Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 20 Februari 2023 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Taasisi ya Kipapa ya Maisha. Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 20 Februari 2023 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Taasisi ya Kipapa ya Maisha.  (Vatican Media)

Mkutano Mkuu wa Taasisi ya Kipapa ya Maisha: Teknolojia na Utu, Heshima na Haki Msingi

Changamoto kuu tatu zinazoendelea kumwandamana mwanadamu kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia katika tiba ya maisha ya mwanadamu: Mosi ni mabadiliko makubwa ya maisha ya mwanadamu. Pili, ni madhara makubwa kuhusu tafsiri ya mtu na mahusiano yake asili, kibaiolojia na kiteknolojia. Tatu ni dhana ya ufahamu na madhara yake. Utu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika Karne ya Ishirini na Moja, kumekuwepo na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya tiba ya mwanadamu ambayo kwa sasa inatishia Injili ya uhai; kwa kusababisha kinzani katika kanuni maadili, kijamii na kisheria, kiasi hata cha kutishia utu na heshima ya binadamu mintarafu nadharia na vitendo vya sayansi. Kanisa kwa upande wake linapenda kujikita katika asili, umuhimu na hatima ya maisha ya binadamu ili kufafanua mambo yanayotishia uhai wa binadamu; ubora wa maisha pamoja na kuangalia fursa zinazotolewa na maendeleo makubwa ya sayansi pamoja na teknolojia katika matamanio halali ya maboresho ya maisha ya binadamu bila kutumbukizwa katika mtego wa wajanja wachache kutaka faida kubwa kwa ajili ya mafao yao binafsi. Licha ya maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia duniani, lakini bado kuna watu wengi wanaoshambuliwa na magonjwa, njaa na umaskini mkubwa wa hali na kipato duniani, changamoto kwa watunga sera na maendeleo ya binadamu kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu. Katika ulimwengu mamboleo kuna teknolojia inayoibuka na kuungana kutokana na maendeleo na mwingiliano mkubwa wa sayansi, kwa ajili ya maboresho ya afya ya mwanadamu.

Injili ya Uhai ipewe Kipaumbele cha kwanza
Injili ya Uhai ipewe Kipaumbele cha kwanza

Hii ni pamoja na teknolojia ya habari na mawasiliano, bioteknolojia na matumizi ya roboti, yanayowawezesha wanasayansi kuingilia kati kwa undani sana katika viumbe hai. Taasisi ya Kipapa ya Maisha katika mkutano wake wa 28 kwa Mwaka 2023 umenogeshwa na kauli mbiu “Huduma kwa mtu mzima teknolojia zinazotukuka kwa mafao ya wengi.” Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 20 Februari 2023 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Taasisi ya Kipapa ya Maisha na hivyo kubainisha changamoto kuu tatu zinazoendelea kumwandamana mwanadamu kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia katika tiba ya maisha ya mwanadamu: Mosi ni mabadiliko makubwa ya maisha ya mwanadamu kutokana na sayansi. Pili, ni madhara makubwa kuhusu tafsiri ya mtu na mahusiano yake asili, kibaiolojia na kiteknolojia. Tatu ni dhana ya ufahamu na madhara yake. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza wajumbe wa Taasisi ya Kipapa ya Maisha kwa kusimama kidete kulinda, na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Katika mkutano wao mkuu wa 28 wanajadili kuhusu uhusiano uliopo kati ya binadamu na teknolojia zinazotukuka kwa ajili ya mafao ya wengi. Mtazamo wa Mama Kanisa ni kutaka kuona kwamba, maendeleo ya sayansi na teknolojia yanajikita zaidi katika huduma kwa binadamu, kwa kulinda utu, heshima na haki zake msingi.

Utu, heshima na haki msingi za binadamu
Utu, heshima na haki msingi za binadamu

Changamoto ya kwanza ni mabadiliko ya maisha ya mwanadamu kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, kama jibu la wito wa kazi ya mikono ya binadamu, ili kumwezesha mwanadamu kutambua zaidi utu wake, karama, akili na uwajibikaji wake mintarafu kazi ya uumbaji. Kumbe, kuna mwingiliano wa karibu sana kati ya: shughuli za kitamaduni, kijamii pamoja na mazingira. Maendeleo ya sayansi na teknolojia yamemwezesha mwanadamu kutambua kwamba, haya ni mambo yanayotegemeana na kukamilishana katika ujumla wake. Changamoto za uharibifu wa mazingira nyumba ya wote yamesababisha mabadiliko makubwa katika maisha ya mwanadamu mintarafu milipuko ya magonjwa kama vile Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, Nishati ya umeme pamoja na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani. Maendeleo fungamani ya binadamu yanapaswa kuzingatia mahusiano na mwingiliano huu. Pili, ni madhara makubwa kuhusu tafsiri ya mtu na mahusiano yake asili, kibaiolojia na kiteknolojia. Hapa kuna haja ya kufanya tafakari ya kina kuhusu: utu, heshima na haki msingi za binadamu; mang’amuzi ya mahusiano ya mtu katika uhalisia wake. Ikumbukwe kwamba, sayansi na teknolojia haiwezi kuwa mbadala wa hali halisi ya binadamu na wala, mahusiano katika mitandao ya kijamii, hayawezi kuchukua nafasi ya mahusiano halisi yanayofumbatwa katika maisha ya binadamu.

Utu wa binadamu hauna mbadala
Utu wa binadamu hauna mbadala

Kumbe, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, utu, heshima na haki msingi za binadamu zinazingatiwa sanjari na huduma ya maboresho ya afya kwa wote kwa kutenga rasilimali fedha ya kutosha kwa ajili ya maboresho ya huduma ya afya kwa wote, maskini na wanyonge ndani ya jamii wakipewa kipaumbele cha kwanza. Kumbe, kuna haja ya kuwa makini mintarafu maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, mahusiano na mafungamano ya kijamii pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na kuzingatia mila, desturi na tamaduni njema za watu husika. Tatu ni dhana nzima ya ufahamu na madhara yake mintarafu kanuni maadili na utu wema, ustawi na maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili, na wala si kuangalia upande mmoja tu wa mwili wa mwanadamu kwani kitu kizima ni kikubwa kuliko sehemu yake. Kila kitu hapa duniani kina uhusiano na mafungamano na kitu kingine. Kumbe, kuna haja ya kujenga na kudumisha majadiliano ya kina katika ukweli na uwazi; sanjari na urafiki wa kijamii; majadiliano ya kidini na kiekumene pamoja na ushirikiano na watu mbalimbali, daima kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Mwenyezi Mungu, chemchemi ya ukweli mfunuliwa. Kumbe, maendeleo fungamani ya binadamu yanapaswa kusimikwa katika uwajibikaji na tunu msingi za maisha na ufundaji wa dhamiri nyofu.

Papa Injili ya Uhai
21 February 2023, 17:03