Hija ya Kitume ya Papa Francisko DRC na Sudan ya Kusini: Shukrani kwa Moyo wa Ukarimu!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 31 Januari 2023 hadi tarehe 5 Februari 2023 amefanya Hija ya 40 ya Kitume nchini DRC na Sudan ya Kusini. Lengo likiwa ni kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu, Injili ya matumaini kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo; amani na majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika nchi hizi mbili. Baba Mtakatifu alikuwa ameambatana na Askofu mkuu Justin Welby, Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani na Mheshimiwa Dr Iain Greenshields Mkuu wa Kanisa la “Presbyterian” la Scotland kama kielelezo cha ushuhuda wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika huduma, maisha ya kiroho, damu na sala, kuanzia Ijumaa tarehe 3 Februari hadi tarehe 5 Februari 2023 wametembelea Sudan ya Kusini. Huu ni shuhuda wa hija ya uekumene wa amani na watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini.
Nchini Sudan ya Kusini hija hii imenogeshwa na kauli mbiu “Wote wawe na umoja” Yn 17:21, hiki ni kielelezo cha ushuhuda wa kiekumene, mshikamano na udugu wa kibinadamu, mwaliko na changamoto ya kujizatiti katika mchakato wa upatanisho na ujenzi wa umoja wa Kitaifa, Hija ya 40 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini DRC kuanzia tarehe 31 Januari 2023 hadi tarehe 3 Februari 2023 ilinogeshwa na kauli mbiu “Wote wapatanishwe katika Yesu Kristo.” Baba Mtakatifu akiwa njiani kurejea mjini Vatican, Dominika tarehe 5 Februari 2023 amewaandikia wakuu wa nchi za Sudan ya Kusini, Sudan, Misri, Ugiriki na Italia ujumbe wa matashi mema alipokuwa anapita kwenye anga la nchi zao.
Kwa namna ya pekee kabisa Papa amemshukuru na kumpongeza Rais Salva Kiir Mayardit wa Sudan ya Kusini kwa ukarimu na mapokezi ya “kukata na shoka” waliomwonesha wakati wa hija yake nchini mwao. Amerudia tena kuwahakikishia sala na sadaka yake kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Sudan ya Kusini. Amewatakia wakuu wa nchi mbalimbali usalama, amani, utulivu, ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu. Amekazia pia udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Rais Sergio Mattarella wa Italia amemwelezea kwa ufupi amana na utajiri wa maisha ya kiroho na kiutu aliyoshuhudia wakati wa Hija yake ya Kitume nchini DRC na Sudan ya Kusini. Hawa ni watu wenye kiu ya haki na amani. Amewatakia amani na utulivu pamoja na kuwahakikishia sala na sadaka yake
Baba Mtakatifu baada ya kuwasili mjini Roma alikwenda moja kwa moja kutembelea na kusali kwenye Sanamu ya Bikira Maria Afya ya Warumi “Salus Populi Romani” iliyoko kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu, lililoko Jimbo kuu la Roma, kushukuru na kuweka matunda yote ya hija ya uekumene wa amani ili iweze hatimaye kuzaa matunda ya toba, wongofu wa ndani, haki, amani na upatanisho na hatimaye, akaelekea mjini Vatican.