Tafuta

Baba Mtakatifu Alhamisi tarehe 2 Februari 2023 amekutana na kuzungumza na makleri, watawa na majandokasisi, kama sehemu ya maadhimisho ya Sikuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni sanjari na Siku ya Kuombea Watawa Duniani Baba Mtakatifu Alhamisi tarehe 2 Februari 2023 amekutana na kuzungumza na makleri, watawa na majandokasisi, kama sehemu ya maadhimisho ya Sikuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni sanjari na Siku ya Kuombea Watawa Duniani   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Sikukuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni na Siku ya Kuombea Watawa Duniani

Papa Francisko amewaalika waamini kuwaombea watawa. Viongozi wa Kanisa wawe ni kielelezo cha huduma na mashuhuda wa upendo. Watawa wajenge utamaduni wa maisha ya sala, kushinda kishawishi cha kumezwa na malimwengu, wazamishe maisha katika: Neno la Mungu, Sakramenti, Mafundisho tanzu na ushuhuda amini kwa Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hayati Baba Mtakatifu Benedikto XVI, katika Waraka wake wa Kitume kuhusu Mwaka wa Imani, "Porta Fidei" yaani “Mlango wa Imani” anabainisha kwamba, kwa njia ya imani, kuna watu ambao wamewekwa wakfu kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake; wakaacha yote ili kuanza kujikita katika mashauri ya Kiinjili, yaani: utii, ufukara na usafi kamili. Hawa ni kielelezo makini cha wale wanaomsubiri Kristo Yesu ambaye, kamwe hatachelewa kurudi. Ni katika muktadha huu, Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1997 akaanzisha Siku ya Kuombea Watawa Duniani inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 2 Februari sanjari na Sikukuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni. Lengo ni kumshukuru Mungu kwa ajili ya watawa ambao wanajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani kwa kufuata mashauri ya kiinjili. Ni fursa kwa watawa kupyaisha tena wito, maisha na utume wao, tayari kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu na kuendelea kumtumainia Mungu katika safari ya maisha yao licha ya changamoto na fursa mbalimbali wanazokumbana nazo katika maisha. Wito wa kitawa ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa la Kristo Yesu. Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, hii ni siku ambayo inapaswa kuwasaidia waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kutambua na kuwaenzi watawa wanaoshiriki kikamilifu katika utume wa kufundisha, kuihubiri na hatimaye, kuishuhudia Injili, ili watu wote wapate imani na kumwongokea Mwenyezi Mungu, kwa njia ya imani, Ubatizo pamoja na kuzishika Amri za Mungu.

Wito na maisha ya kitawa ni muhimu sana kwa utume wa Kanisa
Wito na maisha ya kitawa ni muhimu sana kwa utume wa Kanisa

Watawa wajibidiishe kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha na utume wao, watambue kwamba, wamewekwa wakfu kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani. Hii ni fursa ya kujifunza mafundisho muhimu kuhusu maisha na utume wa watawa ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Mtakatifu Yohane Paulo II anawahimiza watawa kuadhimisha sherehe hii, ili kumshukuru Mungu kwa wema wake wa daima anawaowatendea. Iwe ni nafasi kwa watawa kurejea tena katika wito wao na kuanza kufanya tathmini, ili kujikita zaidi katika huduma kwa Mungu na jirani na kuendelea kushuhudia kweli za Kiinjili. Hija ya 40 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini DRC kuanzia tarehe 31 Januari 2023 hadi tarehe 3 Februari 2023 inanogeshwa na kauli mbiu “Wote wapatanishwe katika Yesu Kristo.” Baba Mtakatifu Alhamisi tarehe 2 Februari 2023 amekutana na kuzungumza na makleri, watawa na majandokasisi, kama sehemu ya maadhimisho ya Sikuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni sanjari na Siku ya Kuombea Watawa Duniani kwa Mwaka 2023. Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu amewaalika watu wa Mungu kuwaombea watawa na kumshukuru Mungu kwa idadi kubwa ya miito kutoka nchini DRC. Viongozi wa Kanisa wawe ni kielelezo cha huduma na mashuhuda wa upendo wa Mungu, alama ya uwepo angavu wa Kristo na upendo wake usiokuwa na kifani. Watawa wanatakiwa kujenga utamaduni wa maisha ya sala, kushinda kishawishi cha kumezwa na malimwengu na kuishi maisha ya wakfu juu juu bila kuzamisha mizizi katika Neno la Mungu, Sakramenti, Mafundisho tanzu na ushuhuda amini kwa Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake.

Kipaumbele cha kwanza ni Kristo Yesu Mkombozi wa Ulimwengu
Kipaumbele cha kwanza ni Kristo Yesu Mkombozi wa Ulimwengu

Sikukuu ya kutolewa Bwana Hekaluni ni mwaliko kwa waamini kumpatia Kristo Yesu kipaumbele cha kwanza katika maisha, ili kuwa na mwelekeo mpya katika maisha na utume, ili kweli Kristo Yesu nuru ya Mataifa aweze kuwafariji kwa Roho wake Mtakatifu, kuwatia shime kwa Neno na kuwaenzi kwa upendo wake usiokuwa na kifani. Kanisa nchini DRC linakabiliwa na matatizo na changamoto pevu, linaishi na kutekeleza utume wake katika mazingira magumu na hatarishi, lakini bado watu watakatifu wa Mungu wanaweza kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa furaha, kielelezo cha neema na baraka ya Mungu inayotenda kazi ndani mwao. Baba Mtakatifu amewakumbusha viongozi wa Kanisa kwamba, Mwenyezi Mungu ni mwaminifu kwa ahadi zake zinazotekeleza katika historia ya maisha ya mwanadamu, jambo la msingi kwa upande wao, ni kuhakikisha kwamba, wanawatumikia watu wa Mungu kama mashuhuda wa upendo wa Mungu, kwa sababu Mungu mwenyewe atawalinda na kuwategemeza katika maisha na utume wao. Huyu ni Mungu ambaye amejifunua kuwa ni mwingi wa huruma na mapendo, kimbilio na nguvu ya wale wanaomtumainia. Baba Mtakatifu anawataka makleri, watawa na majandokasisi kuwa ni wahudumu wa watu wa Mungu, baada ya kukutana na Kristo Yesu, ili kuweza kuwashirikisha wengine ile furaha yao ya ndani kwa njia ya huduma.

Watawa baada ya kukutana na Yesu wawashirikishe wengine furaha yao
Watawa baada ya kukutana na Yesu wawashirikishe wengine furaha yao

Baba Mtakatifu anawaonya kwamba, maisha ya wakfu ni utume na kielelezo cha uwepo angavu wa Kristo Yesu kati pamoja na waja wake, katika upendo na msamaha ili kuwa ni chachu ya upatanisho, na huduma bora kwa maskini. Si mahali pa kujitafutia utajiri au nafasi muhimu katika jamii. Viongozi wa Kanisa wajifunze kujisadaka bila ya kujibakiza, ili waweze kumpeleka Kristo Yesu kwa watu wake, apate kuwaganga na kuwaponya madonda ya moyo, kwani ni Yeye peke yake anayeweza kuifanya kazi hii kwa umakini mkubwa. Baba Mtakatifu anawataka viongozi wa Kanisa kushinda kishawishi cha maisha ya kiroho kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maisha ya sala, ili kujenga mahusiano na mafungamano ya dhati, msingi wa maisha na utume wao, daima wakijitahidi kuwa na imani thabiti. Makleri, watawa na majando kasisi wajenge utamaduni wa kushiriki kikamilifu Ibada ya Misa Takatifu, Sala za Kanisa, Sakramenti na hususan Sakramenti ya Upatanisho na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu. Wajitahidi kusoma, kutafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao na kwamba, Sala ya Rozari Takatifu ni muhimu katika maisha na utume wao, kwani sala inawasaidia kuomba, kushukuru, kusifu na kutukuza na hivyo kuwaundia fursa ya kuwa karibu zaidi na Mwenyezi Mungu. Bila ya mazoea na utamaduni wa kusali vyema, maisha ya wakfu, yatasinyaa na kunyauka, kumbe, kuna haja ya kujifunza kusali, kutafakari na hatimaye, kupata nguvu za kumfuasa Kristo Yesu.

Viongozi wa Kanisa washinde kishawishi cha kumezwa na malimwengu
Viongozi wa Kanisa washinde kishawishi cha kumezwa na malimwengu

Baba Mtakatifu anawataka viongozi wa Kanisa kushinda kishawishi kinachoweza kuwatumbukiza katika anasa na hatimaye, kumezwa na malimwengu, kiasi cha kupoteza dira na mwelekeo wa maisha ya kitawa na utume kwa kumezwa na uchoyo na ubinafsi kiasi cha kushindwa kuonesha ile sanaa ya ukaribu wa Mungu kwa watu wake wateule. Viongozi wa Kanisa wakitanguliza mbele rasilimali fedha, watakosa uhuru wa ndani, watashindwa kukumbatia na kuambata ufukara wa Kiinjili na hivyo kupoteza ile furaha ya Injili. Useja ambao ni kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu utawashinda na hatimaye kumezwa na malimwengu. Huu ni mwaliko wa kukesha na kusali. Mama Kanisa anawahitaji mapadre na watawa walioandaliwa vyema katika maisha na utume wao, watu wanaoweza kusadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Kumbe, malezi makini ya awali na endelevu ni nyenzo muhimu sana katika maisha ya kiroho yatakayowawezesha kuwa karibu na watu wa Mungu. Wajifunze kiini cha mafundiso tanzu ya Kanisa, wasome, kujifunza na kulitafakari na hatimaye, kumwilisha Neno la Mungu, daima wakijitahidi kusoma alama za nyakati na kwamba, majiundo endelevu ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Matatizo, changamoto na fursa za maisha wakfu zinaweza kupewa ufumbuzi kwa kwa kujisadaka katika huduma kwa watu wateule wa Mungu kama mashuhuda wa upendo wa Mungu.

Wawe ni wasamaria wema, tayari kuwaganga watu wa Mungu waliojeruhiwa kutokana na unyonyaji mkubwa, rushwa na ukosefu wa haki kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini. Wawe ni mashuhuda wa udugu wa kibinadamu, amani na vyombo vya mshikamano. Wamwombe Mwenyezi Mungu katika unyenyekevu ili waweze vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu, tayari kujadiliana, kukaribisha, kusamehe na hivyo kupandikiza mbegu ya amani, upendo na mshikamano. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu amewapongeza viongozi wa Kanisa kwa ushuhuda wao kwa Kanisa na katika ulimwengu, waendelee kuwa ni mifereji ya faraja ya Mungu, mashuhuda amini wa furaha ya Mungu; manabii wa amani, Mitume wa upendo, tayari kuganga na kuponya madonda ya maskini na wale wanaoteseka.

Watawa wajitahidi kuwa ni wasamaria wema.
Watawa wajitahidi kuwa ni wasamaria wema.

Wakati huo huo, Kardinali Fridolin Ambongo Besungu, OFM Cap., Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Kinshasa kwa niaba ya Maaskofu wa DRC., amemwelezea Baba Mtakatifu Francisko kwamba, hija yake ya kitume ambayo imesubiriwa kwa muda mrefu imekuwa ni chemchemi ya faraja kwa sadaka yao mbele ya Mwenyezi Mungu. Amesema, Kanisa katika maisha na utume wake nchini DRC na hasa katika uinjilishaji linaishi na kutenda kazi katika mazingira magumu na hatarishi, lakini limekuwa ni chemchemi ya faraja na matumaini kwa watu wa Mungu. Maisha na utume wa watawa nchini DRC yanakabiliwa na changamoto pevu, lakini bado uaminifu kwa Mungu na tunu msingi za Kiinjili, furaha ya kuwahudumia na kuwasindikiza watu wa Mungu, katika kutafuta na kudumisha utu, heshima na haki zao ni mambo muhimu katika kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili. Ni matumaini ya Kanisa nchini DRC kwamba, miito itaendelea kuchipuka na kustawi kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu. Mwakilishi wa Mapadre wa Majimbo amesema, wao kimsingi wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa Kristo Yesu Mfufuka, upendo, mshikamano na jasiri wa tunu msingi za Kiinjili dhidi ya ukabila usiokuwa na mvuto wala mashiko. Ni wajibu na dhamana yao kugundua Uso wa Kristo anayeteseka kati ya waja wake, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza ili kukoleza mchakato wa upatanisho, haki na amani; sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; kwa kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kwa kutambua kwamba, familia ni madhabahu ya maisha, elimu ni mahali pa kujifunza ubinadamu mpya.

Watawa wawe ni nuru na chumvi ya dunia.
Watawa wawe ni nuru na chumvi ya dunia.

Mwakilishi wa watawa kwa upande wake, amekazia umuhimu wa watawa kuwa ni Wasamaria wema katika maisha na utume wao. Baba Mtakatifu awe ni sauti ya watu wa Mungu nchini DRC., ili amana na utajiri wa nchi hii, uweze kuwa ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Wanayo furaha kubwa ya kuwekwa wakfu ili waweze kuwa ni mashuhuda wa Injili kwa wale wote wanaoteseka nchini DRC. Wako tayari kutoka kimasomaso kutangaza na kushuhudia Injili sehemu mbalimbali za dunia. Kwa upande wa majandokasisi ambao bado wako kwenye malezi na majiundo ya kipadre na kitawa wamegusia kuhusu seminari kuwa ni nyumba sala, masomo, ushirika na utu. Maaskofu wanaendelea kuhakikisha kwamba seminari na nyumba za malezi zinatekeleza vyema dhamana na wajibu wake licha ya changamoto za vita, maadili na utu wema, uchumi na kijamii. Majandokasisi nao pia wanaathirika na mambo haya na kwamba, wanaendelea kuunga mkono jitihada za Kanisa katika mchakato wa Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu ni njia, ukweli na uzima. Yn 14:6.

Siku ya Watawa 2023
03 February 2023, 15:51