Tafuta

Baba Mtakatifu akiwa Barani Afrika amebahatika kukutana na kuzungumza na Wajesuit wanaoishi na kufanya utume wao DRC na Sudan ya Kusini. Baba Mtakatifu akiwa Barani Afrika amebahatika kukutana na kuzungumza na Wajesuit wanaoishi na kufanya utume wao DRC na Sudan ya Kusini.  (Vatican Media)

Mahojiano Maalum Kati ya Papa Francisko na Wayesuit Nchini DRC na Sudan ya Kusini

Papa amekazia kuhusu: Utume wa Wayesuit, Jubilei ya Miaka 1700 ya Kanuni ya Imani ya Nicea, Nadhiri ya Utii wa Wayesuit kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, Wito na Utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro; Dhana ya Utamadunisho na Uinjilishaji ndani ya Kanisa, Ndoto ya Papa kwa Kanisa Barani Afrika, Maisha ya Sala, Utakatifu na Ujumbe maalum kwa Wayesuit, Barani Afrika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kauli mbiu iliyonogesha Hija ya 40 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko kwenye Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo, DRC., kuanzia tarehe 31 Januari hadi tarehe 3 Februari 2023 ni “Wote wapatanishwe katika Yesu Kristo.” Na huko Sudan ya Kusini ni “Wote wawe na umoja” Yn 17:21, hiki ni kielelezo cha ushuhuda wa kiekumene, mshikamano na udugu wa kibinadamu, mwaliko na changamoto ya kujizatiti katika mchakato wa upatanisho, matumaini na ujenzi wa umoja wa Kitaifa. Baba Mtakatifu Francisko katika hija hii ya Kitume amekuwa akiambatana na Askofu mkuu Justin Welby, Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani na Mheshimiwa Dr Iain Greenshields Mkuu wa Kanisa la “Presbyterian” la Scotland kama kielelezo cha ushuhuda wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika huduma, maisha ya kiroho, damu na sala, kuanzia Ijumaa tarehe 3 Februari hadi Dominika tarehe 5 Februari 2023 wamekuwa wakitembelea kwa pamoja nchini Sudan ya Kusini. Huu ni shuhuda wa hija ya uekumene wa amani na matumaini kwa watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini, kushuhudia kwamba inawezekana kwa Wakristo kushirikiana na kushikamana katika umoja na hata katika tofauti zao msingi. Baba Mtakatifu akiwa Barani Afrika amebahatika kukutana na kuzungumza na Wajesuit wanaoishi na kufanya utume wao DRC na Sudan ya Kusini.

Papa Francisko akiwa nchini DRC na Sudan ya Kusini amekutana na Wayesuit
Papa Francisko akiwa nchini DRC na Sudan ya Kusini amekutana na Wayesuit

Katika mazungumzo yao, amekazia kuhusu utume wa Wayesuit katika Ulimwengu mamboleo, Jubilei ya Miaka 1700 ya Kanuni ya Imani ya Nicea, Nadhiri ya Utii wa Wayesuit kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, Wito na Utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro; Dhana ya Utamadunisho na Uinjilishaji ndani ya Kanisa, Ndoto ya Papa Francisko kwa Kanisa Barani Afrika, Maisha ya Sala, Utakatifu na Ujumbe maalum kwa Wayesuit, Barani Afrika. Baba Mtakatifu Francisko anawataka Wayesuit katika ulimwengu mamboleo, kuendelea kujikita zaidi na zaidi katika kumwilisha mafungo ya kiroho kadiri ya Mapokeo ya Mtakatifu Inyasi wa Loyola, ili kuwasaidia watu wa Mungu waweze kuwa na mang’amuzi sahihi katika maisha. Wayesuit wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Upatanisho, haki na amani, daima wakisindikizana na kuambatana na maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii, ili kujenga leo na kesho iliyo bora zaidi katika maisha yao. Wawe mstari wa mbele katika kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote kadiri ya Mamlaka fundishi ya Kanisa yaani “Magisterium” na kama yanavyofafanuliwa katika Waraka wake wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote.”

Utunzaji Bora wa Mazingira Nyumba ya Wote
Utunzaji Bora wa Mazingira Nyumba ya Wote

Baba Mtakatifu anasikitika kuona na kushuhudia madhara makubwa yanayotokana na Vita Kuu ya Tatu ya Dunia, inayopiganwa vipande vipande na kimsingi waathirika wakuu ni watoto, wanawake na wazee. Haya ni matokeo ya biashara haramu ya silaha inayokuza na kusambaza utamaduni wa kifo kama ambavyo wameshuhudia wahanga wa vita, nyanyaso na madhulumu sehemu mbalimbali za dunia. Kuna matukio makubwa mawili ambayo yako mbele ya Wakristo wote. Mosi, Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo yanajiandaa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 1, 700 tangu Mtaguso wa Nicea ulipoadhimishwa kunako mwaka 325 na kilele cha maadhimisho haya ni mwaka 2025, tukio la pekee na muhimu sana. Mwaka huo Wakristo wote wataadhimisha Pasaka ya Bwana siku moja, matendo makuu ya Mungu kwa waja wake. Kanuni ya Imani ya Nicea-Constantinopoli ni formula rasmi ambayo ilipitishwa na Mababa wa Mtaguso wa Kwanza wa Nicea (325) ikakamilishwa na Mtaguso wa kwanza wa Konstantinopoli (381) ili kubainisha imani sahihi ya Kanisa Katoliki dhidi ya uzushi, hasa wa Ario na wafuasi wake. Katika mazingira hayo, lengo kuu lilikuwa kwanza kabisa ni kumkiri Kristo Yesu “Mungu kweli kwa Mungu kweli” yaani Mungu kweli sawa na Baba, halafu kwamba Roho Mtakatifu anastahili kuabudiwa pamoja na Baba na Mwana (Utatu Mtakatifu). Wakristo wanataka kutembea pamoja na Kristo ambaye ni njia, ukweli na uzima. Watu wanamtafuta Kristo Yesu hata bila ya kutambua.

Jubilei ya Miaka 1, 700 ya Kanuni ya Imani ya NICEA
Jubilei ya Miaka 1, 700 ya Kanuni ya Imani ya NICEA

Uinjilishaji mpya unaotekelezwa na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo unajikita katika mchakato wa: Majadiliano ya kiekumene na kidini ili kujenga na kudumisha: utu, heshima, haki msingi za binadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wao. Baba Mtakatifu Francisko anakazia uekumene wa: damu, maisha ya kiroho, sala na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ikumbukwe kwamba, uekumene wa utakatifu wa maisha unafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; kwa kujikana na kujivika fadhila ya unyenyekevu; moyo wa ukarimu na udugu; upole, uvumilivu na kutumikia bila ya kujibakiza. Wakristo wanakumbushwa kwamba, kadiri wanavyojitahidi kuishi maisha matakatifu mintarafu Injili, ni kwa kadiri ile ile wataweza kuhamasishana kutekeleza mchakato wa ujenzi wa umoja wa Wakristo na udugu kati yao. Uekumene wa damu unajikita katika ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Majadiliano ya kiekumene ni sehemu ya vipaumbele vya Makanisa Ulimwenguni
Majadiliano ya kiekumene ni sehemu ya vipaumbele vya Makanisa Ulimwenguni

Itakumbukwa kwamba, kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa tangu ulipotokea Mpasuko wa Kanisa kunako mwaka 1054, takribani miaka elfu moja iliyopita, Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli alihudhuria katika Ibada ya Misa Takatifu, Khalifa wa Mtakatifu Petro alipokuwa anaanza utume wake rasmi. Baba Mtakatifu Francisko na Patriaki Bartolomeo wa kwanza, walikutana kwa mara ya kwanza walipokuwa wanapeana busu la amani, katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Papa Francisko tarehe 19 Machi 2013. Patriaki Bartolomeo alinukuriwa akisema kwamba, Makanisa haya mawili kadiri ya siku zinazovidi kusonga mbele yanazidi kudumisha majadiliano ya kiekumene yanayopania kujenga na kuimarisha umoja wa Wakristo. Majadiliano kati ya Makanisa haya mawili yanajikita katika taalimungu, dhamana na nafasi ya Papa katika maisha na utume wa Kanisa. Kuhusu Nadhiri ya Utii wa Wayesuit kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, Baba Mtakatifu Francisko anasema, kimsingi Wayesuit hawapaswi kuwania, au kukubali kupokea dhamana na majukumu ya uongozi ndani ya Kanisa. Kwa mara mbili alikataa kupokea uteuzi wa kuwa Askofu, lakini baada ya kuzingatia Nadhiri ya Utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, mara ya tatu, akakubali na kuteuliwa kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Buenos Aires, Askofu mkuu, Kardinali na hatimaye, kwa sasa ndiye Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Majadiliano ya kidini ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi
Majadiliano ya kidini ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kulihamasisha Kanisa kuhusu umuhimu wa kumwilisha matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kwa kukazia watu wote wa Mungu kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Hiki ni kiini cha “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa”. Baba Mtakatifu anakazia ukuhani wa waamini wote; umuhimu wa waamini kushiriki kikamilifu Sakramenti za Kanisa; umuhimu wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni; ari na mwamko wa kimisionari pamoja na umuhimu wa waamini walei kuwa ni chachu ya uinjilishaji mpya na utakatifu kwa njia ya ushuhuda wa maisha, kama kielelezo makini cha imani tendaji! Umoja, upendo na mshikamano wa dhati ni mambo msingi katika utangazaji na ushuhuda wa Injili ya upendo kwa watu wa Mataifa. Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa inazingatia mambo yafuatayo: Ufahamu wa kina wa Neno la Mungu; umuhimu wa toba na wongofu wa ndani; ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Haya ni mambo msingi katika mchakato mzima wa uinjilishaji mpya katika ulimwengu mamboleo. Dhana ya Sinodi ni wazo lililotolewa na Mtakatifu Paulo VI, linaloihusisha Familia ya Mungu katika ujumla wake. Baba Mtakatifu Francisko analitaka Kanisa kuanza kumwilisha dhana hii katika maisha ya Makanisa mahalia; Mabaraza ya Maaskofu; Mashirikisho ya Kanda hadi kufikia Kanisa la Kiulimwengu. Mtakatifu Paulo VI, Muasisi wa maadhimisho ya Sinodi mara baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican anasema, Sinodi ni chombo cha kimisionari na uinjilishaji mpya unaolisaidia Kanisa baada ya kutembea pamoja katika sala, tafakari, mang’amuzi na hatimaye, utekelezaji wake unaofanywa na watu wote wa Mungu kadiri ya wito na nafasi zao katika maisha na utume wa Kanisa.

Sinodi ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa
Sinodi ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa

Sinodi ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo kumbe, badala ya kuwazia maadhimisho ya Sinodi Maalum ya Kanisa kwa ajili ya DRC, kama ilivyokuwa katika Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia yaliyofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 6-27 Oktoba 2019 kwa kunogeshwana kauli mbiu "Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ya ekolojia fungamani.” Ilikazia kuhusu umuhimu wa: kuona, kung'amua na kutenda! Ni Sinodi ambayo ilipembua tema mbalimbali: kuhusu: haki jamii, malezi ya awali na endelevu, katekesi makini, liturujia na utambulisho wa Kanisa katika Ukanda wa Amazonia. Yote haya yanaweza kuadhimishwa kwa njia ya Sinodi ya Maaskofu Katoliki DRC kwa kujikita zaidi katika uhalisia na vipaumbele vya watu wa Mungu nchini DRC. Kuhusu Wito na Utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, Baba Mtakatifu anakaza kusema, tayari alikwisha kuandika barua ya kung’atuka madarakani pale atakaposhindwa kutekeleza dhamana na majukumu yake ya: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Lakini, huu, haupaswi kuwa ni utamaduni wa Kanisa Katoliki. Hayati Papa Benedikto XVI alikuwa na ujasiri wa kung’atuka madarakani, baada ya kukabiliana na changamoto za Kiafya. Papa Francisko ana amini kwamba, Utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro unapaswa kuwa ni “Ad Vitam”, yaani ni kwa ajili ya maisha yote. Ikiwa watu wanataka kuzoea kulishwa “matango pori” basi italibidi Kanisa Katoliki kufanya uchaguzi mara kwa mara. Kwa upande wa mkuu wa Shirika la Wayesuit, utume huu unapaswa kuwa ni kwa ajili ya maisha yote.

Uinjilishaji na utamadunisho ni chanda na pete
Uinjilishaji na utamadunisho ni chanda na pete

Utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu Barani Afrika ni mchakato unaofumbata uinjilishaji na utamadunisho. Huu ni mchakato unaogusa maisha na mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili na wala Kanisa halina sababu ya kufanya wongofu wa shuruti. Kanisa Katoliki halina utamaduni unaoweza kujitambulisha nao. Waamini watambue kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili, watu ambao wanapaswa kuwa tayari kujisadaka kwa ajili ya uinjilishaji unaopania kuleta upyaisho katika maisha ya watu na kama njia ya kutamadunisha Injili ili kuinjilisha tamaduni mintarafu tunu msingi za Kiinjili na kwamba, Roho Mtakatifu ndiye mhimili mkuu wa mchakato wa Uinjilishaji. Baba Mtakatifu anasema, anapenda na kuthamini sana mchakato wa utamadunisho wa Liturujia nchini DRC na ameshiriki Liturujia hii kwa mara tatu, kama kielelezo cha sanaa na maisha ya watu wa Mungu nchini DRC. Kanisa anasema Baba Mtakatifu linapaswa kuwa ni hospitali ya matumaini kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo; watu walioko kwenye Uwanja wa vita, tayari kuwaganga na kuwaponya wanaosumbuka kiroho na kimwili. Hii ni changamoto ya kugundua na kupyaisha maisha, utume na utambulisho wa Kanisa, ili kutekeleza dhamana na utume wake kadiri ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, kielelezo makini cha Mchungaji mwema, anayejisadaka kwa ajili ya Kondoo wake. Kuna watu wamejeruhiwa sana na malimwengu, wito na maisha ya Kanisa ni kuwaendea hawa ili kuwapa tiba muafaka. Kanisa linapaswa kuwapenda na kuwahudumia: Watakatifu wa Mungu na wadhambi wanaojitahidi kumwongokea Mungu, tayari kutembea katika utakatifu wa maisha.

Makanisa mahalia yanaweza kuadhimisha Sinodi zao
Makanisa mahalia yanaweza kuadhimisha Sinodi zao

Ndoto ya Baba Mtakatifu Francisko kwa Kanisa ni kuona waamini wakiwa imara na madhubuti katika ushuhuda, kielelezo cha imani tendaji. Mapadre wawe ni wahudumu wa watu wa Mungu. Uhusiano kati ya Serikali na Kanisa unapaswa kufumbwa katika misingi: Uhuru na Usalama wa maisha na utume wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu, kwa Neno, Sakramenti na Matendo ya huruma. Utamaduni wa Kikristo, uwawezeshe waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutoa kipaumbele cha kwanza kwa: Imani, matumaini na mapendo; huruma na msamaha wa kweli. Bara la Afrika halina budi kusonga mbele katika medani mbalimbali ili kusaidia mchakato wa maboresho ya maisha ya watu wateule wa Mungu na kamwe Afrika isigeuzwe kuwa kama “kichwa cha mwendawazimu, mahali pa kunyonya na kudhulumu Bara la Afrika linawahitaji viongozi wazalendo, wenye uchungu wa ustawi, maendeleo na mafao ya watu wao: Linawahitaji wanasiasa wenye akili na upeo mpana, watu wenye uwezo wa kukemea na kupambana na saratani ya rushwa na ubadhilifu wa mali ya umma, kwa vitendo; katika kweli na haki. Kuna haja ya kuwekeza katika mchakato wa kuunda wanasiasa wa kweli, waaminifu na waadilifu. Baba Mtakatifu anawaalika makleri, watawa na waamini walei kujenga utamaduni wa kusali daima, kutafakari Neno la Mungu, kuboresha maisha yao kwa Sakramenti za Kanisa na hususan Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho kwa kuongozwa na uhalisia wa maisha.

Kanisa ni Sakramenti ya Huruma ya Mungu
Kanisa ni Sakramenti ya Huruma ya Mungu

Utunzaji bora wa mazingira ni changamoto inayojikita katika misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi kwa sababu mazingira ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu. Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” umegawanyika katika sura kuu sita: Mambo yanayoendelea kujiri katika mazingira; Injili ya Kazi ya Uumbaji na Amani Duniani; Vyanzo vya mgogoro wa Ikolojia na jinsi vinavyohusiana na watu; Ikolojia ya mazingira, uchumi na jamii. Njia za kupanga na kutenda na mwishoni ni kuhusu umuhimu wa elimu ya ikolojia inayojikita katika wongofu wa ndani, furaha na amani, Sakramenti za Kanisa pamoja na sala. Waraka huu una mwelekeo wa umoja na mshikamano ambao unadhihirishwa na mchango uliotolewa na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Waraka huu anasema Baba Mtakatifu umepokelewa kwa mikono miwili Barani Afrika, lakini bado unahitaji kumwilishwa katika vipaumbele vya maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika, hususan kuhusu amana, rasilimali na utajiri wa Bara la Afrika unapaswa kuwa ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Barani Afrika. Baba Mtakatifu anawataka Wayesuit Barani Afrika wawe ni watu wenye huruma na mapendo; watu wa sala wanaotangaza na kushuhudia ukaribu wa Mungu kwa watu wake.

Papa Wayesuit DRC na S. Kusini

 

 

19 February 2023, 15:38