Wasifu wa Hayati Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI: 1927-2022
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kumbukumbu Takatifu na Yakudumu ya kifo, amana na maziko ya Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI “Obitus, depositio et tumulatio Benedicti PP XVI Sanctae Memoriae” ambaye katika mwanga wa Kristo Mfufuka kwa wafu tarehe 31 Desemba 2022 muda wa saa 3: 34 Asubuhi, wakati mwaka wa Serikali ulipokuwa unaishia, tayari kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa shukrani, Te Deum kwa neema na baraka nyingi alizomkirimia Mtumishi wake mwaminifu Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI aliondoka hapa duniani, kuelekea kwenye Makao ya Baba wa milele. Kanisa zima chini ya uongozi wa Baba Mtakatifu Francisko, limemsindikiza Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika safari yake ya kuyaendea maisha na uzima wa milele kwa sala. Baba Mtakatifu Benedikto XVI amekuwa ni Papa wa 265. Kumbukumbu yake ya kudumu itaendelea kubaki katika sakafu ya moyo wa Kanisa na binadamu wote katika ujumla wao. Joseph Aloisius Ratzinger, aliyechaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro tarehe 19 Aprili 2005, alizaliwa tarehe 16 Aprili 1927 huko Markti nchini Ujerumani. Baada ya masomo na majiundo yake ya: Kikristo, kiakili na kiutu akapewa Daraja Takatifu ya Upadre hapo tarehe 29 Juni 1951 wakati wa Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume na miamba ya imani.
Tangu wakati huo, vipaji vyake vilianza kung’ara na kuwa ni kati ya wanataalimungu mahiri waliojipambanua katika miaka 1950 ndani na nje ya Ujerumani. Akabahatika kupata nafasi ya kufundisha vyuo kadhaa vya taalimungu nchini Ujerumani. Katika kipindi cha mwaka 1962 akabahatika kuteuliwa kuwa ni msaidizi binafsi wa Kardinali Joseph Fring na hivyo kushiriki katika maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Tarehe 28 Mei 1977, Mtakatifu Paulo VI akamteuwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Munich na Freising na tarehe 27 Juni 1977 akateuliwa kuwa Kardinali. Hili ni tukio ambalo liliwashangaza watu wengi, kwani Askofu mkuu Joseph Ratzinger hakuwa na uzoefu sana katika shughuli za kichungaji kama Askofu. Akaliongoza Jimbo kuu la Munich na Freising kuanzia mwaka 1977 hadi mwaka 1982. Tangu mwaka 1982 hadi mwaka 2005 alikuwa ni Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho tanzu ya Kanisa; Rais wa Tume ya Taalimungu Kimataifa pamoja na Tume ya Biblia Kimataifa pamoja na Dekano wa Baraza la Makardinali. Tarehe 8 Aprili 2005 kama Dekano wa Makardinali akaongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya mazishi ya Mtakatifu Yohane Paulo II, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.
Tarehe 19 Aprili 2005 akachaguliwa kuwa Papa wa 265, akiwa na umri wa miaka 78 na kuchagua kuitwa Benedikto XVI. Katika hotuba yake ya kwanza kabisa iliyosheheni unyenyekevu mkubwa, alisema, baada ya kifo cha Papa Yohane Paulo II aliyekuwa maarufu sana, Makardinali wamemchagua yeye, mtu wa kawaida na mfanyakazi katika shamba la Bwana kuwa Papa, lakini Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, anatambua jinsi ya kuendeleza kazi yake hata kwa kutumia vyombo dhaifu kama yeye. Baba Mtakatifu Benedikto XVI akajiweka chini ya sala na maombezi ya watu wa Mungu kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Tarehe 24 Aprili akaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kusimikwa rasmi kuwa ni Kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki, Khalifa wa Mtakatifu Petro. Tarehe 7 Mei akasimikwa kuwa ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika maisha na utume wake alikazia zaidi: Imani, Matumaini na Mapendo mambo msingi ambayo yangewawezesha waamini kujenga na kuimarisha mahusiano na mafungamano yao na Kristo Yesu pamoja na Kanisa lake. Akaandika Kitabu cha Yesu wa Nazareth, ambacho kimesheheni amana na utajiri mkubwa wa Maandiko Matakatifu, Mafundisho Sadikifu ya Kanisa, Maisha ya Kiroho pamoja na tema tete katika maisha na utume wa Kanisa na tamaduni katika ulimwengu mamboleo. Alijitahidi kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene na waamini wa Kanisa la Kiianglikani; Majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbalimbali na akaanzisha mchakato wa majadiliano na Mapadre wa Jumuiya ya Papa Pio X.
Ilikuwa ni tarehe 11 Februari 2013, Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Lourdes, (1858) sanjari na Kumbukumbu ya Mkataba wa Lateran (1929), Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI baada ya Makardinali kuwapigia kura wenyeheri watatu waliokuwa wanatarajiwa kutangazwa kuwa watakatifu alipoamua kwa hiyari yake mwenyewe, kung’atuka kutoka madarakani kutokana na uzee pamoja na kuanza kuzorota kwa afya yake, ili kutoa nafasi kwa kiongozi mwingine, kuendeleza dhamana na wajibu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Akatamka rasmi kwamba: “Bene conscius sum hoc munus secundum suam essentiam spiritualem non solum agendo et loquendo exerceri debere, sed non minus patiendo et orando. Attamen in mundo nostri temporis rapidis mutationibus subiecto et quaestionibus magni ponderis pro vita fidei perturbato ad navem Sancti Petri gubernandam et ad annuntiandum Evangelium etiam vigor quidam corporis et animae necessarius est, qui ultimis mensibus in me modo tali minuitur, ut incapacitatem meam ad ministerium mihi commissum bene administrandum agnoscere debeam. Quapropter bene conscius ponderis huius actus plena libertate declaro me ministerio Episcopi Romae, Successoris Sancti Petri, mihi per manus Cardinalium die 19 aprilis MMV commisso renuntiare ita ut a die 28 februarii MMXIII, hora 20, sedes Romae, sedes Sancti Petri vacet et Conclave ad eligendum novum Summum Pontificem ab his quibus competit convocandum esse.”
"Ninafahamu vyema kwamba ofisi hii, kulingana na kiini chake cha kiroho, lazima itekelezwe sio tu kwa kutenda na kuzungumza, lakini sio chini ya mateso na maombi. Walakini, katika ulimwengu mamboleo, chini ya mabadiliko ya haraka na kusumbuliwa na maswali ya umuhimu mkubwa kwa maisha ya imani, ili kuendesha meli ya Mtakatifu Petro na kutangaza Injili, nguvu fulani ya mwili na roho pia ni muhimu, ambayo katika miezi iliyopita imepungua ndani mwangu kwa njia ambayo ninashindwa kutoa kikamilifu huduma niliyokabidhiwa lazima nikiri kwamba ilisimamiwa vyema. Kwa hiyo, nikifahamu vyema uzito wa kitendo hiki, natangaza kwa uhuru kamili kwamba mimi, katika huduma ya Askofu wa Roma, Khalifa wa Mtakatifu Petro, niliyokabidhiwa kwa mikono ya Makardinali tarehe 19 Aprili 2005, kujiuzulu ili kuanzia tarehe 28 Februari 2013, saa nane mchana, Baraza la Jimbo kuu la Roma na Baraza la Makardinali wawe tayari kuitisha uchaguzi mkuu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro kadiri ya nafasi zao.”
Huu ni wajibu unaofumbatwa katika utekelezaji wa majukumu haya kwa njia ya maadhimisho mbali mbali ya Mafumbo ya Kanisa, mikutano pamoja na hija za kitaifa na kimataifa. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI baada ya kutafakari kwa kina, akaona alikuwa anaishiwa nguvu za kuweza kutekeleza majukumu haya kwa ufanisi mkuu. Hili ni tukio ambalo limeweka historia kubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Ni kiongozi ambaye amewashangaza sana walimwengu, kwani walidhani kwamba, ni mtu aliyekuwa na uchu wa madaraka! Lakini, ukweli wa mambo utaendelea kushamiri katika historia ya maisha na utume wa Kanisa. Utashi wa kutaka kuleta mageuzi ndani ya Kanisa ni nguvu aliyoionesha Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro! Tarehe 27 Februari 2013 akang’atuka kutoka madarakani na kwenda kuishi kwa muda mfupi kwenye Ikulu Ndogo ya Castel Gandolf kwa wakati ule. Alisema ataendelea kulisindikiza Kanisa katika hija ya maisha na utume wake kwa sala na tafakari, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Huduma hii aliitekeleza kule Castel Gandolfo na hatimaye, kwenye Monasteri ya Mater Ecclesiae.
Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI ameandika Nyaraka za Kitume zifuatazo: “Deus Caritas Est” yaani “Mungu ni upendo: 25 Desemba 2005”, “Spe salvi” yaani “Matumaini yanayookoa: 30 Novemba 2007”; Caritas in veritate yaani “Ukweli katika upendo: 29 Juni 2009” na Wosia wa kitume, ambao hakuumaliza kuuandika kama hitimisho la maadhimisho ya Mwaka wa Imani ni “Lumen fidei” yaani “Mwanga wa Imani. Baada ya maadhimisho ya Sinodi mbali mbali, Baba Mtakatifu Mstaafu aliandika Wosia zifuatazo”: Verbum Domini” yaani “Neno la Mungu”; “Ecclesia in Medio Oriente yaani “Kanisa Mashariki ya Kati”; “Sacramentum Caritatis” yaani “Sakramenti ya upendo”; Africae munus” yaani “Dhamana ya Afrika.” Alitoa huduma ya Katekesi wakati wa Jumatano na katika maisha na utume wake alifanya hija za kitume 24 sehemu mbalimbali za dunia. Mwaka 2010 kwa barua yake binafsi Motu proprio “Ubicumque et sempre” akaanzisha Baraza la Kipapa la Uinjilishaji Mpya ili kusaidi mchakato wa uinjilishaji mpya na Januari 2013 masuala yote ya Katekesi yakahamishiwa kwenye Baraza hili jipya.
Alipambana bila ya kujibakiza kwa ajili ya kulisafisha Kanisa dhidi ya kashfa ya nyanyaso za kijinsi dhidi ya watoto wadogo na kulitaka Kanisa kujikita katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani; Sala na mchakato wa kujitakasa ili kuambata utakatifu wa maisha. Hayati Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI ni nguli wa taalimungu. Tafakari zake zimekuwa ni chombo ambacho kiko tayari kusaidia mchakato wa kuifahamu, imani, tayari kuitangaza na kuishuhudia, kwa kuwaongoza wenye matumaini katika kuufikia ukweli mfunuliwa. Kwa ufupi kabisa, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika maisha na utume wake, amehubiri katika kipindi cha miaka 71, ameandika vitabu 66; Nyaraka za Kitume 3 na Wosia wa Kitume 4. Machapisho yote haya, ameyatolea muhtasari dakika chache kabla ya kufikwa na mauti kwa kusema, “Yesu Nakupenda.” Fadhila za Kimungu zinapania kuwasaidia waamini kupambana na changamoto mamboleo, kwa kukazia zaidi mambo msingi katika maisha ya Kikristo na hivyo kuendelea kuyaboresha siku kwa siku.