Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 9 Februari 2023 amekutana na kuzungumza na “Chama cha Wanamichezo wa Vatican: Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 9 Februari 2023 amekutana na kuzungumza na “Chama cha Wanamichezo wa Vatican:  

Jubilei ya Miaka 50 ya Chama cha Wanamichezo wa Vatican: Mazoezi, Nidhamu na Malengo

mwaka 1521, kabumbu ilitandazwa kwenye uwanja wa “Belvedere” mjini Vatican na kushuhudiwa na Papa Leo wa X . Lile tukio likachipuka na kuchanua hadi kufikia kuwa ni “Chama cha Wanamichezo wa Vatican." Chama cha Wanamichezo wa Vatican kina jukumu la kuonesha ushuhuda na Vatican kwa kukazia: Mazoezi katika michezo, Nidhamu na Malengo. Ushuhuda!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Michezo inayo nafasi muhimu sana katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Michezo ni nyenzo msingi katika kusimamia na kudumisha haki msingi za binadamu; ni njia ya mchakato wa utakatifu; ni mahali muafaka pa kuonja uzuri na utakatifu wa kazi ya uumbaji, umoja, udugu na mshikamano wa kweli unaovunjilia mbali ubinafsi kwa kukazia umoja katika ukweli wake! Baba Mtakatifu Francisko anasema, michezo ni muhimu sana katika ujenzi wa jamii na ushiriki mkamilifu katika kudumisha: haki, amani na utulivu bila vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Ili kufikia lengo hili kuna haja ya kuendelea kuwafunda vijana wa kizazi kipya kwa njia ya michezo, umuhimu wa kujikita katika urafiki, udugu na haki, mambo muhimu sana katika ulimwengu mamboleo. Lakini, Baba Mtakatifu anasema, kuna haja ya kuandika ukurasa mpya wa michezo katika ulimwengu mamboleo kwa kujikita katika: ushirikishwaji; ukweli, uwazi na uaminifu pamoja kuwa na upendeleo kwa maskini.

Chama cha Wanamichezo Vatican kinaadhimisha Jubilei ya miaka 50
Chama cha Wanamichezo Vatican kinaadhimisha Jubilei ya miaka 50

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 9 Februari 2023 amekutana na kuzungumza na “Chama cha Wanamichezo wa Vatican: all'Associazione Dilettantistica Sportiva del Vaticano” kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50, tangu kuanzishwa kwake kunako mwaka 1972. Lakini kunako mwaka 1521, kabumbu ilitandazwa kwenye uwanja wa “Belvedere” mjini Vatican na kushuhudiwa na Papa Leo wa X na leo hii, lile tukio limeweza kuchipua na kuchanua hadi kufikia kuwa ni “Chama cha Wanamichezo wa Vatican.” Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, Chama cha Wanamichezo wa Vatican kina jukumu la kuonesha ushuhuda na Vatican kwa kukazia: Mazoezi katika michezo, Nidhamu na Malengo.

Papa Francisko: Zingatieni: Mazoezi, NIdhamu na Malengo
Papa Francisko: Zingatieni: Mazoezi, NIdhamu na Malengo

Mtakatifu Paulo katika Waraka wake wa Kwanza kwa Wakorintho 9: 24-25 anasema, “Je! Hamjui, ya kuwa wale washindanao kwa kupiga mbio, hupiga mbio wote, lakini apokeaye tuzo ni mmoja? Pigeni mbio namna hiyo, ili mpate.” 1Kor 9: 24-25. Anakaza kusema “Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la! Bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwa ajili yake nimeshikwa na Kristo Yesu. Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele; nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu.” Flp 3:12-14. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hivi ni vifungu muhimu vya Maandiko Matakatifu vinavyoweza kusaidia kufikia ari na mwamko wa michezo, kwa kuzingatia kanuni msingi, sheria na taratibu za michezo yaani: mazoezi, nidhamu na malengo. Baba Mtakatifu anasema, michezo inasimikwa katika mazoezi, bila mazoezi, ni vigumu sana kufikia malengo ya michezo.

Ushuhuda wa maisha ya imani ni muhimu hata katika michezo
Ushuhuda wa maisha ya imani ni muhimu hata katika michezo

Nidhamu inafumbatwa katika elimu na majiundo makini, ili kuendelea kujinoa ili hatimaye kufikia kiwango kinachokubalika. Nidhamu inahitajika ili mtu kuweza kujitawala, kudhibiti mihemuko na hivyo kumwezesha kila mchezaji kutekeleza wajibu wake anapokuwa uwanjani. Lengo la michezo ni kujipatia ushindi unaopata msukumo wa ndani unaosimikwa hasa zaidi katika uaminifu na udumifu na kwamba kama wanamichezo wa Vatican wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa umoja na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na Sekretarieti kuu.

Michezo Vatican
09 February 2023, 15:53