Wakiwa njiani viongozi wakuu wa Makanisa walipata nafasi ya kuhojiana na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wa Baba Mtakatifu Francisko nchini DRC na Sudan ya Kusini.. Wakiwa njiani viongozi wakuu wa Makanisa walipata nafasi ya kuhojiana na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wa Baba Mtakatifu Francisko nchini DRC na Sudan ya Kusini..  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Hija ya Kitume ya Papa Francisko DRC na Sudan ya Kusini: Mahojiano!

Mahojiano kati ya Viongozi wa Makanisa na waandishi wa habarii. Papa amegusia kuhusu kifo cha Benedikto XVI na jinsi ambavyo baadhi ya watu walitaka kutumia fursa hii kwa ajili ya kujijenga binafsi; hija ya uekumene wa amani na matumaini, uzoefu wa Askofu mkuu Welby kuhusu mchakato wa upatanisho. Amekazia tena msimamo wa Kanisa Katoliki kuhusu utu wa mashoga!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika hija ya 40 ya Kitume amekuwa akiambatana na Askofu mkuu Justin Welby, Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani na Mheshimiwa Dr Iain Greenshields Mkuu wa Kanisa la “Presbyterian” la Scotland kama kielelezo cha ushuhuda wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika huduma, maisha ya kiroho, damu na sala, kuanzia Ijumaa tarehe 3 Februari hadi Dominika tarehe 5 Februari 2023 wamekuwa wakitembelea kwa pamoja Sudan ya Kusini. Huu ni shuhuda wa hija ya uekumene wa amani na matumaini kwa watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini. Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 5 Februari 2023 amehitimisha hija ya uekumene wa amani na matumani nchini Sudan ya Kusini kwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, Dominika ya V ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya “John Garang” na kurejea mjini Vatican kuendelea na maisha na utume wake. Wakiwa njiani viongozi wakuu wa Makanisa walipata nafasi ya kuhojiana na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wa Baba Mtakatifu Francisko nchini DRC na Sudan ya Kusini. Baba Mtakatifu amegusia kuhusu kifo cha Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI na jinsi ambavyo baadhi ya watu walitaka kutumia fursa hii kwa ajili ya kujijenga binafsi.

Hayati Papa Benedikto XVI Shuhuda wa imani na upendo wa udugu wa kibinadamu
Hayati Papa Benedikto XVI Shuhuda wa imani na upendo wa udugu wa kibinadamu

Baba Mtakatifu amekazia kuhusu hija ya uekumene wa amani n matumaini kwa watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini na kwamba, Askofu mkuu Justin Welby, Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani ana uzoefu na mang’amuzi mapana kuhusu mchakato wa upatanisho. Amekazia tena msimamo wa mafundisho jamii ya Kanisa kuhusiana Shauku ya Jinsia ya Aina Moja: Ushoga na Usagaji! Baba Mtakatifu Francisko tarehe 5 Januari 2023, aliongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya mazishi ya Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na baadaye kuendesha Sala ya Mwisho na Ibada ya Buriani “Ultima Commendatio & Valedictio” na mazishi kufanyika kwenye Makaburi yaliyoko chini kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican “Grotte Vaticane.” Baada ya kifo cha Baba Mtakatifu Benedikto XVI tarehe 31 Desemba 2022 kumezuka mjadala mkali kwa baadhi ya viongozi waliotaka kutumia fursa ya kifo na maziko ya Hayati Baba Mtakatifu Benedikto XVI kujingea umaarufu usiokuwa na tija wala mashiko kwa ustawi, maendeleo na maisha ya Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko kwa moyo wa unyenyekevu anakiri kwamba, Hayati Baba Mtakatifu Benedikto XVI alikuwa ni mwandani na mshauri wake, na mara nyingi alipokuwa na mashaka, alimwendea kwa ushauri na majadiliano ya kina. Hata Shauku ya Jinsia ya Aina Moja: Ushoga na Usagaji alimshikirisha baada ya kuona kwamba, kuna baadhi ya Serikali zilikuwa zimeanza kutunga sheria ili kuruhusu mwelekeo huu.

Watu wenye shauku ya jinsia ya aina moja wasibaguliwe
Watu wenye shauku ya jinsia ya aina moja wasibaguliwe

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedito XVI alikaza kusema, Ndoa kwa Kanisa ni Sakramenti. Lakini, kuna mtu mmoja ambaye alijiaminisha kuwa ni rafiki wa karibu wa Hayati Baba Mtakatifu Benedikto XVI alimwendea na kumwelezea eti kuhusu “nia ya Papa Francisko ya kutaka kuhalalisha vitendo vya shauku ya jinsia moja hata ndani ya Kanisa.” Kwa hekima na busara ya kichungaji, Hayati Baba Mtakatifu Benedikto XVI akawaita wanataalimungu mahiri wanne kujadili tuhuma hizi na hatimaye, akaona kwamba zilikuwa hazina mashiko. Hayati Baba Mtakatifu Benedikto XVI alikuwa amesikitishwa sana na shutuma hizi ambazo zilikuwa zinaelekezwa kwa Papa Francisko ambaye alikuwa amechaguliwa hivi punde kuliongoza Kanisa Katoliki. Hayati Baba Mtakatifu Benedikto XVI ni Mtakatifu wa Mungu na Baba wa Kanisa. Kuna baadhi ya wanataalimungu walitaka kujijengea “umaarufu na ujiko” kwa ajili ya mafao yao binafsi. Kimsingi shutuma zitapita na ukweli utaweza kutamalaki ndani ya Kanisa kama historia inavyo fundisha.

Msimamo wa Kanisa kuhusu ushoga umeelezewa kwenye Katekisimu
Msimamo wa Kanisa kuhusu ushoga umeelezewa kwenye Katekisimu

Askofu mkuu Justin Welby, Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani kunako mwezi Januari 2019 alitembelea Sudan ya Kusini na kujionea mwenyewe madhara ya vita, kiasi cha kumshirikisha Baba Mtakatifu Francisko ili kuangalia jinsi gani Makanisa yangeweza kusaidia kuhamasisha mchakato wa haki, amani na upatanisho wa Kitaifa nchini Sudan ya Kusini na matokeo yake likaibuka wazo la kutembelea Sudan ya Kusini mwanzoni mwa Mwezi Januari 2019. Kati ya matukio muhimu sana ni yale Mafungo ya kiroho kwa ajili ya viongozi wa Sudan ya Kusini yaliyofanyika kwenye Hosteli ya “Santa Martha” mjini Vatican kuanzia tarehe 10-11 Aprili 2019 kama sehemu ya mchakato wa toba na wongofu wa ndani, ili kutafuta na hatimaye, kuambata mchakato wa amani na udugu wa kibinadamu nchini Sudan ya Kusini kwa kumpokea Kristo Yesu amani na matumaini ya watu wake. Baba Mtakatifu alipiga magoti na kubusu miguu ya viongozi wa Kisiasa kama kielelezo cha unyenyekevu kwa ajili ya kuombea amani na maridhiano nchini Sudan ya Kusini. Hapa Baba Mtakatifu alikuwa anazungumza nao kutoka katika sakafu ya moyo wake na wala si katika masuala ya kiakili tu. Kwa sasa huu ni wakati wa toba na wongofu wa ndani tayari kuambata mchakato wa upatanisho, haki na amani, ili hatimaye, kipindi hiki cha mpito kiweze kufikia ukomo wake kwa amani na utulivu. Ni wakati kwa viongozi wa Sudan ya Kusini kujizatiti katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi; udhibiti wa biashara haramu ya silaha na kuendeleza ushirikiano kati ya Serikali ya Sudan ya Kusini na Vatican katika misingi ya ukweli na uwazi, ili kuendelea kujielekeza katika mambo mengine msingi.

Watu wana kiu ya haki na amani Sudan ya Kusini
Watu wana kiu ya haki na amani Sudan ya Kusini

Ili uchaguzi mkuu uweze kufanyika katika kipindi cha miakia miwili ijayo, maandalizi yanapaswa kuanza kufanyika mwishoni mwa mwaka 2023. Dr Iain Greenshields Mkuu wa Kanisa la “Presbyterian” la Scotland ameshiriki kwa mara ya kwanza katika mkutano wa uekumene wa amani na matumaini, ingawa watangulizi wake, walikuwa wanashiriki kikamilifu tangu mwaka 2015 kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mchakato wa upatanisho. Sasa ni wakati wa kufanya kwa vitendo kwani maneno matupu hayawezi kuvunja mfupa. Ni wakati kwa wale wenye utashi wa kutaka kuleta mabadiliko kujihusisha kikamilifu, ili kunogesha mchakato huu. Ilikuwa ni tarehe 20 Mei 2016, Vatican na DRC zilipowekeana Mkataba wenye vipengele 21, ili kuheshimu Kanisa liweze kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa uhuru zaidi na kuendeleza mahusiano na mafungamano mema na Serikali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini DRC. Mkataba unatoa haki ya kisheria kwa Kanisa kutekeleza dhamana na utume wake katika uhuru kamili. Mambo mengine yaliyowekwa kwenye Mkataba huu ni pamoja na ufundishaji wa elimu ya dini shuleni, huduma ya Injili ya upendo inayotekelezwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili; huduma ya kiroho kwa vikosi vya ulinzi na usalama sanjari na hospitalini huko DRC. Mambo mengine ni upatikanaji wa nyaraka za kusafiria kwa viongozi wa Kanisa. Utekelezaji wa Mkataba huu unafanywa na Kanisa nchini DRC kwa kushirikiana na Serikali.

Mkataba kati ya Vatican na DRC 20 Mei 2016: Afya na Elimu
Mkataba kati ya Vatican na DRC 20 Mei 2016: Afya na Elimu

Kuhusu Mkataba huu, Baba Mtakatifu Francisko anasema, ni kazi nyeti inayotekelezwa na Sekretarieti kuu ya Vatican chini ya uongozi wa Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa. Baba Mtakatifu anawapongeza vijana wa Bara la Afrika ambao wamekirimiwa na Mwenyezi Mungu kipaji na utajiri wa akili, kumbe wanapaswa kupewa fursa ya kukiendeleza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. DRC ina utajiri mkubwa wa rasilimali zinazokidhi mahitaji ya malighafi kwa viwanda katika nchi zilizoendelea duniani. Ni katika muktadha huu, Bara la Afrika limeendelea kunyonywa bila huruma hata kidogo chini ya mfumo wa ukoloni mamboleo na ukolini wa kiitikadi. Baba Mtakatifu anasema mwelekeo huu unasikitisha na kamwe Bara la Afrika lisigeuzwe kuwa ni mahali pa kunyonya. Akiwa nchini DRC, Baba Mtakatifu anasema, amepata bahati ya kukutana na kuzungumza na waathirika wa vita, kinzani na mipasuko nchini DRC. Hali inasikitisha sana na lazima kuwepo na mabadiliko ya kweli. Askofu mkuu Justin Welby anakiri kwamba, hana ufahamu mkubwa wa Eneo la Mashariki mwa DRC ambalo kwa kiasi kikubwa limeathirika kwa vita. Hapa ukweli hauna budi kusemwa kwamba, DRC haipaswi kuwa kama “kichwa cha mwenda wazimu”, mahali ambapo Mataifa tajiri yanakwenda kuchuma rasilimali za nchi kwa mafao yao binafsi.

Utu, heshima na haki msingi za DRC zilindwe na kuheshimiwa
Utu, heshima na haki msingi za DRC zilindwe na kuheshimiwa

Kuna makampuni ya uchimbaji wa madini yanayofanya kazi zake bila ya kuzingatia sheria, kanuni na taratibu na matokeo yake ni watoto wadogo kufanyishwa kazi katika machimbo, kupelekwa mstari wa mbele kama chambo cha vita; kuenea kwa vitendo vya ubakaji vinavyodhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. DRC ni kati ya nchi tajiri sana Barani Afrika ingeweza kuwa ni msaada mkubwa kwa Mataifa mengine ya Afrika. Jambo hii haliwezekani kwa sasa kwani DRC, bado haijajikwamua kisiasa wala kiuchumi. Kanisa limekuwa mstari wa mbele kusaidia katika mapambano dhidi ya maambukizi makubwa ya ugonjwa wa Ebola ambao umekuwa ni tishio kwa maisha na usalama wa watu wa Mungu. Makanisa yamewekeza sana katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Umefika wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, amana, utajiri na rasilimali za Bara la Afrika na hususan zile za DRC zinatumika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wake. Kumbe, kuna haja ya kujikita katika mchakato wa utunzaji bora wa ikolojia, kujizatiti kikamilifu kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi; yote haya yanawezekana, ikiwa kama mchakato wa amani na matumaini utamwilishwa kikamilifu nchini DRC na wala si kuvutiwa tu kupora amana na utajiri wa DRC. Kwa upande wake, Dr Iain Greenshields anakaza kusema, maendeleo endelevu na fungamani kwa nchi changa duniani hayana budi kutoa kipaumbele cha kwanza kwa wasichana na wanawake, kwa kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki zao msingi.

Utu, heshima na haki msingi za wanawake na wasichana zilindwe
Utu, heshima na haki msingi za wanawake na wasichana zilindwe

Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, leo hii biashara ya silaha duniani inaendelea kushamiri sana, kiasi cha kutishia: amani, usalama, ustawi na maendeleo ya wengi. Hii ni biashara inayo waneemesha watu wachache sana ndani ya jamii kwa kusababisha maafa makubwa kwa watu na mazingira. Umefika wakati wa kufanya toba na wongofu ili kugeuza silaha kuwa ni vyombo vya amani, kazi na uzalishaji, hali ambayo ingesaidia kutokomeza baa la njaa duniani na hatimaye, kukomesha utamaduni wa kifo unaoendelea kupandikiza chuki, uhasama na maafa kwa watu na mali zao. Ni wakati wa kuondokana na ukabila usiokuwa na mvuto wala mashiko kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Vita ni chanzo cha maafa kwa watu na mali zao sanjari na mazingira, nyumba ya wote. Watoto wanafunzwa na kupelekwa mstari wa mbele kuwa ni chambo cha vita. Dr Iain Greenshields anakaza kusema, mipasuko ya kijamii, utengano na ubaguzi ni hatari sana kama ilivyokuwa nchini Scotland iliyojikuta inatumbukia katika “dhana ya vita” kidini, lakini kwa sasa kuna mchakato wa majadiliano yanayoendelea ili kujenga amani na utulivu. Kuna haja ya kudumisha mchakato wa elimu bora na ujenzi wa urafiki wa kijamii. Askofu mkuu Justin Welby anasema, toba na wongofu wa ndani ni muhimu katika mchakato wa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano. Imani isaidie kuleta maboresho katika maisha ya watu kwa kuondokana na tabia ya kutaka kulipiza kisasi na badala yake kwa kujikita katika toba, wongofu wa ndani, upatanisho na uponyaji miongoni mwa watu wa Mungu Sudan ya Kusini.

Vita ina madhara makubwa kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu
Vita ina madhara makubwa kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu

Baba Mtakatifu Francisko ameonesha utashi wa kukutana na kuzungumza na Rais Vladimir Putin wa Urusi pamoja na Rais Volodymyr Oleksandrovych Zelenskyy wa Ukraine, changamoto inayoendelea kufanyiwa kazi. Baba Mtakatifu anasema, kitendo cha kuwapigia magoti viongozi wa Sudan ya Kusini ni jambo ambalo haliwezi kurudiwa tena, kwani hii ilikuwa ni nguvu ya Roho Mtakatifu iliyomsukuma kutenda vile kwa ajili ya amani kwa watu wa Sudan ya Kusini. Baba Mtakatifu anatamani kuona haki, amani, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu vikitawala nchini Siria, Yemen na Myanmar na huko Amerika ya Kusini. Vita inasababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao; waathirika wakuu ni watoto, wanawake na wazee. Katika kundi hili wamo pia watawa wa kike ambao wameuwawa kikatili. Utu, heshima na haki msingi za wanawake zinapaswa kulindwa na kuheshimiwa na kamwe wanawake na wasichana wasitumike kama vichokoo kwa ajili ya matangazo ya biashara. Hatima ya vita kati ya Urusi na Ukraine iko mikononi mwa Rais Vladimir Putin wa Urusi anasema Dr Iain Greenshields na kwamba, vitendo vya kigaidi nchini Nigeria vinaendelea kupandikiza mbegu ya kifo na kwamba, hivi karibuni watu 40 wameuwawa kikatili nchini Nigeria.

Papa Francisko atia nia ya kukutana na Marais wa Urusi na Ukraine
Papa Francisko atia nia ya kukutana na Marais wa Urusi na Ukraine

Kadiri ya mila, tamaduni na desturi njema za Kiafrika, vitendo vya ndoa ya watu wa jinsia moja havikubaliki hata kidogo, ni utovu wa nidhamu, maadili na kwenda kinyume cha mapenzi ya Mungu. Msimamo wa Kanisa Katoliki Kuhusu Shauku ya Jinsia ya Aina Moja: Ushoga na Usagaji! Katekisimu ya Kanisa Katoliki, muhtasari wa: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili na Sala kuhusu makosa dhidi ya usafi wa moyo inasema: “Shauku ya jinsia ya aina moja inamaanisha uhusiano kati ya wanaume au kati ya wanawake wanaoonja mvuto wa kijinsia kuelekea kwa watu wa jinsia ileile tu au wanaooonja mvuto zaidi kwa watu wa jinsia ileile. Shauku hii imechukua sura mbalimbali katika mwenendo wa karne na katika tamaduni mbalimbali. Mwanzo wake kisaikolojia unabaki kwa vikubwa hauelezeki. Yakijitegemeza katika Maandiko Matakatifu yanayaonesha matendo ya kujamiana ya jinsia moja kama matendo yenye uovu mkubwa, mapokeo yametamka daima kwamba “matendo ya kujamiana ya jinsia moja ni maovu kwa yenyewe.” Ni matendo dhidi ya sheria ya maumbile. Yanatenga paji la uhai na tendo la kijinsia. Kwa namna yoyote ile hayawezi kuidhinishwa. Idadi ya wanaume na wanawake waliozama katika maelekeo ya shauku ya jinsia ya aina ileile sio ya kupuuzia. Hawayachagui maelekeo haya na kwa walio wengi ni swala la kujaribu. Uhusiano nao wapaswa kuwa wa heshima, huruma, na uangalifu. Kila ishara ya ubaguzi usio wa haki iepukwe. Watu hawa wanaitwa kutimiza mapenzi ya Mungu katika maisha yao, na kama Wakristo, kuunganisha magumu wanayoweza kukutana nayo kutokana na hali yao na sadaka ya Msalaba wa Bwana. Watu wa shauku ya jinsia moja wanaitwa kuwa na usafi wa moyo. Kwa fadhila za kujitawala zinazowafundisha uhuru wa ndani na mara nyingine kwa kushikizwa na urafiki usiojitafuta, kwa sala na neema ya Sakramenti, wanaweza, na wanatakiwa polepole na kwa uthabiti kukaribia ukamilifu wa Kikristo.” KKK 2357-2359.

Msimamo wa Kanisa kuhusu ushoga umeelezewa kwenye Katekisimu
Msimamo wa Kanisa kuhusu ushoga umeelezewa kwenye Katekisimu

Itakumbukwa kwamba, tarehe 16 Machi 2021 Kardinali Luis Francisco Ladaria Ferrer, S.J., Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa na Askofu mkuu Giacomo Morandi, Katibu mkuu wa Baraza walitoa angalisho kuhusu wasi wasi juu ya kubariki “ndoa” ya watu wa jinsia moja kwa kusema ni marufuku kubariki “ndoa ya watu wa jinsia moja” kwa sababu si mamlaka ya Kanisa. Na hapa hakuna ubaguzi wala maamuzi mbele kuhusiana na mielekeo ya watu hawa kijinsia. Hili ni jibu makini la wasiwasi kuhusu uwezekano wa Kanisa kubariki “ndoa ya watu wa jinsia moja” “Responsum ad dubium”. Ni katika muktadha huu, Mapadre hawana ruhusa ya kubariki “ndoa” ya watu wa jinsia moja wanaotaka mahusiano yao yaweze kutambuliwa na Kanisa Katoliki. Baba Mtakatifu Francisko ameridhia angalisho hili na kutaka lichapwe na Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”, kifungu cha 250 anasema: “Kanisa linaiga kwa dhati kabisa msimamo wa Bwana Yesu, ambaye kwa upendo usio na mipaka amejitoa afe kwa ajili ya kila mtu bila ubaguzi. [275] Pamoja na Mababa wa Sinodi niliangalia hali za familia ambapo ndani yake wapo watu wenye mwelekeo wa ushoga, hali ambayo ni ngumu kwa upande wa wazazi na wa watoto pia. Tungependa kwa mara nyingine tena kusisitiza kuwa, pasipo kujali mwelekeo wake wa kijinsia, kila mtu anastahili kupewa heshima kwa utu wake na anastahili kupokelewa kwa heshima na hivi “kila hali ya ubaguzi usio haki” [276] iepukwe, na hasa kila aina ya mashambulizi na ukatili. Familia za namna hii lazima zipewe kwa heshima huduma za kichungaji, ili wale wenye mwelekeo wa mapenzi ya jinsia moja wapate msaada wanaouhitaji ili katika maisha yao wayatambue na kuyatekeleza kikamilifu mapenzi ya Mungu. [277]”

Ndoa wa Kanisa Katoliki ni Sakramenti
Ndoa wa Kanisa Katoliki ni Sakramenti

Ikumbukwe kwamba, baraka ni sehemu ya Sakramenti ya Ndoa na ni tendo la Liturujia ya Kanisa. “Ndoa” ya watu wa jinsia moja ni kinyume cha mpango wa Mungu uliofunuliwa katika kazi ya uumbaji. Ndoa kimsingi inaundwa kwa ukubaliano kati ya bwana na bibi. Umoja, kutovunjika na uwazi kwa uzazi ni hali ya lazima za ndoa. Tofauti na uelewa huu kuhusu Sakramenti ya Ndoa ni kwenda kinyume cha kanuni maadili na mafundisho ya Kanisa. Kumbe, baraka ya Kanisa inatolewa tu kwa bibi na bwana wanaofunga ndoa kadiri ya mpango wa Mungu katika kazi ya uumbaji. Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, kila wakati hoja ya ndoa wa jinsia moja inapojitokeza kunakuwepo na mitazamo tofauti na hata wakati mwingine misimamo mikali ya kidini, kiimani na kitamaduni. Kanisa Katoliki Kuhusu Shauku ya Jinsia ya Aina Moja: Ushoga na Usagaji limekwisha kutoa msimamo wake kama unavyofafanuliwa na Katekisimu ya Kanisa Katoliki pamoja na Mamlaka Fundishi ya Kanisa yaani “Magisterium.” Hawa ni watoto na sehemu ya familia ya watu wa Mungu, wanapaswa kuheshimiwa jinsi walivyo. Ni kuwakosea haki, kuwahukumu adhabu ya kifo, kuwatenga na kuwanyanyasa. Kuna nchi zaidi ya 50 ambazo ni jinai kuwa na shauku ya jinsia ya aina moja yaani “Ushoga na Usagaji.” Kuna nchi zaidi ya 10 ukipatikana na kosa kama hili hukumu yake ni adhabu ya kifo. Ikumbukwe kwamba, Kanisa linatetea maisha, utu, heshima na haki msingi za watu kama hawa. Hii ni dhambi, lakini dhambi hii haiwezi kugeuzwa na kuwa ni kosa la jinai. Baba Mtakatifu Francisko anasema yuko makini kutetea utu wa mtu na msimamo wa Kanisa Katoliki unafahamika bayana.

Leno ni kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu
Leno ni kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu

Askofu mkuu Justin Welby ameunga mkono hoja ya Baba Mtakatifu Francisko na kwamba, Ushirika wa Kanisa Anglikana Kimataifa hivi karibuni umepitisha Matamko mawili yanayopinga unyanyasaji na ubaguzi wa watu wenye shauku ya jinsia ya aina moja. Matamko haya yamewasaidia watu wengi kubadili misimamo mikali ya kidini, kiimani na kitamaduni. Askofu mkuu Welby anasema, msimamo huu wa Baba Mtakatifu ataufanyia tena rejea wakati wa Maadhimisho ya Sinodi ya Kanisa Anglikana nchini Uingereza. Kwa upande wake Mheshimiwa Dr Iain Greenshields anakaza kusema, Kristo Yesu katika maisha na utume wake, alionesha upendo kwa wote, kumbe, Wakristo hawana sababu ya kubaguana na kutengana, bali waheshimiane na kuthaminiana kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko ametia nia ya kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni, Jimbo kuu la Lisbon, Ureno kuanzia tarehe 1 – 6 Agosti 2023. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, hii ni hija ya maisha ya kiroho, changamoto na mwaliko kwa waamini lakini hasa vijana wa kizazi kipya, kuguswa na moyo wa unyenyekevu, sadaka na majitoleo kwa wengine kama alivyofanya Mtakatifu Yosefu. Awe ni mfano bora wa ujenzi wa mahusiano na mafungamano ya udugu wa kibinadamu katika maisha! Baba Mtakatifu anawataka vijana kujisikia kuwa ni sehemu muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko unaosimikwa katika huduma ya upendo!

Papa Francisko ametia nia ya kushiriki Siku ya Vijana Duniani 2023
Papa Francisko ametia nia ya kushiriki Siku ya Vijana Duniani 2023

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 29 Septemba 2023 anatarajia kutembelea Marsigilia na hatimaye kutembelea Mongolia, lengo ni kuzisaidia nchi ndogo ndogo Barani Ulaya kuweza kufahamika na hivyo kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengi. Hija ya kwanza ya Kitume, Papa Francisko aliifanya nchini Albania. Yote haya yanategemea kwa kiasi kikubwa nchi ambavyo anavyoweza kukabiliana na changamoto za afya na kwamba, afya yake inaendelea kuboreka zaidi. Viongozi wakuu wa Makanisa wanasema, watakuwa na furaha tele watakapopata bahati ya kusafiri pamoja na Baba Mtakatifu Francisko katika hija zake za kitume, ili kusaidiana pale inapowezekana.

Papa Mahojiano 2023

 

 

06 February 2023, 15:50