bidya Devi Bhandari, iliyotiwa saini na Kardinali Pietro Parolin, Katibu wa Vatican, Papa anasema kuhuzunishwa na msiba huo na kutuma salamu zake za rambirambi kwa wale wote walioguswa pamoja na maombi yake kwa wale wanao shiriki katika juhudi za kurejesha hali yao. Papa anaombea Roho za marehemu zipate huruma kwa Mwenyezi Mungu na kuwatumia baraka za Mungu katika uponyaji na amani kwa wale wanaoomboleza kupoteza wapendwa wao.
Waathirika
Ndege ya shirika la ndege la Yeti ilikuwa ikitokea mji mkuu Kathmandu ilipoanguka kati ya uwanja wa ndege wa zamani na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Pokhara. Ndani ya ndege hiyo walikuwamo watu 72, ambapo miongoni mwao wanne ni wafanyakazi. Miili 68 ilipatikana kutoka kwenye vipande vipande vya ndege, kulingana na mamlaka ya eneo hilo. Matumaini ya kupata manusura hayakuwapo kwa mujibu wa Ofisa wa neo la Nepali: “Hadi sasa tumekusanya miili 68. Tunatafuta miili mingine minne. Tunaomba muujiza. Lakini matumaini ya kumpata mtu yeyote hai imepotea”, alisema Tek Bahadur KC, mkuu wa wilaya ya Taksi ambapo ndege ilianguka. Mamia ya wanajeshi wa Nepal walihusika katika operesheni hiyo katika eneo la ajali kwenye korongo la Mto Seti, kilomita moja na nusu kutoka uwanja wa ndege.